2025
Fanya Sehemu Yako kwa Moyo Wako Wote
Novemba 2025


15:22

Fanya Sehemu Yako kwa Moyo Wako Wote

Mtumainie Mwokozi kujihusisha, kwa subira na bidii, katika kufanya sehemu yako kwa moyo wako wote.

Mwaka jana wakati wa safari huko ulaya nilitembelea sehemu yangu ya zamani ya ajira Lufthansa German Airlines huko Uwanja wa Ndege wa Frankfurt.

Ili kuwafunza marubani wake, waliendesha mafunzo ya kisasa ya kuigiza ya kuendesha ndege ambayo yanaweza kutengeneza karibia hali yoyote ya kawaida au ya dharura kwenye ndege. Wakati wa miaka yangu mingi kama rubani wa ndege, ilinibidi kufaulu mtihani wa urubani katika mashine ya kuigiza kuendesha ndege kila baada ya miezi sita ili leseni yangu ya urubani ibaki hai. Nakumbuka vyema nyakati hizo ngumu za shinikizo na hofu lakini pia hisia ya mafanikio baada ya kufaulu mtihani. Nilikuwa kijana kipindi hicho na niliipenda changamoto hiyo.

Wakati wa matembezi yangu, mmoja wa watendaji wa Lufthansa aliomba kama naweza kujaribu tena kuendesha ndege ya 747 kwenye mashine ya kuigiza.

Kabla ya kuchakata jambo hili kikamilifu, nilisikia sauti—ikinijia kwa kushangaza kama ya kwangu—ikisema, “Ndio, ningependa hilo sana.”

Mara tu niliposema maneno hayo, wingi wa mawazo ulifurika akili yangu. Ni kitambo sasa tangu niendeshe 747. Wakati ule nilikuwa kijana na rubani jasiri. Sasa nilikuwa heshima ya kutunza kama rubani mkuu aliyestaafu. Je, nitajiaibisha mwenyewe mbele ya wabobezi hawa?

Lakini tayari haikuwezekana kukataa, hivyo nilikaa kwenye kiti cha rubani, nikaweka mikono yangu kwenye gia ninazozifahamu na pendwa, na kuhisi, kwa mara nyingine, utamu wa urubani wakati ndege kubwa ya 747 ikikimbia kwenye njia na kupaa kwenye anga ya buluu na mbali.

Ni furaha kusema kwamba safari hii ilifanikiwa, ndege ilibaki salama, vivyo hivyo na taswira yangu.

Hata hivyo, uzoefu ulikuwa wa kunyenyekeza kwangu. Nilipokuwa kijana, kuendesha ndege ilikuwa kama jambo lililozoeleka. Sasa, inachukua jitihada zangu zote kufanya vitu vya msingi.

Uanafunzi Huhitaji Nidhamu

Uzoefu wangu kwenye mashine ya urubani ilikuwa ni ukumbusho muhimu kwamba kuwa bora kwenye chochote—iwe kupaisha ndege, kupiga kasia, kupanda au kujua—huhitaji nidhamu binafsi na mafunzo endelevu.

Unaweza kutumia miaka mingi ya kupata ujuzi au kukuza talanta. Unaweza kufanya kazi kwa bidii hadi izoeleke kwako. Lakini kama unafikiri hiyo inamaanisha uache kufanya mazoezi na kujifunza, taratibu unapoteza maarifa na uwezo ambao uliupata hapo awali kwa gharama kubwa.

Hii ni kwa ujuzi kama kujifunza lugha, kupiga kifaa cha muziki na kuendesha ndege. Pia inatumika katika kuwa mwanafunzi wa Kristo.

Kwa neno jepesi, uanafunzi huhitaji nidhamu.

Sio juhudi ya kawaida, na haitokei kwa ajali.

Imani katika Yesu Kristo ni zawadi, lakini kuipokea inahitaji uchaguzi wa dhahiri ambao unahitaji dhamira ya “uwezo, akili na nguvu” zetu zote. Ni tendo la kila siku. Kila saa. Inahitaji mafunzo ya mara kwa mara na dhamira madhubuti. Imani yetu, ambayo ni utiifu wetu kwa Mwokozi, huwa imara pale inapojaribiwa dhidi ya upinzani tunaokutana nao hapa duniani. Imani hustahimili kwa sababu tunaendelea kuilisha, kuendelea kuitumia na kutokata tamaa.

Kwa upande mwingine, ikiwa tunashindwa kutumia imani na na nguvu zake za kusadikisha, tunakuwa na uhakika dhaifu wa vitu tulivyoviona vitakatifu—ujasiri hafifu kwa vitu tulivyojua awali kuwa kweli.

Majaribu ambayo kamwe hayangeweza kutuvutia yanaanza kuonekana ya kuogofya tu kidogo na ya kuvutia zaidi.

Makali ya moto wa ushuhuda wa jana unatupatia joto kwa muda tu. Makali hayo yanahitaji lishe endelevu ili kuendelea kuwa angavu.

Katika agano jipya, Mwokozi anafundisha mfano kuhusu bwana aliyempa kila mtumishi wake tumaini tukufu—kiasi cha pesa kiitwacho talanta. Watumishi waliotumia kwa bidii talanta zao walizikuza. Mtumishi ambaye alizika talanta yake hatimaye aliipoteza.

Somo la kujifunza? Bwana anatupatia vipawa—vya maarifa, vya uwezo, vya fursa—na anatutaka kuvitumia na kuvikuza ili vitubariki sisi na kuwabariki watoto Wake wengine. Hiyo haitatokea kama tukiviweka juu ya kabati kama tuzo ya kutamania kila wakati. Vipawa vyetu hukua na kuongezeka pale tunapovitumia tu.

Wewe una Kipawa

“Lakini Mzee Uchtdorf,” unaweza kusema, “sina kipawa au talanta—angalau chenye thamani hiyo.” Labda unawaangalia wengine ambao vipawa vyao ni dhahiri na vinavutia na unahisi wewe ni wa kawaida tu. Unaweza kudhani kwamba katika maisha kabla ya hapa duniani, katika karamu ya siku ya vipaji vikuu na talanta, sahani yako ilionekana ina kidogo—hasa ukilinganisha na sahani za wengine zilizosheheni na kumwagika.

Ee, ni kiasi gani natamani ningekukumbatia na kukusaidia kuelewa ukweli huu mkuu: Wewe ni binadamu wa nuru uliyebarikiwa, mwana wa kiroho wa Mungu asiye na mwisho! Na unabeba ndani yako uwezekano zaidi ya uwezo wako wa kufikiria.

Kama washairi walivyosema, unakuja duniani kwa “utukufu binafsi wa uungu”!

Chanzo cha hadithi yako ni kitukufu, vivyo hivyo na mwisho wako. Uliondoka mbinguni kuja hapa, lakini mbingu kamwe hazijakuacha!

Wewe ni zaidi ya mtu wa kawaida.

Wewe una kipawa!

Katika Mafundisho na Maagano, Mungu anatangaza:

“Kwani kuna vipawa vingi, na kwa kila [mtu] kipawa kimetolewa na Roho wa Mungu.

“Kwa wengine wamepewa kimoja, na wengine wamepewa kingine, [na] wote waweze kufaidika.”

Baadhi ya vipawa vyetu vimeorodheshwa katika maandiko. Vingi havipo.

Kama nabii mkuu Moroni alivyosema, “Msikatae karama za Mungu, kwani ni nyingi; na zinatoka kwa yule yule Mungu.” Vinaweza kujidhihirisha katika “njia tofauti … ; lakini ni yule yule Mungu azitendaye kazi zote katika wote.”

Inaweza kuwa kweli kwamba vipawa vyetu vya kiroho daima sio vya kuvutia, lakini hiyo haimaanishi si vya muhimu. Je, naweza kushiriki nanyi baadhi ya vipawa vya kiroho ambavyo nimeviona kwa waumini ulimwenguni kote? Tafakari kama umebarikiwa na moja au zaidi ya vipawa kama:

  • Kuonyesha huruma.

  • Kuwatambua watu ambao hawatambuliki.

  • Kutafuta sababu ya kuwa na shangwe.

  • Kuwa mpatanishi.

  • Kutambua miujiza midogo.

  • Kutoa maneno ya dhati ya kusifu.

  • Kusamehe.

  • Kutubu.

  • Kuvumilia.

  • Kuelezea vitu kwa urahisi.

  • Kuunganika na watoto.

  • Kuwakubali viongozi wa Kanisa.

  • Kuwasaidia wengine kuwa sehemu ya kitu.

Unaweza usione vipawa hivi vikionyeshwa kwenye maonyesho ya vipaji ya kata. Lakini natumaini mnaweza kuona jinsi vilivyo vya thamani kwenye kazi ya Bwana na jinsi unavyoweza kumgusa, kumbariki au hata kumwokoa mmoja wa watoto wa Mungu kwa kipawa chako. Kumbuka: “Kupitia vitu vilivyo vidogo na rahisi vitu vikubwa hutendeka.”

Basi tufanye kila mmoja sehemu yetu ndogo.

Fanya Sehemu Yako Ndogo

Wapendwa kaka na dada zangu, marafiki wapendwa, naomba Roho atakusaidia kutambua vipawa na talanta ambazo Mungu amekujalia. Kisha, acha sisi, kama watumishi waaminifu katika mfano wa Bwana, tuviongeze na kuvikuza.

Siku itakuja tutakaposimama mbele ya Baba yetu wa Mbinguni mwenye huruma kutoa maelezo ya uwajibikaji wetu. Atahitaji kujua tulifanyia nini vipawa alivyotupatia—hasa, jinsi tulivyovitumia kubariki watoto Wake. Mungu anatujua sisi ni nani, tumesanifiwa kuwa nani na matarajio Yake kwetu yako juu.

Lakini Yeye hatarajii sisi kupiga hatua kubwa, ya kijasiri au ya kuzidi binadamu ili kufikia hapo. Katika ulimwengu aliouumba, ukuaji hutokea taratibu na kwa uvumilivu—lakini pia ni endelevu na usiokoma.

Kumbuka, ni Yesu Kristo ambaye amekwishafanya sehemu ya kuzidi binadamu wakati aliposhinda kifo na dhambi.

Sehemu yetu ni kumfuata Kristo. Ni sehemu yetu kugeuka kutoka dhambini, kumgeukia Mwokozi na kutembea njia Yake, hatua moja kwa wakati. Tunapofanya hivi, kwa bidii na kwa uaminifu, hatimaye tunaondokana na pingu za kutokuwa wakamilifu na makosa na taratibu tunatakaswa, mpaka siku ile kamilifu tutakayokamilishwa ndani ya Kristo.

Baraka ziko ndani ya uwezo wetu. Ahadi zipo tayari. Mlango umefunguliwa. Ni chaguo letu kuingia na kuanza.

Mwanzo unaweza kuwa mdogo. Lakini hiyo ni SAWA.

Pale ambapo imani ni dhaifu, anza na tumaini katika Kristo Yesu na nguvu Yake ya kusafisha na kutakasa.

Baba yetu anatuomba tufanye changamoto hii ya imani na uanafunzi si tu kama watalii wa kawaida lakini kama waaminio wa dhati, ambao wanaiacha babilonia na kuweka mioyo yao, akili na hatua kuelekea Sayuni.

Tunajua kwamba jitihada zetu pekee haziwezi kutufikisha selestia. Lakini zinaweza kutufanya waaminifu na wenye kudhamiria kwa Yesu Kristo, na Yeye atatufikisha selestia.

Kwa sababu ya Mwokozi wetu mpendwa, hakuna kitu kama tukio lisilo la mafanikio. Kama tukiweka tumaini na imani yetu Kwake, ushindi wetu ni wa uhakika. Ametuahidi kufikia nguvu Zake, uwezo Wake, neema Yake tele. Hatua kwa hatua, kidogo kidogo, tutasonga karibu zaidi na siku hiyo kuu na kamilifu tutakapoishi pamoja Naye na wapendwa wetu katika utukufu wa milele.

Ili kufika hapo, lazima tufanye sehemu yetu leo na kila siku. Tuna shukrani kwa hatua tulizopiga jana, lakini tusikwamie hapo. Tunajua bado tuna njia ndefu ya kusonga, lakini haturuhusu hilo litukatishe tamaa.

Hicho ndicho kiini cha sisi ni nani—kama wafuasi wa Kristo.

Ninawasihi na kumbariki kila muumini wa Kanisa, na wote wanaotamani kuwa sehemu yake, kumwamini mwokozi na kujihusisha, kwa uvumilivu na kwa bidii, katika kufanya sehemu yako kwa moyo wako wote—ili furaha yako iwe kamilifu na kwamba, siku moja, utapokea vyote alivyonavyo Baba. Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Marubani wa ndege wanatakiwa kupitia mtihani kwenye mashine ya kuigiza kila miezi sita ili kutunza ujuzi wao na kufanya upya leseni zao. Mafunzo haya magumu ni takwa la kikanuni lililowekwa na mamlaka za ndege kama FAA

  2. Ona 1 Wakorintho 12:9.

  3. Moroni 10:32.

  4. “Kama vile ambavyo misuli ya mwili haiwezi kujengeka au kuendelezwa bila juhudi dhidi ya kani ya mvutano, kadhalika ukuaji wa duniani unahitaji kuweka juhudi dhidi ya majaribu ya Shetani na upinzani mwingine wa duniani” (Dallin H. Oaks, “Misaada ya Kiungu kwa ajili ya Maisha Haya,” Liahona, Mei 2025, 104).

  5. Ona Alma 32:37–43.

  6. Ona Mathayo 25:14–30. Katika siku za mwanzo za Urejesho, Bwana alirejelea mfano huu alipokuwa akiwarudi wale walioficha talanta alizowapa. Hata aliwaonya kwamba kama wataendelea kuzika talanta zao “kitachukuliwa, hata kile walicho nacho” (Mafundisho na Maagano 60:2–3).

  7. Wakati mwingine tunasisitiza kupita kiasi umuhimu wa vipawa na talanta kwa kuangalia jitihada iliyopo Mmoja wa waandishi waliofanikiwa wa wakati wetu aliandika: “Ndio kunapaswa kuwe na talanta iliyohusika, lakini talanta ni bidhaa nafuu sana, nafuu kuliko chumvi ya mezani. Kile kinachotenganisha mtu mwenye talanta kutoka yule aliyefanikiwa ni kazi kwa bidii na kujifunza, mchakato endelevu wa kujinoa” (Stephen King, Danse Macabre [2011], 88).

  8. “Ode: Intimations of Immortality from Recollections of Early Childhood,” The Poetical Works of William Wordsworth (1835), 249.

  9. Mafundisho na Maagano 46:11–12.

  10. Moroni 10:8).

  11. Miaka iliyopita, Mzee Marvin J. Ashton wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitoa ujumbe mkuu kuhusu baadhi ya vipawa ambavyo havionekani sana (ona “There Are Many Gifts,” Ensign, Nov. 1987, 20–23).

  12. Alma 37:6.

  13. Ona Wakolosai 3:23; Mafundisho na Maagano 64:34.

  14. Ona Mafundisho na Maagano 50:24.

  15. Ona Mwongozo wa Maandiko, “Haki ya Kujiamulia.”

  16. Ona Mafundisho na Maagano 84:38.