2025
Mambo Rahisi na ya Kuvutia ambayo Yanaimarisha Imani na Kujenga Ushuhuda
Januari 2025


Kurasa za Karibu

Mambo Rahisi na ya Kuvutia ambayo Yanaimarisha Imani na Kujenga Ushuhuda

Ni kwa kutumikia bila ubinafsi katika miito yetu ambayo Mungu hutupatia kupitia viongozi wa Kanisa Lake kwamba tunajifunza kuwa na msimamo kwenye injili ya Yesu Kristo.

Mimi ni mtoto wa nane kati ya kumi na wanne katika familia kubwa ambayo inajumuisha wasichana saba na wavulana saba. Nimeolewa na Kaka Patrice M.W. Mukendi.

Mnamo 2001, niliongoka kwenye injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo na kujiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, nikiliacha kanisa la Methodist.

Maandiko yanatufunza kwamba kupitia vitu vidogo na rahisi Bwana anakamilisha kazi Yake (Alma 37:6). Vitu kadha wa kadha vidogo na vya kuvutia vimesaidia kuimarisha imani yangu katika Yesu Kristo na kujenga ushuhuda wangu wa injili iliyorejeshwa. Orodha ya vitu inaweza kuwa ndefu, lakini nimechagua kushiriki vichache ambavyo vimekuwa muhimu zaidi kwangu mimi, kaka zangu na dada zangu katika Sayuni.

1. Mpangilio na Utaratibu

Tangu siku zangu za mwanzo katika kanisa, mpangilio na utaratibu wa Kanisa ambao kupitia huo kila jukumu au wajibu hukamilishwa vilivuta umakini wangu. Kuona darasa la wasichana likiwa na walimu na washauri pamoja na masomo yaliyopangiliwa kwangu ilikuwa ya kustaajabisha. Daima nitamkumbuka rais wangu wa wasichana, wa kwanza kunipa unasihi, Dada SUNGUZA KYU, mwalimu mwenye kujali aliyeongeza tamanio langu la kushiriki katika mikutano yote ya Kanisa na shughuli zenye mada ambazo zilikuwa mahususi kwa wasichana wa umri wangu.

2. Miito na Umoja katika Kanisa

Katika kanisa la kweli lililorejeshwa la Yesu Kristo, akina kaka na akina dada wanaitwa kwa uvuvio wa Mungu kupitia viongozi waliowekwa bila kujali kiwango cha elimu au nafasi ya kijamii, bali kwa tamanio la kuhudumu na kuwasaidia wengine wapige hatua, kwa sababu sote tuko sawa kwa Bwana (Alma 1:26).

Upendo kati ya akina kaka na akina dada hujenga mazingira ya kusaidiana na huimarisha tamanio letu la kukuza miito tunayopokea pasipo ubinafsi.

Miito ambayo nimeikubali na kuikuza pasipo ubinafsi, kwa upendo, hakika imeimarisha imani yangu katika Yesu Kristo na kujenga ushuhuda wangu wa Mungu Baba na Mwanaye Yesu Kristo na wenza wa Roho Mtakatifu. Kila mara tunapotafuta wenza wa Roho Mtakatifu katika kutimiza miito yetu, Roho Mtakatifu hutuongoza, huambatana nasi na huijaza mioyo yetu kwa shangwe (M&M 11:13). Upendo nilionao kwa Mungu wangu na kwa jirani yangu umenisaidia nikuze miito hii na kama matokeo imeimarisha imani yangu katika Yesu Kristo na ushuhuda wangu.

3. Hekalu na Maagano Yake

Imani yetu katika Bwana Yesu Kristo na ushuhuda wetu vinaweza kuongezeka na kuimarishwa kadiri tunavyojiandaa na kustahili, kuwa wenye kustahili kupata kibali cha hekaluni, na kuingia ndani ya nyumba takatifu ya Bwana ili kufanya ibada na maagano pamoja Naye.

Kama msichana, nilijifunza kwamba kwa nguvu ya ukuhani wa Mungu tunaweza kuunganishwa kwa waume zetu, watoto na wanafamilia kwa milele yote. Tunapaswa kuweka lengo binafsi ili kupokea ibada zetu za hekaluni kwa gharama yoyote ile.

Nimepitia uzoefu wa furaha ya kweli ya kuhudhuria mara kwa mara Hekaluni ambapo ni nyumba ya Bwana. Baada ya uhudhuriaji wa mara kadhaa hekaluni, mimi na mume wangu tumeamuna kujitahidi kuifanya nyumba yetu kuwa hekalu, sehemu ya mbingu duniani, nyumba ambapo Roho Mtakatifu anaweza kukaa, nyumba ya utaratibu, nyumba ya sala, na nyumba ya Mungu.

Ninajua kwamba ni kupitia mambo rahisi na ya kuvutia kama vile mpangilio na utaratibu wa Kanisa, miito yenye uvuvio ambayo tunaikubali na kuikuza pasipo ubinafsi, kuingia kwenye maagano na kushika maagano yaliyofanywa ndani ya hekalu, Nyumba ya Bwana, kwamba tunaweza kuimarisha imani yetu katika Yesu Kristo na kujenga ushuhuda wetu wa Mungu Baba, Mwanaye Yesu Kristo na Roho Mtakatifu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.