Mtegemee Mungu na Uishi
Ni katika kumtegemea Mungu pekee ndipo watu, familia na hata mataifa yanaweza kustawi.
Mnamo Juni iliyopita, ajali mbaya sana ilitokea katika nchi ya Lesotho kusini mwa Afrika. Basi dogo lililokuwa limewabeba wasichana 20 wa tawi la Maputsoe la Kanisa na viongozi wao saba wakielekea jiji kuu, Maseru, kwa ajili ya mkutano wa wasichana kutoka wilaya yao. Walipokuwa wanasafiri katika barabara kuu yenye barabara mbili katika saa za asubuhi, gari lililokuwa linatoka upande mkabala, likijaribu kupita gari lingine, lilikuja kwenye barabara basi lilipokuwa. Hakukuwa na nafasi au muda wa kuepuka mgongano wa uso kwa uso, na katika sekunde chache magari yaligongana, kupindukia kando ya barabara, na kuwaka moto.
Katika wote, watu 15 walifariki katika ajali hii, ikijumuisha wasichana, viongozi wawili wa wasichana, na rais wa tawi na mkewe. Manusura, wanafamilia, na marafiki walionyesha hisia mbalimbali, ikijumuisha nyakati za ghadhabu, mfadhaiko, na hata hatia. Licha ya hisia hizi na maswali yasiyojibika, walifarijiana na kumgeukia Mungu kupitia muziki mtakatifu, maandiko, na sala, ambapo walipata faraja. Manusura wa miaka kumi na saba Setso’ana Selebeli alishuhudia, “Yesu Kristo anatupenda sisi na yu pamoja nasi, hata ingawa mioyo yetu ina machungu.”
Msichana na kiongozi waliolazwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ya kuungua walijifunza Kitabu cha Mormoni pamoja. Mmoja alisema, “Hivi karibuni tumekuwa tukisoma katika Moroni, na Moroni anasema kile hasa ambacho nimekuwa nikihisi. … Anapozungumza, ni kama anasema, ‘Unapaswa kujifunza maneno haya kwa sababu yaliandikwa kwa ajili yako kukusaidia kupitia hili.’”
Katika mazishi ya pamoja kwa wale walioangamia, Sabini wa Eneo Mzee Siyabonga Mkhize alishauri, “Sisi sote tunapaswa kumgeukia Bwana wakati huu na kumuomba Yeye kuifariji mioyo yetu na … kupoza maumivu ambayo tunayahisi.” Rais wa Wasichana kutoka katika Tawi jirani la Leribe, Mampho Makura; alihimiza, “Mgeukieni Bwana, na mpate nguvu ya kukubali mapenzi Yake. Yesu Kristo ni ‘mwanzilishi na mtimizaji wa imani yetu’ [Waebrania 12:2]. Msitazame kando, bali mtazameni Yeye.”
Mtengemeeni Yeye. Maneno yake yanatoa mwangwi kwenye ushauri wa Alma kwa mwanawe Helamani: “Ona kwamba umeelekeza jicho kwa Mungu na uishi.” Alma alidondoa uzoefu wa Lehi na watu wake wakiwa na Liahona kama mfano: “Kwani tazama, ni rahisi kama kutii neno la Kristo, ambalo litakuonyesha njia nyoofu kwa raha ya milele, kama vile ilivyokuwa kwa babu zetu kutii hii dira, ambayo ingewaonyesha njia nyoofu kuelekea nchi ya ahadi.” Alma alisema: “Ikiwa wao wangeangalia wao wangeishi. … Na ikiwa sisi … tutaangalia sisi tutaishi milele.”
Wakati mmoja, Alma alidondoa mfano wa nyoka wa shaba aliyenyanyuliwa juu na Musa wakati mmoja Waisraeli wa kale walipokuwa wakiteswa na nyoka wa moto. Bwana alimwambia Musa kutengeneza sanamu ya nyoka na aiweke juu ya mti, kukiwa na ahadi “kwamba kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.” Alma alielezea kwamba sanamu ya shaba ilikuwa aina au ishara ya Kristo, ambaye angeinuliwa msalabani. Wengi walimwangalia na kuishi, lakini wengine wakawa, katika maneno ya Alma, “wagumu sana” kwamba kwa urahisi hawangeweza kumwangalia na waliangamia.
Alma aliuliza:
“Ee ndugu zangu, ikiwa mngeponywa tu kwa kutupa macho yenu kwamba mponywe, si mngeangalia upesi, au ni afadhali mshupaze mioyo yenu kwa kutokuamini, na kuwa wazembe, kwamba hamngetupa macho yenu ili mwangamie?
“… Basi zungusha macho yako na uanze kuamini katika Mwana wa Mungu, kwamba atakuja kukomboa watu wake, na kwamba atateseka na kufa ili alipe dhambi zao; na kwamba atafufuka tena kutoka kwa wafu, na kutimiza ufufuo, kwamba watu wote watasimama mbele yake, kuhukumiwa katika siku ya mwisho, kulingana na matendo yao.”
Bila shaka, ushauri huu “mtegemee Mungu na uishi” una maana kwetu siyo tu katika umilele, lakini pia huleta tofauti yote katika sifa na kiwango cha maisha yetu ya duniani. Kumbuka maneno ya Dada mdogo Selebeli nchini Lesotho yaliyotajwa tayari—”Yesu Kristo anatupenda sisi na yu pamoja nasi, hata ingawa mioyo yetu ina machungu.”
Iko katika asili ya ulimwengu ulioangauka—ambapo ibilisi ana ghadhabu na pale ambapo kila mmoja si mkamilifu—pale ambapo kutakuwa na kuvunjika moyo na maudhi, kuteseka na huzuni, kushindwa na kupoteza, mateso na kutokuwa na haki. Ni katika kumtegemea Mungu pekee ndipo watu, familia na hata mataifa yanaweza kustawi. Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Kwa sababu Mwokozi, kupitia Upatanisho Wake usio na kikomo, alimkomboa kila mmoja wetu kutokana na udhaifu, makosa, na dhambi, na kwa sababu Yeye alipitia kila maumivu, wasiwasi, na mzigo ambao umewahi kuwa nao [ona Alma 7:11–13], basi unapotubu kwa dhati na kutafuta msaada Wake, unaweza kuinuka juu ya ulimwengu huu hatari wa sasa.”
Hakuna ahadi iliyorudiwa kila mara katika maandiko ya Kitabu cha Mormoni kuliko hii: “Kama mtashika amri zangu mtafanikiwa nchini; lakini kama mtakataa amri zangu mtatengwa kutoka uwepo wangu.” Uzoefu wa watu wa Kitabu cha Mormoni katika karne nyingi unaonyesha ukweli wa maneno haya. “Kufanikiwa” kulimaanisha kufurahia mwongozo na baraka za mbinguni katika katika maisha yao. “Kufanikiwa” kulimaanisha kufikia viwango vya hali nzuri ya uchumi ambayo iliwawezesha kuoa, kukuza familia, na kuhudumia mahitaji ya wengine. “Kufanikiwa” kulijumuisha uwezo wa kuinuka kushinda magumu na majaribu. Kupitia neema ya Kristo, “mambo yote [yalifanya] kazi kwa faida [yao],” yaliwatakasa, kuzidisha uhusiano wao na Yeye.
Alma alielezea kwamba kumtegemea Mungu ni kushika amri Zake, kumlilia Yeye kila mara kwa ajili ya msaada Wake, kushauriana Naye katika mambo yako yote, na kuacha moyo wako kujawa na shukrani Kwake mchana na usiku. Amri za Mungu na ushauri hupatikana katika maandiko na maneno ya watumishi Wake. Kanuni na mawazo bora yaliyoelezwa katika “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” ni mfano mkuu. Mwingine ni mwongozo unaopatikana katika kijitabu cha Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana. Dhima ya Wavulana na Wasichana kwa ajili ya mwaka huu ni “Mtegemee Kristo,” inayopatikana kutoka kwenye maelekezo ya kufariji ya Bwana kwa Joseph Smith na Oliver Cowdery: “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana huzungumzia amri na viwango vingi vya Mungu vilivyo muhimu na hufundisha jinsi ya kumtegemea Bwana katika kufanya maamuzi mazuri. Ni mwongozo sio tu kwa vijana bali kwetu sote.
Kama mfano mmoja muhimu sana, Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana ina mwongozo muhimu sana katika sura yenye kichwa cha habari “Mwili Wako Ni Mtakatifu.” Inaelekeza: “Utendee mwili wako—na miili ya wengine—kwa heshima. Unapofanya maamuzi kuhusu nguo zako, mtindo wa nywele na mwonekano, jiulize mwenyewe, ‘Je, ninauheshimu mwili wangu kama zawadi takatifu kutoka kwa Mungu?’”
Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana inasema zaidi: “Tunza hisia za kimapenzi na kujamiana kwa utakatifu. Hazipaswi kuwa suala la mzaha au burudani. Nje ya ndoa kati ya mwanamume na mwanamke, ni makosa kugusa sehemu za siri, takatifu za mwili wa mtu mwingine hata kama amevaa nguo. Katika chaguzi zako kuhusu nini cha kufanya, kutazama, kusoma, kusikiliza, kufikiri, kuposti au kuandika ujumbe, epuka kitu chochote kile ambacho kwa makusudi kinaamsha hisia za matamanio kwa wengine au kwako wewe mwenyewe.”
Hii inatukumbusha maonyo ya Rais Nelson ya hivi karibuni:
“Vitu vichache vitafanya kwa haraka maisha yako kuwa magumu ikilinganishwa na kuvunja hii sheria takatifu [ya usafi wa kimwili]. Kwa wale ambao wamefanya maagano na Mungu, zinaa ni moja ya njia za haraka za kupoteza ushuhuda wako.
“… Nguvu ya kuumba maisha ni fursa moja ya uungu ambayo Baba wa Mbinguni huwaruhusu watoto Wake duniani kuitumia. Hivyo, Mungu aliweka mwongozo wa wazi kwa ajili ya matumizi ya nguvu hii takatifu. Mahusiano ya kimwili ni kwa mwanamume na mwanamke ambao wameoana tu.
“Sehemu kubwa ya ulimwengu haiamini hili, lakini mtazamo wa umma si mamlaka yatoayo ukweli. Bwana ametamka kwamba mtu yeyote mchafu kimaadili hatafikia ufalme wa selestia. … Kama umekuwa mchafu kimaadili, ninakusihi utubu. Njoo kwa Kristo na pokea ahadi Yake ya msamaha kamili wakati unapotubu kwa dhati dhambi zako [ona Isaya 1:16–18; Mafundisho na Maagano 58:42–43].”
Kumbuka kwamba katika ahadi ya Kitabu cha Mormoni, kinyume cha kufanikiwa haikuwa umasikini—ilikuwa ni kukatiliwa mbali kutoka kwenye uwepo wa Bwana. Uwepo wake hurejelea ushawishi wa Roho Yake katika maisha ya mtu. Watu wote wanajazwa na Nuru ya Kristo wanapokuja ulimwenguni. Katika kuongezea, baadhi wanatenda ili kubatizwa na kupokea zawadi na ongezeko la nuru ya Roho Mtakatifu. Yeye huleta msukumo na mwongozo, huboresha na kutakasa vipawa vya mtu vya kiasili na uwezo, na husaidia kuepukana na ushawishi muovu, maamuzi duni, na miisho ya kukwama.
Kama vile wewe, ninajua baadhi ambao walifurahia kipawa cha Roho Mtakatifu lakini ambao kupitia kushindwa kushika amri za Mungu wamepoteza baraka hiyo. Mmoja hasa anakuja akilini ambaye uumini wake wa Kanisa ulikuwa umeondolewa kwa sababu ya uvunjaji amri. Alisema kwamba jibu lake la kwanza lilikuwa kuhisi kukosewa. Alihisi kuhukumiwa na viongozi wasio wakamilifu. Alijua mwenendo wake mwenyewe haukuwa sahihi, lakini aliuhalalisha kwa kuonesha makosa na mapungufu ya wengine. Baada ya muda, alianza kuhisi faraja katika mtindo wa maisha nje ya Kanisa bila majukumu ya miito, matarajio ya kuhudhuria ibada za kuabudu na kuwahudumia wengine.
Hii iliendelea kwa muda fulani, lakini alianza kuhisi kwa kina ukosefu wa Roho Mtakatifu—uwepo wa Mungu—katika maisha yake. Kutokana na uzoefu, alijua vile ilivyokuwa, siku baada ya siku, faraja, mwongozo, na kujiamini kunatokana na Roho, na alihisi kumkosa Roho. Hatimaye, alifanya kile kilichohitajika ili kutubu, na kustahili tena kwa ajili ya ubatizo wa maji na wa Roho.
Inaonekana hakuna mwisho wa vyanzo tofauti tofauti watu wanavyotegemea kwa ajili ya maana, furaha, na msaada. Wengi “wanangalia zaidi ya lengo.” Lakini hatuhitaji kuwa “watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu [au mtindo].” Katika kumtegemea Mungu, tunaweza kupata amani katika magumu, na imani yetu inaweza kuendelea kukua hata katika nyakati za shaka na changamoto ya kiroho. Tunaweza kupata nguvu katika kukabiliana na upinzani na kutengwa. Tunaweza kupatanisha ukamilifu na uhalisi wa sasa. Kwa kweli, hakuna njia nyingine zaidi ya ile ambayo Mungu ameiweka: “Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia: maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.”
Kumtegemea Mungu humaanisha kwamba Yeye sio tu mojawapo ya vipaumbele; inamaanisha, hakika, kwamba Yeye ndiyo kipaumbele chetu cha juu zaidi. Ninakumbuka tena ajali mbaya sana huko Lesotho Juni iliyopita. Kutoka kwenye kitanda chake hospitalini, mmoja wa viongozi wa Wasichana ambaye alinusurika, ambaye hakuwa akiamini katika Mungu kabla ya kujiunga na Kanisa, alisema kwamba madhumuni yake sasa ni kugundua kwa nini maisha yake yaliokolewa. “Kila mara kumtumikia Mungu ndiyo jinsi ambavyo nitakuja kupata jibu, ikiwa nitapata jibu,” alisema. “Nilikuwa nimezoea kufikiria kwamba ninampenda Mungu, lakini sasa, kwa kweli, kweli, kweli, kweli, kweli ninampenda Yeye. Sasa Yeye ni kipaumbele [nambari moja] katika maisha yangu.”
Ninatoa ushahidi wa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu ambao ni wakamilifu katika umoja wa neno, wazo, kusudi, na matendo. Wao ni Mungu mmoja, ambao kwao tunaweza kutazamia mambo yote mazuri. Ninatoa ushuhuda wa Upatanisho wa Yesu Kristo, ambapo huja nguvu ya kutimiza ahadi ya kupendeza, “Nitazameni mimi, na mvumilie hadi mwisho, na mtaishi; kwani kwa yule ambaye huvumilia hadi mwisho nitampatia uzima wa milele.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.