2025
Maelezo ya Habari Njema
Novemba 2025


10:39

Maelezo ya Habari Njema

Itakuwaje pale utakapomwongeza Yesu Kristo zaidi katika maisha yako?

Kama umewahi kutembelea jimbo la nyumbani kwetu la Louisiana, unaweza pengine ukafahamu vizuri vyakula vyetu vingi vitamu—gumbo, jambalaya, étouffée, na orodha inaendelea na kuendelea.

Mara kwa mara, ninajihisi jasiri vya kutosha kupika mojawapo ya mapishi haya matamu. Hatua ya mwisho ambayo haijaandikwa baada ya kuchanganya viungo vyote na kufuata maelekezo ni mtihani wa mwisho wa kuonja na kuona kama kuna chochote kinakosekana. Kwenye hatua hii, ningeweza kuwasikia wapishi wabobezi wa Kreole wakinong’ona masikioni mwangu, “Weka kiungo cha Tony zaidi ndani yake.” Tony ni kiungo cha kreole kilichotengenezwa huko Opelousas, Louisiana, mji wa nyumbani kwangu. Mara nyingi inatumika kama “kiungo cha siri” ili kufidia mapungufu yaliyofanyika wakati wa kufuata maelezo ya upishi.

Mimi pamoja na mke wangu Michelle tulipata heshima ya kuhudumu kama viongozi wa misioni huko Louisiana. Tulikuwa na desturi ya kuwafundisha wamisionari jinsi ya kupika mapishi yake maalumu ya jambalaya usiku wao wa mwisho katika makazi ya misioni kabla ya kurudi katika familia zao. Kama ziada kwenye shuhuda zao juu ya injili ya urejesho ya Yesu Kristo, wamisionari wetu waliaga misioni wakishukuru maelezo hayo ya upishi.

Miezi michache iliyopita, nilikuwa nikivinjari kupitia Chombo cha Habari cha Kanisa na nikaona kiungo kwenye kusanyiko la video fupi zinazoitwa Mazungumzo ya Urejesho na Rais Russell M. Nelson. Jina la mojawapo ya video hizi fupi kwenye orodha lilivuta usikivu wangu na kunifanya nitabasamu. Inaitwa “Maandiko ni Maelezo ya Mapishi ya Mungu kwa ajili ya Maisha ya Furaha.” Haraka nilibofya kwenye hiyo video ya dakika mbili na kumwangalia Rais Nelson akifundisha kikundi cha Watoto ujumbe rahisi wenye nguvu wa jinsi ya kuwa na furaha. Yeye alifundisha: “Kama unaoka keki, unafuata maelekezo, au siyo? Na utapata matokeo mazuri kila wakati, au siyo?”

Aliendelea, akizungumzia kuhusu kuwa na umri wa miaka 95 hivi karibuni: “Watu wanasema, ‘Wewe unakula nini? Siri yako ni nini?’” Yeye alijibu, “Siri zinaitwa maandiko. Unaweza kuyasoma na kuyajaribu.”

Ndiyo, hiyo ndiyo siri. Siri rahisi kwa ajili ya maisha ya furaha ni kufuata tu maelezo ya mapishi hayo ya Mungu kama yalivyoainishwa katika maandiko. Nayaita “Maelezo ya Habari Njema.”

Je, wewe hufanya nini wakati kitu kinaenda mrama wakati wa kufuata maelezo ya mapishi? Ndiyo, akiwa amewekwa katika Maelezo ya Habari Njema yeye ni “kiungo cha siri” ili kuhakikisha daima hatimaye unafika kwa usahihi mwishoni. Jibu daima ni Yesu Kristo.

Nafikiri sisi sote tunazo nyakati tunapohisi viungo vyetu siyo vizuri vya kutosha, au tunahangaika kufuata maelekezo, au pengine tunafanya kitu nje ya utaratibu, au kitu fulani kinatokea kilicho nje ya udhibiti wetu, na kadhalika.

Tiba ni nini? Ni kuongeza zaidi tu kile kinachomwalika Yesu Kristo katika maisha yetu.

Hivyo, ni nini kinaweza kuonekana kama kumwongeza Yesu Kristo zaidi katika maisha yako?

Wakati nikihudumu kama rais wa misioni, nilipata heshima ya kukutana ana kwa ana na kila mmisionari kijana kila baada ya wiki sita. Wakati wa mkutano huu wa ana kwa ana, ilikuwa ni kawaida kwa wamisionari kutafuta mwongozo wa jinsi ya kuboresha ufanisi wa wenza wao.

Katika tukio moja, mmisionari mmoja alikuja katika usaili wake binafsi na kukaa nchini. Niliweza kutambua kutokana na lugha ya mwili wake kwamba kuna kitu kinamsumbua sana akilini mwake. Nilimwuliza, “Mzee ungetaka leo tujadili nini?” Alielezea baadhi ya changamoto alizokuwa nazo na mwenza wake na jinsi gani inaathiri uwezo wake wa kufanya kazi ya umisionari. Kwa machozi machoni mwake, alinitazama na kuuliza, “Rais, napaswa kufanya nini?”

Katika wakati huo, kwa uaminifu kabisa sikujua jinsi ya kujibu. Baada ya muda mfupi, nilimuuliza kama ingekuwa SAWA kwa sisi kupiga magoti pamoja katika sala kwa ajili ya mwongozo kutoka kwa Roho. Alikubali, na tulipiga magoti pamoja na kusali kwa ajili ya mwongozo wa kiungu.

Baada ya sala, tuliendelea kupiga magoti kwa muda mfupi na kisha tukakaa katika viti vyetu tukitazamana. Nikaomba kama tungeweza kusoma andiko kwa pamoja. Tulipokuwa tukifungua maandiko yetu, nilisimama kidogo na kumwambia, “Mzee, tunaposoma andiko hili, tafadhali jiulize mwenyewe swali lifuatalo: Kama nitaishi sifa hizi, je, zitaboresha umoja wetu na kazi yetu ya umisionari?”

Kisha tukafungua Moroni 7:45 na kusoma kwa sauti: “Na hisani huvumilia, na ni karimu, na haina wivu, na haijivuni, haitafuti mambo yake, haifutuki kwa upesi, haifikirii mabaya, haifikirii maovu lakini hufurahia katika ukweli, huvumilia vitu vyote, huamini vitu vyote, hutumaini vitu vyote, hustahmili vitu vyote.”

Yule mzee kisha akaniangalia akiwa na machozi machoni mwake na kusema, “Ndiyo, Rais, lakini hilo ni gumu kutenda.” Nilikubali na kumkumbusha kwamba yeye ni mwana wa Mungu, mwenye uwezekano wa kiungu wa kufanya hili pamoja na Bwana.

Kisha kwa kifupi tukajadili mfano wa mpando uliofundishwa na Mzee Clark G. Gilbert wa Sabini, ambao ulitukumbusha kwamba tunapaswa kuanzia pale tulipo na, pamoja na Bwana, tukisonga mbele na juu katika mwelekeo chanya. Niliweza kuona kwamba bado alikuwa akihisi kuzidiwa na hatua zinazofuata, hivyo nilimwomba aelezee uelewa wake kwenye andiko lisemalo “kwa vitu vidogo na rahisi vitu vikubwa hutokea.” Alielezea dhana hiyo kwamba kwa kufanya vitu vidogo na rahisi, vitu vikubwa hutokea. Nilimwomba achukue dakika moja na ataje vitu vidogo viwili na rahisi anavyoweza kufanya ili kuwa mkarimu kwa mwenza wake.

Baada ya dakika chache alishiriki mawazo yake. Kisha nikamwomba kuchukua dakika chache na kutambua vitu vidogo na rahisi viwili anavyoweza kufanya ili kuwa mvumilivu kwa mwenza wake. Mara moja alishiriki mawazo hayo mawili. Ilikuwa ni dhahiri kwamba amekuwa tayari akitafakari hili kabla ya mkutano wetu. Nilimwalika kuchukua vile vitu vichache kwa Mungu katika sala na kuomba uthibitisho, mwelekeo, na mwongozo wa kiungu kuhusu jinsi gani ya kutekeleza mpango wake kwa kusudi halisi. Alikubali. Tulipokuwa tukihitimisha, nilimwomba kutoa usasisho mfupi katika barua yake ya kila wiki.

Wiki iliyofuata ilipopita, niliweza kuona katika barua zake za kila wiki kwamba mambo yalikuwa yakifanya vizuri. Lakini siyo tu niliweza kuona maboresho katika barua zake za kila wiki, niliweza pia kuona katika barua za kila wiki za mwenza wake. Wakati wa mkutano wetu wa ana kwa ana uliofuata, niliona tofauti ya usiku na mchana katika uso wake na roho. Nilimwuliza, “Hivyo, Mzee, ni kweli hisani haishindwi?” Alijibu kwa tabasamu kubwa: “Ndiyo, na kwa vitu vidogo na rahisi vitu vikuu hutokea.”

Unapofuata Maelezo ya Upishi ya Habari Njema kwa ajili ya kuishi kwa furaha, kumbuka mafundisho ya Rais Nelson: “Maswali au matatizo yoyote uliyo nayo, jibu daima linapatikana katika maisha na mafundisho ya Yesu Kristo. Jifunzeni zaidi kuhusu Upatanisho Wake, upendo Wake, rehema Yake, mafundisho Yake na injili Yake ya urejesho ya uponyaji na ukuaji. Mgeukie Yeye! Mfuateni Yeye!”

Unapohitaji “kumsikia Yeye” na kujua jinsi ya kumwalika Yesu Kristo maishani mwako, zingatia kufuata hatua za Rais Nelson alizotufundisha kuhusu ufunuo binafsi:

“Tafuta sehemu ya ukimya ambako utakwenda mara kwa mara. Jinyenyekeze mbele za Mungu. Mimina moyo wako kwa Baba yako wa Mbinguni. Mgeukie Yeye kwa ajili ya majibu na faraja.

“Omba katika jina la Yesu Kristo kuhusu matatizo yako, hofu zako, udhaifu wako—ndio, mahitaji halisi ya moyo wako. Na kisha sikiliza! Andika mawazo ambayo yanakuja kwenye akili yako. Andika hisia zako na zifuatilie kwa vitendo ambavyo unashawishiwa kufanya. Unaporudia utaratibu huu siku baada ya siku, mwezi baada ya mwezi, mwaka baada ya mwaka, ‘utakua katika kanuni za ufunuo.’”

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Yeye “amekamilisha kila kitu tunachohitaji kuweza kurudi kwa Baba [yetu] wa Mbinguni.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.