“Kazi za Mungu Zilidhihirishwa,” Liahona, Jan. 2025.
Taswira za Imani
Kazi za Mungu Zilidhihirishwa
Sikujua kama ningeponywa au kubaki kipofu. Nilijua tu kwamba mapenzi ya Mungu yangetendeka na kwamba Yeye angenibeba kupitia majaribu yangu.
Picha na Christina Smith
Mnamo Januari 7, 2023, niliamka na upofu zaidi katika jicho langu la kulia na takribani asilimia 10 tu ya uoni katika jicho langu la kushoto. Ulimwengu ghafla ulikuwa unaonekana kuwa kijivu—kiuhalisia. Rangi na nuru vilikuwa vimetoweka. Nilikuwa gizani, mwenye hofu na shaka.
Kama msanii, yote niliyotaka kufanya yalikuwa ni kuongezea kwenye uzuri wa ulimwengu kupitia sanaa—shauku ambayo nimekuwa nayo karibu maisha yangu yote. Ningefanya nini kama nisingeona tena, kushiriki katika, au kuthamini uzuri wa ulimwenguni?
Siku chache kabla, macho yangu yalikuwa yanaogopa mwanga, na mistari mikali ya mwanga ilianza kulengalenga katika uoni wangu. Nikiwa na wasiwasi, nilikwenda kumwona daktari wa macho. Baada ya kunichunguza, alisema kujaa kwa ute wa ubongo na uti wa mgongo ulikuwa unasababisha shinikizo katika fuvu langu, na kusababisha dalili kama za uvimbe wa ubongo, ikiwa ni pamoja na kupoteza uoni.
Aliniambia uoni wangu ungepungua polepole kwa miezi kadhaa ijayo ikiwa sitapata tiba. Alinihakikishia, hata hivyo, kwamba nilikuwa na muda mwingi wa kupata daktari wa neva, ambaye angeweza kutibu kujaa kwa ute.
Nikiwa na wasiwasi, niliomba baraka ya uponyaji na faraja kutoka kwa baba yangu, ambaye anahudumu kama askofu. Wakati yeye na mmoja wa washauri wake waliponibariki, hadithi yangu pendwa ya Biblia ilinijia akilini mwangu:
“Wanafunzi wa Yesu walimwuliza, “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?
“Mwokozi alijibu, “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake: bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake” (Yohana 9:2–3).
Tena na tena akilini mwangu, niliwaza, “nguvu za Mungu zitadhihirika katika hili.” Sikujua kama hiyo ilimaanisha ningeponywa au kubaki kipofu. Nilijua tu kwamba mapenzi Yake yangetendeka na kwamba Yeye angenibeba kupitia majaribu yangu.
“Unaweza Kuona Vidole Vingapi?”
Nilikuwa na miadi iliyopangwa siku chache baadaye na daktari wa neva, lakini asubuhi ile ya Januari, dada yangu mkubwa, Kylie, alihisi msukumo kwamba familia yangu inapaswa kunipeleka kwenye chumba cha dharura katika hospitali iliyo karibu. Madaktari haraka waliamuru kipimo cha skani cha CT na wa kwanza ya vipigo vyepesi kadhaa kwenye uti wa mgongo ili kupunguza shinikizo la ute kwenye ubongo na uti wa mgongo. Siku iliyofuata, nilichuliwa MRI mbili (magnetic resonance imaging). Kisha daktari wa macho alinichunguza.
“Unaweza kuona vidole vingapi?” aliuliza, akinyanyua juu vidole kadhaa kutoka usoni mwangu. Sikuweza kuona chochote.
Baada ya uchunguzi wake, alihitimisha kwamba nilikuwa na dalili za uvimbe uliojifichika ubongoni na uvimbe wa neva za macho. Hakuna hali peke yake iliyoonekana kuhusika kikamilifu. Alieleza kwamba kwa uzito wa kupoteza uoni wangu, kupona kungeweza kuchukua zaidi ya mwaka mmoja na kwamba uoni wangu usiweze kurudi kikamilifu. Alipendekeza kipimo kikubwa cha sindano za kusisimua msuli na dawa nyingine.
Baada ya kuondoka, nilianza kulia. Mama yangu alinihakikishia, “Kama huwezi kushikilia imani yako hivi sasa, unaweza kutegemea yetu.”
“Tafadhali Nifariji”
Katika siku yangu ya tatu hospitalini, daktari wa neva aliomba MRV (magnetic resonance venography) ya safu yangu ya uti wa mgongo na ubongo, kutafuta uvimbe au kizuizi. Saa 10:00 usiku, siku mbili baada ya kuamka kipofu, nilianza saa tano za MRV. Katika maandalizi, familia yangu ilipanga kusali na kufunga kwa ajili yangu asubuhi ile. Baba yangu, ambaye alilala kando yangu kwenye benchi kila usiku katika chumba changu cha hospitali, alinipa baraka nyingine—baraka ya pili kati ya kadhaa nilizopokea.
Wakati fundi wa hospitali alipouliza kama nilitaka kusikiliza muziki wakati wa kupimwa kwangu, niliomba nyimbo kutoka kwa mwimbaji nimpendaye. Fundi huyo aliweka visikiliza mziki ndani ya masikio yangu na kubana kichwa changu kwa kitambaa cha uso cha matundu ili kuniweka sawa. Katika mchakato huo, alipiga vitoa sauti vya kichwani karibu kutoka masikioni mwangu. Sikuweza kusikia muziki wowote wakati MRV ilipoanza.
Muda mrefu kadri utaratibu ulivyochukua, ndivyo nilivyohisi joto ndani ya mashine ya kuskani. Baada ya kile kilichoonekana kama milele, niliambiwa nilikuwa nafanya vizuri sana na kuendelea kwenda kwa muda mrefu kidogo. Lakini nilihisi hofu na kufadhaika kutokana na joto, sauti kubwa, na vizuizi vikinishikilia bado.
Katika sala ya kimya kimya, nililia: “Baba wa Mbinguni, tafadhali nifariji. Nipo mpweke sana. Ninahitaji msaada Wako. Ninahitaji familia yangu.”
Mara moja, sauti laini ya kinanda ilipiga mwangwi masikioni mwangu. Ilikuwa ni kutoka kwenye moja ya nyimbo nizipendazo—moja ambayo dada yangu mdogo, Morgan, hucheza kwenye kinanda. Nisingetarajia kusikia kutoka kwa vitoa sauti vya masikioni kutokana na kelele za mashine ile. Ilionekana kama Morgan alikuwa pamoja nami, na sikuwa peke yangu. Kelele zilitoweka. Joto likatoweka. Hofu ya kuwa sehemu ile finyu ikatoweka.
Nilihisi kuwa nje ya mwilini mwangu, kama vile nilikuwa nikielea juu ya bahari katika anga. Nilihisi kuzungukwa na upendo wa Mungu na kwa upendo wa familia yangu. Hivyo tu, nilikuwa mtulivu. Ilikuwa saa 1:30 asubuhi, wakati familia yangu ilipoanza kufunga kwa ajili yangu. Sehemu iliyobaki ya saa tano za MRV ilipita mara moja, na kisha nikasikia, “Umekamilisha.”
Upendo niliohisi kutokana na uzoefu huo uliniacha nikiwa na machozi na kupunguza uchovu niliohisi wakati wa kukaa kwangu hospitalini. Sikujua kama uoni wangu ungerudi, lakini nilijua kwamba Mungu alikuwa pale na alikuwa amesikia sala yangu. Baada ya siku nne hospitalini, niliruhusiwa.
“Huu Ni Muujiza!”
Kila siku kwa wiki mbili zilizofuata, nilirudi hospitalini kwa ajili ya dawa, na kila siku nilihitaji mabadiliko katika uoni wangu—kijivu cheusi kikififia kuwa kijivu chepesi, vivuli vikitokea kuzunguka vidole vyangu mbele ya uso wangu, ukungu wa rangi ya chungwa kwenye TV ukigeuka kuwa ua. Kila uboreshaji mdogo ulikuwa ushindi.
Wiki mbili baada ya kuruhusiwa kutoka, upimaji ulionyesha kwamba uoni wangu ulikuwa umetoka sifuri hadi karibu uoni kamili kwa macho yote.
“Bronwyn, nini kimetokea?” daktari wangu wa macho aliuliza.
“Vema, tumekuwa tukisali, na nimepokea baraka,” nilijibu.
“Huu ni muujiza!” alisema. “Sijawahi kuona hili likitokea. Hatupaswi kuwa na matokeo hata karibu na haya kwa angalau miezi sita.”
Baadaye aliniambia kwamba wagonjwa ambao wana uoni wa sifuri mara chache hupata uoni wa kawaida. Katika wiki kadhaa, nilikuwa nimekwenda kutoka mojawapo ya mgonjwa wake aliye katika hali mbaya zaidi hadi mgonjwa aliyeponya vizuri.
“Fuata Nuru ya Kristo!”
Mwishoni mwa mwaka 2022, viongozi katika kata ya baba yangu walichagua dhima ya kata kwa mwaka 2023. Ilikuwa na msukumo kutoka kwa mafundisho kutoka kwa Rais Russell M. Nelson, ambaye mapema mwaka huo alikuwa amesema, “Tafuta na tarajia miujiza.”
Wakati huo, baba yangu alifikiri dhima hiyo ingewasaidia waumini wa kata ambao walikuwa wakipitia nyakati ngumu. Hakuwa anajua ingekuwa ya kibinafsi sana kwa familia yetu.
“Fuata nuru ya Kristo,” dhima ilisoma. “Tarajia miujiza! Tarajia shangwe!”
Miaka miwili baadaye, uoni wangu ni bora sasa kuliko ilivyokuwa kabla sijaupoteza. Ninamshukuru Baba wa Mbinguni kila siku kwa muujiza wangu na kwa imani isiyoyumba ya familia yangu. Kupitia jaribu hili, kazi ya Mungu ilijidhihirisha yenyewe. Nilikuza ushuhuda imara zaidi, shukrani ya kina kwa ajili ya maisha, na upendo mkubwa Kwake na kwa familia na marafiki.
Leo, ninafanya kila niwezalo, ikijumuisha kama msanii, kuzitumia sana baraka, karama, na shangwe ambayo Mungu amenipa—kumtukuza Yeye na kuwabariki wengine.
Leo, Bronwyn anatumia sanaa yake, kama vile kielelezo hiki cha Mwokozi, kumtukuza Mungu na kuwabariki wengine.