Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Siku Nzuri Sana
Bwana alitumia asili ya baba yangu kumsaidia kupatanisha familia yetu.
Baba yangu marehemu, Claude Roy, alifariki mwaka 2015, si muda mrefu baada ya kubatizwa. Wakati huo, mama yangu, ndugu zangu, na mimi tulikuwa waumini wa Kanisa kwa muda fulani, lakini kwa miongo kadhaa baba yangu alibaki bila nia ya kujiunga.
Baada ya muda, alisema, “moyo wangu ulishupazwa, na nikakasirishwa na kutembelewa na watoto na wajukuu wangu na nilitaka kujitenga na familia yangu. Mivutano ilikua katika nyumba yangu, na uhusiano wangu na mke wangu ukawa mgumu.”
Karibu wakati huu, alianza kuwatafuta mababu zake wa Kanada waliokuwa wazao wa mataifa ya Mi’kmaq na Huron-Wendat. Baada ya kufika katika jumuiya ya Mi’kmaq karibu na mahali alipokulia, alialikwa kwenye powwow, sherehe ya Asili ya Kiamerika.
Wakati wa jioni ya powwow, chifu mkuu alifungua mikono yake na kuwaomba watoto waje kwake ili aweze kuwabariki. Mahubiri yaliyofuata juu ya umuhimu wa familia na uzao yalimpiga baba yangu kama radi.
Katika wakati huo, alisema, “Niliona familia yangu ikishikilia mikono yao kwangu wakati nimewaguezia mgongo wangu. Nilijawa na huzuni kubwa, isiyoelezeka kana kwamba moyo wangu ulikuwa unavunjika vipande vipande. Nilijua katika wakati huo kwamba Bwana alikuwa ametumia maneno ya kabila la mababu zangu kulainisha moyo wangu. Nilijua ilinibidi nimgeukie Baba yangu wa Mbinguni na kurekebisha uharibifu niliosababishia familia yangu.”
Baba alianza kuleta amani na familia yetu, akiomba msamaha kutoka kwa kila mwanafamilia. Kwa mfano wa mke na watoto wake, alianza kusali na kusoma Kitabu cha Mormoni. Akiwa amesoma historia nyingi kuhusu bara la Amerika, alihisi kuvutwa kwenye Kitabu cha Mormoni. Ukweli wake ulithibitishwa kwake mara moja.
“Nikiwa nimezungukwa na familia yangu, nilibatizwa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho,” alisema. “Hii ilikuwa siku nzuri sana katika maisha yangu! Ninashuhudia juu ya nguvu ya mfano wa upendo. Kwa miaka 36, mke wangu alishikilia imani yake na alikuwa mfano kama wa Kristo kwangu, ingawa moyo wangu ulikuwa mgumu. Kisha, wikiendi moja ilibadilisha kila kitu kwangu.”
Hadithi ya baba yangu kwa uzuri inatukumbusha kwamba “mikono ya Mwokozi ya rehema imenyoshwa kwetu [sisi]” na kwamba tunapotubu, hakika Yeye atatupokea (ona Alma 5:33).