2025
Kwa Sababu ya Hekalu
Mei 2025


“Kwa sababu ya Hekalu ,” Rafiki, Septemba. 2025, 30–31.

Waanzilishi katika Kila Nchi

Kwa sababu ya Hekalu

Hadithi ya kweli kutoka Vanuatu.

Uso wa mvulana mwenye tabasamu mbele ya ramani ya Vanuatu

“Wamisionari wako hapa!” Graham aliita. Aliwapungia wamisionari walipokuwa wakitembea kuelekea nyumbani kwao.

Mama, Baba na kaka mkubwa wa Graham, Nunu, walikuwa wamebatizwa mwaka jana. Graham na kaka yake mdogo, Job, walikuwa wadogo sana kuweza kubatizwa. Lakini bado walipenda kujifunza kutoka kwa wamisionari.

“Leo tunataka kuzungumza kuhusu hekalu,” Mzee Hale alisema. “Ni jengo maalumu ambapo unaweza kufanya ahadi na Mungu na kuunganishwa na familia yako. Hiyo inamaanisha mnaweza kuwa pamoja milele!”

“Hekalu lililo karibu zaidi liko New Zealand.” Mzee Singh alishikilia picha ya jengo jeupe maridadi. “Safari iko mbali. Lakini baraka ni za muhimu.”

“Tunataka kwenda,” Mama alisema.

Wazazi wa Graham walipanga safari yao ya hekaluni na familia nyingine kutoka kanisani. Zingekuwa familia mbili za kwanza kutoka Vanuatu kuingia ndani ya hekalu!

Ndege ikiruka kwenda hekaluni pamoja na basi likiendeshwa kuelekea hekaluni

Miezi michache baadaye, siku ikaja kuondoka kwa ajili ya safari yao. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Graham kwenye ndege, na ilikuwa ya kufurahisha. Alitazama nje kwenye mawingu na bahari chini ya mawingu. Alipiga taswira ya jengo refu jeupe akilini mwake. Hakutaka kuchelewa kuliona!

Mara walipotua, walipanda basi. Ilikuwa safari yenye kurushwa kwingi, na Graham alikuwa amechoka. Lakini walikuwa karibu wamefika.

“Tazama!” Graham alionyoosha kidole dirishani. Ni lile pale! Lilikuwa la kupendeza zaidi kuliko zile picha.

Ndani ya hekalu, kulikuwa kimya na kwenye amani. Walivaa wote nguo nyeupe. Kwa muda, Graham na kaka zake walikaa katika chumba cha kusubiria na kuangalia picha za Yesu Kristo.

Kisha mfanyakazi wa hekaluni aliwaongoza kwenye chumba cha kuunganishwa. Wazazi wa Graham walikuwa wamepiga magoti na madhabahu yaliyofunikwa kwa kitambaa laini. Walionekana kuwa na furaha sana.

Graham na kaka zake walipiga magoti kando ya Mama na Baba. Waliangalia vioo vikubwa, virefu kwenye kuta. Kuakisi kwa vioo kuliendelea na kuendelea.

“Vioo viko kuwakumbusha kwamba mnaweza kuwa pamoja milele,” mfanyakazi wa hekalu alisema.

Graham alihisi furaha na salama. Alihisi kama Mwokozi alikuwa anampa kumbatio kubwa.

Punde ikawa wakati wa kwenda nyumbani. Kwenye basi na kwenye ndege, Graham aliendelea kufikiria hisia maalumu alizokuwa nazo hekaluni.

Siku chache baadaye, upepo mkubwa ulikuja. Miti ya mitende ilionekana kama ingeweza kukatika nusu!

Graham aliogopa. “Je, tutakuwa SAWA?”

“Ndiyo!” alisema Baba. “Lakini pepo hizi zina nguvu. Wamisionari walisema kusanyikeni pamoja katika jengo la kanisa hadi dhoruba itakapomalizika.”

Familia imekaa kwenye benchi wakiangalia dirishani kwenye miti inayovuma

Graham alimsaidia Mama kubeba baadhi ya chakula na mablanketi kanisani. Upepo ulikuwa unavuma kwa nguvu sana!

Ndani, Graham alijihisi vizuri kidogo. Marafiki zao wote kutoka kanisani walikuwa pale. Lakini bado aliweza kusikia upepo ukivuma.

“Vipi kuhusu nyumba yetu?” Graham aliuliza.

“Tutasubiri mpaka baada ya tufani ili kuona.” Mama alimkumbatia kwa karibu. “Kilicho muhimu zaidi ni kwamba familia yetu iko salama. Kumbuka jinsi ulivyohisi mle hekaluni?”

Graham aliitikia kwa kichwa “Nilihisi joto na salama.”

Baba akatabasamu. “Na kwa sababu ya Yesu Kristo na kuunganishwa kwetu hekaluni, tunaweza kuwa pamoja milele.”

Graham alifikiria hisia nzuri, za amani alizohisi hekaluni. Baba alikuwa sahihi. Kwa sababu ya Yesu Kristo na maagano ya hekaluni, wangeweza kuwa familia milele. Na kwa sababu alijua kwamba, kila kitu kingekuwa sawa.

PDF ya hadithi

Vielelezo na Eduardo Marticorena