2025
Baraka za mwaka 1836 na Magumu ya mwaka 1837
Januari 2025


“Baraka za mwaka 1836 na Magumu ya mwaka 1837,” Liahona, Jan. 2025.

Baraka za mwaka 1836 na Magumu ya mwaka 1837

Kukumbuka hali yetu ya juu ya kiroho kunatukumbusha kwamba hatimaye tutakombolewa kutoka hali zetu za chini.

ndani ya Hekalu la Kirtland

Ndani ya Hekalu la Kirtland

Picha na George Edward Anderson, 1907

Mnamo Machi 2024, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lilikubali usimamizi mtakatifu wa umiliki wa Hekalu la Kirtland kutoka Jumuiya ya Kristo. Hekalu hilo ni mahali maalumu, kwa kiasi kikubwa bila kubadilika tangu kuwekwa wakfu kwake mnamo 1836. Siku ya Jumapili ya Pasaka, Aprili 3, 1836, Yesu Kristo alilikubali kama nyumba Yake (ona Mafundisho na Maagano 110). Katika hekalu hilo, tunaweza kuhisi uwepo Wake na maono katika akili zetu pale Yeye aliposimama.

Hekalu la Kirtland lina masomo kadhaa kwa ajili ya maisha yetu leo, ambayo baadhi yake tunaweza kujifunza kwa kufikiria kuhusu matukio ya mwaka 1836 na 1837.

Mambo Muhimu ya Kiroho ya mwaka 1836

Mnamo Januari 1836, hekalu lilipokaribia kukamilika, Watakatifu walianza kupata baraka za kiroho za hekalu miongoni mwao. Walikuwa wameahidiwa kwamba katika Hekalu la Kirtland watajaliwa nguvu (ona Mafundisho na Maagano 38:32, 38). Ahadi hii ilitoa mwangwi wa kile Mwokozi alichowaambia Mitume Wake huko Yerusalemu katika Agano Jipya. Baada ya Ufufuko Wake, Yeye aliwaambia kwamba wasiache kuhubiri mpaka watakapokuwa wamejaliwa “uwezo kutoka juu” (Luka 24:49). Kisha, katika siku ya Pentekoste, Mitume Wake walipokea nguvu hii wakati Roho alipowashukia kama “upepo mkali ukenda kasi. … Na wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, na kuanza kuzungumza kwa lugha zingine” (Matendo ya Mitume 2:2, 4).

Mnamo Januari 1836, Joseph Smith alikutana na viongozi wengine wa Kanisa kuomba, kubarikiana na kuendesha shughuli za Kanisa. Baada ya kumbariki Nabii Joseph, aliona ono la ufalme wa selestia. Aliwaona Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, Adamu na Ibrahimu, wazazi wake (bado walikuwa wanaishi), na kaka yake mkubwa Alvin, ambaye alikuwa amekufa bila ubatizo. Joseph alijifunza kwamba, “wote waliokufa bila kuifahamu injili hii, ambao wangeliipokea kama wangeruhusiwa kuishi, watakuwa warithi wa ufalme wa selestia wa Mungu” (Mafundisho na Maagano 137:7).

Miezi miwili baadaye, mnamo Machi 27, 1836, Watakatifu walijazana ndani ya Hekalu la Kirtland kwa ajili ya kuwekwa wakfu kwa hekalu. Walisikiliza sala ya kuweka wakfu ya Joseph, ambapo alimwomba Baba wa Mbinguni kukubali Hekalu la Kirtland kama mahali ambapo Mwokozi “angeweza … jidhihirisha kwa watu wake“ (Mafundisho na Maagano 109:5). Wakiwa wamebanana katika sehemu hiyo takatifu, Watakatifu waliimba “Roho wa Mungu.” Walipiga kelele kwa sauti moja, “Hosana! Hosana! Hosana, hosana Mungu na Kristo!”

Walipata baraka za kiroho wakati wa kuwekwa wakfu na wakati wa wiki iliyofuata. Walifunga, wakaomba, wakapokea sakramenti, wakaoshana miguu na kupata maono. Walihisi kuwezeshwa kwenda na kuhubiri injili. Walikuwa wamejaliwa uwezo kutoka juu.

Lakini maonyesho ya kiroho hayakuwa mwishoni. Mnamo Aprili 3, 1836, Mwokozi aliwatokea watumishi Wake wawili. “Pazia liliondolewa kutoka akilini mwetu, na macho yetu ya ufahamu yakafunguliwa. “Tulimwona Bwana amesimama kwenye jukwaa la mimbari, mbele yetu … , akisema: Mimi ni wa kwanza na wa mwisho; Mimi ni yeye aliye hai, Mimi ni yule aliyeuawa; Mimi ni mwombezi wenu kwa Baba” (Mafundisho na Maagano 110:1–4).

Kufuatia matembezi ya Mwokozi, Musa, Elia, na Eliya kila mmoja aliwatokea Joseph na Oliver na kukabidhisha kwao funguo ambazo zingewawezesha kuhubiri injili ya Yesu Kristo na kuikusanya Israeli, kubariki dunia na agano la Ibrahimu, na kuunganisha familia (ona mstari wa 11–16).

Changamoto za mwaka 1837

Lakini hadithi ya Kirtland haimaliziki na maonyesho haya ya ajabu. Mwaka mmoja baada ya kuwekwa wakfu kwa hekalu, jamii ilikuwa inadhoofika. Mgogoro wa kimataifa wa kiuchumi ulisababisha ukosefu mkubwa wa ajira nchini Marekani. Benki zilianguka kote nchini, ikijumuisha benki ndogo iliyoanzishwa na viongozi wa Kanisa huko Kirtland ili kuchochea maendeleo ya jamii. Joseph Smith na viongozi wengine wa Kanisa walijaribu sana kuokoa uchumi wa jamii. Lakini mawimbi ya mgogoro wa kiuchumi duniani yalikuwa makali sana. Watu walianza kupoteza ajira na nyumba. Wengi walianza kunung’unika dhidi ya Mungu na Kanisa. Kwa nini Bwana aliruhusu watu Wake kuanguka kiuchumi? Baadhi walianza kunong’ona na kisha kutangaza kwamba Joseph alikuwa nabii aliyeanguka.

Katika mkutano mmoja katika majira ya joto ya mwaka 1837 katika Hekalu la Kirtland, Joseph Smith Sr., patriaki wa Kanisa, alizungumza wakati mwanawe akiwa hayupo. Alipokuwa akiongea, mpinzani alijaribu kumvuta kutoka kwenye mimbari. Wakati William Smith alipomtetea baba yake, Mtume mwenzake alitishia kumuua William kwa upanga. Wanaume wengine wenye visu na bastola walimzunguka William. Hekalu, ambalo lilikuwa mahali pa utakatifu na mambo ya kiroho mwaka mmoja uliopita, sasa lilikuwa mahali pa vita, mafarakano na vurugu.

Wakati Joseph Smith aliporudi Kirtland, waumini wengi wa Kanisa walimkubali kama nabii, lakini Mitume watatu waliondolewa kwenye Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Matatizo ya kiuchumi yalikuwa yamegeuka kuwa matatizo ya kiroho. Ndani ya miezi michache, Bwana alimwambia Joseph kuondoka Kirtland kwa ajili ya usalama wa familia yake na kwa ajili ya maisha yake mwenyewe.

Maelezo ya mashahidi hushuhudia ugumu wa wakati huo. Vilate Kimball, mke wa Mtume Heber C. Kimball, alituma barua kwa mume wake, ambaye alikuwa akihudumu kama mmoja wa wamisionari wa kwanza huko Uingereza. “Sina shaka lakini itaumiza moyo wako,” aliandika kwa Heber, akimwambia kuhusu wapinzani. “Wanakiri kuamini Kitabu cha Mormoni na Mafundisho na Maagano lakini katika matendo ni tofauti.”

Vilate alijua kwamba Joseph hakuwa mkamilifu. Alikuwa amefanya makosa katika mgogoro wa kiuchumi wa Kirtland. Na aliendelea kuwapenda wengi miongoni mwa wapinzani. Lakini aliona somo la kina zaidi katika matukio ya mwaka 1837: “Bwana anasema, yule ambaye hawezi kuvumilia kurudiwa lakini ananikana hawezi kutakaswa.”

Katika barua hiyo hiyo, Marinda Hyde aliongeza ujumbe kwa mumewe, Orson, pia Mtume aliyekuwa anahudumu Uingereza. Kaka mkubwa wa Marinda alikuwa mmoja wa Mitume ambao walikuwa wameacha Kanisa. “Nyakati kama hizo katika Kirtland kamwe hujawahi kushuhudia kama tulivyo sasa, kwani inaonekana kwamba ujasiri wote katika kila mmoja umetoweka,” aliandika.

Masomo ya 1836–37

Kwa nini kukumbuka janga la mwaka 1837 na sio tu ushindi wa mwaka 1836? Kwa sababu, bila shaka, mawili haya hayawezi kamwe kutenganishwa. Ndivyo hivyo katika maisha yetu wenyewe. Mungu hutupatia sisi sote vipindi vya baraka za kiroho, nyakati ambazo Yeye huzungumza na nafsi zetu na kutuongoza kwa mkono kwenye njia ya agano. Yeye anatupatia vipindi vya uthabiti, nyakati ambazo tunavyo vya kutosha na kusaza, nyakati ambazo familia zetu zina afya na furaha, nyakati ambazo marafiki zetu wako karibu nasi na wanashirikiana nasi. Sote tunaishi nyakati ambazo ni kama mwaka 1836.

Lakini Mungu kamwe hakuahidi kwamba tungepata tu uzoefu wa mwaka 1836. Kwa kila mmoja wetu, 1837 huja. Huja na kuyumba yumba kiuchumi, tunapokuwa na wasiwasi juu ya wapi fedha itatoka. Huja na kuyumba yumba kibinafsi, wakati familia zetu zinapopatwa na magonjwa ya ghafla, magonjwa sugu, msongo wa mawazo au wasiwasi. Huja na kuyumba yumba kijamii, wakati marafiki zetu wanapotuondokea au kutusaliti.

Kama hatukumbuki uzoefu wetu wenyewe wa mwaka 1836—nyakati zetu wenyewe ambapo tumehisi mikono ya Bwana katika maisha yetu—1837 inaweza kuleta kuyumba yumba kiroho. Inaweza kutujaribu tuseme, “Hii haistahili.” Inaweza kutujaribu tuseme, “Mungu hanipendi.” Inaweza kutujaribu tuseme, “Joseph Smith hakuwa nabii” au “Rais Nelson si nabii wa Mungu.” Inaweza kutujaribu sisi kusema, “Njia ya agano siyo kwa ajili yangu.”

Lakini tukifanya kazi ya kiroho ya kukumbuka na kuishi kiroho mnamo 1836 hata tunapopitia majaribu ya mwaka 1837, bado tunaweza kujengwa katika imani yetu katika Yesu Kristo, bado tunaweza kujua kwamba Mungu anatupenda, na bado tunaweza kujua kwamba Urejesho wa injili na Kanisa la Yesu Kristo ni halisi na kwamba Bwana huongoza Kanisa Lake kupitia watumishi Wake wateule.

Muhtasari

  1. Nukuu za kihistoria kutoka kwenye Watakatifu: Hadithi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, juzuu. 1, The Standard of Truth, 1815–1846 (2018), 297, 298.