Mkutano Mkuu
Mpango wa Rehema
Mkutano mkuu wa Aprili 2025


11:5

Mpango wa Rehema

Bwana ni mwenye rehema na mpango wa wokovu wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kweli ni mpango wa rehema.

Mwaliko wa Nabii

Aprili iliyopita, mara baada ya habari njema kwamba Kanisa limepata Hekalu la Kirtland, Rais Russell M. Nelson alitualika kusoma sala ya kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Kirtland, iliyoandikwa katika sehemu ya 109 ya Mafundisho na Maagano. Sala ya uwekaji wakfu, alisema Rais Nelson, “ni mafunzo kuhusu jinsi gani hekalu katika hali ya kiroho hututia nguvu wewe na mimi ili kukabiliana na changamoto za maisha kwenye siku hizi za mwisho.”

Nina uhakika kujifunza kwenu sehemu ya 109 kulitoa ufahamu uliowabariki. Jioni hii, ninashiriki mambo kadhaa niliyojifunza nilipofuata mwaliko wa nabii wetu. Njia ya kutoa amani ambayo kwayo utafiti wangu uliniongoza ilinikumbusha kwamba Bwana ni mwenye rehema na kwamba mpango wa wokovu wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kweli ni mpango wa rehema.

Wamisionari Wapya Walioitwa Kuhudumu Hekaluni

Kama unavyoweza kufahamu, “wamisionari wapya walioitwa wanahimizwa kupokea endaumenti ya hekaluni haraka iwezekanavyo na kuhudhuria hekaluni mara nyingi kadiri hali zinavyoruhusu.” Mara baada ya kupatiwa endaumenti, wao pia “wanaweza kuhudumu kama wafanyakazi … wa hekaluni kabla hawajaanza huduma ya umisionari.”

Muda katika hekalu kabla ya kuingia katika chuo cha mafunzo ya wamisionari (MTC) unaweza kuwa baraka ya ajabu kwa mmisionari mpya kujifunza zaidi kuhusu maagano ya hekaluni kabla ya kushiriki baraka za maagano hayo na ulimwengu.

Lakini katika kusoma sehemu ya 109, nilijifunza kwamba hekaluni, Mungu anawawezesha wamisionari wapya—ndiyo, sisi sote—katika njia ya ziada, njia takatifu. Katika sala hiyo ya uwekaji wakfu, iliyotolewa kwa ufunuo, Nabii Joseph Smith aliomba kwamba “wakati watumishi wako watakapo waendea kutoka nyumbani kwako … kutoa ushuhuda wa jina lako,” “mioyo” ya “watu wote” ingeweza “kulainishwa”—wote “wakubwa wa dunia” na “maskini wote, wahitaji, na [wale] wanaoteseka.” Aliomba kwamba “chuki zao zipate kutoa njia mbele ya ukweli, na watu wako wapate kukubalika machoni pa wote; ili miisho yote ya dunia ipate kujua kwamba sisi, watumishi wako, tumeisikia sauti yako, na kwamba wewe umetutuma sisi.”

Hii ni ahadi nzuri kwa mmisionari mpya aliyeitwa—kuwa chuki “zipate kutoa njia mbele ya ukweli,” “kupata kukubalika machoni pa wote,” na kuifanya dunia ijue kuwa wametumwa na Bwana. Kila mmoja wetu anahitaji baraka sawa na hizo. Ni baraka iliyoje kuwa na mioyo iliyolainishwa tunapozungumza na majirani na wafanyakazi wenzetu. Sala ya kuweka wakfu haielezei hasa jinsi gani muda wetu hekaluni utakavyolainisha mioyo ya wengine, lakini ninashawishika kuwa inaungana na jinsi gani muda katika nyumba ya Bwana unavyolainisha mioyo yetu wenyewe kwa kutuweka sisi kwenye kiini cha Yesu Kristo na rehema Yake.

Bwana Anajibu Ombi la Joseph Smith kwa Rehema

Nilipokuwa nikisoma sala ya kuweka wakfu ya Kirtland, nilishangazwa pia kwamba Joseph tena na tena aliomba rehema—kwa ajili ya waumimi wa Kanisa, kwa maadui wa Kanisa, kwa viongozi wa nchi, kwa ajili ya mataifa ya dunia. Na, binafsi sana, alimsihi Bwana amkumbuke na kumhurumia mpendwa wake Emma na watoto wao.

Ni jinsi gani Joseph alipata kuhisi wakati, wiki moja baadaye, siku ya Pasaka, Aprili 3, 1836, katika Hekalu la Kirtland, Mwokozi alipomtokea yeye na Oliver Cowdery na, kama ilivyoandikwa katika sehemu ya 110 ya Mafundisho na Maagano, alisema, “Nimekubali nyumba hii, na jina langu litakuwa hapa; nami nitajidhihirisha kwa watu wangu kwa rehema katika nyumba hii.” Ahadi hii ya rehema lazima ilikuwa na maana maalumu kwa Joseph. Na kama Rais Nelson alivyofundisha Aprili iliyopita, ahadi hii pia inatumika kwa kila hekalu lililowekwa wakfu leo.”

Kupata Rehema katika Nyumba ya Bwana

Kuna njia nyingi ambazo kila mmoja wetu anaweza kupata rehema katika nyumba ya Bwana. Hii imekuwa kweli tangu kwa mara ya kwanza Bwana alipoiamuru Israeli kujenga hema na kuweka katikati yake “kiti cha rehema.” Hekaluni, tunapata rehema katika maagano tunayofanya. Maagano hayo, kama nyongeza ya agano la ubatizo, yanatufunga kwa Baba na Mwana na kutupatia ufikiaji wa kile ambacho Rais Nelson amefundisha kuwa ni “aina maalumu ya upendo na rehema … unaoitwa hesed” kwa Kiebrania.

Tunapata rehema katika fursa ya kuunganishwa na familia zetu milele. Katika Hekalu, pia tunakuja kuelewa kwa uwazi zaidi kwamba Uumbaji, Anguko, dhabihu ya Mwokozi ya kulipia dhambi, na uwezo wetu wa kuingia tena katika uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni—hakika, kila sehemu ya mpango wa wokovu—ni madhihirisho ya rehema. Inaweza kusemwa kwamba mpango wa wokovu ni mpango wa furaha hasa kwa sababu ni “mpango wa rehema.”

Kutafuta Msamaha Kunafungua Mlango kwa Roho Mtakatifu

Ninashukuru kwa ahadi nzuri katika sehemu ya 110 kwamba Bwana atajidhihirisha Mwenyewe kwa rehema katika mahekalu Yake. Pia nina shukrani kwa kile inachofunua kuhusu jinsi Bwana atakavyojidhihirisha Mwenyewe kwa rehema wakati wowote ambapo sisi, kama vile Joseph, tunapoomba kwa ajili ya rehema.

Ombi la Joseph Smith la rehema katika sehemu ya 109 halikuwa mara ya kwanza kwa maombi yake ya rehema kusababisha ufunuo. Katika Kijisitu Kitakatifu, kijana Joseph aliomba siyo tu kujua ni Kanisa gani lilikuwa la kweli, lakini pia alisema kwamba “alimlilia Bwana kwa rehema, kwa maana hakukuwa na mtu mwingine ambaye ningeweza kumwendea ili kupata rehema.” Kwa namna fulani, kutambua kwake kwamba alihitaji rehema ambayo ni Bwana pekee ndiye angeweza kuitoa kulisaidia kufunguka kwa madirisha ya mbinguni. Miaka mitatu baadaye malaika Moroni alionekana kufuatia kile ambacho Joseph alikuwa amesema kilikuwa “sala na dua yake kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya msamaha wa dhambi zangu zote na upumbavu.”

Mpangilio huu wa ufunuo kufuatia ombi la rehema ni wa kawaida katika maandiko. Enoshi alisikia sauti ya Bwana baada tu ya kuomba kwa ajili ya kupata msamaha. Uongofu wa baba wa Mfalme Lamoni, unaanza kwa sala yake, “Nitaacha dhambi zangu zote ili nikujue wewe.” Huenda tusibarikiwe kwa uzoefu huu wa kushangaza, lakini kwa wale ambao wakati mwingine wanahangaika kuhisi majibu ya sala, kutafuta rehema za Bwana ni moja ya njia zenye nguvu zaidi za kuhisi ushahidi wa Roho Mtakatifu.

Kutafakari Rehema za Mungu Kunafungua Mlango wa Ushuhuda wa Kitabu cha Mormoni

Kanuni kama hiyo inafundishwa vizuri katika Moroni 1:3–5. Mara nyingi tunafupisha mistari hii kufundisha kwamba, kupitia sala ya dhati, tunaweza kujua kama Kitabu cha Mormoni ni cha kweli. Lakini ufupisho huu unaweza kupuuza jukumu muhimu la rehema. Sikiliza jinsi Moroni anavyoanza mawaidha yake: “Ningewasihi kwamba wakati mtakaposoma mambo haya, … kwamba mngekumbuka jinsi vile Bwana amekuwa na huruma kwa watoto wa watu, kutokea kuumbwa kwa Adamu hadi chini mpaka wakati ambapo mtapokea vitu hivi, na kuvitafakari katika mioyo yenu.”

Moroni anatuhimiza sio tu kusoma mambo haya—kumbukumbu ambazo alikuwa karibu kuzifunga—lakini pia kutafakari mioyoni mwetu kile ambacho Kitabu cha Mormoni kinafunua kuhusu “jinsi Bwana alivyokuwa na huruma kwa watoto wa watu.” Ni kutafakari juu ya rehema za Bwana ambazo zinatuandaa “kumuuliza Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo, ikiwa vitu hivi si vya kweli.”

Tunapotafakari juu ya Kitabu cha Mormoni, tunaweza kuuliza: Je, ni cha kweli, kama Alma alivyofundisha, kwamba mpango wa Mungu wa rehema unahakikisha kwamba kila mtu aliyewahi kuishi hapa duniani atafufuliwa na kwamba “watarejeshwa kwa … sura kamili”? Je, Amuleki yuko sahihi—je, rehema ya Mwokozi inaweza kukidhi mahitaji yote ya kweli ya haki ambayo tungelazimika kulipa na badala yake “[kutuzingira] katika mikono ya usalama”?

Je, ni kweli, kama Alma alivyoshuhudia, kwamba Kristo aliteseka si tu kwa ajili ya dhambi zetu bali kwa ajili ya “maumivu na mateso” ili kwamba aweze “kujua … jinsi ya kuwasasidia watu wake kulingana na unyonge wao”? je, Bwana kweli ni mwenye rehema, kama Mfalme Benyamini alivyofundisha, kwamba kama zawadi ya bure, alitoa dhabihu ya kulipia dhambi “za wale … ambao wamekufa bila kujua mapenzi ya Mungu juu yao, au ambao wametenda dhambi kwa ujinga”?

Je, ni kweli, kama Lehi alivyosema, kwamba “Adamu alianguka ili wanadamu wawe; na wanadamu wapo, ili wapate shangwe”? Na je, ni kweli, kama Abinadi alivyoshuhudia, akimnukuu Isaya, kwamba Yesu Kristo “alijeruhiwa kwa ajili ya makosa yetu, alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake; na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”?

Kwa jumla, je, mpango wa Baba kama ulivyofundishwa katika Kitabu cha Mormoni kweli ni wa rehema? Ninashuhudia kwamba ni wa rehema na kwamba mafundisho ya amani na tumaini la rehema katika Kitabu cha Mormoni ni ya kweli.

Bado, nadhani kwamba inawezekana wengine wanapambana, licha ya kusoma kwa uaminifu na sala zako, kutambua ahadi ya Moroni kwamba Baba wa Mbinguni “atadhihirisha ukweli kwako, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.” Najua mahangaiko haya kwa sababu niliyahisi, miaka mingi iliyopita, wakati usomaji wangu wa kwanza wa Kitabu cha Mormoni haukutoa jibu la haraka na la wazi kwa sala zangu.

Ikiwa unapambana, naomba nikualike ufuate ushauri wa Moroni ili kutafakari juu ya njia nyingi ambazo Kitabu cha Mormoni kinafundisha “jinsi Bwana alivyokuwa na huruma [kwa] watoto wa watu”? Kulingana na uzoefu wangu, natumaini kwamba, unapofanya hivyo, amani ya Roho Mtakatifu inaweza kuingia moyoni mwako na unaweza kujua, kuamini, na kuhisi kwamba Kitabu cha Mormoni na mpango wa rehema unaofundishwa ni vya kweli.

Ninatoa shukrani zangu kwa mpango mkuu wa rehema wa Baba na kwa utayari wa Mwokozi kuutekeleza. Ninajua kwamba atajidhihirisha Mwenyewe kwa rehema katika hekalu Lake takatifu na katika kila sehemu ya maisha yetu ikiwa tutamtafuta. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Russell M. Nelson, “Furahia Katika Zawadi ya Funguo za Ukuhani,” Liahona, Mei 2024, 121.

  2. Russell M. Nelson,“Kufurahia katika Zawadi ya Funguo za Ukuhani,” 121.

  3. Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 24.5.1, Maktaba ya Injili.

  4. Kama ilivyo kwa baraka zote za hekaluni, utoaji wa Mungu wa baraka hizi unategemea kushika kwetu maagano tunayofanya hekaluni. Ona Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 96: “Kila mtu anayefanya maagano … hekaluni—na kuyashika—ameongeza ufikiaji kwenye uweza wa Yesu Kristo.”

    Kama mfano mwingine, fikiria kauli ya Urais wa Kwanza juu ya kuvaa gamenti ya hekaluni: “Unaposhika maagano yako, ikijumuisha fursa takatifu ya kuvaa gamenti kama ilivyoelekezwa katika ibada za mwanzo, utakuwa na ufikiaji mkubwa wa rehema, ulinzi, nguvu na uwezo wa Mwokozi” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 26.3.3.2; msisitizo umeongezwa).

  5. Mafundisho na Maagano 109:55–57.

  6. Ona Russell M. Nelson, “Bwana Yesu Kristo Atakuja Tena,” Liahona, Nov. 2024, 121–22: “Hapa kuna ahadi yangu kwako: Kila mtafutaji wa dhati wa Yesu Kristo atampata hekaluni. Utahisi rehema Yake.”

  7. Ona Mafundisho na Maagano 109:34: “Uwarehemu watu hawa, na kama vile watu wote hutenda dhambi, samehe uvunjaji sheria wa watu wako, na wafutiwe milele.”

  8. Ona Mafundisho na Maagano 109:50.

  9. Ona Mafundisho na Maagano 109:54. Joseph pia alimwomba Bwana “awarehemu wana wa Yakobo, ili Yerusalemu, kuanzia saa hii, ianze kukombolewa; na nira ya utumwa inaweza kuanza kuvunjwa kutoka kwa nyumba ya Daudi; na wana wa Yuda waanze kurudi katika nchi ulizompa Ibrahimu, baba yao.” (Mafundisho na Maagano 109:62–64).

  10. Ona Mafundisho na Maagano 109:68.

  11. Ona Mafundisho na Maagano 109:69. Kamusi ya Kiingereza ya Oxford inafafanua rehema kama “msamaha na huruma inayoonyeshwa kwa mtu ambaye yuko katika hali ya kutokuwa na nguvu.” (“mercy,” oed.com). Rehema, kama neema, ni kielelezo cha upendo na fadhili za Mungu—Hesed Yake. Lakini rehema inazingatia kuzuia adhabu tunayostahili, neema kwa kawaida hurejelea Mungu akitupatia baraka tusizostahili na bila kujali wema wetu.

  12. Mafundisho na Maagano 110:7.

  13. Katika dhihirisho la rehema binafsi, Joseph na Oliver waliambiwa, “Tazama, dhambi zenu zimesamehewa; nanyi ni wasafi mbele zangu; kwa hiyo, inueni vichwa vyenu na kufurahi” (Mafundisho na Maagano 110:5).

  14. Russell M. Nelson, “Kufurahia katika Zawadi ya Funguo za Ukuhan,” 119. Rais Nelson alisema, “Ninawaalika kutafakari ahadi ya Bwana inamaanisha nini kwenu binafsi.”

  15. Tazama Kamusi ya Biblia, “Tabernacle”: “Patakatifu pa Patakatifu kulikuwa na samani moja tu: Sanduku la Agano. … Juu ya sanduku na kikiwa kama mfuniko, kilikuwa kiti cha rehema. Kilitumikia, pamoja na sanduku chini yake, kama madhabahu ambayo upatanisho wa juu zaidi unaojulikana kwa sheria ya Kiyahudi ulitekelezwa. Juu yake ilinyunyizwa damu ya sadaka ya dhambi ya Siku ya Upatanisho (Mambo ya Walawi 16:14–15). Kiti cha rehema kilikuwa mahali pa dhihirisho la utukufu wa Mungu(Kutoka 25:22).”

  16. Russell M. Nelson, “Agano lisilo na Mwisho,” Liahona, Okt. 2022, 5. Kama Rais Nelson alivyoonyesha, hesed haina Kiingereza sawa, lakini tafsiri yake ya kawaida katika Agano la Kale ni rehema. Mara zote 248 neno hesed linajitokeza katika Toleo la King James kwenye Agano la Kale, rehema limetumika mara 149, fadhili mara 40, na upendo mara 30. (ona Blue Letter Bible, blueletterbible.org/lexicon/h2617/kjv/wlc/0-1/).

  17. Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 27.2. Mwokozi anatufundisha kwamba hakuna hata mmoja wetu anayeweza kuja kwa Baba isipokuwa kupitia Yeye (ona Yohana 14:6). Katika Mafundisho na Maagano, Mwokozi anatoa maelezo haya mazuri ya ombi lake la rehema kwa niaba yetu:

    “Msikilize yeye aliye mwombezi kwa Baba, anayetetea teto lako mbele zake—

    “Akisema: Baba, tazama mateso na kifo chake yeye ambaye hakutenda dhambi, ambaye ulipendezwa naye; tazama damu ya Mwanao iliyomwagika, damu yake yeye ambaye ulimtoa ili upate kutukuzwa;

    “Kwa hiyo, Baba, wasamehe hawa ndugu zangu ambao wanaamini juu ya neno langu, ili waweze kuja kwangu na kupata uzima usio na mwisho” (Mafundisho na Maagano 45:3–5).

  18. Rais Jeffrey R. Holland aliwahi kusema: “Hakika jambo ambalo Mungu anafurahia zaidi kwenye kuwa Mungu ni msisimko wa kuwa na rehema, hasa kwa wale ambao hawatarajii na mara nyingi wanahisi hawastahili” (“The Laborers in the Vineyard,” Liahona, Mei 2012, 33). Ona pia Mafundisho na Maagano 128:19: “Sasa, tunasikia nini katika injili ambayo tumeipokea? Sauti ya furaha! Sauti ya rehema kutoka mbinguni; na sauti ya ukweli kutoka duniani; habari njema kwa wafu; sauti ya furaha kwa walio hai na wafu; habari njema ya shangwe kuu.”

  19. Alma 42:15. Rehema daima imekuwa katikati ya mpango wa wokovu. Maandiko matatu ya asili yanatoa kielelezo. Nefi anahitimisha sura ya kwanza kabisa ya Kitabu cha Mormoni kwa kusema “Tazama, mimi, Nefi, nitawaonyesha ninyi kuwa Bwana ana huruma nyororo juu ya wale ambao amewachagua, kwa sababu ya imani yao, kuwatia nguvu hata kwenye uwezo wa ukombozi” (1 Nefi 1:20).

    Katika Kutoka 34:6, Bwana anatangaza jina lake kwa Musa kama “Bwana Mungu, mwenye rehema na neema, mvumilivu, na mwingi wa wema na kweli.” Wengine wamependekeza kwamba aya hii yaweza kuwa imerejelewa na manabii wa Agano la Kale zaidi ya aya nyingine yoyote katika Agano la Kale.(tazama, kwa mfano, Mradi wa Biblia, “Aya Iliyonukuliwa Zaidi katika Biblia,” bibleproject.com/podcast/most-quoted-verse-bible/).

    Katika Agano Jipya, katika kitabu cha Luka, kumbuka kwamba Zakaria alipigwa kuwa “bubu, na hakuweza kusema” wakati alipotilia shaka ahadi ya malaika kwamba Elisabeti katika uzee wake angezaa mtoto wa kiume, ambaye angekuwa Yohana Mbatizaji (Luka 1:20). Wakati sauti ya Zakaria ilipoachiliwa, “alijazwa na Roho Mtakatifu” na, katika tamko la kwanza la umma kwamba wakati wa Masiya ulikuwa umefika, “alitabiri” kwamba Bwana atakuja “kutekeleza rehema iliyoahidiwa kwa baba zetu, na kukumbuka agano lake takatifu; kiapo alichomwapisha baba yetu Ibrahimu” (Luka 1:67–73; msisitizo umeongezwa).

  20. Gospel Topics Essays, “First Vision Accounts,” Gospel Library; ona hususani the 1832 account.

  21. Joseph Smith—Historia ya 1:29. Mafundisho na Maagano 20:5–6 hutoa maelezo mengine ya nafasi ya toba katika maono haya mawili yenye nguvu. Joseph alisema kwamba “hakuna mtu anayehitaji kunidhania nina hatia ya dhambi yoyote kubwa au mbaya,” lakini “alihisi kuhukumiwa kwa udhaifu [wake] na kutokamilika” na alihitaji msamaha (Joseph Smith—Historia 1:28, 29).

  22. Ona Enoshi 1:1–8.

  23. Alma 22:18. Sala ya Alma, “Ee Yesu, Ewe Mwana wa Mungu, nihurumie,” inaongoza kwa mafuriko ya nuru na nafuu dhidi ya maumivu (Ona Alma 36:17–20). Rais Jeffrey R. Holland aliwahi kusema juu ya ombi la Alma: “Labda sala kama hiyo, ingawa ni fupi, ndiyo muhimu zaidi ambayo inaweza kutamkwa katika ulimwengu ulioanguka. Maombi mengine yoyote tunayotoa, mahitaji mengine yoyote tuliyo nayo, yote yanarudi kwenye ombi hilo: ‘Ee Yesu, Ewe Mwana wa Mungu, nihurumie’” (Our Day Star Rising: Exploring the New Testament with Jeffrey R. Holland [2022], 170–71).

  24. Mzee Kyle S. McKay alifundisha kwa uzuri, “Maisha ya Joseph ya toba ya mara kwa mara hunipa ujasiri wa ‘kuja kwa ujasiri kwenye kiti cha enzi cha neema, ili nipate rehema’” (“Mwanamume Aliyenena na Yehova,” Liahona, Nov. 2024, 61).

  25. Moroni 10:3.

  26. Ombi la Moroni ni hitimisho la kauli ya Nefi mwanzoni mwa Kitabu cha Mormoni, ambapo anasema kusudi lake mwenyewe kwa kuandika kwenye mabamba: “Tazama, mimi, Nefi, nitakuonyesha kwamba huruma nyororo za Bwana ziko juu ya wale wote aliowachagua, kwa sababu ya imani yao, ili kuwafanya wawe hodari hata kwa nguvu ya ukombozi” (1 Nefi 1:20).

  27. Moroni 10:4.

  28. Ona Mormoni 9:13.

  29. Alma 40:23: “Roho itarudishwa kwa mwili, na mwili kwa roho; ndiyo, na kila sehemu na kiungo kitarudishwa kwa mwili wake; ndiyo, hata nywele ya kichwa haitapotea; lakini vitu vyote vitarudishwa kwa umbo lake sahihi na kamilifu.”

  30. Alma 34:16. Tunapofikiria jinsi ambavyo Bwana amekuwa mwenye rehema, tunaweza kujaribiwa kutenganisha rehema kutoka kwa haki—kufikiri kwamba rehema ya upendo ya Baba yetu wa Mbinguni pekee inaweza kushinda haki. Lakini kama Alma alivyofundisha, “mpango wa rehema usingetimizwa isipokuwa upatanisho ufanywe; kwa hivyo Mungu mwenyewe hulipia dhambi za ulimwengu, kutimiza mpango wa rehema, kuwezesha mahitaji ya haki, kwamba Mungu angekuwa mkamilifu, na Mungu mwenye haki, na Mungu wa huruma pia” (Alma 42:15; msisitizo umeongezwa).

    Upendo wote wa rehema wa Mwokozi kwetu haungeweza kutuokoa. Badala yake, ilikuwa mateso yake mahitaji halisi na machungu ya haki ambayo yanatuokoa. Hii haipunguzi, kwa kweli, umuhimu wa upendo Wake. Hakika, ilikuwa upendo Wake kwetu—na hamu Yake ya kufanya mapenzi ya Baba, ambaye pia anatupenda—ambayo ilimfanya Yeye kuwa tayari kuteseka (ona Yohana 3:16; Mafundisho na Maagano 34:3). Lakini upendo pekee usingefanya kazi.

    Wakati mwingine, tunaweza kufokasia sana upendo wake kwetu jinsi hasa tulivyo kiasi kwamba tunapoteza ukweli kwamba jinsi tulivyo—kama wanaume na wanawake wa asili ambao tabia zetu bila shaka zina mapungufu kwenye kutii amri—zinahitaji kwamba haki itosheleze. Ikiwa hatuelewi na kuona upendo wake kama kuondoa matakwa ya haki, tunapunguza zawadi ya dhabihu yake ya kulipia dhambi na mateso aliyoteseka kulipa gharama kali ya haki. Ingekuwa kejeli sana ikiwa upendo Wake kwetu ungeeleweka kutoa dhabihu Yake ya kulipia dhambi isiyo ya lazima. Ni bora sana kuangalia kwa uwazi mahitaji kamili ya haki na kisha kushukuru kwamba alitupenda vya kutosha kubeba mahitaji hayo ya kweli kwa niaba yetu.

  31. Alma 7:11–12.

  32. Mosia 3:11.

  33. 2 Nefi 2:25.

  34. Mosia 14:5.

  35. Moroni 10:4.

  36. Moroni 10:3.

  37. Rais M. Russell Ballard alituhimiza kutoa ushuhuda wa “kile unachojua na kuamini na kile unachohisi” (“Kumbuka Kile Kilicho na Maana Zaidi,” Liahona, Mei 2023, 107).

  38. Katika kutoa pendekezo hili, sina nia ya kutoa “kanuni” mbadala kwa ushuhuda wa ukweli wa Kitabu cha Mormoni au injili. Kama Mzee David A. Bednar alivyofundisha, ufunuo unaweza kuja kama “nuru iliyowashwa katika chumba chenye giza,” ambapo ufunuo unapokelewa “haraka, kwa ukamilifu na wote kwa mara moja.” Unaweza pia kuja kama “ongezeko la taratibu la mwanga unaotokana na jua linalochomoza, … mstari juu ya mstari, amri juu ya amri (2 Nefi 28:30). … Mawasiliano kama hayo kutoka kwa Baba wa Mbinguni hatua kwa hatua na kwa upole ‘yatatonatona juu ya [nafsi zetu] kama umande utokao mbinguni’ (Mafundisho na Maagano 121:45). Mtindo huu wa ufunuo huwa wa kawaida zaidi kuliko nadra” (“Roho wa Ufunuo,” Liahona, Mei 2011, 88).