Mkutano Mkuu
Upendo Wangu kwa Mwokozi Ndiyo “Kwa Nini” Yangu
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


10:29

Upendo Wangu kwa Mwokozi Ndiyo “Kwa Nini” Yangu

Ninampenda Mwokozi wetu. Hii ndiyo sababu halisi na yenye nguvu zaidi ya kufanya kile ninachokifanya.

Je, umewahi kugundua kwamba nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, mara kwa mara anatoa mialiko kwetu? Si ya kushangaza, ametualika tusome na tutafakari jumbe zilizotolewa kwenye mikutano mikuu miwili iliyopita. Mnamo Aprili 2024, alisema, “Ninatumaini mtajifunza jumbe za mkutano huu katika miezi yote ijayo.” Kisha, mwezi wa Oktoba 2024, alisema: “Ninawahimiza kujifunza jumbe za [wazungumzaji hao]. Zitumieni kama kipimo cha kuamua kipi ni kweli na kipi si kweli kwa miezi sita ijayo.”

Mialiko hii inaweza kuongezwa kwenye mialiko ya kinabii tuliyoipokea katika maisha yetu yote, ikijumuisha na hasa ile tuliyoipokea katika miaka ya hivi karibuni. Tunaweza kuhisi au kudhani mialiko hii ni kitu kingine tunachopaswa kuongeza kwenye orodha zetu za mambo ya kufanya, kwa sababu tulialikwa au kuombwa kufanya jambo. Lakini je, panaweza kuwa na zaidi kwenye hilo?

Nikitafakari juu ya hili na mialiko yote tuliyokuwa tumepokea, nilikumbuka jambo fulani ambalo nilijifunza na kuliamua hapo zamani. Ninajaribu kufanya mambo haya, ambayo ni muhimu kwangu kwa sababu ninampenda Yeye; Ninampenda Mwokozi wetu. Hii ni sababu halisi na yenye nguvu zaidi ya kufanya kile ninachokifanya, na kisha lililounganika na hili ni upendo wangu kwenu, akina kaka wenzangu na dada zangu.

Kama kaka yenu, ninatumaini mtazingatia maneno yangu kama mwaliko wa dhati wa kutafuta kuelewa fursa ya kuunganisha kila jambo tunalolifanya na upendo wetu kwa Mwokozi.

Kufanya hivi kutatusaidia tuelewe “kwa nini” halisi nyuma ya kila jambo tunalolifanya kama wanafunzi wa Mwokozi. Hii itatusaidia kuimarisha muunganiko wetu wa kimaagano na Mungu, kuelewa kweli Zake za kiungu na za milele—kweli Zake za milele na za hakika ambazo hazitabadilika kamwe. Kweli za milele kama vile “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Inafurahisha kwamba nyakati zingine kwa sababu mara nyingi tumefanya mambo hadi kufikia mahali ambapo yamegeuka kuwa desturi, tunaruhusu desturi hizi au shughuli hizi kuamua juhudi zetu za kujenga imani katika Yesu Kristo. Inaonekana kwamba tunafanya mambo haya kwa sababu tumeyafanya kwa miaka mingi, bila kuzingatia matokeo yake kwenye muunganiko wetu wa kimaagano na Mwokozi.

Katika ulimwengu wetu, mara nyingi tunafokasi kwenye kile tunachokifanya na kwenye kutimiza majukumu na malengo. Katika mazingira ya kiroho, tuna fursa ya kwenda zaidi ya kufanya tu mambo au kufikia malengo kwa kuelewa kwa nini tunayafanya hayo Kama tunaweza kuelewa na kuunganisha kwamba sababu iliyo nyuma ya matendo yetu inahusiana na upendo wetu kwa Mwokozi na Baba yetu wa Mbinguni, kwa kutumia vyema fursa hizi tutaelewa kwamba japokuwa kufanya mambo ya haki, kama vile kuwa na shughuli au desturi za Kanisa na kuyafanya kwa usahihi ni jambo jema, tunapoyaunganisha na “kwa nini,” tutabarikiwa kuelewa sababu. Haitakuwa tu kufanya mambo mema au kuyafanya kwa usahihi; tutayafanya pia kwa usahihi.

Kwa mfano, unapoweka lengo la kusoma maandiko, kusali kwa dhati au kuandaa shughuli kwa ajili ya familia yako au kata yako, je, lengo halisi ni kukamilisha tu majukumu haya? Au je, matendo haya ni njia, zana ulizo nazo, ili kufikia lengo la kweli? Je, madhumuni ni kufanya tu shughuli kwa sababu tumefanya hivyo kwa miaka mingi na kisha kuweka alama ya vema kwenye kisanduku kwamba tumeikamilisha? Au, kwa mara nyingine, je, hizi ni njia tunazotumia kujifunza, ili kuhisi na kuunganika na Mwokozi?

Tafadhali usielewe vibaya hoja yangu kuhusu kuwa na shughuli na desturii au kuweka malengo na kufanya kazi kwa bidii ili kuyafikia; hakuna lo lote baya kwenye hili. Hata hivyo, ninawaalika muifungue mioyo na akili zenu kwenye fursa na baraka za kuelewa sababu ya kufanya mambo haya na jinsi tunavyofanyia kazi dini yetu.

Mfano mzuri wa desturi zenye kiini kwa Kristo ni changamoto ambayo Rais Dallin H. Oaks aliitoa kwetu sote kwa niaba ya Urais wa Kwanza. Rais Oaks alisema: “Tunapoingia mwaka huu mpya, na tujiandae kwa sherehe za Pasaka ya dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi. … Bila kujali kile wengine wanachoamini na kufanya, tunapaswa kusherehekea Ufufuko wa Mwokozi wetu aliye hai kwa kujifunza mafundisho Yake na kusaidia kukuza tamaduni za Pasaka katika jumuiya zetu kwa ujumla, hususani ndani ya familia zetu wenyewe.” Kama mnavyoona, si tu mwaliko wa kuwa na desturi. Badala yake, tunatumia desturi hizi kama njia za kujifunza zaidi kumhusu Mwokozi na kukumbuka Ufufuko Wake.

Tunapounganisha zaidi sababu na upendo wetu kwa Mwokozi, ndivyo zaidi tutakavyoweza kupokea kile tunachokihitaji au tunachokitafuta. Rais Nelson alisema, “Maswali au shida zo zote mlizonazo, jibu daima linapatikana katika maisha na mafundisho ya Yesu Kristo.” Na kisha akatoa mwaliko huu: “Jifunzeni zaidi kuhusu Upatanisho Wake, upendo Wake, rehema Yake, mafundisho Yake na injili Yake iliyorejeshwa ya uponyaji na upigaji hatua. Mgeukieni Yeye! Mfuateni Yeye!”

Tafakarini hili mioyoni mwenu na akilini mwenu: Je, mnaamini mwaliko wa Rais Nelson ulikuwa na kusudi la kutusaidia kuandaa orodha ya kuweka alama ya vema ambapo tungekusanya ufahamu zaidi na kukamilisha majukumu ili sisi tutie alama ya vyema kwenye orodha yetu ya vitu vya kufanya? Au je, anatualika tuzingatie vipengele vya kweli hizi za milele na kanuni kama fursa ya kuelewa ile “kwa nini” na kuunganisha upendo wa kimaagano wa Mwokozi kwetu na safari ya maisha yote ya uanafunzi wetu?

Acha nifafanue kanuni ambayo ninajaribu kuielezea. Namna moja, ambayo inawezakana kuzidi kiasi, ingekuwa kusoma jumbe zote kutoka kwa mkutano mkuu mara moja kisha ninapomaliza, nitawekea alama ya vema mwaliko huu kwenye orodha yangu ya mambo ya kufanya bila kufanya jambo lingine lo lote kwenye kile nilichokisoma. Ninaelewa hili ni suala kubwa, lakini ni halisi Pengine, wengi wako sehemu fulani katikati ya hili na lile lililo bora.

Mwaliko ni kusoma na kutafakari jumbe kutoka mkutano mkuu na kuzitumia kuamua na kuelewa kile kila mmoja wetu anachoweza kufanya ili kuwa bora.

Tunapokubali mwaliko, tukielewa “kwa nini” ya mwaliko huo, tutakuwa na fursa zaidi za kuwa karibu zaidi na Mwokozi. Tunapoanza kuelewa kwamba kwa sababu ninampenda Mwokozi, ninataka kujifunza zaidi kumhusu Yeye kwa kujifunza maneno ya manabii walio hai. Na kwa sababu ninawapenda binadamu wenzangu, nitashiriki mafundisho ya manabii, waonaji, na wafunuzi pamoja na wengine, kuanzia na wapendwa wangu.

Katika mifano yote miwili, unafanya jambo la haki. Katika mmoja, lengo linaonekana kuwa linatumia njia ambazo Baba wa Mbinguni na Mwokozi wametupatia, ambazo ni jumbe zilizotolewa wakati wa mkutano mkuu. Toleo la pili linakumbatia baraka kuu ya kupata umaizi kwenye sababu zilizopo, ikitoa njia ya kuelewa ukweli wa milele na baraka zilizoahidiwa kwa wote wanaofanya mafundisho na maisha ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo, kituo cha fokasi ya maisha yao.

Wapendwa akina kaka na akina dada, ninatumaini mtahisi na kuona umuhimu wa kuunganisha matendo yetu na upendo wetu kwa Mwokozi. Katika ulimwengu wenye kuongezeka kwa kimuungano, sauti nyingi zitajaribu kukushawishi na, ikiwezekana, kukuongoza kuamini kwamba baadhi ya kweli za msingi za injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo si muhimu. Sauti hizi zikianza na ukweli muhimu wa hitaji la urejesho katika siku hizi za mwisho, ikijumuisha hitaji la kuwa na ufalme wa Mungu duniani, unaowakilishwa na Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Unaweza kusikia sauti zikisisitiza kwamba uhusiano binafsi au uelewa pekee kwa Mwokozi unatosha na kwamba dini au Kanisa lililorejeshwa si muhimu au sio lazima. Ninawaalika msiwe na haraka ya kuzingatia au hata muwe na kinga ya kushawishiwa na dhana hizi za kupotosha na kuwa wepesi kukumbuka kile ambacho Mwokozi amekuwa akituambia na kutufundisha tangu nyakati za kale—akianza na upendo wa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kwa ajili yetu na kuunganisha upendo wetu Kwao kama sababu ya kuwafuata Wao.

Mungu Baba na Mwanawe walikuja na kuzungumza na Joseph Smith ili kurejesha Kanisa la Kristo na ili kuanzisha kipindi cha utimilifu wa nyakati, Ufalme Wake duniani. Kwa hiyo, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni njia iliyoanzishwa na Baba wa Mbinguni ili kufikia maagano yanayotuwezesha sisi kurejea nyumbani. Hivyo, tunahitaji zaidi ya uhusiano binafsi na Baba wa Mbinguni na Mwana Wake; tunahitaji ibada muhimu za ukuhani ambazo kupitia hizo tunafanya Nao maagano. Hii hutoa muunganiko wa kiagano na Wao na hutupatia ufikiaji kwenye upendo Wao wa kiagano, ikiwezesha upatikanaji wa ufalme wa juu zaidi wa utukufu ulioandaliwa kwa ajili ya wale wote walio wakweli na waaminifu kwenye maagano yao.

Kwa nguvu zote za nafsi yangu, ninatoa ushahidi kwenye uhalisia na uungu wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye anakupenda. Yeye anafahamu kile kinachotokea katika maisha yako. Mikono Yake imenyooshwa, ikitoa mwaliko, “Njooni kwangu, … nami nitawapumzisha.”

Ninampenda Mwokozi, na upendo wangu Kwake ndiyo “kwa nini” yangu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.