Mkutano Mkuu
Mfumo Wetu wa Mwongozo wa Mbinguni
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


10:48

Mfumo wa Wetu wa Mwongozo wa Mbinguni

Tunapofokasi maisha yetu kwa Yesu Kristo, tutapata njia ya kurejea nyumbani, kuvumilia hadi mwisho na kushangilia hadi mwisho.

Yesu Kristo alibadilisha maisha yangu nilipobatizwa nikiwa na miaka 26 katika jiji langu pendwa la Frutillar, Chile. Wakati huo, kazi yangu ilinifanya kuvuka bahari, mito na maziwa ya Patagonia nzuri ya Kichile. Baada ya ubatizo wangu, niliona kazi yangu na maisha yangu katika njia mpya na tofauti, nikitambua kwa dhati kwamba “vitu vyote vinaonyesha kwamba kuna Mungu.”

Kwa asili, samoni huzaliwa katika vyanzo vya mito. Kuna wakati katika maisha yao, wanahitaji kuogelea kufuata mkondo wa mto kuifikia bahari, ambapo hupata malisho na hali muhimu kwa ajili ya maendeleo yao.

Lakini bahari pia ni mahali hatari ambapo wanyama wawindaji huvizia na ambapo wavuvi hujaribu kukamata samoni kwa ndoano za kulaghai mfano wa chakula lakini haziwalishi. Kama watastahimili vitisho hivi, watakuwa tayari kutumia mfumo wao imara wa mwongozo kurejea juu kinyume na mkondo wa mto sehemu ile ile walipozaliwa, kukabiliana na changamoto mpya na baadhi zinazofahamika. Wanasayansi wamejifunza tabia zao za kuhama kwa miaka mingi na wamegundua kwamba wanatumia aina fulani ya ramani yenye sumaku, inayofanana na GPS, kuwaongoza kwenye eneo lao kwa ufasaha wa hali ya juu.

Sote tunaweza kurejea siku moja kwenye makao ya mbinguni mahali tulikotoka. Na kama samoni, tuna ramani yetu yenye sumaku, au Nuru ya Kristo, kutuongoza huko. Yesu aliwafundisha wanafunzi Wake, “Mimi ndimi njia, kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”

Tunapofokasi maisha yetu kwa Yesu Kristo, tutapata njia ya kurejea nyumbani, kuvumilia hadi mwisho na kushangilia hadi mwisho. Rais Nelson alifundisha kwamba “shangwe tunayohisi haichangiwi kwa kiasi kikubwa na mazingira ya maisha yetu na kila kitu kinachohusiana na fokasi ya maisha yetu.”

Asili na Majaaliwa Yetu ya Kiungu

Kutoka kwenye tangazo la familia tunasoma kwamba “kila mmoja [wetu] ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni, na, kwa hivyo, kila mmoja ana asili na majaaliwa ya kiungu. … Katika maisha ya kabla ya duniani, wana na mabinti wa kiroho walimjua na kumwabudu Mungu kama Baba yao wa Milele na kukubali mpango Wake ambao ungewezesha watoto Wake kupokea mwili na kupata uzoefu wa kidunia ili kukua kwa ukamilifu na hatimaye kutambua majaaliwa yao ya kiungu kama warithi wa uzima wa milele.”

Kabla ya kuzaliwa Kwake hapa duniani, Yesu Kristo alimtokea Musa na kuongea naye kwa niaba ya Baba. Yeye alimwambia Musa kwamba Yeye alikuwa na kazi kubwa ya yeye kufanya. Wakati wa kikao hicho, Bwana alimwita Musa “mwanangu” mara kadhaa.

Baada ya tukio hilo, Shetani alikuja kumjaribu, akisema “Musa, mwana wa mtu, niabudu mimi.”

Musa alijibu jaribu hilo kwa kukumbuka asili yake ya kiungu, kwa kusema, “Wewe ni nani? Tazama, mimi ni mwana wa Mungu.” Ukweli ulimweka Musa huru dhidi ya mashambulizi ya adui.

Akina kaka na akina dada, ndoano za maisha haya zipo kweli. Mara kwa mara hushawishi, lakini hutafuta lengo moja tu: kutuondoa katika njia ya maji hai yanayoongoza kwa Baba na uzima wa milele.

Ninajua jinsi ndoano za maisha zinavyoweza kuwa. Jumapili moja, kama mwongofu mpya, nilikuwa nafundisha darasa la ukuhani wakati mazungumzo yenye vurugu yalipoibuka. Nilihangaika kukamilisha somo langu. Nilikasirishwa na kuhisi kukosewa. Bila kusema neno, nilielekea mlango wa kutokea nikiwa na wazo kwamba nisingerejea kanisani kwa muda fulani.

Kwa wakati huo huo, kuhani mwenye kujali alisimama mbele yangu. Kwa upendo alinialika nifokasi kwa Kristo na sio kwenye tukio lililotokea darasani. Nikitafakari kuhusu tukio hili pamoja naye, alishiriki pamoja nami kwamba alisikia sauti ikimwambia, “Mfuate, yeye ni wa muhimu kwangu.”

Mzee Vargas na kiongozi aliyemfuata.

Marafiki zangu wapendwa, sisi sote ni wa muhimu Kwake. Rais Nelson alifundisha kwamba “Kwa sababu ya agano letu pamoja na Mungu, Yeye kamwe hatachoka katika juhudi Zake za kutusaidia, na kamwe hatuwezi kumaliza subira Yake ya rehema kwetu.” Asili yetu ya kiungu na uhusiano wa agano pamoja na Mungu hutufanya tuwe na haki ya kupokea msaada wa kiungu.

Hitaji la Virutubisho

Kama vile samaki samoni anavyohitaji kurutubishwa katika bahari ili kukua, nasi pia tunahitaji kujirutubisha wenyewe kiroho ili kuepuka kifo kitokanacho na utapiamlo wa kiroho. Sala, maandiko, hekalu na mahudhurio yetu ya mara kwa mara ya mikutano ya Jumapili ni vya msingi katika menyu yetu ya kiroho.

Mnamo Novemba 1956, Ricardo Garcia aliingia kwenye maji ya ubatizo huko Chile, na kuwa muumini wa kwanza wa Kanisa katika nchi yangu. Siku moja kabla ya kufariki, alitamka kwa familia yake na marafiki, “Miaka mingi iliyopita, wamisionari walinialika niwe na furaha pamoja na familia yangu. Mimi ni mtu mwenye furaha. Mwambie kila mtu katika Chile injili ni furaha.”

Baada ya kurutubishwa na injili ya Yesu Kristo, Ricardo aliweka wakfu maisha yake yote katika kumtumikia Mungu na jirani yake kwa upendo. Mfano wake wa uanafunzi umebariki vizazi vingi, ikijumuisha mimi. Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba “mtu aliyejaa upendo wa Mungu, hatosheki na baraka za familia yake pekee, bali huenda ulimwenguni kote, akijitahidi kubariki jamii yote ya binadamu.”

Kurudi Nyumbani Kwetu Mbinguni

Ndani kabisa ya kila mmoja wetu ni hamu ya kurejea nyumbani kwetu mbinguni, na Yesu Kristo ndiye mfumo wetu wa mwongozo wa mbinguni. Yeye ni njia. Dhabihu Yake ya kulipia dhambi hufanya iwezekane kwetu sisi kufanya maagano matakatifu pamoja na Mungu. Tunapofanya maagano, wakati mwingine tutajikuta tukiogelea kinyume na mkondo wa maji. Hatari, kuvunjwa moyo, majaribu na mateso vitaijaribu imani yetu na uimara wetu wa kiroho. Omba msaada. Yesu Kristo anaelewa na daima ana shauku ya kushiriki mizigo yetu.

Kumbuka kwamba Yeye anajulikana kama “mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko.” Mwokozi alifundisha, “Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Dhabihu yake ya kulipia dhambi huruhusu dhambi zetu kusamehewa kwa kiwango ambacho Yeye hazikumbuki tena.

Yawezekana tusizisahau dhambi zetu kabisa kama sehemu yetu ya kujifunza hapa duniani ili tukumbuke kutokuzirudia tena. Badala yake, tutamkumbuka Yeye tunaposhiriki sakramenti kanisani kila Jumapili. Ibada hii ni sehemu muhimu ya kuabudu na ukuaji wa kiroho. Shangwe huja pale tunapoelewa kwamba hii sio tu siku nyingine. “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu,” ikiwa na nia ya kutupatia mapumziko kutoka ulimwenguni na kufanya upya miili na roho zetu.

Pia tunamkumbuka Yeye pale tunapokwenda hekaluni—nyumba ya Bwana. Hekalu hutupatia uelewa wa kina juu ya Yesu Kristo kama kitovu cha agano ambacho huongoza hadi kwenye uzima wa milele, ambayo ni “zawadi kuu … zawadi zote za Mungu.”

Kuhudhuria hekaluni kumenipa faraja na tumaini kuu kuhusu hatima ya milele. Nimepitia uzoefu wa muunganiko wa kimbingu pamoja na watu wa pande zote mbili za pazia. Nimeona miujiza ya uponyaji katika maisha ya watoto wangu wadogo, wawili kati yao wanaishi na ugonjwa usiojulikana unaohitaji matunzo ya kila siku kwa maisha yote yaliyobakia.

Familia yetu hushangilia tunaposhiriki kuhusu mpango wa furaha. Watoto wangu wanafurahia wanaposikia, kwamba kwa shukrani kwa Yesu Kristo, “mateso [yao] yatakuwa kwa muda mfupi.” Tunawapenda watoto wetu kwa dhati, na tunajua kwamba siku moja, kama Rais Jeffrey R. Holland alivyofundisha, “watasimama mbele yetu wakiwa wametukuzwa na kupendeza, wakamilifu kimwili na kiakili.” Maagano yetu hutuleta karibu na Mungu kwa kiwango cha kufanya yasiyowezekana yawezekane, kwa kujaza kila sehemu yenye giza na wasiwasi kwa nuru na amani.

Shukrani kwa Yesu Kristo, kuna tumaini na sababu nzuri za kuendelea kupenda, kusali na kuwasaidia wale tunaowajali.

Ninajua Yeye yu hai. Yeye anatujua na Yeye anatupenda. Yeye ni njia, kweli na uzima wa ulimwengu.

Ninawaalika sisi sote hivi leo kukita maisha yetu kwa Yesu Kristo na mafundisho Yake. Kwa kufanya hivyo kutatusaidia kuepuka kumeza ndoano za majaribu, chuki na kujihurumia. Tutasimama kama mahekalu—watakatifu, imara na madhubuti. Tutapambana na tufani, na tutafika nyumbani, tukivumilia hadi mwisho na kushangilia hadi mwisho. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Nilifanya kazi kama mwandisi kwa zaidi ya miaka 20 nikikuza kilimo cha ndani ya maji huko Chile.

  2. Alma 30:44

  3. Ona Steve Lundeberg, “Magnetic Pulses Alter Salmon’s Orientation, Suggesting They Navigate via Magnetite in Their Tissue,” Oregon State University Newsroom, May 2, 2020, oregonstate.edu.

  4. Yohana 14:6.

  5. Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona,, Nov. 2016, 82.

  6. Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Maktaba ya Injili.

  7. Ona Musa 1:4–13.

  8. Russell M. Nelson, “Agano Lisilo na Mwisho,” Liahona, Okt. 2022, 6.

  9. Ona Dallin H. Oaks, “Nourishing the Spirit,” Ensign, Dec. 1998, 6–13; Liahona, Aug. 2001, 10–19.

  10. Ona Trent Toone, “Builders and Blessings: How Early Latter-day Saint Pioneers Shaped the Growth of the Church in Chile,” Church News, Feb. 18, 2025, thechurchnews.com.

  11. Usaili binafsi pamoja na Perla García, binti wa Ricardo García.

  12. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 426.

  13. Isaya 53:3.

  14. Yohana 16:33.

  15. Ona Mafundisho na Maagano 58:42.

  16. Ona Neil L. Andersen, “Repent … That I May Heal You,” Liahona, Nov. 2009, 40–43.

  17. Ona Mada na Maswali, “Sakramenti,” Gospel Library.

  18. Marko 2:27.

  19. Ona Russell M. Nelson, “Agano Lisilo na Mwisho,” 4–11.

  20. Mafundisho na Maagano 14:7.

  21. Mafundisho na Maagano 121:7.

  22. Jeffrey R. Holland, “Kama Chombo Kilichovunjika,” Liahona, Nov. 2013, 42.

  23. Ona Waebrania 3:6.