Kurasa za Karibu
Kungoja Kwa Muda Mrefu Kulikuwa Kumefika Mwisho
Uunganisho wa/Ndoa ya Hekaluni, Machi 8, 2024: Hekalu la Ghana Accra
Jinsi ilivyoanza.
Siku hii ilipofika, nilipata fursa ya kutafakari ni kwa kiasi gani tumepiga hatua pamoja. Safari haijapata kuwa rahisi sana lakini katika kila gumu tulilokabiliana nalo, Bwana aliandaa njia kwa ajili yetu. Safari yetu ilianza toka siku nilipoushika mkono wa Joanita kwa ajili ya ubatizo wake mwaka 2017 katika maji ya Kata ya Makindye ambapo sote tulianza safari yetu kwenye njia ya agano. Siku chache baadaye tulipokuwa tukisafisha nyumba ya ibada, nilisimama mlangoni mwa ukumbi wetu wa mkutano na kumtazama akisafisha nyumba ya ibada. Nilimpenda wakati huo na ninakumbuka kumfikiria yeye kama mke wangu pembeni yangu lakini sikutilia maanani jambo hilo. Chini ya uongozi wa Askofu wetu Gerald Baryamujura, nilikuwa na fursa ya kuhudumu kama karani wa kata na kushiriki katika mabaraza ya kata. Katika wakati huu, Joanita alikuwa amesafiri kikazi nje ya Uganda, hatukuwahi kubadilishana namba za simu na hatukuwa na ukaribu. Kwa sababu kadhaa jina lake kamwe halikutoweka akilini mwangu kila wakati tulipowajadili waumini ambao walikuwa hawahudhurii tena kanisani.
Mnamo 2019, niliwaalika waumini kwa ajili ya ibada ya Krismasi kwa kutumia mfumo wa kanisa wa barua pepe na Joanita alikuwa mmoja wa waumini wachache ambao walijibu barua pepe hiyo. Kumtafuta kwa muda mrefu hatimaye sasa kulifikia mwisho. Kwa bahati mbaya, sikuona jibu lake mpaka ilipofika Februari 2020, baada ya misioni yangu kuanza.
Kulelewa na kutunzwa
Je, hii inaonekana kama ndoto? Je, ilikuwa ni ufunuo kwangu kuhusu mwanamke ambaye atakuwa mwenza wangu wa milele?
Hamu yangu ya kwenda na kumtumikia Bwana ikiwa angavu, niliondoka kwenda misioni mnamo Septemba 2, 2020 na hakuacha kuniandikia kila wiki kwa miaka miwili. Je, hii ilikuwa ni dalili? Sikuwa nimefikiria hili bado, lakini nilihisi kuna ukuaji imara wa muunganiko kati yetu kutokana na muda aliowekeza katika kuandika na kuuliza zaidi kuhusu mipango niliyonayo baada ya misioni. Karibu na mwishoni mwa misioni yangu, tuliandikiana kuhusu uwezekano wa kuwa na miadi ya kukutana, tulipanga muda kwa ajili ya hilo, lakini hili halikuonekana kama jambo linalowezekana japo bado tulitumainia muda sahihi.
Hofu iliyojitokeza katika safari hiyo.
Wakati akili yangu ikihangaika na mawazo ya jinsi ya kuoa na lini nioe, sikuwa na kazi, nilikuwa na hofu ya kuanzisha familia, na kuishi ilikuwa bado vigumu kwangu kwani ilikuwa kama vile najitegemea mwenyewe. Siku niliyorejea nyumbani kutoka misioni, katika ushauri wake, Askofu Baryamujura alisisitiza kwamba nitakapooa mambo yataniendea vizuri. Nilisikiliza, lakini nitaanzia wapi? Bwana alijua kwamba nina kiu ya haki Yake na ufalme Wake na aliandaa njia kwa ajili yangu. Hili lilijidhihirisha kupitia viongozi niliokuwa nao. Nilijiwajibisha kwa askofu wangu na rais wangu wa kigingi tangu nilipoanza miadi na Joanita. Nakumbuka wakati mwingine kukaa chini na bila kuelewa ni jinsi gani mambo yatafanikiwa. Nilikuwa na hofu lakini alinigeukia na kuniuliza tatizo lilikuwa ni nini. Nilijibu, “Sijui kesho yetu itakuwaje.” Tokea wakati huo nilianza kuhisi kwamba mambo yatafanikiwa aliponiambia kwamba Bwana angeandaa njia kwa ajili ya uhusiano huu na kwamba sipaswi kuhofia. Ni kweli, maisha yalikuwa magumu kwa mmisionari aliyerejea lakini nilijua kwamba hili ndilo Baba yetu wa Mbinguni anatamani kwa kila mmoja wetu na ni amri kwa ajili ya kuinuliwa kwetu.
Kusubiri kwa muda mrefu kunafika mwisho.
Miezi 11 ilipita baada ya kurejea kutoka misioni yangu na tulioana kisheria mnamo Agosti 5, 2023. Tulisaidiana kwa pamoja kushinda madhaifu yetu, na tulishauriana pamoja kwa mambo yahusuyo ustawi wa kimwili na wa kiroho wa familia yetu. Lengo letu na hamu kuu ilikuwa ni kuwa na familia ya milele na ilikuwa tangu siku tuliyoamua kuoana na kukua kila siku kadiri tunavyozidi kuelewana vyema katika uhusiano wetu kama mume na mke. Kwa shangwe hii, shangwe iliongezwa ya kutazamia mtoto. Kwa baraka hizi kuwekwa juu yetu kama familia, kwa dhati nilikuwa na sababu ya kutoa machozi ya shangwe katika chumba cha selestia tulipokuwa tunasubiri kuongozwa katika chumba cha kuunganishia. Kusubiri kwa muda mrefu kulikuwa kumefika mwisho, moyo wangu ulikuwa karibu sana na wake tulipokaa na kutafakati uzoefu huu na umbali ambao Bwana ametuvusha. Macho yangu yalikuwa kama yamebadilishwa kuuona urembo wake wa milele. Kwa kweli, Hakukuwa na mwingine ambaye moyo wangu na maisha yangu yote yalitamani kuongea naye kwa wakati huu tofauti na mke wangu. Hisia hii ilichochea na kukuza tamanio langu lote nililokuwa nalo la kuwa naye na kuwa wa kwake daima. Tulipopiga magoti kwenye madhabahu, ahadi ya kuwa mume atakayesimamia nyumba yake kwa upole na upendo usiochuja ilifuatiwa na baraka zingine na nilitamka “ndiyo” ambayo ilikuwa imara na isiyotingishika. Ningeweza kuhisi jibu lake pia na uso wake uling’ara kuthibitisha hili.