“Shukrani Kukusanyika,” Liahona, Januari 2025.
Shukrani Kukusanyika
Na tuwe wenye shukrani daima kwa ajili ya heshima na tumaini ambalo Bwana ametupatia tunapokusanyika kwa Mwokozi, tupokusanyika pamoja na Watakatifu, na kukusanyika katika huduma Yake.
Kwa Unyenyekevu, Mwokozi Wetu,, na Jay Bryant Ward, isinakiliwe
Kwa miaka mingi, nilimiliki saa nzuri ya mfukoni ambayo wakati mmoja ilikuwa ya babu yangu Andrew C. Nelson, ambaye sikuwahi kukutana naye. Alikufa wakati baba yangu alipokuwa na umri wa miaka 16 tu.
Baba yangu alirithi saa ya Babu Nelson. Nilipozidi kuzeeka, alinipa saa hiyo. Niliitunza saa hiyo kama muunganiko wa kushikika kwa mmoja wa mababu zangu waaminifu.
Wazazi wa Babu Nelson, kama mababu zangu wote, walijiunga na Kanisa katika Ulaya yao ya asili. Nitakuwa mwenye shukrani milele kwa watangulizi hawa waanzilishi. Kwa sababu ya imani yao na dhabihu ya kukusanyika pamoja na Watakatifu, uzao wangu na mimi tumefurahia baraka za injili ya urejesho ya Yesu Kristo.
Saa ya Babu Nelson ilinikumbusha wajibu wetu wa dhati kama Watakatifu wa Siku za Mwisho kuwakusanya watoto wa Baba yetu pande zote mbili za pazia. Saa yake pia ilinikumbusha kwamba mababu zetu wanatuangalia na kutusubiri tuwatambue na kuona kwamba ibada zao za hekaluni zinafanywa ili kwamba wapate fursa ya kukusanywa milele katika zizi la Baba.
Kukusanyika kwa Mwokozi
Pamoja na Ndugu zangu katika Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, tunatangaza: “Kanisa hili limetia nanga katika maisha makamilifu ya jiwe lake kuu la pembeni, Yesu Kristo, na katika Upatanisho Wake usio na mwisho na Ufufuko Wake halisi. … Yeye anatualika sote kuja Kwake na kwenye Kanisa Lake, ili kupokea Roho Mtakatifu, ibada za wokovu, na kupata shangwe ya kudumu.”
Kwa sababu Urejesho unasonga mbele kupitia ufunuo endelevu, “dunia kamwe haitakuwa sawa tena, kwani Mungu ‘atayakusanya pamoja mambo yote katika Kristo’ (Waefeso 1:10).”
“Vitu vyote” hujumuisha kondoo Wake. Mwokozi anatuita kuacha nyuma uovu wa ulimwengu na kukusanyika Kwake. Yeye anataka kondoo Wake wawe nuru inayong’aa kwa uangavu, wakiweka kiwango kwa ulimwengu wote kwa kutafakari jinsi wanafunzi wa kweli wanavyoishi, ikijumuisha jinsi wanavyopata furaha ya kweli wanapofokasi maisha yao kwa Mwokozi.
Tunakusanyika kwa Mwokozi tunapokuja Kwake (ona Mathayo 11:28) kwa kuwa na imani iletayo toba, kukubali ubatizo katika Kanisa Lake, na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Tunakusanyika kwa Mwokozi tunapopata uzoefu wa uponyaji wa kiroho ambao huja kutokana na kupokea sakramenti, tukishuhudia kwamba tuko tayari kujichukulia juu yetu jina Lake, daima kumkumbuka Yeye, na kutii amri Zake (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79).
Tunakusanyika kwa Mwokozi kila siku tunapojaza maisha yetu kwa maneno Yake na ukweli Wake, ikijumuisha mafundisho ya manabii Wake, waonaji, na wafunuzi.
Tunakusanyika kwa Mwokozi tunapoboresha uwezo wetu wa kumsikiliza Yeye, tukiishi kwa kustahili minong’ono ya Roho Mtakatifu.
Tunakusanyika kwa Mwokozi tunapoimarisha uongofu wetu, kuongeza imani yetu, kuongeza uanafunzi wetu kwa kina, kuiga mfano Wake, na kujitahidi kuwa bora kidogo kila siku.
Tunakusanyika kwa Mwokozi tunapofanya maagano matakatifu na kupokea ibada takatifu hekaluni.
Tunakusanyika kwa Mwokozi tunapojiweka chini kwa uvumilivu na ujasiri “kwa vitu vyote ambavyo Bwana anaviona vinafaa kuvileta juu [yetu]” (Mosia 3:19).
Hatimaye, tunakusanyika kwa Mwokozi tunapofundisha na kushuhudia juu Yake, tukialika familia zetu, marafiki na majirani kukusanyika pamoja nasi kwenye “nuru, uzima na tumaini la ulimwengu.”
Kukusanyika pamoja na Watakatifu
Tunapokuja pamoja na kuungana kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunaingia katika ushirika na wenza mmoja kwa mwingine. Tunaidhinishana, kufundishana na kuadilishana. Tunajitahidi, katika maneno ya Mwokozi, “kuwa wamoja” (Yohana 17:21; ona pia Mafundisho na Maagano 38:27) na “kupendana” (Yohana 13:34).
Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, amefundisha, “Uhudhuriaji Kanisani hutupatia nguvu na ongezeko la imani ambalo huja kutokana na kujumuika na waaminio wengine na kuabudu pamoja na wale ambao wanajitahidi pia kubaki kwenye njia ya agano na kuwa wanafunzi wazuri wa Kristo.”
Kanisani tunapata pumziko la kiroho na kufanywa upya. Tunapata ibada na mamlaka ya ukuhani ya kuzisimamia. Tunapata ukweli uliorejeshwa, mafundisho halisi na ufunuo binafsi. Tunapata mikono ya kukaribisha, mioyo yenye faraja na sauti za kutia moyo. Tunapata fursa za kuishi amri kuu mbili (ona Marko 12:30–31).
Bwana ametuonya kwamba “adui ameungana” (Mafundisho na Maagano 38:12). Ili kulinda familia zetu na kukinza ushawishi unaokua wa Shetani, kuabudu kwetu pamoja kama Watakatifu huwa muhimu zaidi.
Kukusanyika katika Huduma Yake
Nabii Joseph pia alisema, “Siku yaja kwa haraka wakati urejesho wa vitu vyote utatimizwa, ambao manabii wote watakatifu wametoa unabii juu yake, hata kwenye kukusanyika katika nyumba ya Israeli.” Mmoja wa wale waliotoa unabii huo alikuwa Yeremia katika Agano la Kale:
“Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, ambapo hawatasema tena, Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya Misri;
“Lakini, Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya kaskazini, na toka nchi zote alikowafukuza” (Yeremia 16:14–15).
Nabii Joseph alitangaza zaidi, “Sisi ni watu waliopendelewa ambao Mungu ametuchagua wa kuleta utukufu wa siku za mwisho … wakati Watakatifu wa Mungu watakapokusanywa pamoja kutoka kila taifa, na kabila, na watu, na lugha.”
Ili kutimiza kazi hiyo, “Nitatuma watu kuwaita wavuvi wengi, nao watawavua; na baada ya hayo nitatuma watu kuwaita wawindaji wengi, nao watawawinda, watoke katika kila mlima, na kila kilima, na pango za majabali” (Yeremia 16:16).
Akina kaka na akina dada, kama Israeli ya agano la siku za mwisho—waumini wa Kanisa la urejesho la Yesu Kristo—sisi ni wavuvi na wawindaji wa Bwana. Tumeitwa kuwakusanya wateule wa Bwana kutoka kila mlima, kilima na kitongoji. Tumeitwa kuwapa watoto wa Mungu fursa ya kuwa warithi kamili kwa yote Yeye aliowaahidi watoto Wake waaminifu. Hiyo ndiyo huduma kubwa zaidi ambayo tungeweza kutoa.
Tunatimiza maelekezo hayo matakatifu kwa kukusanya Israeli pande zote mbili za pazia—kushiriki habari njema za Urejesho pamoja na wengine, kuwatafuta mababu zetu waliofariki na kufanya ibada kwa niaba yao hekaluni. Pia tunatimiza maelekezo haya tunaposhiriki upendo wa Mwokozi kupitia huduma yetu, mfano, ushuhuda, na mwaliko kwa wengine kujiunga nasi.
“Bwana anaongoza Urejesho wa injili Yake na Kanisa Lake,” alisema Rais Henry B. Eyring, Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza. “Yeye anakwenda mbele yetu. Yeye anaujua wakati ujayo kikamilifu. Yeye anakualika wewe kwenye kazi. Yeye anakujumuisha wewe katika hilo.
Fursa na Tumaini
Ni nini kilitokea kwenye saa ya mfukoni ya Babu Nelson? Miaka michache iliyopita, nilimkabidhi mwanangu. Kama ilivyofanya kwangu, hiyo saa sasa inamuunganisha na wazao wake na kumkumbusha juu ya wajibu wake kwa uzao wake.
Na hivyo ndivyo inavyoenda. Kila kizazi cha agano hubeba kazi ya Bwana, kikifanya sehemu yake katika kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.
Na tuwe wenye shukrani daima kwa ajili ya heshima na tumaini ambalo Bwana ametupatia tunapokusanyika kwa Mwokozi, tupokusanyika pamoja na Watakatifu, na kukusanyika katika huduma Yake.