2025
Katika Mikono ya Yesu
Januari 2025


Kurasa za Karibu

Katika Mikono ya Yesu

Kwa asili ya uaminifu wa mtoto, Kennedy mwenye miaka minne kutoka Lusaka, Zambia alikimbilia kwenye mikono wazi ya Yesu! Tukio hilo baadaye liliwekwa kwenye picha na mchoraji Mtakatifu wa Siku za Mwisho Lemon Swindle katika mchoro wa kuvutia sana wenye kichwa cha habari Thamani ya Nafsi. Tangu 2008 mchoro huu umechukua nafasi katika mioyo yetu. Tunamwona Mwokozi akimleta mtoto huyu mdogo mwaminifu kwake. Tunapotazama macho ya mtoto huyu mdogo inaweza ikawa tunajiona sisi wenyewe. Kama tukimruhusu Roho ndani yetu, yeye atashuhudia kwamba ni kila mmoja wetu ambaye amewekwa katika mikono Yake.

Kennedy alikuwa yatima wakati wazazi wake wote walipofariki kwa mpishano wa miezi kadhaa kutokana na ugonjwa usiojulikana. Wazazi hao waliacha watoto wazuri wanane, mdogo akiwa na wiki tatu tu. Maisha ya Kennedy na maisha ya kaka na dada zake yalibadilika kabisa. Hisia za kuwakosa na upotevu vilimnyima tumaini. Hisia hiyo ingemfuata kwa miaka mingi. Roho yake ilitamani kukubalika, upendo na kuwa sehemu ya jamii.

Miaka miwili baada ya vifo vya wazazi, katika siku ya jua kali huko Lusaka Magharibi, Zambia kwenye Kituo cha Watoto cha Akina Mama Wasio na Mipaka, ambako Kennedy na baadhi ya ndugu zake walikuwa wanalelewa, mwanaume aliyepangwa kumwakilisha Yesu alifika pamoja na mchoraji na mpiga picha ambapo mazingira yalitengenezwa kwa lengo la kupiga picha ya watoto wa Kiafrika pamoja na Mwokozi ili kwamba mchoro kama huo uweze kutengenezwa.

Kennedy sasa alikuwa na miaka minne. Kwa wema wa mtoto, na akiamini kabisa mtu huyu kuwa Mwokozi, aliponyoka kutoka mikono ya dada yake Bridget na kumkimbilia mtu huyo. Aliruka kwenye mikono yake iliyonyooka. Kwa siku nzima, Kennedy alijitahidi kutokumwacha mtu huyu. Je, Roho alikuwa akimnong’oneza kwamba kuna kitu hapa anaweza akawa anakijua?

Kama yatima mdogo, Kennedy aliwategemea wengine ili kuishi. Kabla ya kuletwa kwenye Kituo cha Watoto, yeye pamoja ya nduguze walikuwa wametawanywa miongoni mwa ndugu. Kama uzoefu ulivyo katika maisha, kuna kipindi yalikuwa mazuri, wakati mwingine mabaya. Katika yote, na licha ya kuishi mbali mbali, ndugu hawa walibakia wameunganika pamoja. Kaka yake mkubwa Bwalya daima alikuwepo kwenye maisha yake na alijichukulia jukumu la baba na mlinzi ingawa alikuwa miaka miwili zaidi ya Kennedy.

Kennedy alitambulishwa katika Kanisa la Yesu kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho alipokuwa na miaka tisa na alibatizwa alipokuwa na miaka kumi na moja. Ndugu zake watano pia walibatizwa.

Kama kijana mdogo, maisha yalikuwa magumu kwa Kennedy wakati fedha ilipokosekana kwa ajili ya makazi, chakula na elimu iliyokuwa inatakiwa. Ilikuwa katika muda huu kwamba BJ Wrnick, Sandra Peters na Anthony Mulenga -ambao walimjua Kennedy tangu akiwa na miaka minne- waliweza kumchukua kwa ajili ya kumlea. Kupitia taasisi yao ya Heart To Hands Foundation, yeye pamoja na Bwalya waliasiliwa kwenye malezi yao. Wakati ilikuwa dhahiri kwamba Kennedy alihitaji mambo ya msingi kwa ajili ya maisha ya kila siku, kile alichokuwa anahitaji hasa ilikuwa ni tumaini na upendo na waliowaasili walikuwa navyo hivi vingi vya kuwapa. Kennedy alisema ilikuwa ‘bora zaidi’.Sasa alikuwa na Mama wawili. Kwa msaada wa familia yake mpya, aliweza kumaliza shule ya upili, alipata leseni ya udereva na kumaliza shule ya ufundi wa magari. Pia, alikuwa amefunikwa kwenye mikono ya Mwokozi wake, lakini ilikuwa kupitia matendo ya wengine. Kennedy alisimulia “Sijui ningekuwa nani bila upendo endelevu wa familia yangu kubwa na marafiki ambao wamejitolea muda mwingi kwangu.”

Ilikuwa ni mwaka uliopita kwamba Kennedy alifanya maamuzi ya kuhudumu misioni na kuwa ile mikono ya Mwokozi kwa wengine. ‘Familia yake bora iliyomuasili’, kaka yake Bwalya na Askofu wake imara Simbeya katika Kata ya Libala walimsaidia kujiandaa. Alipokuwa MTC ya Ghana kabla ya kwenda Misioni ya Kenya Nairobi, miujiza ilitokea na aliweza kuhudhuria hekalu na kushiriki siyo tu katika kazi ya ibada ya baba yake, lakini pia kwenye uunganishwaji wa wazazi wake na mwisho uunganishwaji wake kwa wazazi wake kwa muda na milele yote.

Sasa, kama Mzee Chitalu, katika ofisi za misioni alikutana na Dada Stacie Stuart, kiongozi wa misioni kwa ajili ya Misioni ya Kenya Nairobi. Dada huyu ndiye aliyepiga picha hii ya Mzee Kennedy Chitalu akiwa amesimama mbele ya picha ya utoto wake, akiwa amefunikwa katika mikono ya mwokozi. Sasa mtoto huyu anavalia beji ya jina kama mwakilishi wa Yesu Kristo. Ni zamu yake kuwafunika wengine na kuwasaidia waje kwa Kristo. Anashuhudia: “Ninajua na kusimama kama shahidi wa dhati kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu na ninajua kwamba Upatanisho Wake una nguvu ya uponyaji kwa kila aina ya mateso”.