“Wote Wanahitajika katika Mwili wa Kristo,” Liahona, Jan. 2025.
Wanawake wa Agano
Wote Wanahitajika katika Mwili wa Kristo
Tunaweza kusaidia kujenga udada ulimwenguni kote ambao ni mzuri zaidi, thabiti zaidi, na wenye kuunganika zaidi kwa sababu ya uhusiano wetu wa agano na Mungu.
Sisi sote tunataka kuhisi kwamba tuna nafasi na kwamba sisi ni sehemu ya na tunahitajika katika Kanisa la urejesho la Yesu Kristo. Tunaweza kumsaidia kila mmoja wa dada zetu na kaka zetu, bila kujali umri au hali gani, kuhisi kwamba wana nafasi na ni sehemu ya na wanahitajika pia. Sisi sote ni watoto wa wazazi wa mbinguni na hivyo ni akina dada na kaka wa kiroho. Miunganiko hiyo kwa kila mmoja ni muhimu sana.
Tunapoingia katika uhusiano wa agano na Mungu, siyo tu huongeza kwa kina na huboresha uhusiano wetu na Yeye bali pia huathiri uhusiano wetu na watoto Wake wengine—ndugu zetu wa kiroho. Asili katika maagano tunayofanya na Mungu, kuanzia na ubatizo, ni jukumu letu la kupendana na kujaliana.
Tatizo la Upweke
Daktari mkuu wa upasuaji wa Marekani, mwalimu mkuu wa afya wa Marekani, alishiriki kauli hii kuhusu umuhimu wa mahusiano: “Janga letu la upweke na kutengwa limekuwa mgogoro wa afya ya umma usiothibitishwa ambao umedhuru afya ya mtu binafsi na jamii. Uhusiano wetu ni chanzo cha uponyaji na hali nzuri iliyojificha kutoka kwenye uoni wetu. … Kutokana na matokeo makubwa ya afya ya upweke na kutengwa, lazima tuweke kipaumbele katika kujenga uhusiano wa kijamii kwa njia sawa na vile tulivyoyapa kipaumbele masuala mengine muhimu ya afya ya umma. … Kwa pamoja, tunaweza kujenga [jamii] ambayo ni yenye afya zaidi, thabiti zaidi, isiyo na upweke na imeunganishwa zaidi.”
Kwa pamoja sisi tunaweza kusaidia kujenga udada wa ulimwenguni kote wa rika zote ambao ni mzuri zaidi, thabiti zaidi, usio na upweke, na uliounganishwa zaidi kwa sababu ya uhusiano wetu wa agano na Mungu na jukumu letu kwa kila mmoja kama wanafunzi wa Yesu Kristo.
Kama Mwokozi wetu alivyosema, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:35).
Miunganiko na Kila Mmoja
Tunaweza kusaidia kupunguza kasi ya janga la upweke kwa kutengeneza nafasi za kukaribisha na salama ndani ya mikusanyiko yetu na hasa ndani ya Muungano wetu wa Usaidizi, ambapo wote wanaweza kuhisi upendo wa Bwana kwa sababu wamezungukwa na upendo wetu.
Uzoefu wetu kanisani umekusudiwa kutoa uhusiano huo muhimu pamoja na Bwana na kila mmoja wetu ambao unahitajika sana kwa ajili ya hali yetu ya kimwili, kihisia na kiroho. Kuna nguvu kubwa katika umoja na uzuri wa utofauti; yote yanahitajika katika mwili wa Kristo (ona 1 Wakorintho 12:12–27). Kama vile miti mikubwa ya redwood inavyounganisha mizizi yao na inaweza kustahimili nguvu za asili kwa sababu inasimama pamoja, tunahitaji kuunganisha mikono, kusimama pamoja, na kuimarishana katika dhoruba za maisha.
Tunapopata kuwajua wale tunaohisi kuwa ni tofauti na sisi, tunatambua tunayo mengi yanayofanana kuliko tulivyofikiria. Kila mtu ana mengi ya kuchangia, uzoefu mwingi mzuri na tofauti wa maisha ambao unaweza kubariki maisha yetu. Kusikiliza hadithi za wengine na kutafuta kuzielewa kutabadili mioyo yetu, na hukumu na hofu tuliyokuwa nayo kwa wengine inaweza kubadilishwa na hisia za shukrani ya kuwa pamoja nao katika maisha yetu.
Bwana anaweza kutusaidia kuwaona watu wengine kama Yeye anavyowaona, na Yeye anaweza kujaza mioyo yetu kwa upendo, kutuwezesha kuinua, kufariji, kucheka, kulia nao, na kukuza kuwa sehemu ya kwa wale wanaotuzunguka. Yeye atatusaidia kujua kile kinachohitajika na jinsi ya kuwa baraka kwa wengine katika safari yao.
Bila shaka, kuna Mmoja tu ambaye anaweza kuelewa kikamilifu na kuhisi huruma kikamilifu. Kama sehemu ya dhabihu Yake ya upatanisho, Yeye aliteseka “maumivu na masumbuko na majaribu ya kila aina; … [akijichukulia] maumivu na magonjwa ya watu wake” (Alma 7:11) ili kwamba tuweze kuhakikishiwa kwamba kamwe hatuko peke yetu kamwe.
Kila mmoja wetu ameitwa kuwapenda na kuwahudumia watoto wa Baba yetu wa Mbinguni kama ambavyo Mwokozi angefanya. Tunashirikiana Naye katika kuwabariki wengine ili kwamba wao na sisi tuweze kuhisi kikamilifu upendo wa Mwokozi wetu. Acha tuunganishe mikono na kwa furaha tutembee pamoja nyumbani. Ninashuhudia kwamba hii ni kazi takatifu ambayo sisi sote tumeitwa kuifanya.