Kukamilishwa Kiroho katika Yeye
Kukamilishwa si lazima kumaanishe urejesho kimwili na kihisia katika maisha haya. kukamilishwa ni tunda la imani katika Yesu Kristo na uongofu kwa Yesu Kristo.
Wenye ukoma 10 walipaza sauti kwa mwokozi “Turehemu.” Na Yesu Kristo alifanya hivyo. Yeye aliwaambia wakajionyeshe kwa kuhani, na, wakati wakienda zao, walitakaswa ugonjwa wao.
Na mmoja wao, alipoona kwamba amepona, alipaza sauti kumtukuza Mungu. Alirudi kwa Mwokozi, akaanguka miguuni pake na kutoa shukrani.
Na Mwokozi alimwambia yule aliyeshukuru “Imani yako imekuponya.”
Yesu Kristo alikuwa amewaponya wenye ukoma kumi. Lakini mmoja, aliyerudi kwa Mwokozi, alipokea kitu cha ziada. Alikamilishwa.
Wenye ukoma tisa walikuwa wameponywa kimwili.
Mmoja alikuwa ameponywa kimwili na kukamilishwa kiroho.
Katika kutafakari hadithi hii, nimejiuliza kama kinyume chake ni kweli. Kama uponyaji na kukamilishwa ni vitu tofauti, je mtu anaweza kukamilishwa kiroho kupitia Yeye, lakini bado kutoponywa kimwili na kihisia?
Mponyaji mkuu ataponya magonjwa yetu yote—ya kimwili na kihisia—kwa kadiri ya muda Wake. Lakini katika kusubiri uponyaji, je, mtu anaweza kukamilishwa?
Inaamanisha nini kukamilishwa kiroho?
Tunakamilishwa katika Yesu Kristo wakati tunapotumia haki yetu ya kujiamulia ili kumfuata Yeye katika imani, kunyenyekeza mioyo yetu Kwake ili kwamba aweze kuibadilisha, kushika amri Zake na kuingia kwenye uhusiano wa kimaagano pamoja Naye, kwa unyenyekevu tukivumilia na kujifunza kutokana na changamoto za maisha haya ya duniani mpaka pale tutakaporudi kwenye uwepo Wake na kuponywa kwa kila namna. Ninaweza kukamilishwa, wakati nikisubiri uponyaji ikiwa uhusiano wangu na Yeye ni wa dhati.
Imani katika Yesu Kristo huzaa tumaini. Ninapata tumaini katika kujaribu kukamilishwa—kukamilishwa kupitia imani katika Yesu Kristo. Imani katika Yeye huongeza tumaini langu kwa ajili ya uponyaji, na tumaini hilo huimarisha imani yangu katika Yesu Kristo. Ni mzunguko imara.
Bwana alimwambia Enoshi imani yake ilimfanya “mkamilifu” kukamilishwa kulikuja wakati Enoshi alipotafakari maneno ya nabii Yakobo baba yake wakati akitamani kuelewa fursa kwa ajili ya uzima wa milele, wakati alipomlilia Mungu katika sala kuu. Na katika hali hiyo ya kutamani na unyenyekevu, sauti ya Bwana ilimjia, ikitangaza kuwa dhambi zake zilikuwa zimesamehewa. Na Enoshi alimuuliza Bwana, “je, inawezekanaje? Na Bwana alijibu: “Kwa sababu ya imani yako katika Kristo, … imani yako imekufanya mkamilifu.”
Kupitia imani zetu kwa Yesu Kristo, tunaweza kutafuta kukamilishwa kiroho wakati tukisubiri na kutumaini kwa ajili ya uponyaji wa kimwili na kihisia.
Kwa wema wa dhabihu ya upatanisho Wake, na wakati tunapotubu kwa dhati, Mwokozi hutuponya kutokana na dhambi, kama ilivyokuwa kwa Enoshi. Upatanisho Wake usio na mwisho pia huzifikia taabu na huzuni zetu.
Lakini Anaweza asitoe uponyaji kutokana na magonjwa —maumivu makali, kutokuwa na kinga ya kutosha kama vile matatizo ya kukakamaa kwa misuli ya mwili, saratani, woga, msongo wa mawazo na mengine kama hayo. Uponyaji wa namna hiyo ni kulingana na ratiba ya Bwana. Na kwa sasa, tunaweza kuchagua kukamilishwa kupitia kutumia imani Kwake!
Kukamilishwa kunamaanisha kuwa kamili na kujazwa. Kama vile wanawali watano wenye busara ambao walikuwa na taa zao zilizojaa mafuta wakati bwana harusi alipokuja, tunaweza kukamilishwa kupitia Yesu Kristo wakati tunapojaza taa zetu kwa mafuta ya kustawisha ya uongofu Kwake. Katika njia hiyo, tunaandaliwa kiishara kwa ajili ya chakula cha karamu ya harusi, ujio Wake wa Pili.
Katika mfano wanawali wote kumi walikuwa katika sehemu sahihi, wakimsubiri bwana harusi. Kila mmoja wao alikuja na taa.
Lakini Bwana harusi alipokuja, katika usiku wa manane usiotarajiwa, watano wapumbavu hawakuwa na mafuta ya kutosha kwenye taa zao. Hawakuelezewa kama waovu bali kama wapumbavu. Wapumbavu walishindwa kujiandaa vya kutosha kuweka taa zao zikiwaka kwa mafuta ya uongofu.
Na hivyo, katika kujibu ombi lao la kuruhusiwa kuingia kwenye karamu ya harusi, bwana harusi alijibu, “Hamkunijua.”
Ikimaanisha, kwa wakati ule, kwamba wanawali watano wenye busara walimjua Yeye. Walikamilishwa katika Yeye.
Taa zao zilikuwa zimejaa mafuta ya thamani ya uongofu, ambayo yaliwaruhusu wanawali wenye busara kuingia kwenye karamu ya harusi kwenye mkono wa kuume wa bwana harusi.
Kama ilivyoelezwa na Mwokozi, “Kuweni waaminifu, na mkisali daima, mkitengeneza na kuziwasha taa zenu, mkiwa pamoja na mafuta yake, ili kwamba muweze kuwa tayari Bwana harusi ajapo”
Wanawali Watano Wenye Busara, na Ben Hammond
Sanamu ya kupendeza ikielezea wanawali watano wenye busara hivi karibuni iliwekwa huko Temple Square nje ya malango ya Jengo la Muungano wa Usaidizi na kwenye kivuli cha Hekalu la Salt Lake.
Ni kwenye eneo linalofaa kuonyesha matumizi ya mfano huo. Kwa sababu wakati tunapofanya na kushika maagano, hasa yale yanayopatikana kwenye nyumba ya Bwana, tunajaza taa zetu kwa mafuta ya uongofu.
Wakati wanawake waliowakilishwa kama wanawali watano wenye busara hawashiriki mafuta ya uongofu wao, wanashiriki nuru yao wakati wanapoinua taa zao, ambazo zimejaa mafuta na zinawaka kwa uangavu. Kwa umuhimu wanaelezewa kuwa wanasaidiana—bega kwa bega, wakikumbatiana na kutazamana usoni.
Bila shaka, “[Sisi] ni nuru ya ulimwengu.” Mwokozi alitangaza:
“Ninawapa ninyi muwe nuru ya watu hawa. Mji uliojengwa kwenye kilima hauwezi kufichwa.
“… Je, [sisi] tunawasha taa na kuiweka chini ya pishi? La, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani;
“Kwa hivyo acha nuru yenu iangaze mbele ya hawa watu, ili wapate kuyaona matendo yenu, na kumtukuza Baba yenu aliye mbinguni.”
Tunaamriwa kushiriki nuru Yake. Basi endeleeni kujaza taa zenu kwa mafuta ya uongofu katika Yesu Kristo na kuweni tayari kuzifanya taa zenu ziwake kwa uangavu. Kisha acheni nuru hiyo iangaze. Wakati tunaposhiriki nuru yetu, tunaleta faraja ya Yesu Kristo kwa wengine, uongofu wetu Kwake unaongezeka kwa kina na tunaweza kukamilishwa hata wakati bado tunasubiri uponyaji. Na tunapoacha nuru yetu iangaze kwa uangavu, tunaweza kuwa na shangwe hata wakati tukisubiri.
Mfano wa maandiko unafaa kuimarisha kanuni kwamba tunaweza kukamilishwa wakati tunapoongoka katika Yesu Kristo na kuvuta nguvu kutoka Kwake, hata wakati tukisubiri uponyaji.
Mtume Paulo alikuwa na aina fulani ya masumbuko—kile alichokielezea kama “mwiba katika mwili,” ambapo mara tatu alikuwa amemsihi Bwana kuuondosha. Na Bwana alimwambia Paulo, “Neema yangu yakutosha: maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.” Ambayo kwayo Paulo alitangaza:
Basi … nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.
Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, … na ufidhuli kwa ajili ya Kristo: maana niwapo dhaifu, ndipo nilipo na nguvu.”
Mfano wa Paulo unapendekeza kwamba hata katika udhaifu wetu, nguvu yetu katika Yesu Kristo inaweza kufanywa kamilifu—hiyo ni kwamba, iliyokamilika. Wale ambao wanasumbuka na changamoto za kidunia na wakamgeukia Mungu kwa imani kama Paulo, wanaweza kupokea baraka za kumfahamu Mungu.
Paulo hakuponywa masumbuko yake, lakini alikamilishwa kiroho katika Yesu Kristo. Na hata katika majaribu yake, nuru ya uongofu wake juu ya, na nguvu kutoka kwa Yesu Kristo iling’ara, na alikuwa na shangwe. Katika waraka wake kwa Wafilipi alisema, “Furahini katika Bwana siku zote: tena nasema, Furahini.”
Akina dada na akina kaka, jibu ni ndio, tunaweza kukamilishwa kiroho, hata wakati tunaposubiri uponyaji wa kimwili na kihisia. Ukamilifu si lazima umaanishe urejesho kimwili na kihisia katika maisha haya. Kukamilishwa ni tunda la imani katika Yesu Kristo na uongofu kwa Yesu Kristo na kuacha nuru ya uongofu huo iangaze.
“Waitwao ni Wengi, bali wachache [huchagua] kuteuliwa.”
Wote wataponywa kimwili na kihisia katika Ufufuko. Lakini je, wewe utachagua sasa kukamillishwa katika Yeye?
Ninatangaza, kwa shangwe kwamba nineongoka katika Bwana Yesu Kristo. Ninajitahidi kukamilishwa katika Yeye. Nina uhakika kwamba vitu vyote vitarejeshwa na uponyaji utakuja, katika ratiba Yake, kwa sababu Yeye yu hai.
Mariamu Magdalena alikuwa mwanamke aliyeponywa na Yesu Kristo. Na alikuwa mwanamke aliyekamilishwa katika Yesu Kristo. Kama mwanafunzi Wake, alikuwa na Mwokozi huko Galilaya na alimhudumia.
Alikuwepo chini ya msalaba, shuhuda wa kifo Chake.
Alikwenda kwenye kaburi Lake kukamilisha maandalizi ya maziko na aligundua kwamba jiwe lilikuwa limeondolewa, kwamba mwili wa Bwana haukuwepo. Mariamu alikuwa kaburini akilia wakati alipoulizwa, kwanza na malaika na kisha na Mwokozi mwenyewe, “Mwanamke kwa nini unalia? Unamtafuta nani?”
Mariamu alilia, “Wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka.”
Na Yesu kwa huruma alimwita kwa jina, “Mariamu.” Na Mariamu alimtambua na kwa unyenyekevu alijibu “Rabi, … Bwana”
Akitoa unabii kuhusu Mwokozi, Isaya alisema “Atameza mauti hata ushindi; na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote.”
Ufufuko Wake uliruhusu machozi ya Mariamu kufutwa. Hakika Yeye atafuta machozi yako pia.
Mariamu alikuwa shahidi wa kwanza wa Mwokozi aliyefufuka. Na alikuwa wa kwanza kushuhudia kwa wengine juu ya kile alichokuwa amekiona.
Kwa unyenyekevu ninaongeza ushuhuda wangu juu ya ule wa Mariamu. Amefufuka. Yesu Kristo yu hai. Hatimaye wote wataponywa, kimwili na kihisia, katika Yeye. Na katika kusubiri uponyaji huo, imani katika Mponyaji Mkuu itatukamilisha kiroho. Katika jina la Yesu Kristo, amina.