2025
Nyuso Zenye Kutabasamu na Mioyo Yenye Shukrani
Novemba 2025


10:53

Nyuso Zenye Kutabasamu na Mioyo Yenye Shukrani

Uzuri wa Watakatifu wetu katika Afrika unadhihirika zaidi wanapokabiliana na changamoto za maisha na mahitaji ya Kanisa linalokua.

Kidogo zaidi ya mwaka mmoja uliopita, nilipumzishwa kutoka katika jukumu langu la Urais wa Sabini, mabadiliko yaliyotangazwa hapa kwenye mkutano mkuu. Kwa sababu jina langu lilisomwa karibu na yale ya Viongozi Wakuu wenye mamlaka wanaostaafu na kubaki na heshima, wengi walidhani nilikuwa nikimaliza muda wangu wa huduma. Baada ya mkutano, nilipokea jumbe nyingi za shukrani na kunitakia mema kwa awamu yangu inayofuata katika maisha. Wengine hata walitoa maombi ya kununua nyumba yangu huko North Salt Lake. Ilipendeza kuona kwamba nitakumbukwa na pia kujua kwamba hatutakuwa na shida kuuza nyumba pale nitakapofika mwisho wa kazi yangu. Lakini sijafika hapo bado.

Kazi yangu mpya imetupeleka Monica na mimi katika Afrika nzuri, mahali ambapo sasa Kanisa linanawiri. Imekuwa baraka kuhudumu miongoni mwa Watakatifu waminifu katika Eneo la Afrika Kusini na kushuhudia upendo wa Bwana kwao. Inatia moyo kuona familia za vizazi kutoka mazingira yote, ikiwa ni pamoja na wengi wa waumini wa Kanisa, waliofanikiwa na walioelimika wakitenga muda na talanta zao ili kuwahudumia wengine.

Wakati huo huo, kutokana na idadi ya watu katika eneo hilo, watu wengi wa kipato cha kati wanajiunga na Kanisa na kubadilisha maisha yao kupitia baraka za uaminifu katika zaka na fursa za elimu zinazotolewa na Kanisa. Programu kama vile Succeed in School, EnglishConnect, BYU–Pathway Worldwide, na Mfuko Endelevu wa Elimu vinawabariki watu wengi, haswa wale wa kizazi kinachoinukia.

Rais James E. Faust aliwahi kusema, “Imesemekana kwamba kanisa hili siyo lazima liwavutie watu wakuu lakini mara nyingi huwafanya watu wa kawaida kuwa watu wakuu.”

Ukuu wa Watakatifu wetu katika Afrika unadhihirika zaidi wanapokabiliana na changamoto za maisha na mahitaji ya Kanisa linalokua. Daima wao wanakabiliana na changamoto hizo kwa mtazamo chanya. Wanatoa mfano unaojulikana vyema wa mafundisho kutoka kwa Rais Russell M. Nelson:

“Shangwe tunayoihisi inahusika kwa kiasi kidogo sana na hali za maisha yetu na inahusika na kila kitu kinachohusu fokasi ya maisha yetu.

“Wakati fokasi ya maisha yetu inapokuwa katika mpango wa Mungu wa wokovu … na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi shangwe bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu.”

Wanapata shangwe licha ya changamoto zao. Wamejua kwamba uhusiano wetu na Mwokozi hutuwezesha kuyakabili magumu tukiwa na nyuso zenye kutabasamu na mioyo yenye shukrani.

Watakatifu Waafrika

Hebu nishiriki baadhi ya uzoefu wangu na watakatifu hawa waaminifu wanaoonesha kanuni hii, kuanzia na Msumbiji.

Msumbiji

Miezi michache iliyopita, niliongoza mkutano wa kigingi chenye mwaka mmoja ambacho tayari kilikuwa na vitengo 10. Zaidi ya watu 2,000 walijaa kwenye kanisa dogo na mahema matatu yaliyowekwa nje. Rais wa kigingi ana umri wa miaka 31, mke wake miaka 26, na wana watoto wawili wadogo. Anakiongoza kigingi hiki kinachokua na chenye changamoto bila ya malalamiko—akiwa tu na uso wenye kutabasamu na moyo wenye shukrani.

Katika mahojiano na patriaki, nilijifunza kwamba mke wake alikuwa mgonjwa sana, na alikuwa akikabiliwa na changamoto ya kumhudumia. Baada ya kushughulikia suala hili na rais wa kigingi, tulimpa baraka za ukuhani. Nilimuuliza patriaki ni baraka ngapi za kipatriaki anatoa kwa wastani.

“Nane hadi kumi,” alisema.

Nilimuuliza, “Kwa mwezi?”

Alijibu, “Kwa wiki!” Nilimshauri kwamba kufanya hivyo kwa idadi hiyo kwa wikendi haikuwa busara.

“Mzee Godoy,” alisema, “wanaendelea kuja kila wiki, ikiwa ni pamoja na waumini wapya na vijana wengi.” Tena, bila ya malalamiko—akiwa na uso wenye kutabasamu na moyo wenye shukrani.

Baada ya kikao cha Jumamosi jioni cha mkutano wa kigingi, nilipokuwa njiani kuelekea hotelini, niliona watu wakinunua chakula kando ya barabara usiku sana Nilimuuliza dereva wangu kwa nini walikuwa wanafanya hivyo wakati ilikuwa giza sana badala ya mchana. Alijibu kwamba walikuwa wakifanya kazi mchana ili wawe na pesa kufanya hivyo baadaye.

“Ooh, walikuwa wanafanya kazi leo ili wale kesho,” nilisema.

Lakini alinirekebisha, “Hapana, walikuwa wanafanyakazi mchana ili wale usiku.” Nilikuwa na matumaini kwamba waumini wetu yawezekana walikuwa katika hali nzuri zaidi, lakini alithibitisha kwamba wengi walikabiliwa na changamoto kama hizo katika sehemu hiyo ya nchi. Asubuhi iliyofuata, wakati wa kikao chetu cha Jumapili na nikawa na ufahamu mpya wa hali yao, nilifurahishwa zaidi nyuso zao zenye kutabasamu na mioyo yenye shukrani.

Zambia

Tukiwa njiani kwenda kwenye mkutano wa Jumapili, rais wa kigingi na mimi tuliwaona wanandoa wakitembea kando ya barabara wakiwa na mtoto mchanga na watoto wadogo wawili. Tulisimama ili kuwabeba. Walishangaa na kufurahia. Nilipowauliza ni umbali gani walitakiwa kutembea kwenda kanisani, baba alijibu kwamba inaweza kuchukua dakika 45 hadi saa moja, itategemea mwendo wa watoto. Waliikabili safari hii kwenda na kurudi, kila Jumapili, bila malalamiko—ni nyuso zenye kutabasamu na mioyo yenye shukrani tu.

Malawi

Jumapili moja kabla ya mkutano wa kigingi, nilitembelea matawi mawili yaliyokuwa yakitumia shule za umma kama nyumba za mikutano. Nilishtushwa na uduni wa hali ya majengo hayo, ambayo hayakuwa na hata huduma za msingi. Nilipokutana na waumini wachache pale, nilikuwa tayari kuomba msamaha kwa hali duni ya nyumba yao ya mkutano, lakini walifurahia kuwa na mahali pa karibu pa kukusanyika, wakiepuka kutembea mwendo mrefu. Tena, hakukuwa na malalamiko—ni nyuso tu zenye kutabasamu na mioyo yenye shukrani

Zimbabwe

Kufuatia Jumamosi ya mafunzo ya uongozi, rais wa kigingi alinipeleka kwenye ibada za Jumapili zinazofanyika katika nyumba ya kukodi. Kulikuwa na watu 240 waliohudhuria. Kisha askofu aliwatambulisha waumini wapya 10 waliobatizwa wiki hiyo. Umati ulikuwa umeenea katika vyumba viwili vidogo, huku baadhi ya waumini wakikaa nje ya jengo, wakitazama mkutano kupitia madirishani na milangoni. Tena, hakukuwa na malalamiko—ni nyuso tu zenye kutabasamu na mioyo yenye shukrani

Lesotho

Nilitembelea nchi hii ndogo na nzuri, pia ikijulikana kama “ufalme wa mlimani,” kuona wilaya ya Kanisa ikijiandaa kuwa kigingi. Kufuatia Jumamosi ya mikutano, nilihudhuria kipindi cha Jumapili katika moja ya matawi yao katika nyumba ya kukodisha. Chumba cha sakramenti kilikuwa kimefurika, watu wakiwa wamesimama nje ya mlango ili wapate kushiriki. Nilimwambia rais wa tawi kwamba alihitaji nyumba kubwa. Kwa mshangao wangu, alinijulisha kwamba hii tu ni nusu ya waumini wake. Nusu nyingine wangehudhuria mkutano wa pili wa sakramenti baada ya saa ya pili. Tena, hakukuwa na malalamiko—ni nyuso tu zenye kutabasamu na mioyo yenye shukrani

Nilirejea Lesotho baadaye kutokana na ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha vijana wetu kadhaa, ambayo tayari ilitajwa na Mzee Todd D. Christofferson hapo awali. Wakati nilipozitembelea familia na viongozi, nilitarajia hali ya huzuni. Badala yake, nilikutana na Watakatifu wenye nguvu na wakakamavu ambao walikuwa wakikabiliana na hali hiyo kwa njia inayoinua na kuhamasisha.

Mpho Aniciah Nku

Mpho Aniciah Nku, 14, mwaathirika wa ajali aliyenusurika katika ajali hii kwenye picha hii, imeelezwa vizuri kwa maneno yake mwenyewe: “Mtumainie Yesu na kila wakati mtegemee Yeye, kwa maana kupitia Yeye utaipata amani, na Yeye atakusaidia katika mchakato wa kupona.”

Hii ni mifano michache ambapo tunaona mitazamo yao chanya kwa sababu wameyaweka maisha yao katika injili ya Yesu Kristo. Wanajua mahali pa kupata msaada na tumaini.

Nguvu ya Uponyaji ya Mwokozi

Kwa nini Mwokozi anaweza kuwasaidia wao na sisi katika hali zo zote za maisha yetu? Jibu linaweza kupatikana katika maandiko:

“Na atakwenda, na kuteseka maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina. …

“… Na atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, … ili ajue … jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao.”

Kama alivyofundisha Mzee David A. Bebnar, hakuna maumivu ya kimwili, huzuni, au udhaifu tunaoweza kupata ambao Mwokozi hajui. “Wewe na mimi katika wakati wa udhaifu tunaweza kulia, ‘Hakuna anayeelewa [kile ninachopitia]. …’ Hakuna mwanadamu, pengine, anayejua. Ila Mwana wa Mungu anajua vizuri na anaelewa.” Na kwa nini? Kwa sababu Yeye alihisi na alibeba mizigo yetu kabla hatujafanya hivyo.”

Ninamalizia kwa ushuhuda wangu wa maneno ya Kristo yanayopatikana katika Mathayo 11

“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Kama tu wale Watakatifu huko Afrika, nami najua kuwa ahadi hii ni ya kweli. Ni kweli kule, na ni kweli kila mahali. Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. James E. Faust, “Five Loaves and Two Fishes,” Ensign, Mei 1994, 5.

  2. Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 82.

  3. Alma 7:11–12.

  4. David A. Bednar, “The Atonement and the Journey of Mortality,” Liahona, Apr. 2012, 19.

  5. Mathayo 11:28–30.