2025
Kuwakumbuka Kondoo
Novemba 2025


12:14

Kuwakumbuka Kondoo

Kanuni ya kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu inafanya kazi. Ni njia ya Bwana.

Yesu Kristo ni Mchungaji Mwema. Kila mmoja wetu ni wa thamani Kwake. Aliweka mfano wa huduma na kutufunza kwa maneno na vitendo sifa za mchungaji mwema, ikijumuisha kuwajua kondoo wako kwa majina, kuwapenda, kuwatafuta wale waliopotea, kuwalisha, na , hatimaye, kuwarudisha tena nyumbani. Anatutarajia tufanye vivyo hivyo kama watumishi walio chini Yake.

Tunaweza kujifunza mengi kuhusu kuhudumu katika njia ya Bwana kutoka kwa nabii wa kale—na mchungaji wa kipekee—Moroni. Aliishi katika nyakati ngumu sana, bila kuwa na simu za mkononi, kompyuta na intaneti. Lakini aliweza kujua idadi ya kondoo. Hii ilifanyikaje? Tunapata mtazamo kidogo kwenye mbinu yake katika Moroni 6. Hapo tunasoma kwamba waumini “walihesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo; na majina yao yalichukuliwa ili wakumbukwe na kulishwa kwa neno zuri la Mungu, kuwaweka katika njia nzuri. … Kanisa walikutana pamoja mara kwa mara, kufunga na kuomba, na kuzungumza mmoja na mwingine kuhusu ustawi wa nafsi zao” (Moroni 6:4–5; msisitizo umeongezwa).

Kwa Moroni, yote ilikuwa kuhusu watu—majina! Alifanyia kazi kanuni ya “kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu” ili kwamba wote waweze kukumbukwa. Yeyote aliyesumbuka au kutangatanga alionwa, hii ikiruhusu Watakatifu kujadili ustawi wao katika mabaraza. Kama vile mchungaji aliyewaacha tisini na kenda (salama na kwenye ulinzi, nina hakika) na kumwendea mmoja aliyekuwa amepotea (ona Luka 15:4–7), tumeombwa kuwajua wale tunaowahudumia—kuwagundua na kuwakumbuka na kwenda na kufanya vivyo hivyo.

Kama kiongozi wa misioni nchini India, nakumbuka kumuuliza rais wa tawi kijana kuhusu baadhi ya malengo yake kwa ajili ya mwaka uliofuata: “Ni wanaume wangapi utawaandaa ili wapokee ukuhani wa Melkizedeki?” Jibu lake la haraka lilikuwa “Saba!”

Nilijiuliza ni wapi katika kitabu cha Etheri alipotoa idadi hiyo mahususi! Kabla sijasema neno, alitoa kipande cha karatasi chenye namba moja mpaka saba zikiwa zimeandikwa pembeni. Mistari mitano ya mwanzo ilikuwa na majina—watu halisi ambao yeye na akidi yake ya wazee walikuwa wakienda kuwaalika na kuwahimiza kuwa na baraka ya ukuhani katika maisha yao. Ndiyo, ilibidi niulize kuhusu mistari tupu ya namba sita na saba. “Oh, Rais,” alisema, akitikisa kichwa chake kwa uhakika, “hakika tutabatiza angalau wanaume wawili mwanzoni mwa mwaka ambao wanaweza kupata ukuhani kufikia mwisho wa mwaka.” Kiongozi huyu hodari alielewa kanuni ya kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu.

Kristo amepangilia Kanisa Lake katika njia ambayo inakuwa vigumu kuisahau nafsi, kwani kila moja ni pendwa Kwake. Kila mtu katika kata, bila kujali umri ama jinsia, ana wahudumiaji wengi—wachungaji—ambao wana jukumu la kuwatazama, kwa kuwakumbuka. Mvulana, kwa mfano, amepangiwa uangalizi wake kwa uaskofu, akina kaka wahudumiaji, washauri watu wazima wa vijana, walimu wa seminari, marais wa akidi, na kisha baadhi—wote wakihudumu kama vyandarua salama, vilivyotundikwa imara kando ya kijana huyo ili kumdaka ikiwa ataanguka. Hata ikiwa ni chandarua kimoja pekee kimewekwa vyema, mvulana huyo atakuwa salama, ataonwa, na kukumbukwa. Na bado, mara nyingi tunakuta hakuna chandarua kilichowekwa vyema. Watu wanatangatanga gizani—na hakuna anayewaona. Tunawezaje kuwa wachungaji bora zaidi? Tunaweza kujifunza kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu.

Kanisa linatupatia ripoti na nyenzo za kufanya hilo—kukumbuka. Ripoti ya kila robo mwaka ni mfano mzuri. Inaturuhusu kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu kwa kila muumini mara nyingi na kuwagundua wale ambao hawaonekani au wanahitaji msaada wetu na upendo wetu. Orodha ya hatua na usaili huwabainisha wale wanaohitaji umakini wetu sasa, kama ilivyo kwa ripoti ya hali ya kibali cha hekaluni na zinginezo. Nyenzo hizi za Kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu huweka fokasi yetu kwa watu. Nani anahitaji wito, kupiga hatua kwenye ukuhani au kusaidia kupeleka jina la familia hekaluni? Nani tunapaswa kuwa tunamsaidia kujiandaa kwa ajili ya umisionari? Nani hakuonekana mwezi huu? Nyenzo hizi hutusaidia kuwakumbuka watu.

Niliifahamu familia kutoka Marekani ambayo ilichukua jukumu huko Afrika. Jumapili yao ya kwanza waliingia ndani ya Kanisa lililokuwa moja pekee nchini, ambapo walikaribishwa kwa shauku. Mwishoni mwa asubuhi, mke wa mwanamume yule alikuwa ameitwa kuwa rais wa Muungano wa Usaidizi na mwanamume kuwa kiongozi wa wavulana! Alimuuliza rais wa tawi aliyeonekana kuchoka ni wavulana wangapi walikuwepo. Kiongozi huyu mwaminifu, wa kizazi cha kwanza cha waumini alionesha kwa kidole nyuma ya ukumbi wa sakramenti na kusema, “Wale pale wawili.” Yule mwanamume alikuwa na mashaka, hivyo alienda na orodha ya tawi nyumbani, kwa haraka akagundua kwamba kulikuwa na wavulana 20 kwenye orodha. Alirejea kwa rais wa tawi na kuomba vijana wakubwa wawili wa kuaminika, wanaozungumza lugha mbili kuhudumu kama washauri wake na kisha kuketi nao pamoja na wavulana wale wawili ili kupitia majina.

Kisha vijana hawa shupavu wakaingia kufanya kazi. Kwa miezi michache iliyofuata, walimpata kila mvulana kwenye orodha ile. Jina kwa jina, kondoo wale waliopotea walikaribishwa tena na vijana wenzao na kulishwa kiroho na kimwili! Ndani ya mwaka, kwenye Jumapili yoyote, kulikuwa na wastani wa wavulana 21 kwenye mahudhurio. Shukrani nyingi kwa wavulana ambao walihesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu.

Rafiki yangu mpendwa, akiwa mwanafunzi kijana aliyehitimu, alihama na familia yake kwenda jiji kubwa la Marekani kuendeleza elimu yake. Haraka akaitwa kusimamia akidi ya wazee. Akiwa na hofu kidogo kuhusu usaili wake wa kwanza na rais wa kigingi, alidhamiria kwenda akiwa amejiandaa. Alimwambia rais wa kigingi kwamba alikuwa na malengo matatu kwa mwaka ujao: (1) asilimia 90 uhudumiaji, (2) somo muhimu la injili kila wiki, na (3) shughuli ya akidi iliyopangiliwa vyema kila mwezi.

Akitabasamu kwa rafiki yangu, rais huyu wa kigingi mwenye hekima aliuliza, “Je, unaweza kumtaja mshiriki wa akidi asiyeshiriki kikamilifu ambaye ungependa kumsaidia kufika hekaluni na familia yake mwaka huu?” Hilo lilimshangaza rafiki yangu. Alifikiri kwa makini na kuja na jina. “Liandike,” alielekeza rais wa kigingi. Kisha kiongozi huyu mwenye uzoefu aliuliza swali hilohilo mara tatu zaidi—na usaili ulimalizika. Mvulana huyu alitoka nje ya usaili ule akiwa amejifunza moja ya masomo yake makuu juu ya uongozi na uhudumiaji. Alikwenda kwenye usaili akiwa na programu, masomo na shughuli. Alitoka nje akiwa na majina! Majina yale manne baadaye yalikuwa fokasi muhimu ya huduma yake na ya akidi yake.

Kama kiongozi wa misioni, nilitembelea moja ya matawi yangu Jumapili moja asubuhi. Niligundua kwamba rais wa tawi alikuwa akitoa kadi ya karatasi mfukoni mwake na kuandika juu yake. Niliamua kumuuliza kuhusu hilo baada ya sala ya kufunga. Mara baada ya mkutano kumalizika, na kabla sijauliza kuhusu kadi, kiongozi wa wamisionari wa tawi aliharakisha kwenye jukwaa, ambapo alipewa karatasi. Kwa haraka nilimfuata kiongozi huyu mwenye shauku kwenye mkutano wake wa uratibu wa umisionari wa tawi. Kabla hawajaanza, alitoa karatasi mfukoni mwake. Ilikuwa imejaa majina ya waumini ambao hawakuwepo kwenye mkutano wa sakramenti. Ndani ya dakika chache, kila mshiriki wa baraza alikuwa amechagua jina moja au mawili, akiweka ahadi ya kuwatembelea siku ileile ili kuhakikisha walikuwa SAWA na kuwajulisha kwamba walikuwa wamekumbukwa. Sasa hiyo ndiyo Kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu.

Nakumbuka wilaya, iliyo masaa mengi kwa ndege kutoka hekalu la karibu, ambapo kutunza kibali hai ilikuwa kipaumbele cha juu, licha ya ukweli kwamba pengine kisingetumika kabisa. Jumapili ya kwanza ya kila mwezi, viongozi walitumia nyenzo zao za kuhesabu ili kutunza kumbukumbu za mahesabu kwa ajili ya waumini wao waliopokea endaumenti. Ikiwa wangekuta kwamba kibali kingeisha muda wake karibuni, katibu mtendaji angepanga usaili wa kibali kipya. Watu wenye vibali vilivyoisha muda walijadiliwa, kisha kutafuta kuwasaidia katika kurejea kwenye njia ya agano. Niliuliza ni waumini wao wangapi waliopokea endaumenti walikuwa na kibali hai. Jibu lilikuwa la kustaajabisha asilimia 98.6. Walipoulizwa kuhusu sita ambao vibali vyao vilikuwa vimeisha muda, viongozi waliweza kuwabainisha kwa majina na kunifafanulia juhudi zinazofanywa ili kuwarejesha!

Miaka michache iliyopita, familia yangu ilihama kurudi Marekani. Tulikuwa na shauku ya kuhudhuria Kanisani hapa baada ya miaka 26 ya kupendeza ndani ya matawi madogo, yaliyojitenga. Niliitwa kama mmisionari wa kata. Tulikuwa na kiongozi mzuri wa wamisionari na tulikuwa tukifanya mambo ya kuvutia na kuwafundisha watu wema. Niliomba kuhudhuria mkutano wa baraza la kata ili kusikiliza na kupata usaidizi wao kwa marafiki tuliokuwa tukiwafundisha. Nilishangazwa pale ambapo yote yaliyojadiliwa yalikuwa shughuli ijayo ya kata. Nilimwendea kiongozi wa wamisionari baadaye na kutoa maoni kwamba hakupata nafasi ya kurudi na kutoa ripoti juu ya watu wetu. Jibu lake? “Oh, sipati kabisa nafasi ya kutoa ripoti.”

Nilitofautisha hilo na mkutano wa baraza la tawi huko Lahore, Pakistan, ambao nilihudhuria wiki chache kabla. Kundi hili dogo liliketi kuzunguka meza ndogo, na yote waliyozungumza yalihusu watu. Majina. Kila kiongozi aliripoti uhudumiaji wake kwa mtu mmoja mmoja na familia ambazo walikuwa na wasiwasi kuwahusu. Wote walipata nafasi ya kuongeza mawazo yao juu ya njia bora zaidi ambazo wangeweza kuwabariki wale waliojadiliwa. Mipango iliwekwa na majukumu yakatolewa. Somo la kupendeza lililoje katika kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu kwa jina kutoka kwa kaka zetu na dada zetu wa kizazi cha kwanza cha waumini.

Katika Kanisa la Yesu Kristo, tumeelekezwa na manabii waliopita na waliopo sasa—na kwa mpangilio uliowekwa na Mwokozi wetu—jinsi ya kuhudumu. Tunachukua majina, tunakumbuka, na tunashauriana juu ya ustawi wa nafsi. Viongozi wanaofanya hili kamwe hawataishiwa vipengele vya ajenda katika mikutano yao ya baraza! Kanuni ya kuhesabu na kutunza kumbukumbu za mahesabu inafanya kazi. Ni njia ya Bwana. Tunaweza kufanya vizuri zaidi. Kwa Mungu, aliyeumba ulimwengu na anayetawala juu ya vyote, kazi hii—kazi Yake na utukufu Wake—ni kwa mmoja mmoja. Na ndivyo inavyopaswa kuwa kwa kila mmoja wetu, kama vyombo katika mikono Yake katika kazi Yake ya kupendeza ya wokovu na kuinuliwa. Miujiza kwenye maisha ya watu halisi itatendeka. Katika jina la Yesu Kristo, amina.