Ujumbe wa Urais wa Eneo
Kujifunza na Kuitumia Injili Nyumbani
Kila muumini wa Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo anaweka ahadi iliyoonyeshwa mwanzoni kwenye ubatizo wetu na hatimaye kwa kushiriki sakramenti ili kuwa wafuasi halisi wa Yesu Kristo. Kama majibu ya ahadi yetu, Bwana anafanya iwezekane kwetu kuwa na roho Wake daima na kutuongoza kwenye njia ya agano.
Ahadi moja ya ufuasi ni kuendelea kujifunza zaidi kuhusu Yesu Kristo na injili yake na kutumia kile tunachojifunza kwenye maisha yetu ya kila siku. Katika Mathayo, Yesu aliwaalika wanafunzi wake “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.…” (Mathayo 11:29). Bwana amewaelekeza waumini wa Kanisa Lake jipya lililorejeshwa “kujifunza kutoka kwangu, na kuwa mpole na mnyenyekevu wa moyo…” (M&M 32:1) na “tafuteni maarifa, hata kwa kujifunza na pia kwa Imani…” (M&M 88:118). Katika aya hizi Bwana anatualika kuendelea kusoma na kujifunza kama sehemu muhimu ya ufuasi wetu.
Katika dini nyingi, maelekezo ya kidini na kuabudu hutokea tu katika majengo ya kanisa au misikitini. Katika Kitabu cha Mormoni, Alma na Amuleki waliwapata watu ambao waliamini kwamba wangeweza kuabudu tu katika sinagogi. Amuleki aliwafundisha kwamba wangeweza na wanapaswa pia kuabudu (kusali, kujifunza na kuimba) katika majumba yao na sehemu zingine. Rais Russell M. Nelson alitufundisha katika Mkutano Mkuu mnamo Oktoba 2018, “Kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tumezoea kufikiria ‘kanisa’ kama kitu kinachotokea katika sehemu zetu za mikutano, kikiongezewa na kile kinachotokea nyumbani. Tunahitaji mabadiliko ya mfumo huu. Ni muda wa Kanisa linalolenga nyumbani, likisaidiwa na kile kinachoendelea ndani ya majengo yetu ya tawi, kata na kigingi.” Alielezea zaidi kwamba hii “ingewaimarisha waumini wetu na familia zao.”
Katika Mkutano Mkuu huo huo, Kanisa lilitangaza kupunguzwa kwa mikutano ya Jumapili kutoka masaa matatu hadi mawili na kutambulisha Njoo Unifuate, mtaala kwa ajili ya mafunzo ya injili ya familia na mtu binafsi. Lengo la mabadiliko haya lilielezewa na Mzee Quentin L. Cook: “Lengo letu ni kuweka usawa wa uzoefu wa Kanisani na nyumbani katika njia ambayo itaongeza imani kwa wingi na roho na kukuza uongofu kwa Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo.”
Kama watu binafsi na wazazi, tuna jukumu la kujifunza injili nyumbani na kutumia kile tunachojifunza katika maisha yetu ya kifamilia na jamii. Masomo na kujifunza kwetu vinalenga nyumbani. Kanisa husaidia kwa kutoa nyenzo za kusaidia kujifunza kwetu ikijumuisha:
-
Maandiko
-
Mafundisho ya Mkutano Mkuu
-
Mwongozo wa Kujifunza wa Njoo Unifuate wa Nyumbani na Kanisani
-
Nyimbo za Dini
-
Video
-
Majarida ya Kanisa ikijumuisha Liahona, Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana na Rafiki
Nyenzo hizi zote zinaweza kupatikana katika aplikesheni yaMaktaba ya Injili.
Familia na watu binafsi wanapangilia mafunzo yao ya injili kulingana na mahitaji yao na ratiba. Njia za kujifunza hutofautiana kulingana na familia. Vipengele vya muhimu vya kujumuisha ni:
-
Soma aya kutoka kwenye maandiko;
-
Shiriki na jadili kile unachojifunza na kuhisi kulingana na usomaji wako;
-
Zungumza jinsi mnavyoweza Kutumia kile mlichojifunza kwenye maisha yenu siku hiyo.
Majadiliano ya mara kwa mara ya injili huipatia familia yetu msingi wa kanuni za kweli za kuongoza maamuzi na shughuli zetu za kila siku. Huwasaidia watoto wetu kujifunza na kutumia kweli za injili katika maisha yao.
Wakati mimi na Dada Pieper tulipokuwa tunalea familia yetu tulitaka kuwafundisha lishe bora. Tulipanga vyakula vya lishe kamili na kuwahimiza watoto wetu kujaribu kula kila chakula kilichotengwa. Kama matokeo, tulitengeneza sheria kwamba ni wale tu watakaoonja japo kidogo ya kila chakula kilicho mezani ndio watakaopata pipi siku hiyo.
Jioni moja wakati wa chakula cha jioni, mwana wetu, Chris, alisema kwamba hatopenda kula njegere zake. Tulimhimiza ajaribu japo kijiko kimoja na kumkumbusha kuhusu kanuni kwamba kama angekula angeweza kupata aiskrimu baada ya mlo. Chris alisema kwamba anataka aiskrimu. Tulimkumbusha kwamba kama anataka aiskrimu kwanza angetakiwa aonje njegere zake. Aliendelea kusisitiza kwamba anataka aiskrimu lakini alikataa kula njegere zake. Kama matokeo, alitazama wakati kaka na dada zake wakila aiskrimu baada ya mlo, akilalamika kwamba kanuni haikuwa na usawa.
Siku iliyofuata katika mafunzo ya maandiko ya familia tulikuwa tunasoma mafundisho ya Alma kwa mwana wake, Koriantoni, kuhusu sheria na adhabu. Tulisoma kwamba daima kuna matokeo pale sheria zinapovunjwa. Ghafla, Chris aliropoka, “hilo la njegere na aiskrimu”. Tulikuwa na mjadala mzuri wa jinsi tulivyo na haki ya kujiamulia ya kuchagua kile tutakachofanya lakini hatuwezi kuchagua matokeo ya matendo yetu. Hii ilitusaidia sote kujifunza kanuni za muhimu na kuzitumia katika maisha yetu.
Uzoefu huu wa kujifunza unaolenga nyumbani unasaidiwa na masomo ya Njoo Unifuate Kanisani siku ya Jumapili katika Darasa la Watoto na Shule ya Jumapili. Kanisani, walimu wanapaswa kutoa fursa kwa ajili ya watoto, vijana na watu wazima kushiriki kile ambacho wamejifunza wakati wa masomo yao ya injili nyumbani na wanadarasa wengine. Hii huwaruhusu waumini kushiriki vitu wanavyojifunza na huleta nguvu na kutia moyo kwa waumini wote. Lengo la madarasa yetu sio kumaliza somo, bali kushiriki na kujifunza pamoja.
Mtazamo huu wa kusoma na kujifunza injili unaolenga nyumbani, ukisaidiwa na Kanisa ndio mfumo wa kuabudu ambao Bwana ameuanzisha katika siku hizi za mwisho ili kumsaidia kila mtu na familia kupokea nguvu ya kiroho ya kuvumilia majaribu tunayokabiliana nayo kila siku. Tunapofanya mfumo huu mpya kuwa sehemu ya maisha yetu, nabii wa Mungu ameahidi kwamba “siku za Sabato zitakuwa zenye furaha. Watoto [Wetu] watafurahia kujifunza na kuishi mafundisho ya Mwokozi, na ushawishi wa adui katika maisha [yetu] na katika nyumba [zetu] utapungua. Mabadiliko katika familia yako yatakuwa makubwa na endelevu.” Ninashuhudia kwamba ahadi hizi ni za kweli na kutualika sote kufokasi katika kuboresha kusoma na kujifunza injili majumbani kwetu mwaka 2025.