Mkutano Mkuu
Nyakati za Urejeshaji wa Mambo Yote
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


15:21

Nyakati za Urejeshaji wa Mambo Yote

(Matendo ya Mitume 3:21)

Kilicho muhimu sana na “habari njema” tukufu ni ujumbe kwamba Bwana Yesu Kristo amerejesha injili na Kanisa Lake katika siku za mwisho.

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lilianzishwa siku kama ya leo, Aprili 6, 1830, miaka 195 iliyopita.

Mkusanyiko mdogo wa waumini na marafiki walikusanyika kwa ajili ya tukio hili kuu na la shangwe. Mmiminiko mkubwa wa Roho uliwabariki wote waliokuwepo wakati ibada ya sakramenti ilipokuwa ikifanyika, kipawa cha Roho Mtakakatifu kilitunukiwa, kutawazwa kwenye ukuhani kulifanyika na kweli za injili ya Yesu Kristo zilihubiriwa.

Katika kuanzisha tena Kanisa Lake, Bwana alimteua kupitia ufunuo Joseph Smith mwenye umri wa miaka 24 kama kiongozi wake duniani: “Mwonaji, mfasiri, nabii, mtume wa Yesu Kristo, mzee wa kanisa kwa mapenzi ya Mungu Baba, na neema ya Bwana wenu Yesu Kristo.”

Ninasali kwa dhati kwa ajili ya msaada wa Roho Mtakatifu tunapo tafakari umuhimu wa matokeo endelevu ya tukio hili kuu kwenye historia ya ulimwengu huu.

Ono la Kwanza

Uanzishwaji rasmi wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ulikuwa umefikia kilele cha mlolongo wa matukio ya kimiujiza. Matukio ya kwanza ya hayo yalitokea miaka 10 kabla huko upstate New York.

Mnamo majira ya kuchipua ya mwaka 1820, kijana aliyeitwa Joseph Smith alikwenda kwenye kisitu karibu na nyumba yake ili kusali. Alikuwa na maswali kuhusu wokovu wa nafsi yake, na alitamani kujua “lipi kati ya [makanisa] yote lilikuwa la kweli, ili [ajue] lipi la kujiunga nalo.” Joseph aliamini kwamba Mungu angejibu sala yake na kumwelekeza.

Tafadhali zingatia kwamba Joseph hakusali tu kwa ajili ya kujua kipi ni sahihi. Badala yake, alisali kujua kipi ni sahihi ili kwamba afanye kilicho sahihi. Joseph aliuliza kwa imani na alikuwa na nia ya kutenda kulingana na jibu alilopokea.

“Kwenye [jibu] la sala yake ya [dhati], Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo walimtokea Joseph na kuzindua ‘urejeshaji wa vitu vyote’ (Matendo ya Mitume 3:2) kama ilivyotabiriwa kwenye Biblia. Katika ono hili, alijifunza kwamba kufuatia kifo cha Mitume wa mwanzo, Kanisa la Kristo la Agano Jipya lilitoweka duniani” Joseph Smith angekuwa chombo kwenye kurejesha kwa mara nyingine tena mafundisho, mamlaka na maagano na ibada za Kanisa la kale la Mwokozi.

Ono la Kwanza

Joseph alisisitiza: “Niliwaona viumbe wawili, ambao mng’aro na utukufu wao wapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!

Kupitia ono hili na uzoefu uliofuatia baada ya hapo, Joseph Smith alikuja kuelewa kwamba Mungu na Yesu Kristo walimjua kama mtu binafsi, walijali kuhusu wokovu wake wa milele na walikuwa na jukumu kwa ajili yake. Pia alijifunza masomo muhimu kuhusu tabia, sifa na utimilifu wa Uungu—na kwamba Baba na Mwana ni viumbe wawili tofauti. Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu kiroho na kimwili.

Joseph Smith alitamka kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo ni viumbe wanaohusiana. Alisema, “Baba ana mwili wa nyama na mifupa wenye kushikika kama wa mwanadamu; na Mwana vile vile; lakini Roho Mtakatifu hana mwili wa nyama na mifupa, bali ni mtu wa Kiroho.”

Ninashuhudia kwamba kutembelewa kwa Joseph Smith na Baba na Mwana lilikuwa tukio la kuanzisha “urejesho mkuu wa mambo yote yaliyozungumzwa kwa vinywa vya manabii wote watakatifu tangu mwanzo wa ulimwengu.”

Kitabu cha Mormoni

Wa pili katika mlolongo wa uzoefu wa kimiujiza ambao ulipelekea kwenye kuanzishwa rasmi kwa Kanisa la lililorejeshwa la Mwokozi ni tafsiri na ujio wa Kitabu cha Mormoni.

Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo

“Joseph Smith alipewa kipawa na nguvu ya Mungu ili kutafsiri kumbukumbu ya kale: Kitabu cha Mormoni—Ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo. Kurasa za maandishi haya matakatifu zinajumuisha maelezo ya huduma binafsi ya Yesu Kristo miongoni mwa watu wa sehemu ya Ulimwengu wa Magharibi punde baada ya Ufufuko Wake. [Kitabu cha Mormoni] kinafundisha juu ya lengo la maisha na kuelezea mafundisho ya Kristo, ambayo ni kiini cha lengo hilo. Kama maandiko mwenza kwa Biblia, Kitabu cha Mormoni kinashuhudia kwamba wanadamu wote ni wana na mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo, kwamba Yeye anao mpango wa kiungu kwa ajili ya maisha yetu, na kwamba Mwanawe, Yesu Kristo, anazungumza leo kama vile ilivyokuwa katika siku za kale.”

Kama waumini wa Kanisa lililorejeshwa la Kristo “Tunaamini katika Biblia kuwa ni neno la Mungu alimradi imetafsiriwa kwa usahihi; pia tunaamini Kitabu cha Mormoni kuwa ni neno la Mungu.” Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo, kikithibitisha ukweli wa Biblia na kurejesha kweli zilizo wazi na za thamani ambazo zilipotea kutoka kwenye Biblia.

Ukuhani Umerejeshwa

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hufundisha kwamba kanisa la asili lililoanzishwa na Mwokozi, likiwa na mamlaka ya kiungu, mafundisho na maagano na ibada, lilitoweka ulimwenguni. Kama sehemu ya unabii juu ya urejesho wa vitu vyote katika siku za mwisho, manabii wa kale na mitume wao wenyewe walitunuku mamlaka ya ukuhani kwa Joseph smith na kumpa funguo za ukuhani. Hili lilikuwa tukio la tatu katika mlolongo wa matukio ya kimiujiza ambayo yaliongoza kwenye uanzishwaji rasmi wa Kanisa la Mwokozi lililorejeshwa.

Mamlaka ya Ukuhani huwaruhusu watumishi wa Mungu “kumuwakilisha [Yeye] na kutenda katika jina Lake.” “Funguo za Ukuhani ni mamlaka ya kuelekeza matumizi ya ukuhani kwa niaba ya watoto wa Mungu.”

Urejesho wa Ukuhani.

Chini ya mwongozo wa Baba na Mwana, Yohana Mbatizaji aliyefufuka alirejesha, mnamo 1829, mamlaka ya ubatizo kwa kuzamishwa majini kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Katika mwaka huo huo, watatu kati ya Mitume wa mwanzo—Petro, Yakobo na Yohana—walirejesha utume na nyongeza ya mamlaka na funguo za ukuhani.

Miaka sita baada ya kuanzishwa kwa Kanisa, Musa, Elia na Eliya walikabidhi kwa Joseph ndani ya Hekalu la Kirtland mamlaka muhimu ya ziada ili kukamilisha kazi ya Mungu katika siku za mwisho.

Musa alikabidhi funguo za kuikusanya Israeli.

Elia alikabidhi kipindi cha maongozi ya injili ya Ibrahimu ikijumuisha urejesho wa agano la Ibrahimu.

Eliya alikabidhi funguo za nguvu ya kuunganisha, akitoa mamlaka ambayo yanaruhusu ibada zinazofanyika duniani kufungwa milele yote, kama vile kuunganisha familia pamoja kwenye uhusiano wa milele ambao unaendelea kupita kifo.

Kanisa la Yesu Kristo Linaanzishwa

Wakati Joseph Smith akitafsiri Kitabu cha Mormoni alipokea funuo zikionyesha kwamba Kanisa la Yesu Kristo litaanzishwa upya. Lakini Bwana alimuelekeza Joseph asilianzishe Kanisa Lake mara moja. Badala yake, “kwa roho ya unabii na ufunuo” Bwana alifunua kwa Joseph “siku maalum … ambayo [yeye] angetakiwa kuanzisha Kanisa Lake kwa mara nyingine [tena] duniani.”

Kanisa lilianzishwa katika mlolongo sahihi baada tu ya urejesho wa ukuhani na kuchapishwa kwa Kitabu cha Mormoni. Nakala za kwanza za Kitabu cha Mormoni zilipatikana mnamo Machi 26, 1830 na Kanisa lilianzishwa rasmi mnamo Aprili 6.

Mwokozi Yesu Kristo.

“Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni Kanisa la Kristo la Agano Jipya lililorejeshwa. Kanisa linajikita katika maisha makamilifu ya jiwe lake kuu la pembeni, Yesu Kristo, na katika Upatanisho Wake usio na mwisho na Ufufuko wake halisi. Yesu Kristo kwa mara nyingine tena amewaita Mitume na amewapa mamlaka ya ukuhani. Anatualika sote kwenda Kwake na Kanisa Lake, ili kumpokea Roho Mtakatifu, ibada za wokovu, na kupata shangwe ya kudumu.”

Kipindi cha Maongozi ya Mungu cha Utimilifu wa Nyakati

Kutokea huku kwa Baba na Mwana kwa Joseph Smith, tafsiri na ujio wa Kitabu cha Mormoni na urejesho wa mamlaka na funguo za ukuhani vilikuwa vitu muhimu vilivyopaswa kutangulia kabla ya uanzishwaji wa Kanisa la Bwana lililorejeshwa miaka 195 iliyopita siku kama ya leo.

Katika agano la kale, nabii Danieli alitoa tafsiri ya ndoto kuhusu jiwe ambalo lingechongwa bila kazi ya mikono kutoka mlimani na kuijaza dunia yote. Mwaka mmoja baada ya kuanzishwa kwa Kanisa, Bwana alimuelekeza Joseph Smith kwamba funguo za ufalme wa Mungu zilikuwa tena “zimetolewa kwa mwanadamu duniani” na “injili [ya Yesu Kristo ingesonga] mbele mpaka miisho ya dunia, kama jiwe ambalo limechongwa bila kazi ya mikono kutoka mlimani.”

Bwana anatimiza ahadi Yake. Kanisa la Mwokozi lililorejeshwa linaendelea kuanzishwa kote ulimwenguni na ni chombo ambacho Mungu “atavikusanya kwake vitu vyote katika Kristo, vyote ambavyo viko mbinguni na vilivyoko duniani.”

Kazi ya Bwana katika siku za mwisho “ni jukumu ambalo limewavutia watu wa Mungu kwenye kila enzi; ni dhima ambayo kwayo manabii, makuhani na wafalme wamestaajabia; wametazamia kwa matamanio ya shangwe kwenye siku ambayo sisi tunaishi; na wakiwa na shauku ya kimbungu na matarjio ya furaha wameimba na kuandika na kutoa unabii wa hii siku yetu.”

Katika kipindi hiki kikuu na cha mwisho cha injili, “muunganiko wa vyote na mtimilifu na muunganiko wa pamoja wa nyakati, funguo na nguvu na utukufu utafanyika na kufunuliwa kutoka siku za Adamu hadi katika wakati huu uliopo. Na si hili tu, lakini vitu vile ambavyo havikuwahi kufunuliwa tangu kuwepo misingi ya dunia … vitafunuliwa … katika kipindi hiki cha utimilifu wa injili.”

Nabii Joseph alifafanua zaidi, “Ibada zote na majukumu ambavyo vimekuwa vikitakiwa katika Ukuhani, chini ya maelekezo na amri za Mtukufu katika kipindi chochote cha injili, vitakuwepo katika nyakati za mwisho za utimilifu wa injili … vikileta kuwezekana kwa urejesho uliozungumziwa kwa midomo ya Mababii Watakatifu wote.”

Ahadi na Ushuhuda

Nimejaribu kufanya ufupisho wa sehemu za mambo ambayo ni ya muhimu sana na ya kitukufu “habari njema” mtu yoyote mahali popote ulimwenguni anaweza kupokea—ujumbe kwamba Bwana Yesu Kristo amerejesha injili na Kanisa Lake katika siku za mwisho.

Nina waalika nyote kujifunza kuhusu na kuthibitisha ujumbe huu. Ninaahidi kwamba watu “wanaojifunza kwa dhati ujumbe wa Urejesho na kutenda kwa imani watabarikiwa [kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu] kupata ushuhuda wao wenyewe wa utukufu wake na wa dhumuni lake la kuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili ulioahidiwa wa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo.” Unaposali kwa dhati kwa mategemeo ya vyote, kupokea na kutenda kulingana na jibu kutoka kwa Mungu, kama alivyofanya kijana Joseph Smith, uwezo wako wa kutambua na kuitikia ushuhuda huo wa kiungu utaongezeka.

Ninatoa ushahidi kwamba Mungu Baba wa Milele ni Baba yetu. Ninashuhudia na kutoa ushahidi kwamba Yesu Kristo ni Mwana Mpendwa wa Baba na Mwana Wake wa Pekee katika mwili. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu.

Kwa shangwe ninatoa ushahidi kwamba Baba na Mwana walimtokea mvulana Joseph Smith, na hivyo kuanzisha Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika siku za mwisho. Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo na kina maneno ya Mungu. Mamlaka ya ukuhani ili kumwakilisha Mwokozi na kutenda katika jina Lake yapo tena duniani. Na kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni lile Kanisa la Kristo la Agano Jipya lililorejeshwa. Ninatoa ushahidi wangu wa uhakika kwamba vitu hivi vyote ni vya kweli katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.