Je, Wanipenda?”
Kama tunataka kuonyesha upendo wetu kwa Mungu, tunapaswa kuelewa jinsi Yeye anavyotambua upendo wetu.
Katika mfano wa mwana mpotevu, kaka mkubwa mwanzoni alihangaika katika kumsherehekea mdogo wake aliyerudi nyumbani baada ya kipindi cha chaguzi mbaya na kutapanya urithi wake kwa maisha ya tamaa.” Kiburi cha kaka mkubwa na kujiona kuwa mwenye haki vilimzuia kukubali shangwe ya kurudi kwa kaka yake aliyetubu. Nasi pia yawezekana tukaacha fursa zitupite kwa kutowafanya wapendwa wetu kujua upendo wetu kwao, kupitia maneno na matendo.
Kuna mifano mingi yenye nguvu katika maandiko ya upendo wa dhati uliotolewa na kupokelewa: Naomi na Ruthu, Ammoni na Mfalme Lamoni, mwana mpotevu na baba yake, Mwokozi na wanafunzi Wake.
Wakati upendo unapotolewa bure na kupokelewa kwa dhati, mduara wa wema huanzishwa wenye ongezeko la upendo kati ya mtoaji na yule mpokeaji.
Upendo wa Mungu ni mkamilifu, hauna mwisho, wenye kuvumilia, na “ni mtamu zaidi.” Unaijaza nafsi “kwa shangwe kuu kupita kiasi.” Hata hivyo, nyakati zingine huonekana ni vigumu kutambua upendo wa Mungu katika maisha yetu. Hata hivyo, Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo aliye mkamilifu kwa upendo wa kina sana anatamani sisi tuonje upendo Wake kwamba Yeye “anasema kwetu [sisi] kulingana na … uelewa [wetu].” Yeye ataonyesha upendo Wake kwa ajili yetu katika njia ambazo sisi, binafsi, tunaweza kutambua. Tunaweza kuona upendo wa Mungu kwa ajili yetu tunapotazama urembo katika mazingira asili, au tunapo pokea majibu ya sala, au kupata wazo akilini mwetu muda huo huo wa uhitaji, au tunapopitia nyakati za shangwe. Dhihirisho kuu la upendo wa Baba wa Mbinguni kwa ajili yetu ambao unaafikiana na vyote akili na moyo ni pale Yeye aliporuhusu Mwanawe Mpendwa kujitoa kama dhabihu ya kulipia dhambi.
Kama yule kaka mkubwa wa mwana mpotevu, fokasi yetu mara nyingi huwa kwetu binafsi. Tunazama sana kwenye kutafuta ushahidi wa upendo wa Mungu kwa ajili yetu sisi, na tunakanganywa tunapokosa ushahidi huo. Lakini mfano wa kupendeza ni kwamba kadiri tunavyo fokasi zaidi kwenye kuonyesha upendo wetu kwa Mungu, ndivyo kwa urahisi zaidi tunavyotambua upendo Wake kwetu. Pengine hii ndiyo sababu Mwokozi alijibu swali “Amri kuu ni ipi?” kwa mwaliko huu rahisi na muhimu: “Nawe umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.”
Wakati mwingine jinsi tunavyo onyesha upendo wetu kwa wale tuwapendao sio lazima iwe jinsi ambayo wao huutambua upendo. Hii yaweza kuwa ya kukanganya kwa wote wawili mtoaji na mpokeaji. Inaweza kuwa yenye msaada kuwauliza wale tuwapendao wanatambuaje onyesho la upendo. Vile vile, kama tunataka kuonyesha upendo wetu kwa Mungu, tunapaswa kuelewa jinsi Yeye anavyo tambua upendo wetu. Kwa bahati nzuri, Yeye kwa uwazi kabisa amebainisha njia kadhaa katika maandiko ambazo tunaweza kuonyesha upendo wetu Kwake.
Je, Wanipenda Mimi Zaidi Ya Hawa?
Katika mazungumzo kati ya Petro na Bwana Aliyefufuka kwenye Bahari ya Tiberia, tunajifunza juu ya njia ambazo sisi tunaweza kuonyesha upendo wetu kwa Bwana.
“Yesu alimwambia Simon Petro, Simoni, mwana wa Yona, je, wanipenda mimi zaidi ya hawa? Yeye akamwambia, Ndiyo, Bwana; wewe wajua kwamba nakupenda.”
Swali muhimu katika maulizo ya Bwana ni “Wanipenda zaidi kuliko hawa?” Tunaonyesha upendo kwa Bwana tunapomweka Yeye juu ya “hawa,” na “hawa” inaweza kuwa mtu ye yote, shughuli yo yote, au kitu cho chote ambacho kinachukua nafasi Yake kutokana na kuwa ushawishi muhimu zaidi katika maisha yetu.
Kamwe hapatakuwa na muda wa kutosha kwenye siku, wiki, mwezi, au mwaka wa kufanya yote tunayotaka au tunayohitaji kukamilisha. Sehemu ya mtihani wa maisha ya duniani ni kutumia rasilimali ya thamani ya muda kwa kile kilicho muhimu zaidi kwa faida yetu ya milele na kuachana na mambo ambayo hayana umuhimu sana.
Rais Russell M. Nelson alisema: “Swali kwa kila mmoja wetu … ni lile lile. … Je, wewe uko radhi kuacha Mungu awe na ushawishi muhimu zaidi katika maisha yako? Je, utaruhusu neno Lake, amri Zake, na maagano Yake, yashawishi kile unachofanya kila siku? Je, utaruhusu sauti Yake ichukue kipaumbele cha juu zaidi ya sauti zingine zote? Je, wewe uko radhi kuruhusu cho chote Yeye anachohitaji ukifanye kiwe cha kwanza juu ya lengo lingine lo lote? Je, wewe uko radhi kuruhusu mapenzi yako yamezwe katika Yake?” Tunaonyesha uanafunzi wetu na upendo kwa Mungu tunapomfanya Yeye kuwa kipaumbele chetu cha juu.
Lisha Kondoo Wangu
Katika mstari unao fuata wa mazungumzo yale yale kati ya Petro na Mwokozi, tunajifunza juu ya njia nyingine ambayo kwayo Bwana anatambua uonyeshaji wetu wa upendo: “[Bwana] anamwambia tena kwa mara ya pili, Simoni, mwana wa Yohana, je, wanipenda? Petro akamjibu, “Ndio, Bwana; wewe wajua kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo wangu.”
Tunaonyesha upendo wetu kwa Baba wa Mbinguni tunapo hudumu, tunapo msikiliza, tunapo mpenda, kuinua, au kuwatumikia watoto Wake. Huduma hiyo yaweza kuwa rahisi kama kuwaona wengine bila kuwa hukumu. Katika sehemu ya 76 ya Mafundisho na Maagano, tunapata picha ya tabia za wale watakao urithi utukufu wa selestia: “Wao wanaona kama wanavyoonwa, na kujua kama wanavyojulikana.” Wanawaona wengine kama vile Mungu anavyowaona wao, na Yeye anawaona kama wanavyoweza kuwa, wenye uwezekano mtukufu wa kiungu.
Baada ya kurudi nyumbani kutoka misioni, nilisimamia biashara ya kutunza bustani ambayo mimi na kaka zangu tulikuwa tumeianzisha tukiwa vijana wadogo. Pia nilikuwa na kazi nyingi za masomo yangu ya chuo kikuu. Wiki moja ya majira kuchipua, mvua nyingi na mitihani ya mwisho wa muhula vilinizidia na nikawa nyuma kwenye kazi zangu za utunzaji wa bustani.
Katikati ya wiki anga zikawa wazi, nami nikapanga kukamilisha kazi za bustani baada ya madarasa. Lakini nilipowasili nyumbani, gari langu pamoja na vifaa vilikuwa vimetoweka. Kwa shauku, nilitembelea bustani zilizokuwa kwenye ratiba; kila moja ilikuwa tayari imefyekwa. Kwenye uwanja wa mwisho wa bustani iliyo kwenye ratiba, nilimwona kaka yangu mdogo akisukuma mashine ya kukata nyasi. Aliniangalia, akatabasamu, na kupunga mkono. Nikiwa nimezidiwa kwa shukrani, nilimkumbatia na kumshukuru. Kitendo chake cha maana cha huduma kwa kina kiliimarisha upendo wangu na heshima kwake. Kuhudumiana ni njia dhahiri ya kuonyesha upendo wetu kwa Mungu na Mwanawe Mpendwa.
Kiri Mkono Wake katika Mambo Yote”
Pia tunadhihirisha upendo wetu kwa Mungu kwa kuwa na moyo wa shukrani. Bwana alisema, “Katika cho chote mwanadamu hamkosei Mungu, … isipokuwa wale wasio kiri mkono wake katika mambo yote.” Tunaonyesha upendo wetu kwa Mungu kwa kumtambua Yeye kama chanzo cha kila jambo jema katika maisha yetu.
Katika siku za mwanzo za uzinduzi wa kampuni, mimi na mwenzangu katika biashara tungesali kwa dhati kabla ya mikutano muhimu, tukiomba msaada wa Baba wa Mbinguni. Muda baada ya muda, Mungu alijibu sala zetu, na mikutano yetu ilienda vyema. Baada ya mkutano mmoja, mwenzangu alieleza kwamba tumekuwa wepesi katika kuomba msaada lakini wazito kutoa shukrani. Kuanzia hapo, tulifanya hii iwe tabia yetu kutoa sala ya dhati ya shukrani, tukiukiri mkono wa Bwana katika mafanikio yetu. Tunaonyesha upendo wetu kwa Mungu kwa kuwa na “mtazamo wa shukrani.”
“Mkinipenda, Mtazishika Amri Zangu”
Njia nyingine tunayo onyesha upendo wetu kwa Baba wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa ni kuchagua kuwatii Wao. Mwokozi alisema, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Utii wa aina hii si wa upofu wala si wa lazima lakini ni wa dhati na onyesho la hiari la upendo. Baba wa Mbinguni anataka sisi tutake kuwa watiifu. Dada Tamara W. Runia aliita huu “utii wa upendo.” Yeye alisema, “Ingawa hatuna utii mkamilifu bado, tunajaribu utii wa kupenda sasa, kuchagua kubaki, tena na tena, kwa sababu sisi Tunampenda.”
Baba wa Mbinguni alitupatia haki ya kujiamulia ili kutuvutia sisi tutake kumchagua Yeye. Kazi na utukufu Wake siyo tu kuleta uzima wetu wa milele lakini pia inajumuisha tumaini kwamba hamu yetu kuu ni kurudi Kwake. Hata hivyo, Yeye kamwe hatatulazimisha kutii. Katika wimbo wa dini “Tuko Huru Kuchagua,” tunaimba:
Kama viongozi wa misioni, mimi na Christina, mke wangu, tulivutiwa na wamisionari wengi ambao walichagua kuwa watiifu, siyo tu kwa sababu ilikuwa ni kiwango cha umisionari lakini kwa sababu wao walitaka kuonyesha upendo wao kwa Bwana kwa unyenyekevu kuchagua kumwakilisha Yeye.
Mzee Dale G. Renlund alisema “Lengo la Baba yetu wa Mbinguni katika malezi siyo kufanya watoto Wake kutenda kile kilicho sahihi; ni kufanya watoto Wake wachague kufanya kile kilicho sahihi na hatimaye kuwa kama Yeye. Kama Yeye angetaka tu sisi tuwe watiifu, Yeye angetumia zawadi za papo kwa papo na adhabu ili kushawishi tabia zetu.” Tunaonyesha upendo kwa Mungu tunapo chagua kumtii Yeye.
Baba wa Mbinguni na Mwokozi wetu wanatambua dhihirisho letu la upendo Kwao tunapo waweka Wao kwanza katika maisha yetu, tunapo tumikiana, kwa shukrani tunapo kiri kila baraka kutoka Kwao, na tunapo chagua kutii na kuwafuata Wao.
Ninashuhudia kwamba kila mmoja wetu hakika ni mtoto wa Mungu, na kwamba anatupenda sote kikamilifu. Ninashuhudia kwamba Yeye ana hamu ya kuona sisi tunaonja upendo Wake katika njia tunazo weza kutambua na kuelewa. Na fumbo zuri ni kwamba tutapata upendo Wake kwetu hata kwa kina zaidi tunapo onyesha upendo wetu Kwake. Katika jina la Yesu Kristo, amina.