Mkutano Mkuu
“Songeni Karibu Nami”
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


17:4

“Songeni Karibu Nami”

Yesu Kristo anampenda kila mmoja wetu. Yeye hutupa fursa ya kumkaribia zaidi.

Wapendwa wangu akina kaka na akina dada, ni shangwe kwangu kuwa pamoja nanyi katika mkutano huu mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Hili ni Kanisa Lake. Tunakusanyika katika majengo na nyumbani kote ulimwenguni katika jina Lake.

Tunajichukulia jina Lake wakati tunaingia katika ufalme Wake kwa agano. Yeye ndiye Mwana wa Mungu aliyefufuka na kutukuka. Sisi ni wanadamu tunaothiriwa na dhambi na kifo. Hata hivyo, katika upendo Wake kwa kila mmoja wetu, anatualika tuje karibu Naye.

Mwokozi akitoka kaburini.

Huu ndio mwaliko Wake kwetu: “ Songeni karibu nami na mimi nitasogea karibu nanyi, nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata, ombeni, nanyi mtapewa, bisheni nanyi mtafunguliwa.”

Kuna nyakati tunahisi kuwa karibu na Mwokozi Yesu Kristo. Na bado, wakati mwingine katika majaribu ya maisha ya duniani, tunahisi kiasi fulani kuwa mbali Naye na kutamani uhakikisho kwamba Yeye anajua kile kilicho moyoni mwetu na kutupenda kama watu binafsi.

Mwaliko wa Mwokozi hujumuisha njia ya kuhisi uhakikisho huo. Songa karibu Naye kwa daima kumkumbuka Yeye. Mtafute kwa bidii kupitia kujifunza maandiko. Omba kwa sala ya dhati kwa Baba wa Mbinguni ili kuhisi ukaribu na Mwana Wake Mpendwa.

Kuna njia rahisi ya kulifikiria hili. Hiki ndicho ambacho ungekifanya kama ungetenganishwa kwa muda kutoka kwa marafiki wa dhati. Ungetafuta njia ya kuzungumza nao, ungethamini ujumbe wowote unaopokea toka kwao, na ungefanya yote uyawezayo ili kuwasaidia.

Kadiri hili linavyotendeka, linavyozidi kuendelea, uhusiano wa kina wa upendo ungeimarishwa, na mngehisi kukaribiana. Kama muda mrefu ungepita bila mawasiliano ya kuthaminiwa na fursa za kusaidiana, muunganiko ungekuwa dhaifu.

Yesu Kristo anampenda kila mmoja wetu. Yeye hutupa fursa ya kumkaribia zaidi. Kama vile rafiki mwenye upendo, utafanya katika njia sawa na hiyo, kwa kuwasiliana kupitia sala na Baba wa Mbinguni katika jina la Yesu Kristo, kusikiliza mwongozo wa thamani kutoka kwa Roho Mtakatifu na kuwatumikia wengine kwa ajili Mwokozi kwa furaha. Punde wewe utahisi ile baraka ya kusogea karibu Yake.

Katika ujana wangu, nilipitia shangwe ya kuwa karibu na Mwokozi—na Yeye kuwa karibu nami—kupitia matendo rahisi ya utiifu wa amri. Nilipokuwa mdogo, sakramenti ilitolewa wakati wa mkutano wa jioni. Bado ninaweza kukumbuka hususani jioni moja, zaidi ya miaka 75 iliyopita, wakati nje pakiwa na giza na baridi. Ninakumbuka hisia ya mwanga na joto nilipotambua kwamba nilikuwa nimeshika amri ya kukutana na Watakatifu kushiriki sakramenti, kuweka maagano na Baba yetu wa Mbinguni ya daima kumkumbuka Mwanawe na kushika amri Zake.

Mwishoni mwa mkutano usiku ule, tuliimba wimbo “Baki Nami; Kumekuchwa,” ikiwa ni pamoja na maneno ya kukumbukwa “Mwokozi, baki nami.”

Maneno haya yalileta kwangu hisia kali toka kwa Roho, na hata katika uvulana wangu. Nilihisi upendo na ukaribu wa Mwokozi jioni ile kupitia faraja ya Roho Mtakatifu.

Miaka mingi baadaye nilitaka kuhisi hisia sawa na zile za upendo na ukaribu wa Mwokozi nilizozihisi Kwake wakati wa mkutano wa sakramenti ujanani mwangu. Hivyo basi nikatii amri nyingine rahisi: Nilipekua maandiko.

Kwenye kitabu cha Luka, nilisoma kuhusu siku ya tatu baada ya Kusulubiwa Kwake na kuzikwa, wakati watumishi waaminifu walipokuja, kutokana na upendo wao kwa Mwokozi, ili kuupaka mwili Wake mafuta. Walipofika, walikuta jiwe limeviringishwa kutoka kaburini na wakaona kwamba mwili Wake haukuwemo kaburini.

Malaika nje ya kaburi alilozikwa Kristo.

Malaika wawili walisimama na kuwauliza ni kwa nini walikuwa wakiogopa:

“Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?

“Hayupo hapa, amefufuka: kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa bado akiwa Galilaya,

“Akisema, imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mkononi mwa wenye dhambi, na kusulubiwa, na kufufuka siku ya tatu”

Yesu na wanafunzi wakiwa njiani kuelekea Emau.

Jioni ile kwenye giza hafifu, wanafunzi wawili walitembea kutoka Yerusalemu kwenda Emau na Bwana aliyefufuka aliwatokea na kutembea nao.

Kitabu cha Luka kinaturuhusu kutembea nao jioni ile:

“Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.

“Macho yao yakafumbwa wasimtambue.”

“Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea na mna huzuni?

“Akijibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliotukia humo siku hizi?”

Walimwambia kuhusu huzuni yao kwamba Yesu alikuwa amekufa wakati walikuwa wameamini kuwa Yeye angekuwa Mkombozi wa Israeli.

Lazima kungekuwa na upendo katika sauti ya Bwana aliyefufuka alipozungumza na wanafunzi hawa wawili wenye huzuni na kuomboleza.

Wakati nilipoendelea kusoma, yalikuja maneno haya ambayo yaliufurahisha moyo wangu, sawa na vile nilivyohisi wakati nikiwa mvulana mdogo:

“Wakakaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele.

“Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.”

Yesu akiwa amekaa na wanafunzi.

Mwokozi alikubali usiku ule mwaliko wa kuingia nyumbani kwa wanafunzi Wake. Aliketi mezani nao. Akachukua mkate, akaubariki, akaumega na kuwapa. “Mara macho yao yakafumbuliwa, na wakamtambua ni yeye. Kisha akapotea kutoka uwepo wao.

Luka alituandikia hisia za wanafunzi hao waliobarikiwa: “Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?”

Wanafunzi hao wawili walikimbia kurudi Yerusalemu na kuwaambia Mitume wale kumi na moja kile kilochokuwa kimetendeka. Wakati wakishiriki uzoefu wao, Mwokozi alitokea tena.

Alisimama katikati yao, “akawaambia, Amani iwe kwenu.” Kisha alirejelea unabii kuhusu kazi Yake ya kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watoto wote wa Baba Yake na kuvunja pingu za kifo.

“Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu:

“Na kwamba mataifa yote yatahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.

“Nanyi ndiye mashahidi wa haya.”

Alma akifundisha karibu na Maji ya Mormoni.

Kama vile kwa wanafunzi wake wapendwa, kila mtoto wa Baba wa Mbinguni ambaye amechagua kuingia kupitia lango la ubatizo yuko kwenye agano la kuwa shahidi wa Mwokozi na kwa maisha yote kuwatunza wale wenye uhitaji. Kujitoa huku kuliwekwa wazi kwetu kupitia Alma, nabii mkuu wa Kitabu cha Mormoni karne nyingi zilizopita kwenye Maji ya Mormoni:

“Kama mnatamani kujiunga na zizi la Mungu, na kuitwa watu wake, na mko radhi kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, ili iwe miepesi;

“Ndiyo, na mko tayari kuomboleza na wale wanaoomboleza; ndiyo, na kufariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa, na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote … ,hata hadi kifo, ili muweze kukombolewa na Mungu, na …, kwamba mpokee uzima wa milele.”

Mnapokuwa wakweli kwenye ahadi hizi, mtagundua kwamba Bwana hutimiza ahadi Zake za kuwa nanyi kwenye huduma yenu, akifanya mizigo yenu kuwa miepesi. Mtakuja kumjua Mwokozi, na baada ya muda mtakuwa kama Yeye na “kukamilishwa kupitia Yeye.” Kwa kuwasaidia wengine kwa ajili ya Mwokozi, mtagundua kwamba mnasonga karibu Naye.

Wengi wenu mnao wapendwa wanaopotea kutoka kwenye njia ya maisha ya milele. Mnajiuliza mnaweza kufanya nini zaidi ili kuwarudisha. Mnaweza kumtegemea Bwana kusonga karibu yao wakati mnapomtumikia Yeye kwa imani.

Unaweza kukumbuka ahadi ya Bwana kwa Joseph Smith na Sidney Rigdon walipokuwa mbali na familia zao katika kazi Yake: “Marafiki zangu Sidney na Joseph, familia zenu ni njema, wako mikononi mwangu, na nitawafanyia nionavyo kuwa ni vyema; kwani ndani yangu kuna uwezo wote.”

Mnapofunga vidonda vya wale wenye uhitaji, nguvu ya Bwana itawasaidia. Mikono Yake itanyooshwa pamoja na ya kwenu kuwakomboa na kuwabariki watoto wa Baba wa Mbinguni.

Kila mtumishi mwenye maagano wa Yesu Kristo atapokea mwongozo Wake kutoka kwa Roho wakati wanapobariki na kutumikia wengine kwa ajili Yake. Kisha wao watahisi upendo wa Mwokozi na kupata shangwe ya kusonga karibu Yake.

Mimi ni shahidi wa ufufuko wa Bwana kwa uhakika kama vile nilikuwepo jioni sawa na ile pamoja na wanafunzi wawili nyumbani waliokuwa wakielekea Emau. Ninajua kuwa Yeye anaishi.

Hili ni Kanisa la kweli—Kanisa la Yesu Kristo. Sisi, katika Siku ya Hukumu, tutasimama uso kwa uso na Mwokozi. Utakuwa ni wakati wa shangwe kuu kwa wale, katika maisha haya, wamesonga karibu Naye katika huduma Yake na wanaweza kwa shauku kutegemea kusikia maneno Yake: “Vyema, mtumwa mwema na mwaminifu.”

Ninashuhudia kama shahidi wa Mwokozi aliyefufuka na Mkombozi wetu, katika jina la Yesu Kristo, amina.