Mkutano Mkuu
Pokea Zawadi Yake
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


14:4

Pokea Zawadi Yake

Wewe ni binti mpendwa wa Mungu, wewe ni mwana mpendwa wa Mungu, na Yeye amekuzawadia wewe na Mwanawe, Mkamilifu.

Utoaji Zawadi

Utoaji zawadi ni desturi ya kijamii ambayo inahusisha tamaduni zote, ustaarabu na milenia. Kwa nyakati zote watu wamepeana zawadi wao kwa wao kuimarisha uhusiano, kuonyesha upendo, shukrani, na kuadhimisha matukio muhimu kama vile harusi, tarehe za kuzaliwa na sikukuu. Na wanadamu siyo viumbe wa Mungu pekee wanaopeana zawadi! Miongoni mwa mifano mingine mingi ambayo tunaweza kuangazia, ni pengwini ambao wanafahamika kwa kutoa kokoto zinazong’ara kwa wenzi wao watarajiwa, bonobo (binamu wa sokwe) hupeana tunda ili kupanua wigo wa urafiki.

Pengwini wakitoa kokoto.
Bonobo akitoa tunda.

Je, wewe ni zawadi gani umetoa? Fikiria wakati ulipopata—au kufanya—ile zawadi kamilifu kwa mtu unayempenda. Wewe ulijua zawadi hiyo ilikuwa haswa ndicho mpendwa huyu alikitaka na kitu ambacho angekithamini. Ilikuwa zawadi gani? Ilikuwa ni kwa ajili ya mama yako? Rafiki? Mtoto wako? Mwalimu? Babu yako? Ulijisikiaje ulipoipata zawadi hii? Ulijisikiaje wakati ulipofikiria kuhusu mtu huyu unayempenda akifungua zawadi hiyo? Vivyo hivyo, ni lini mtu alikupa wewe zawadi kamilifu, na ulihisije ulipoipokea?

Zawadi ya Baba Yangu Kwangu Mimi

Nilipokuwa na umri wa miaka saba hivi, niliishi na wazazi wangu huko Arabia, filamu ya watoto iitwayo Chitty Chitty Bang Bang iliachiliwa. Filamu hii ni kuhusu gari la kimaajabu ambalo linaweza kujiendesha lenyewe, kuelea juu ya maji na hata kuruka angani! Nilijua kule nyumbani Uingereza walitengeneza gari ndogo mwanasesere kama Chitty Chitty Bang Bang, na ah, nilitamanije kuwa na moja! Ungeweza kuvuta wenzo, na mabawa ya gari mwanasesere yangejitokeza! Baba yangu alienda Uingereza kwa safari ya kikazi na akaniuliza kama ningetaka yeye aniletee chochote kutoka huko, na nikamwambia ni kiasi gani ningetamani kupata moja ya yale magari ya Chitty Chitty Bang Bang.

Alirudi nyumbani kutoka safari yake, na hakuna gari lililoonekana. Nilisikitika sana na nikafikiri lazima atakuwa alisahau. Lakini karibia siku 10 hivi ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa, na paketi ndogo iliyofungwa kwa maridadi, ilikuwa ikinisubiri. Kwa matarajio makubwa, na vigumu kuthubutu kutarajia mengi sana, nilifungua ile zawadi yangu na nikakuta gari yangu. Nilifurahi sana kiasi kwamba nililia. Nilivuta wenzo, na mabawa yakachomoza, kama vile ile gari kwenye filamu. Nilimshukuru sana baba yangu kwa zawadi hii kuu ya thamani. Nilicheza na gari ile kwa miaka mingi na nikaiweka kwa miaka mingine mingi zaidi. Nafikiri baba yangu alipenda kunipa gari lile kama vile mimi nilivyopenda kuipokea.

Kutoa, Kukubali na Kufungua na Kupokea

Tunaweza kufikiri juu ya utoaji wa zawadi kama una sehemu tatu:

  1. Utoaji wa zawadi, ambapo mtoaji anachagua, anatengeneza au anaiandaa zawadi hiyo, na kuiwasilisha kwa mpendwa wake. Hii inahusisha nia ya kufikiria kwa upendo wa mtoaji kutoa kitu cha maana.

  2. Kukubali na kufungua ile zawadi, pale mpokeaji anapokubali zawadi kutoka kwa mtoaji—mara nyingi akiwa na onyesho la mshangao, shukrani, na shauku—kabla ya kuifungua, wakati mwingine kufungua kamba na kufungua kifurushi ili kugundua ni zawadi gani.

  3. Na kisha pengine kuna sehemu muhimu sana, ni kule kupokelewa kwa zawadi. Kupokea zawadi iliyotolewa kwa dhati ni zaidi sana kuliko kuikubali na kisha kuifungua. Ni zaidi, hata, kuliko kutambua thamani ya zawadi na kuelezea shukrani kwa mtoaji. Kwa kweli kupokea zawadi, tunakuja kuithamini kwa ajili yetu wenyewe, kuiweka katika matumizi kamili katika maisha yetu na kisha tunamkumbuka kwa shukrani mtoaji.

Kupokea zawazi siyo mchakato baridi bali ni mchakato wa kusudi na maana ambao unaenda mbali zaidi ya kufungua kifurushi. Kupokea ni kuthamini na kuunganika na vyote viwili zawadi na moyo wa mtoaji katika njia ambayo inaimarisha muunganiko kati ya yule mtoaji na mpokeaji. Nikifikiria juu ya ile gari mwanasesere hunirudishia lundo la kumbukumbu za dhahabu, ninapohisi kwa mara nyingine tena upendo wa kina wa baba yangu na kunijali kwake, kulikowakilishwa na zawadi ile na vitendo vingine vingi vya ukarimu.

Zawadi za Baba Yetu wa Mbinguni

Baba yetu wa Mbinguni anazo zawadi zisizo na idadi za nuru na kweli zilizoandaliwa kumwagwa chini juu ya kila mmoja wetu, watoto Wake wa thamani. Zinatiririka kutoka Mtoaji Mkarimu kama kisima cha maji kilicho nyikani kutoka kwenye moyo Wake mzuri. “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, na huja chini kutoka kwa Baba wa mianga.” Katika muunganiko wetu wa kiagano na Baba, Yeye daima ndiye mtoaji nasi tu wapokeaji wanyenyekevu.

Zawadi Kuu Kuliko Zawadi Zote za Baba, Ambapo Kwayo Zawadi Nyingine Zote Hutiririka

Lakini tusingeweza kupokea chochote pasipo zawadi iliyo kuu kuliko zawadi zote za Baba, Mwanakondoo Wake mpendwa, Mwanawe, Yesu Kristo. Zawadi zote za Baba hutiririka kutoka kwa na huhuishwa na matoleo ya hiari ya Mwokozi katika Gethsemane na juu ya msalaba na Ufufuko Wake wa ushindi. Yesu Kristo, Mkombozi wetu mwenye rehema, ndiye zawadi kuu kutoka kwa Baba wa mianga. “Katika zawadi ya Mwanawe Mungu ametuandalia [sisi] njia iliyo bora.”

Zawadi Moja Inayojumuisha Yote ya Ukweli wa Milele

Ningependa kuzungumza kuhusu zawadi moja inayojumuisha-yote ya ukweli wa milele ambayo inatoa uwezo wetu wa kupokea mengine yote ambayo Baba anatamani kutupatia—zawadi muhimu ya maarifa ambayo ikikubaliwa kwa ukamilifu na kupokelewa kwa kina ndani ya nafsi, inaweka mazingira ya shangwe na magumu ya maisha, na maswali yetu yasiyojibiwa: Sisi hakika ni watoto wa Mungu. Ukweli huo unasisimua! Unashangaza! Na hii siyo ya kiisitiari.

Fikiria unasikia hili kwa mara ya kwanza! Wewe hakika ni binti Yake wa thamani. Wewe hakika ni mwana Wake wa thamani. Njia uliomo sasa ni mpango Wake wa furaha. Pamoja na upendo Wake unaojua yote, Yeye anajua hasa wewe ulikuwa nani kabla haujatumwa huku ulimwenguni, kile ilichopitia kufika hapa katika maisha yako ya duniani, na Yeye amepanga kwa neema kwa ajili ya kila kesho yako. Na lo, anatamani kiasi gani kwamba siku moja urejee Kwake, ili upokee dhamira kuu ya zawadi Zake zote nzuri, uzima wa milele pamoja na Yeye.

Swali siyo kama zawadi hii ya ukweli ipo bali kama tutaigundua na kuipokea. Zawadi tayari imetunukiwa juu yetu na Baba. Bei ya dhumuni muhimu la zawadi tayari imekwisha kulipwa na Mwokozi. Lakini kama umekuwa ukifundishwa hili, kusema hili, na ukaimba ukweli huu kwa miaka mingi, huenda ajabu yake ya kupendeza imefifia kitambo sana na huhisi tena nguvu na amani yake.

Ikiwa hii zawadi ya thamani mno ya uelewa—na mema yote, amani na tumaini ambavyo hutiririka kutoka kwayo—inaachwa bila kukubaliwa, bila kufunguliwa na bila kupokelewa, ni hasara ilioje kwetu! Ni huzuni iliyoje kwa Mtoaji! “Kwani itamfaidia mtu nini kama zawadi imewekwa juu yake, na hapati zawadi hiyo? Tazama, hafurahii katika kile ambacho kimetolewa kwake, wala hamfurahii yeye aliyetoa zawadi.

Ninakualika kupokea iwe kwa mara ya kwanza au kwa ukubwa mpana kuliko hapo awali, ukuu wa ufahamu kwamba wewe hakika ni mtoto mpendwa wa Mungu. Lazima ufungue kamba, uichane karatasi iliyofungiwa, fungua boksi na kwa shauku pokea kwa shukrani yenye unyenyekevu wa kweli, uelewa safi wa ukweli wa kimsingi. Roho Mtakatifu anaweza kutoa ushuhudia kwenye moyo wako kwamba wewe hakika ni mtoto wa yule Aliye Juu Sana.

Unapokaribisha uhalisi huu mkuu katika nafsi yako na kuhisi vyote faraja na msisimko wake, kielelezo chako kinabadilika kabisa! Unaweza kuhisi upendo Wake, kusikia sauti Yake, na kuutambua mkono Wake, bila kujali kile kinachotokea au kisichotokea katika maisha yako. Unaweza kufafanua upya jinsi unavyojiona mwenyewe na unavyowaona wengine. Kifungo cha agano lako na Mwokozi wako huwa imara zaidi, na kupitia lenzi za hii zawadi tamu, maisha huchukua uangavu mpya, urembo, na tumaini.

Tafadhali, je, utasali ili kuelewa kama hakika unapokea maarifa haya yenye kubadilisha kwa kina nafsini mwako? Tafadhali kubali zawadi hii? Je, utafanya hivyo kwa kina zaidi, kwa uhuru zaidi, kwa wingi zaidi kuliko hata hapo kabla-na kwa kufanya hivyo ukanyeshewe pamoja na zile zawadi nyingi ambazo huja pamoja na hizo?

Kupokea Zawadi Hii ya Ukweli wa Milele

Unaweza kuwa unashangaa, “Ni nini ninapaswa kufanya ili kupokea zawadi hii kutoka kwa Mungu? Kwa kweli, hasa, hakuna chochote. Ni zawadi kutoka kwa Mtoaji. Ni ukweli rahisi. Iache tu iingie ndani. Wewe ni mtoto Wake. Wewe ni mpendwa Wake. Usiifanye kuwa tatanishi. Usizuie upokeaji wa zawadi hii kwa mawazo kwamba wewe kwa namna fulani ustahili. Ukweli ni kwamba hakuna ye yote miongoni mwetu “anayestahili”—zawadi zote za Baba zinapokelewa tu kupitia fadhila, rehema na neema za Masiya Mtakatifu, lakini ni kwa jinsi gani moyo Wake wa ukarimu anatamani watoto Wake wazipokee! Kisha, kama uelewa wako mpya au uliofanywa upya hupambazuka kwako, furahia katika kumshukuru Mtoaji wa zawadi hii.

Tangu kupata imani yangu katika miaka yangu ya 20 na, nimeziduka kwenye utambuzi kwamba kwa kweli mimi ni mwana wa Mungu. Kwa ukamilifu zaidi ninapoifanya zawadi hii kuwa yangu, ndivyo zaidi ninavyojua kwa makini kuwa mimi ni nani na jinsi kikamilifu ninavyopendwa. Baadhi ya vitu ambavyo vimenisaidia kukua katika uelewa ni maneno ya maandiko, baraka yangu ya kipatriaki, kuabudu hekaluni, kuwatumikia wengine, kuelezea shukrani, na sala takatifu kwa Baba yangu. Ninashangaa jinsi huzuni ya awali, maumivu na uchungu katika maisha yangu vingeweza kubadilishwa na kutulizwa na mengi yake hushinda kama ningejua ukweli huu mzuri.

Njooni kwa Kristo na Mpokee

Moroni anatusihi “tusikatae karama za Mungu” bali “mje kwa Kristo, na kushikilia kila karama nzuri.” Mnaweza kuja kwa Kristo kwa kujiamini katika upendo Wake wa ukarimu na kupokea karama Zake zote za shangwe, amani, tumaini, nuru, ukweli, ufunuo, maarifa na hekima—na kichwa chako kikiinuliwa juu, mikono kunyooshwa na viganja vikiwa wazi, tayari kupokea. Na unaweza kupokea zawadi hizi kwa sababu wewe uko salama na umejengwa katika maarifa ya kwamba wewe ni binti mpendwa wa Mungu, wewe ni mwana mpendwa wa thamani wa Mungu, na amekupa wewe zawadi ya Mwanawe mkamilifu mtakatifu ili akukomboe, kukuhalalisha na kukutakasa.

Wewe ni mtoto wa Mungu!” Huu siyo tu wimbo mzuri tunaoimba. Je, tafadhali utakubali, utafungua na kupokea zawadi hii ya maarifa na uelewa kutoka kwake Yeye? Je, utaikumbatia kwa karibu kama hazina ya thamani kwani ndiyo ilivyo? Ipokee upya zawadi hii au pengine hakika ipokee kwa mara ya kwanza kabisa, na acha ibadilishe kila kipengele cha maisha yako. Hii ni njia iliyo bora zaidi ambayo Mungu ameiandaa kwa ajili yako kupitia Mwanawe. Wewe kweli upo ili upate kuwa na shangwe! Katika jina la Yesu Kristo, amina.