Kurasa za Karibu
Ndoa ni muhimu kwenye mpango wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa ubinadamu
Mnamo Jumamosi, Agosti 24, 2024, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kwa ushirikiano na Baraza la Taifa la Dini kwa ajili ya Amani (CNRP) na Wizara ya Jinsia, Familia, na Watoto waliwasindikiza wenza kadhaa wakati wa sherehe za ndoa yao ya kiserikali, ambazo zilifanyika huko Palais du Peuple Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ukumbi wa matukio wa Palais du Peuple uliandaliwa kuhimili wenza 100, na 98 ndoa zao zilisherehekewa katika uwepo wa mamlaka za kiserikali, kisiasa, na kidini. Tukio lilikusudiwa kukabili ugumu wa kifedha unaohusiana na hali za ufikiaji wa ndoa ambazo wenza wanakabiliana nazo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ni mila kwa wenza kutoa kwanza mahari kwa familia ya bi harusi na kisha ada ya maombi ya ndoa kama sehemu ya utaratibu wa kisheria wa ndoa. Mahari ni kigezo cha uandikishaji wa ndoa katika usajili wa kiserikali, ambao huifanya iwe ndoa pekee inayotambulika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hata hivyo, kwa miaka mingi, ada hizi zimekuwa na ongezeko la juu, zikisababisha vikwazo kwa wenza vijana wanaotamani kufunga ndoa. Wakitambua tatizo hili, Wizara ya Jinsia, Familia, na Watoto wameanza kufanyia kazi uondoaji wa ada za maombi na kuweka kiwango cha mahari. Hatua hii ni sehemu ya juhudi pana ya kufanya ndoa ya kisheria ifikike kwa urahisi na wenza wote kuweza kuimudu.
Sherehe iliwajumuisha wazungumzaji kadhaa, kila mmoja akitoa mtazamo wa kipekee kwenye tukio.
Sheikh Abdallah Mangala Lwaba, mwakilishi wa kisheria wa jumuiya ya Kiislamu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alizungumza kwa niaba ya CNRP, akiwasilisha mtazamo wa Kiislamu juu ya ndoa. Alisisitiza tamaduni zilizo sawa kwa madhehebu tofauti tofauti ya kidini na umuhimu wa kiishara wa mahari katika Uislamu. Pia aliangazia jukumu la taasisi za kidini katika kuunga mkono na kuimarisha ndoa na familia.
Mzee Thierry K. Mutombo, Rais wa Eneo la Kati la Afrika la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, aliwahutubia hadhira, akisisitiza umuhimu wa ndoa kati ya mwanamume na mwanamke na umuhimu wa familia ndani ya jumuiya, hususani umuhimu wake katika mpango wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa ubinadamu: “Kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya tamaduni ambazo zinaendelea kuwa kikwazo zikizuia wahusika wakuu kutofikia lengo hili. baadhi ya tamaduni hizi hujumuisha:
-
Kiwango kikubwa sana cha mahari kinachowekwa na upande wa mwanamke kwa mume mtarajiwa.
-
Orodha ndefu sana ya bidhaa zinazoombwa na familia ya mke.
-
Mfumo huu wa mahari unaoleta umasikini kwa vijana, unawatajirisha kizazi cha wazee, na unaleta ukosefu wa usawa.
-
Gharama za uendeshaji na zawadi zingine zinazoombwa na huduma mbalimbali za nchi kabla ya sherehe na usajili wa ndoa.
-
Na hitaji la kuwa na wafungisha ndoa kwenye maeneo na sekta za vijijini.”
Pia alisema, “Ni yenye umuhimu wa juu sana kwamba sisi (Makanisa, Serikali, na Bunge) tuweke mazingira bora zaidi kwa ajili ya ufikiaji wa ndoa. Hili linapaswa kuzingatia ushindwaji, kutokutimizwa kwa malengo na ahadi zilizofanywa na wenza watarajiwa, pamoja na uahirishaji wowote unaofanyika wakati wa sherehe za ndoa ndani ya familia na mbele ya mamlaka ya serikali ya usajili.”
Bwana Roger Sesani, mtaalamu anayeshughulikia miradi ya ndoa, alitoa muhtasari wa juhudi zilizofanywa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, CNRP, na serikali ili kupata marekebisho ya sheria za ndoa na kupunguza vikwazo vya kifedha kwa wenza. Alisema, “Ndoa ni msingi wa maisha ya familia. Ndoa ndicho kinachotengeneza familia. Hata hivyo, nchi inatambua ndoa zinazosherehekewa hadharani na zilizo rasmi, au zilizoandikishwa kwenye ofisi ya usajili, kufuatia sherehe za kimila za familia.” Alitoa pia pendekezo kwamba “juhudi za nchi za kukuza umoja na uimara wa familia zinapaswa kujumuisha uundaji wa chombo cha kisheria na kuanzisha ofisi za usajili wa kiserikali ili kuweka pamoja mfumo wa usajili wa ndoa.”
Mheshimiwa Leonnie Kandolo, Waziri wa Jinsia, Familia, na Watoto, alifafanua ono la wizara na msimamo wa kuunga mkono na kuongeza idadi ya ndoa, familia, na watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alitambua kwamba tofauti za viwango vya mahari zinawekwa kulingana na makundi na mila za kikabila. “Kipaumbele changu kitakuwa kuendelea kufanya kazi kushughulikia changamoto za mahari wakati tukiheshimu mila za makundi tofauti tofauti ya kikabila yaliyopo nchini. Kama nyongeza, ninakusudia kuondoa taratibu taratibu baadhi ya ada za utawala zinazohusiana na ndoa za kiserikali. Wizara ya Jinsia, Familia, na Watoto ina misheni mtambuka na inajihusisha katika sekta zote za nchi. Nina msimamo wa kufanya kazi kwa juhudi ili kuendeleza sheria zote zinazohusiana na ndoa, familia, na watoto nchini Kongo.”
Baada ya hotuba, meya wa jumuiya ya Matete aliendelea wikiendi hii kwenye sherehe rasmi za wenza 98. Tukio lilipambwa na onyesho la muziki kutoka kwaya ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, likitengeneza mazingira ya shangwe na ya kuinua kwa ajili ya siku hii ya kukumbukwa. Sherehe hii ya ndoa inadhihirisha maendeleo muhimu katika kukuza ndoa zinazofikika na zenye gharama za kawaida katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tukio si tu lilisherehekea muunganiko wa wenza bali pia lilidhihirisha ari ya kukuza ndoa imara, zenye ufanisi, na zinazotambulika kisheria kote nchini.