Mkutano Mkuu
Na Tunazungumza Kuhusu Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


14:26

Na Tunazungumza Kuhusu Kristo

Sisi tu wafuasi wa Yesu Kristo, na tunatafuta kupokea na kushiriki nuru Yake.

Utangulizi

Kwenye hitimisho la jukumu la muda mrefu la nje ya nchi, mimi pamoja na mke wangu, Lesa tulifika uwanja wa ndege kwa ajili ya maandalizi ya safari moja ya mwisho—safari ya usiku—kufika nyumbani. Tuliposimama na wengine wengi tukipiga hatua moja moja baada ya muda kwenye mistari mirefu, tungeweza kuhisi wasiwasi wa wasafiri wenzetu wakihofia kama watafika kwa wakati, kukaguliwa pasipoti na viza na kupita sehemu za usalama kwa mafanikio.

Hatimaye tulifika kituo ambacho kulikuwa na ofisa wa forodha aliyeonekana kutoathiriwa na kiwango kikubwa cha msongo wa mawazo na wasiwasi ndani ya chumba hicho. Alichukua nyaraka zangu, bila kuniangalia usoni, akahakiki picha yangu, akifungua ukurasa mmoja hadi mwingine na hatimaye kugonga muhuri pasipoti yangu kwa mshindo mkubwa.

Kisha alichukua nyaraka za Lesa. Pasipo hisia yoyote, kichwa chini na aliyefokasi kwenye kazi yake, alifungua kurasa kwa jicho la kitaalamu, akiangazia maelezo ya nyaraka zilizo mbele yake. Kwa kiasi tulishtushwa pale ghafla alipoacha kwa muda, akanyanyua kichwa chake na kumwangalia Lesa kwa mtazamo wa uangalifu na wa upendo. Kwa tabasamu mwororo, aligonga muhuri pasipoti ya Lesa na kumrudishia nyaraka zake. Mke wangu alitabasamu pia, akachukua nyaraka na wakaagana kwa maneno ya upendo.

Ni nini kimetokea?” Niliuliza kutaka kujua.

Kisha Lesa alinionyesha kile ambacho afisa amekiona—kadi ndogo yenye picha ya Mwokozi. Kwa bahati mbaya iliteleza kutoka kwenye mkoba wa Lesa na kuingia kwenye nyaraka za pasipoti yake. Hiki ndicho afisa wa forodha alikipata. Hiki ndicho kilichobadili mwenendo wake.

Picha ya Mwokozi ikiwa ndani ya pasipoti.

Neema na Kweli, na Simon Dewey, kwa hisani ya altusfineart.com, © 2025, iliyotumika kwa ruhusa

Picha hii ndogo ya Mwokozi iliunganisha mioyo ya wawili hawa ambao vinginevyo ni watu wasiojuana. Ilibadilisha asiyejali watu hadi mwenye kujali watu, ikinasa uzuri, miujiza na uhalisia wa Nuru ya Yesu Kristo. Kwa siku ile iliyobakia na mara kwa mara tangu siku hiyo, nimetafakari wakati huo mzuri, rahisi kwa mshangao na nimeshangilia kwenye matokeo tukufu ya Nuru ya Kristo kwa watoto wa Mungu.

Tunazungumza Kuhusu Kristo

Sisi tu wafuasi wa Yesu Kristo, na tunatafuta kupokea na kushiriki nuru Yake. Dokezo katika jina la Kanisa ni teolojia yetu ya “Yesu Kristo mwenyewe akiwa ni jiwe kuu la pembeni.” Kwa kupitia manabii wa kale na wanaoishi, Baba yetu wa Mbinguni ametuamuru “Tumsikilize Yeye!” na “njooni kwa Kristo.” “Na tunazungumza juu ya Kristo, tunashangilia katika Kristo, tunahubiri juu ya Kristo, [na] tunatoa unabii juu ya Kristo.”

Sisi hufundisha kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, na wakati wa huduma yake duniani, Yesu alifundisha injili Yake na kuanzisha Kanisa Lake.

Sisi hushuhudia kwamba mwishoni mwa maisha Yake, Yesu alitoa dhabihu ya dhambi zetu pale alipoteseka katika Bustani ya Gethsemane, kusulubiwa msalabani, na kisha kufufuliwa.

Sisi hushangilia kwamba kwa sababu ya dhabihu ya Mwokozi ya kulipia dhambi, sisi tunaweza kusamehewa na kutakaswa dhambi zetu pale tunapotubu. Hii hutuletea amani na kufanya iwezekane kwa sisi kurudi katika uwepo wa Mungu na kupokea utimilifu wa shangwe.

Kristo na Mariamu kwenye kaburi,

Sisi hutoa unabii kwamba kwa sababu ya Ufufuko wa Yesu, kifo sio mwisho bali hatua muhimu ya kusonga mbele. “Sote tutafufuliwa baada ya kufa. Hii inamaanisha kwamba roho na mwili wa kila mtu vitaunganika tena na kuishi milele.”

Njooni kwa Kristo

Manabii wanaoishi katika siku yetu—ambao hupokea ufunuo kutoka kwa Mungu kutufundisha na kutuongoza—kwa wingi hutualika kuja kwa Kristo. Wanatusaidia kukita mioyo yetu,masikio na macho kikamilifu Kwake. Tunaweza kutoa mifano mingi ya marekebisho na viwezeshi vilivyotangazwa na Urais wa Kwanza ambavyo vimenuiwa kutufokasi sisi kwa Yesu Kristo. Baadhi ya haya hujumuisha:

  • Uamuzi wa kuliondoa jina la “Kanisa la Mormoni” na kuweka jina sahihi, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

  • Upatikanaji wa sanaa mpya, yenye dhamira iliyovuviwa ya Kristo kwa ajili ya kuonyesha katika nyumba za mikutano.

  • Dhima za Wasichana na akidi za Ukuhani wa Haruni na muziki vinavyofokasi kwa Yesu Kristo, kama vile “Mimi ni Mwanafunzi wa Kristo” na “Mtegemee Kristo.”

  • Msisitizo mkubwa kwenye Upatanisho na Ufufuko halisi wa Yesu Kristo kama matukio ya kitukufu zaidi katika historia.

  • Sherehe za Pasaka kama msimu na sio tu sikukuu, zenye msisitizo juu ya Yesu Kristo.

  • Kuanzishwa kwa kielelezo cha utambulisho wenye kuonekana wa Kanisa la Yesu Kristo na uhalisia wa ishara yake.

Hebu tuone kwa ukaribu matokeo ya baadhi ya haya. Kwanza, nembo ya Kanisa.

Nembo ya Kanisa

Nembo ya Kanisa

Mnamo 2020, Rais Russell M. Nelson alianzisha utambulisho wa kuonekana kwa ajili ya Kanisa. Nembo hii inaakisi ukweli kwamba Kristo ndiye kiini cha Kanisa Lake na anapaswa kuwa kiini cha maisha yetu. Sasa tunaona nembo hii tuliyoizoea kwenye vibali vya hekalu, kwenye tovuti na majarida ya Kanisa, kama ikoni kwenye app ya Gospel Library na hata kwenye beji za utambulisho za jeshini kwa waumini wengi wa Kanisa wanaohudumu katika vikosi vya jeshi. Nembo hii hujumuisha jina la Kanisa lililo ndani ya jiwe la pembeni, ukumbusho kwamba Yesu Kristo ndiye jiwe kuu la pembeni, inayoonyeshwa hapa katika Kikambodia na inatumika katika lugha 145.

Nembo ya Kanisa katika Kikambodia

Katikati ya nembo hii ni uwakilishi wa sanamu pendwa ya marumaru ya Bertel Thorvaldsen ya Christus, ambayo imehusishwa sana na Kanisa na hupatikana katika vituo vya wageni kwenye maeneo ya hekalu kote ulimwenguni. Umaarufu wake katika alama hii ya Kanisa hupendekeza kwamba Kristo anapaswa kuwa kiini cha yote tuyafanyayo. Kadhalika, mikono iliyonyooshwa ya Mwokozi huonyesha ahadi Yake ya kuwakumbatia wote ambao huja Kwake. Nembo hii ni uwakilishi wa kuonekana wa upendo wa Mwokozi Yesu Kristo na ukumbusho endelevu wa Kristo Aliye Hai.

Yesu akiibuka kutoka kaburini

Kwa udadisi, nimeuliza familia nyingi na marafiki kuhusu kipengele kimoja muhimu cha nembo hii ya Kanisa. Kwa mshangao, wengi hawatambui kipengele kitukufu kilichopo hapo. Yesu Kristo anasimama chini ya tao. Hii humaanisha Mwokozi aliyefufuka akiibuka kutoka kaburini. Kwa dhati tunasherehekea Kristo mfufuka, aliye hai, hata kwenye matumizi ya nembo ya Kanisa.

Pasaka ya Hali ya Juu na Tukufu Sana

Sasa acha tutafakari umuhimu wa Pasaka. Katika jumbe za Urais wa Kwanza za hivi karibuni kuhusu Pasaka, tumepewa changamoto ya “kusherehekea Ufufuko wa Mwokozi aliye hai kwa kujifunza mafundisho Yake na kusaidia kukuza tamaduni za Pasaka katika jumuiya zetu kwa ujumla, hususani ndani ya familia zetu wenyewe.” Kwa ufupi, tumehimizwa kuishi katika njia iliyo ya juu zaidi na takatifu zaidi ya Pasaka.

Napenda ufunuo endelevu kuhusu Pasaka na ninapendezwa na jitihada zenu nyingi za kufanya Pasaka tukio la heshima na tukufu. Kwa kuongezea kwenye kuwa na lisaa limoja tu la sakramenti kwenye Jumapili ya Pasaka, mifano mingine ya shughuli zinazofaa hujumuisha ibada za kata na kigingi kwenye Jumapili ya Matawi pamoja na Wiki Takatifu. Ukumbusho huu hujumuisha shughuli pamoja na watoto na vijana na mara nyingi hujumuisha kwaya za dini tofauti. Wengine wamefanya matembezi ya wazi ya “Kristo Aliye Hai” kwa waumini na marafiki na kushiriki katika matukio ya kijamii ya Pasaka ya madhehebu mbalimbali.

Shughuli kama hizo huwaonyesha wengi katika jiji la Yerusalemu ambao sauti zao ziliungana pamoja kumsifu Mwokozi wakati wa kuingia Kwake kwa ushindi. Ya kuvutia sawa na hiyo ni ripoti ya majibu yenu kwa mwaliko wa Urais wa Kwanza wa kuabudu nyumbani kama familia ili kukumbuka sikukuu hii muhimu sana.

Ninaamini kwamba ibada za familia siku ya Pasaka zimeongezeka kwa wingi. Miaka miwili iliyopita, niliongea kuhusu uthubutu wetu wa familia wa kuboresha njia ya kuheshimu Pasaka. Hakika, hii ni kazi ambayo bado ni endelevu. Daima tumefurahia mlo maalumu wa Jumapili ya Pasaka, vikapu vya Pasaka, na kutafuta mayai ya Pasaka na bado tunafanya. Hata hivyo, kwa dhati kuongeza kiwango cha kiroho kinachofokasi kwa Yesu Kristo na Upatanisho Wake kwenye sherehe zetu kumeleta usawa mzuri kwenye kumbukumbu zetu za matukio haya matukufu kati ya yote.

Mchezo wa Siku ya Pasaka kwa familia ya Stevenson.

Mwaka huu itakuwa ni jaribio letu la tatu la kufanya Pasaka kuwa iliyojikita kwa Kristo zaidi. Kama ukumbusho wa Krismasi wa Kuzaliwa kwa Yesu, mchezo wa siku yetu ya familia ya Pasaka hujumuisha mavazi ya kawaida, kusoma maandiko kutoka Agano Jipya na Kitabu cha Mormoni, muziki, picha za Pasaka, matawi ya mtende—na fujo kidogo, nikiwa mwaminifu kabisa kwenye hili. Watoto na wajukuu wakisoma na kukariri sifa za Jumapili ya Matawi ya Mitende za “Hosana … Mbarikiwa Yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni” na “Huyu ni Yesu … wa Galilaya” inaonekana kuzoeleka kama vile “Amani duniani, kwa watu wenye mapenzi mema” ilivyo wakati wa Krismasi.

Na sasa tunashangilia mchanganyiko wa mapambo. Kile kilichotaka kuwa kama watoto wa sungura na mayai ya Pasaka pekee sasa kimewekwa sawa na Kristo na picha za kaburi tupu, Mwokozi aliyefufuka akitokea katika bustani nje ya kaburi, na kutokea kwa Mwokozi kwa Wanefi. Pia tunajitahidi kuifanya Pasaka kuwa msimu na sio tu siku moja. Tunajaribu kuwa wenye uelewa mzuri, tafakari nzuri na washerehekeaji wa Jumapili ya Matawi na Ijumaa Kuu na matukio matukufu ambayo yalitukia wakati wa kipindi chote cha Wiki Takafu.

Pasaka huturuhusu kuikumbuka dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi na Ufufuko Wake halisi na wa shangwe. Mioyo yetu ni mizito tunapotafakari mateso ya Mwokozi katika ile bustani na juu ya Msalaba, lakini mioyo yetu hushangilia tunapoangalia kaburi tupu na tangazo la kimbingu la “Amefufuka!”

Ufufuko Halisi

Hivi karibuni Urais wa Kwanza umetuhimiza sisi “kutazamia Pasaka na Ufufuko wa Yesu Kristo—ujumbe mtukufu kati ya wote kwa binadamu” ukiangazia ukuu wa msimu huu. Wakati inaonekana kuna ongezeko miongoni mwa wana teolojia wa Kikristo kutazama Ufufuko katika maneno ya kufikirika na kiishara, tunathibitisha mafundisho yetu kwamba “Ufufuko humaanisha kwamba wale wote waliopata kuishi watafufuliwa na Ufufuko ni jambo halisi.” “Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.” Yesu Kristo alikata kamba za kifo kwa kila nafsi hai.

Kweli sote tunashangaa kwa neema ambayo Yesu anatupatia. Tunakumbatia maneno Yake kwamba “hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”

C. S. Lewis alisema kwamba “kufundisha Ukristo ilimaanisha hasa [kwa Mitume] kuhubiri Ufufuko. … Ufufuko ni dhima kuu katika kila mahubiri ya Kikristo yaliyotolewa katika Matendo ya Mitume. Ufufuko na matokeo yake, ndivyo vilikuwa ‘injili’ au habari njema ambayo Wakristo walileta.”

Ninatangaza kwamba “kuna ufufuko, …kaburi halina ushindi, na uchungu wa kifo umemezwa katika Kristo.”

Hitimisho na Ushuhuda

Katika kuhitimisha, ninashuhudia kwamba wote wanaokubali mialiko kutoka kwa nabii wetu anayeishi na washauri wake kwa dhati kukumbuka matukio matukufu ambayo huwakilisha Pasaka watapata kwamba muungano wao na Yesu Kristo unakua imara zaidi.

Siku chache zilizopita, nilijifunza kuhusu bibi aliyekariri hadithi ya Pasaka pamoja na mjukuu wake wa miaka minne kwa kutumia nakala rahisi za kaburi, jiwe lililofunika kaburi, Yesu, Mariamu, wanafunzi na malaika. Mvulana mdogo aliangalia na kusikiliza kwa makini wakati bibi yake alishiriki maziko, kufunikwa na kufunguliwa kwa kaburi na tukio la bustanini la Ufufuko. Baadaye mvulana huyo kwa umakini alirudia hadithi kwa maelezo ya kushangaza kwa wazazi wake alipokuwa akisogeza maumbo yeye mwenyewe. Kufuatia tukio hili zuri, aliulizwa kama alijua kwa nini tuna Pasaka. Mvulana yule alitazama juu na kwa mawazo ya kitoto alijibu, “Sababu Yeye anaishi.”

Mvulana mdogo akisimulia hadithi ya Pasaka.

Ninaongeza ushuhuda kwa ule wake—na wako na ule wa malaika na manabii—kwamba Yeye amefufuka na kwamba Yeye yu Hai, ambavyo juu yake ninashuhudia, katika jina la Yesu Kristo, amina.