Maandalizi Binafsi Kukutana na Mwokozi
Fuata mafundisho ya Mwokozi. Maelekezo Yake wala si ya ajabu au changamano. Tunapoyafuata, hatuhitaji kuogopa au kuwa na wasiwasi.
Wapendwa akina kaka na akina dada, Oktoba iliyopita, Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Sasa ni wakati wako na mimi wa kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo.” Wakati Rais Nelson anapozungumza kuhusu Ujio wa Pili, daima ni kwa matumani mema ya shangwe. Hata hivyo, msichana wa Darasa la Watoto hivi karibuni aliniambia kwamba yeye anakuwa na wasiwasi wakati wowote Ujio wa Pili unapotajwa. Alisema, “Ninakuwa na woga kwa sababu vitu vibaya vinatokea kabla Yesu hajaja tena.”
Sio tu watoto ambao wanahisi hivyo. Ushauri bora kwake, kwako na kwangu ni kufuata mafundisho ya Mwokozi. Maelekezo Yake wala si ya ajabu au magumu. Tunapoyafuata, hatuhitaji kuogopa au kuwa na wasiwasi.
Kuelekea mwisho wa huduma Yake ya duniani, Yesu Kristo aliulizwa ni lini Yeye angerudi tena. Katika kujibu, Yeye alifundisha mafumbo matatu, yaliyorekodiwa katika Mathayo 25, kuhusu jinsi ya kujiaanda kukutana Naye—Iwe ni katika Ujio Wake wa Pili au wakati wowote tunapoondoka ulimwenguni humu. Mafundisho haya ni muhimu kwa sababu maandalizi binafsi ya kukutana na Yeye ndiyo kiini cha dhumuni la maisha.
Mwokozi kwanza alisema fumbo la wanawali kumi. Katika fumbo hili, wanawali kumi walienda kwenye karamu ya harusi. Watano kwa busara walileta mafuta ya kujaza taa zao, na watano wapumbavu hawakufanya hivyo. Wakati kuwasili kwa bwana harusi kulipotangazwa, wanawali wapumbavu waliondoka kwenda kununua mafuta. Waliporejea, walikuwa wamechelewa; mlango wa kuingia kwenye karamu ulikuwa umefungwa.
Yesu Kristo alitambulisha vipengele vitatu vya fumbo hili kutusaidia sisi. Yeye alieleza:
“Na siku ile, wakati nitakapokuja katika utukufu wangu, ndipo mfano utakapotimia ambao nilisema kuhusu wanawali kumi.
“Kwani wale walio na hekima na kupokea ukweli, na wamemchukua Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao, na hawajadanganyika—amini ninawaambia … watastahimili siku ile.”
Kwa maneno mengine, hawahitaji kuogopa au kuwa na wasiwasi kwa sababu watanusurika na kustawi. Watashinda.
Ikiwa sisi tuna hekima, tutapokea ukweli kwa kukubali injili ya Yesu Kristo kupitia ibada za ukuhani na maagano. Kisha, tunajitahidi kubaki wenye kustahili kuwa na Roho Mtakatifu daima pamoja nasi. Uwezo huu sharti upatikane kwa kila mtu binafsi, tone kwa tone. Vitendo thabiti, binafsi, vya kiibada humwalika Roho Mtakatifu kutuongoza.
Kipengele cha tatu ambacho Yesu aliangazia ni kuepuka udanganyifu. Mwokozi alionya:
“Angalieni kwamba hakuna mtu atakaye wadanganya.
“Kwa sababu wengi watakuja katika jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo—nao watawadanganya wengi.”
Mwokozi alijua wenye kujifanya wangejaribu kuwadanyanya hasa wateule na kwamba wafuasi wengi wangedanganywa. Hatupaswi kuwaamini wale ambao kwa uongo wanadai kibali cha uungu au kutembelea majangwa ya kiistiari au vyumba vya siri ili kufundishwa na vitu bandia.
Kitabu cha Mormoni kinatufundisha jinsi tunavyoweza kutofautisha wadanganyifu na wanafunzi. Wanafunzi daima hukuza kuamini katika Mungu, kumtumikia Yeye na kufanya mema. Hatutadanganywa wakati tunapotafuta na kupata ushauri kutoka kwa watu wanaoamimika ambao wao wenyewe ni wanafunzi waaminifu wa Mwokozi.
Tunaweza pia kuepuka udanganyifu kwa kuabudu kila mara katika hekalu. Hii hutusaidia kudumisha mtazamo wa milele na kutulinda kutokana na ushawishi ambao ungeweza kutuvuruga au kutuchepusha kutoka kwenye njia ya agano.
Somo muhimu la fumbo hili la wanawali kumi ni kwamba tunakuwa na hekima tunapokubali injili, kutafuta kuwa na Roho Mtakatifu kuwa pamoja nasi na kuepuka udanganyifu. Wale wanawali watano wenye hekima hawangeweza kuwasaidia wale ambao hawakuwa na mafuta; hakuna mtu anayeweza kukubali injili, kuwa na Roho Mtakatifu kama kiongozi na kuepuka udanganyifu kwa niaba yetu. Tunapaswa kufanya hivi kwa ajili yetu wenyewe.
Mwokozi kisha alisema fumbo la talanta. Katika fumbo hili, mtu alitoa viwango tofauti vya fedha, vilitajwa kama talanta, kwa watumishi watatu. Kwa mtumishi mmoja alitoa talanta tano, kwa mwingine alitoa talanta mbili, na kwa wa tatu alitoa talanta moja. Baada ya muda, watumishi wawili wa kwanza walizalisha maradufu ya kile walichopokea. Lakini mtumishi wa tatu alizika chini ile talanta yake moja. Kwa watumishi wote wawili ambao walizalisha maradufu talanta zao, yule mtu alisema: “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.”
Yule mtu kisha alimkaripia mtumishi ambaye alikuwa amezika talanta yake kwa kuwa “mtumwa mbaya na mlegevu.” Talanta ya mtumishi huyu ilitwaliwa, na akafukuzwa. Bado, kama mtumishi huyu angelirudufu talanta yake, angepokea sifa na tuzo kama wale watumishi wengine.
Ujumbe mmoja wa fumbo ni kwamba Mungu anatutarajia sisi kutanua uwezo tuliopewa, lakini Yeye hataki sisi tulinganishe uwezo wetu na ule wa wengine. Fikiria umaizi uliotolewa na msomi wa Hasidic karne ya 18, Zusya wa Anipoli. Zusya alikuwa mwalimu maarufu ambaye, alianza kuogopa alipokaribia kifo. Wanafunzi wake waliuliza, “Bwana, mbona unatetemeka? Umeishi maisha mazuri; hakika Mungu atakupa tuzo kubwa.”
Zusya alisema: “Kama Mungu akisema kwangu, ‘Zusya, kwa nini wewe haukuwa Musa mwingine? Nitasema, “Kwa sababu wewe haukunipa ukuu wa nafasi ambayo ulimpa Musa.’ Na kama nikisimama mbele za Mungu na Yeye anasema, ‘Zusya, kwa nini wewe haukuwa Sulemani mwingine? Nitasema, ‘Kwa sababu wewe haukunipa hekima ya Sulemani.’ Lakini, ole, kama nikisimama mbele za Muumba wangu na Yeye aseme, ‘Zusya, kwa nini wewe haukuwa Zusya? Kwa nini wewe haukuwa mtu ambaye nilikupa uwezo wa kuwa? Aa, hii ndiyo sababu ninatetemeka.”
Kwa kweli, Mungu atasikitika kama hatutategemea fadhili, rehema na neema ya Mwokozi ili kutanua uwezo uliotolewa na Mungu tuliopokea. Kwa usaidizi Wake wenye upendo, Yeye anatutarajia kuwa toleo bora la sisi wenyewe. Kwamba tunaweza kuanza kwa uwezo unaotofautiana si kitu Kwake. Na inabidi iwe hivyo kwetu.
Mwishowe, Mwokozi alisema fumbo la kondoo na mbuzi. Wakati Yeye atakaporudi katika utukufu Wake, “na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.”
Wale walio upande Wake wa kulia wakawa warithi katika ufalme Wake, na wale walio upande Wake wa kushoto hawatapokea urithi. Sifa bainifu ilikuwa ni kama wao walimlisha Yeye wakati Yeye alipokuwa na njaa, walimpa Yeye kinywaji wakati Yeye alipokuwa na kiu, walimpa Yeye makazi wakati Yeye alipokuwa mgeni, walimvisha Yeye wakati Yeye alipokuwa uchi na walimtembelea Yeye wakati Yeye alipokuwa mgonjwa au kifungoni.
Kila mtu alikanganywa, wote wale walio mkono wa kulia na wale walio mkono wa kushoto. Waliuliza ni lini walimpa au hawakumpa Yeye chakula, kinywaji, mavazi, au kumsaidia Yeye wakati alipokuwa na uhitaji. Kwa kujibu Mwokozi alisema “Amin, nawaambia kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”
Ujumbe wa fumbo ni wazi: tunapowatumikia wengine, tunamtumikia Mungu; tusipofanya hivyo, tunavunja moyo. Yeye anatutarajia sisi kutumia vipawa vyetu, talanta na uwezo kubariki maisha ya watoto wa Baba yetu wa Mbinguni. Msukumo wa kiungu wa kuwatumikia wengine ulionyeshwa katika shairi lilioandikwa katika karne ya 19 na mshairi Mfini Johan Ludvig Runeberg. Mimi pamoja na ndugu zangu tulisikia shairi hili likirudiwa rudiwa “Mkulima Paavo” kote katika utoto wetu. Katika shairi, Paavo alikuwa mkulima masikini ambaye aliishi pamoja na mke wake na watoto katika ukanda wa ziwa katikati ya Finland. Kwa miaka kadhaa mfulululizo, mengi ya mazao yake yaliharibiwa, iwe ni kutokana na uyeyukaji wa theluji ya majira ya kuchipua, dhoruba za majira ya joto, au baridi ya mapema ya majira ya kupukutika majani. Kila wakati mavuno haba yalipopatikana, mke wa mkulima aliomboleza, “Paavo, Paavo, wewe mtu mzee mwenye bahati mbaya, Mungu ametutelekeza.” Paavo, akijibu, kwa ukakamavu alisema, “Changanya maganda na unga wa shayiri utengeneze mkate ili watoto wasiwe na njaa. Nitafanya bidii kukausha maji maji kwenye shamba. Mungu anatujaribu, lakini Yeye atatupatia.”
Kila wakati mimea ilipoharibiwa, Paavo alimwelekeza mke wake kuongeza mara mbili ya kiasi cha maganda ambayo alichanganya na unga ili kuzuia wasife na njaa. Pia alifanya kazi kwa bidii sana, akichimba mitaro ili kutoa maji kutoka kwenye ardhi ili kupunguza uwezekano wa shamba lake kuharibiwa na maji ya majira ya kuchipua na barafu ya majira ya kupukutika majani.
Baada ya miaka ya ugumu, Paavo hatimaye alipata mavuno mengi. Mke wake alishangilia, “Paavo, Paavo hizi ni nyakati za furaha! Ni wakati wa kutupa maganda, na kuoka mkate wa shayiri pekee.” Lakini kwa umakini Paavo aliutwaa mkono wa mke wake na kusema, “Changanya nusu ya unga na maganda, kwani mashamba ya jirani yetu yamefunikwa na barafu.” Paavo alitoa dhabihu mavuno yake na ya familia yake ili kumsaidia jirani masikini aliyekuwa anaangamia.
Somo la fumbo la Mwokozi la kondoo na mbuzi ni kwamba tunapaswa kutumia vipawa vyetu tulivyopewa—muda, talanta na baraka—kuwatumikia watoto wa Baba wa Mbinguni, hasa wale walio hatarini na wenye uhitaji.
Mwaliko wangu kwa yule mtoto wa Darasa la Watoto mwenye wasiwasi niliyemtaja hapo awali, na kwa kila mmoja wenu, ni kumfuata Yesu Kristo na kumtumainia Roho Mtakatifu kama vile ambavyo ungefanya kwa rafiki wa thamani. Wategemee wale ambao wanakupenda na wale wanaompenda Mwokozi. Utafute mwongozo wa Mungu ili kukuza uwezo wako wa kipekee, na wasaidie wengine, hata pale ambapo si rahisi kufanya hivyo. Utakuwa tayari kukutana na Mwokozi, na unaweza kuungana na Rais Nelson katika kuwa mwenye kutumainia mema kwa shangwe. Kwa kufanya hivyo, unasaidia kuutayarisha ulimwengu kwa ajili Ujio wa Pili wa Yesu Kristo, na utabarikiwa kwa tumaini la kutosha kuingia katika pumziko na shangwe ya Bwana, sasa na katika siku zijazo.
Kama tunavyoimba katika moja ya nyimbo zetu mpya:
Katika jina la Yesu Kristo, amina.