“Habari Njema za Upendo na Shangwe,” Liahona, Januari 2025.
Habari Njema za Upendo na Shangwe
Baraka za Urejesho zinapaswa kuifurahisha mioyo yetu na kutujaza na shukrani kwa ajili ya upendo mkuu wa Mungu.
Ujumbe wetu wa tumaini na amani kwa wote ni kwamba Yesu Kristo yu hai na amerejesha injili Yake na Kanisa Lake katika siku hizi za mwisho.
“Ni kwa jinsi gani mambo haya ni matukufu kwa mwanadamu!” Nabii Joseph Smith alitamka. “Kwa ukweli yanaweza kufikiriwa kuwa ni habari ya shangwe kuu kwa watu wote; na habari, pia, ambayo inapaswa kuijaza dunia na kuifurahisha mioyo ya kila mmoja inaposikika masikioni mwake.”
Kwa karne kadhaa kufuatia huduma ya Mwokozi duniani, watoto wa Mungu walimtafuta Yeye na wakitamani nuru zaidi na ukweli. Sasa habari njema ya injili ya Yesu Kristo na Urejesho unaoendelea vinasonga mbele vikibariki watu wote na kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya siku ambayo Yesu Kristo atarudi ili “atawale kama Mfalme wa Wafalme na kutawala kama Bwana wa Mabwana.” Hili ni onyesho kubwa la upendo usio na mwisho wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu. Ninashangilia kwamba ninaweza kutumia maisha yangu nikitangaza kweli hizi kwa ulimwengu wote.
Visivyoyamkinika na vya Ajabu
Siku mpya ilipambazuka kwa ajili ya familia ya binadamu katika kijisitu cha miti, ambapo Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, walimtokea na kuzungumza na Joseph Smith katika kujibu sala ya kijana Joseph kuhusu kanisa lipi angepaswa kujiunga nalo (ona Joseph Smith—Historia 1:14–20). Yesu Kristo alimwambia Joseph asijiunge na kanisa lolote. Aliahidi kwamba utimilifu wa injili Yake ungefunuliwa kwa Joseph katika siku zijazo.
Kwa wengi, Joseph alionekana kutoyamkinika kabisa kuitwa kwenye kazi muhimu kama hiyo, na walikuwa sahihi. Yeye alikuwa kijana asiye na elimu na asiye maarufu kutoka shamba dogo katika mji usiofahamika. Kama vile baadhi yao walivyosema kuhusu Mwokozi katika siku Yake, “Kunaweza kutokea kitu chochote kizuri kutoka Nazareti?” (Yohana 1:46), wengi walishangaa ni kipi kizuri kingeweza kutoka kwa kijana asiye na elimu mwenye umri wa miaka 14 huko Palmyra, New York. Lakini kupitia Joseph—kama vile alivyoonekana—Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo kwa kweli wangetimiza ya kustaajabisha. Hii inapaswa kutuletea tumaini kwamba kwa njia yetu ndogo na ya unyenyekevu, tunaweza pia kuchangia katika njia za maana kwenye kazi ya Bwana.
Baada ya muda, Bwana alimwita Joseph “na kusema naye kutoka mbinguni, na akampa amri” (Mafundisho na Maagano 1:17). Joseph alipokea ufunuo wa thamani na mafundisho muhimu ambayo yalileta nuru mpya kwenye uelewa wetu juu ya mpango wa upendo wa Baba wa Mbinguni na upendo wenye kukomboa wa Yesu Kristo na nguvu ya dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Cha kushangaza, habari hizi njema zilikuja wakati sahihi ambapo maendeleo muhimu katika usafiri, mawasiliano, na maeneo mengine yangeruhusu nuru ya Mungu kung’ara ili kubariki watoto Wake zaidi na zaidi.
Malaika Moroni Akitoa Mabamba kwa Joseph Smith, na C. C. A. Christensen
Ushuhuda Wenye Nguvu wa Upendo wa Mungu
Kujitokeza kwa malaika Moroni kwa Joseph Smith ilikuwa muhimu kwa Urejesho na ushahidi wenye nguvu wa upendo wa Mungu. Moroni alimwambia Joseph juu ya kumbukumbu, iliyoandikwa kwenye mabamba ya dhahabu, iliyozikwa jirani na hapo (ona Joseph Smith—Historia 1:33–34). Hatimaye, Joseph angepewa “uwezo kutoka juu” (Mafundisho na Maagano 20:8) ili kutafsiri kumbukumbu hiyo katika kile ambacho kingekuwa Kitabu cha Mormoni, ambacho kinasimama sambamba na Biblia na ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo.
Kote katika Kitabu cha Mormoni, tunasoma juu ya watu ambao, mamia ya miaka kabla ya Kristo, walijua na kutabiri juu ya ujio Wake na kutamani ujio huo. Pia tunapata maelezo yasiyo ya kawaida juu ya kutokea binafsi kwa Mwokozi aliyefufuka na huduma miongoni mwa Wanefi, ambapo aliwaalika wote kuja Kwake na kugusa alama ubavuni Mwake na alama za misumari katika mikono na miguu Yake (ona 3 Nefi 11:14–15). Aliwaponya wagonjwa, viwete, vipofu—“wote walioteseka kwa njia yo yote”—na kisha akawabariki watoto wadogo na kusali kwa ajili yao (ona 3 Nefi 17:7–9, 21). Tunajifunza mengi kuhusu upendo na huruma ya Mwokozi kutokana na historia hili takatifu.
Kitabu cha Mormoni kinashuhudia kwamba “Yesu ndiye Kristo.“ Hakikisho katika Kitabu cha Mormoni kwa kurudia rudia hutukumbusha kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu wanatupenda zaidi ya kitu cho chote tunachoweza kufikiria.
Baraka za Ukuhani na Kanisa
Urejesho uliendelea kwa kuonekana kwa wajumbe wengine wa mbinguni kwa Joseph Smith. “Yohana Mbatizaji aliyefufuka alirejesha mamlaka ya kubatiza kwa kuzamishwa majini kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Watatu kati ya Mitume kumi na wawili wa mwanzo—Petro, Yakobo, na Yohana—walirejesha utume na funguo za mamlaka ya ukuhani. Wengine pia walikuja, ikiwa ni pamoja na Eliya, aliyerejesha mamlaka ya kuunganisha familia pamoja milele katika uhusiano usio na mwisho ambao unavuka mipaka ya kifo.”
Mnamo Aprili 6, 1830, Yesu Kristo alianzisha kupitia Nabii Joseph kanisa katika mpangilio wa kanisa aliloanzisha katika nyakati za Agano Jipya (ona Makala ya Imani 1:6), kamili likiwa na “msingi wa mitume na manabii, Yesu Kristo mwenyewe akiwa jiwe kuu la pembeni” (Waefeso 2:20). Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hufanya baraka za nguvu za ukuhani zilizorejeshwa zipatikane kwa watoto wote wa Mungu ambao hujiandaa kuipokea.
Kama Rais Russell M. Nelson alivyotufundisha, tunaweza kupata shangwe katika toba ya kila siku tunapomgeukia Baba wa Mbinguni na Mwokozi wetu. Kwa ye yote anayehisi kulemewa au kwamba anajiona hatoshi au si sehemu ya: wote wanaalikwa kuja kwa Kristo na Kanisa Lake. Kanisa siyo utawa kwa walio wakamilifu bali ni kama hospitali kwa wagonjwa. Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili anatukumbusha kwamba “tunakuja kanisani sio kuficha matatizo yetu bali kuyaponya.”
Kanisani tunapata shangwe katika fursa za kujigeuza wenyewe nje, kuwahudumia wengine kwa upendo, na kushiriki uzoefu wetu binafsi kwa wingi wa wema wa Kristo. Tunaweza “kuhesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo” na “kukumbukwa na kulishwa na neno zuri la Mungu” (Moroni 6:4). Ni baraka kubwa iliyoje!
Sababu ya Shangwe Kuu
Nabii Joseph Smith wakati mmoja alitamka, “Sasa, tunasikia nini katika injili ambayo tumeipokea? Sauti ya furaha! Sauti ya rehema kutoka mbinguni; na sauti ya ukweli kutoka duniani; habari njema kwa wafu; sauti ya furaha kwa walio hai na wafu; habari njema ya shangwe kuu” (Mafundisho na Maagano 128:19).
Habari hizi njema zimekuja kwa sababu Baba wa Mbinguni na Mwanawe mpendwa, Yesu Kristo, wanatupenda na wanatamani—zaidi ya cho chote—kutukaribisha kurudi katika uwepo Wao, ili tuweze kuwa na aina ya maisha ya milele Wanayoishi. Urejesho unaonyesha kwamba Wao wamefanya kila kitu kinachohitajika ili kufanya hili kuwa uwezekano mtukufu kwetu sote. Katika safari yetu ya milele, tutapitia majaribu na magumu, lakini “[sisi] tupo, ili [sisi] tupate shangwe” (2 Nefi 2:25) katika maisha haya na yajayo. Nabii Joseph alijua hili vizuri zaidi ya wengi.
Joseph alikabiliwa na upinzani na mateso ya mara kwa mara, lakini bado alitunza “joto lake la furaha ya asili” (Joseph Smith—Historia 1:28). Alibakia mwenye furaha, imara, na thabiti, na alikamilisha kazi isiyo ya kawaida aliyokuwa amepewa kufanya. Ninatoa shukrani kwa Watakatifu wote wa mwanzo ambao walimwamini, walimuunga mkono, na kumfuata Nabii Joseph Smith na kujiweka wakfu wenyewe kwenye ujenzi wa Kanisa. Tunadaiwa na wao deni kama hilo la shukrani na heshima.
Ilikuwa kazi ngumu katika siku za mwanzo za Kanisa, na inaweza kuwa ngumu leo. Lakini Urejesho unaendelea. Pamoja na Yesu Kristo kwenye kichwa cha Kanisa hili, manabii walio hai wataendelea kutuongoza. Nyumba za Bwana zitaendelea kujengwa, ili baraka za maagano ya milele na Mungu ziweze kutuunganisha Kwake na kwa wapendwa wetu pande zote mbili za pazia (ona Mathayo 16:19). Upendo wa Mungu na Yesu Kristo utaenea ulimwenguni kote tunapofuata amri ya Mwokozi ya kuwalisha kondoo Wake na kushiriki injili Yake. Tutashuhudia kweli za Urejesho zikisonga mbele katika njia na kwenye maeneo ambayo hayangefikirika katika siku za Joseph.
Tunaweza kupata nguvu na shangwe kuu—kama Nabii Joseph alivyofanya—tunapokumbatia na kuishi kweli hizi za thamani. Wito ambao Joseph aliufanya kwa Watakatifu katika siku yake unaendelea nasi leo: “Je, si lazima sisi tuendelee katika kazi hii iliyo kuu? Nenda mbele na siyo nyuma. Ujasiri … na mbele, mbele kwenye ushindi! Acha mioyo yenu ifurahi, na iwe na furaha tele” (Mafundisho na Maagano 128:22).
Na habari njema ya upendo na shangwe kwamba Urejesho ulete baraka na kuongoza maisha yetu—sasa na daima.