Mkutano Mkuu
Kama Mtoto Mdogo
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


15:9

Kama Mtoto Mdogo

Ninashuhudia kwamba watoto wachanga na watoto na vijana ni sura ya ufalme wa Mungu ikinawiri duniani katika nguvu zake zote na uzuri.

Yesu alianza mwaka wa mwisho wa maisha Yake duniani kwa mafunzo ya kina kwa Mitume Wake. Kama ujumbe Wake na Kanisa Lake vingepasa kibakia baada yake, vingi vingepaswa kuandikwa katika mioyo ya wanaume hawa 12 wa kawaida ambao walikuwa wamemjua Yeye kwa takribani miezi 24.

Siku moja Yesu alishuhudia mabishano miongoni mwa wale Kumi na Wawili na baadaye akawauliza “Mlishindania nini njiani?” Ni wazi wakiona aibu kwa kubishana kule, “walinyamaza,” kumbukumbu inasema hivyo. Lakini huyu mkuu zaidi ya waalimu wote aliona mawazo ya mioyo yao na kuhisi mwanzo wa ukuaji wa majivuno binafsi. Hivyo “alimuita mtoto mdogo, …

“Na akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka, na kuwa kama watoto wadogo, hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.

“Yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni”

Ikumbukwe kwamba hata kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, mahubiri ya mwisho ya Mfalme Benjamini yalijumuisha maoni muhimu kuhusu unyenyekevu wa mtoto. Yanasema “Mwanadamu wa kawaida ni adui kwa Mungu, … na atakuwa, milele na milele, asipokubali … kuwa mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana, na kuwa kama mtoto, mtiifu, …mnyenyekevu, … wingi wa upendo, …kama vile mtoto [hunyenyekea] kwa baba yake.”

Sasa, ni wazi kuna baadhi ya mienendo ya kitoto ambayo hatuihimizi. Miaka ishirini na tano iliyopita, mjukuu wangu wa miaka mitatu aliuma mkono wa dada yake wa miaka mitano. Mkwe wangu akiwa na watoto usiku huo, kwa hasira alimfundisha bintiye masomo yote ambayo angeweza kufikiria kuhusu msamaha, akihitimisha kwamba kaka yake mdogo pengine hakujua hata jinsi kung’atwa mkono kunakuwaje. Mawazo haya ya baba ambayo hayakuwa yamefikiriwa vizuri yalifanya kazi kwa karibu dakika moja, labda dakika moja na nusu, mpaka kuliposikika sauti kali ya kilio kutoka chumba cha kulala cha watoto ambapo mjukuu wangu wa kike alisema, “Sasa anajua.”

Basi ni kipi ambacho tunapaswa kukiona kwenye maisha ya wadogo? Kilikuwa ni kipi kilichomfanya Kristo Mwenyewe kutokwa machozi katika tukio la kinyeyekevu kwenye Kitabu cha Mormoni? Kilikuwa ni kipi Yesu alikifundisha wakati alipoamuru moto toka mbinguni na malaika wenye kulinda kuwazunguka watoto wale, akiwaamuru wakubwa “kuwatazama watoto [wao] wadogo”?

Hatujui kile kilicholeta haya yote, lakini ninafikiria ilikuwa ni kuhusu usafi na utakatifu wao, unyenyekevu wao wa kuzaliwa nao, na kile ambacho kingeweza kuletwa katika maisha yetu kutokana na hayo.

Kwa nini siku zetu za kukatisha tamaa zilipewa jina na mtu mmoja kama “Ubatili mtupu”? Ni kwa jinsi gani kwamba “mawazo yasiyofaa na kiburi cha watoto wa watu” ni maneno ambayo ni sifa za jengo kubwa na pana ambalo limekufa kiroho katika ono la Lehi? Na Wazoramu, lile kundi ambao waliosali kwa kujitukuza wenyewe? Kuhusu wao Alma alisema, “Tazama, Ee Mungu, [wanaomba] kwako na midomo yao, na bado mioyo yao imezidiwa na kiburi chao … kwa hivi vitu vingine vya ulimwengu.”

Ukilinganisha, je, kuna kingine chochote kizuri zaidi, kisafi zaidi, au kinyenyekevu zaidi kuliko mtoto akisali? Ni kama vile mbingu iko chumbani. Mungu na Kristo kweli wapo, lakini kwa wengine uzoefu huu unaweza kuwa wa kijuuju sana.

Kama Mzee Richard L. Evans alivyonukuu karibia miaka 60 iliyopita: “Wengi wetu tunakiri kuwa Wakristo, na bado sisi … hatumchukulii Yeye kwa uzito mkubwa. … Tunamheshimu Yeye, lakini hatumfuati Yeye. … Tunanukuu maneno Yake, lakini hatuyaishi.” “Tunapendezwa Naye, lakini hatumuabudu.”

Maisha yangekuwa tofauti jinsi gani kama ulimwengu ungemtukuza Yesu zaidi ya kiwango cha kuapa bure mara kwa mara.

Lakini watoto kwa dhati wanampenda Yeye, na upendo huo unaweza kubebwa hata katika mahusiano yao mengine katika maisha yao. Kama sheria, hata katika miaka yao ya uchanga, watoto wanapenda kwa urahisi sana, wanasamehe mara moja na kucheka kwa furaha sana hata moyo katili na mgumu unaweza kuyeyuka.

Basi, orodha inaendelea na kuendelea. Usafi? Kuamini? Ujasiri? Hulka?

Njoo pamoja nami kutazama unyenyekevu mbele ya Mungu ulivyoonyeshwa na rafiki yangu mpendwa mdogo.

Easton Darrin Jolley

Mnamo Januari 5, 2025—siku 91 zilizopita—Easton Darrin Jolley alipata Ukuhani wa Haruni na aliwekwa kuwa shemasi katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Kwa kadiri ya kumbukumbu zake Eston alikuwa ametamani kupitisha sakramenti ya Bwana. Lakini fursa hii takatifu iliendana na hisia za mchafuko wa tumbo za woga kwamba angeshindwa, kwamba angeanguka, kwamba atataniwa au kuleta fedheha kwake na kwa familia yake.

Easton ana ugonjwa adimu na wenye kumsumbua.

Sasa, Easton ana ugonjwa adimu na wenye kumsumbua, Ullrich congenital muscular dystrophy. Umeendelea kujaza maisha ya utoto wake kwa changamoto za kuleta woga wakati ukizima matumaini na ndoto zake za siku zijazo. Muda si mrefu angekuwa daima kwenye kiti mwendo. Familia yake haizungumzii kuhusu nini kitafuata kwake baada ya hapo.

Jumapili baada ya utawazo wake, Easton angepitisha sakramenti kwa mara ya kwanza. Na msukumo wake binafsi ulikuwa ni kwamba angeweza kutoa ishara hizi takatifu kwa baba yake, ambaye alikuwa ni askofu wa kata. Katika kutarajia jukumu alilotamani na kuliomba, akilia na kusihi, ilitoa uhakikisho kwamba hakuna yeyote, yeyote, ambaye angejaribu kumsaidia. Kutokana na sababu nyingi, za kibinafsi, alihitaji kufanya hili mwenyewe na bila usaidizi.

Baada ya kuhani kumega mkate na kuubariki—ishara inayowakilisha mwili uliovunjwa wa Kristo—Easton, kwa mwili wake uliodhoofika, alichechemea kupokea trei yake. Hata hivyo, kulikuwa na ngazi tatu kubwa kiasi kutoka sehemu ya watu kukaa hadi kwenye sehemu ya viongozi wanapokaa. Hivyo, baada ya kupokea trei yake, alijinyoosha kwa kadiri alivyoweza na kuiweka trei juu ya sehemu ya kushikwa kwa mikono ya ngazi. Kisha, alikaa kwenye moja ya ngazi ya juu, kwa mikono yake miwili alivuta mguu wake wa kulia kufikia ngazi ya kwanza. Kisha alivuta mguu wake wa kushoto kufikia ngazi ile ile, na kuendelea kwa namna ile mpaka, kwa juhudi hizo kuu, aliweza kufika kwenye kilele cha Mlima wake binafsi wa Everest wa ngazi tatu.

Kisha alitafuta njia yake mpaka kwenye mhimili wa sehemu ya ngazi ya kushikwa kwa mkono ambapo angetumia kusimamia. Akaiendea trei yake. Baada ya hatua chache za ziada alisimama mbele ya askofu, baba yake ambaye machozi yalilowanisha macho yake na kufurika usoni mwake, ilibidi ajizuie kumpa kumbatio mwana huyu mkamilifu mwenye ujasiri na mwaminifu. Na Easton, kwa ahueni na tabasamu pana usoni mwake, angeweza pia kusema, “Nimemtukuza [baba yangu na] nimeimaliza kazi ile [aliyonipa] niifanye.”

Imani, uadilifu, usafi, utii, heshima na, hatimaye upendo kwa kile ambacho baba anatamani kiwe. Hivi na dazeni ya sifa zingine hutufanya sisi pia kusema, “Yeyote … ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.”

Akina dada na akina kaka na marafiki, kilicho juu zaidi kwenye orodha ya mtazamo mzuri niujuao ni watoto wachanga na wadogo na vijana wenye sifa kama zile nilizoelezea leo. Ninashuhudia kwamba wao ni sura ya ufalme wa Mungu duniani wakistawi katika nguvu zake zote na uzuri.

Katika Roho hiyo hiyo ya ushuhuda, ninatoa ushahidi kwamba katika ujana wake, Joseph Smith aliona kile alichosema aliona na kuzungumza na wale aliosema alizungumza nao. Ninashuhudia kwamba Russell M. Nelson ameitwa na Mungu na ni nabii mwenye kipawa na mwonaji. Nikitokea katika maisha ya kusoma kila mara, ninatoa ushahidi kwamba Kitabu cha Mormoni ni kitabu cha thamani kuliko vyote ambavyo nimewahi kusoma na ni jiwe la kati la teo la makazi yangu madogo katika ufalme wa nyumba nyingi. Ninatoa ushahidi kwamba ukuhani na sala zinarejesha maisha yangu—ukuhani wa Kristo na sala zenu. Ninajua yote haya kuwa ni ya kweli na ninatoa ushuhuda juu ya hili katika jina la yule aliye mwaminifu na mnyenyekevu kuliko wana wote wa Mungu—Alfa na Omega, Mimi Ndiye, aliyesulubiwa, shahidi mwaminifu—hata Bwana Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Marko 9:33.

  2. Marko 9:34.

  3. Ona Luka 9:47.

  4. Mathayo 18:2–4.

  5. Mosia 3:19.

  6. 3 Nefi 17:23; ona pia mstari wa 11–24

  7. Mhubiri 1:2

  8. 1 Nefi 12:18.

  9. Alma 31:27

  10. James W. Clarke, quoted in Richard L. Evans, in Conference Report, Apr. 1965, 136. Elder Evans notes that this quotation came from a radio sermon given by Dr. James W. Clarke, which was quoted by William H. Danforth.

  11. Clarke, in Richard L. Evans, in Conference Report, Apr. 1965, 136.

  12. Yohana 17:4. Tukio binafsi lililoshirikiwa na Brian na Charisa Jolley kwa Jeffrey R. Holland, Januari 2025.

  13. Mathayo 18:4.

  14. Ona Ufunuo 1:5.