Nguvu ya Kumhudumia Yule Mmoja
Kila tunapomhudumia yule mmoja, tunamwalika huyo mmoja kuja kwa Kristo na kuabudu katika nyumba ya Bwana.
Akina dada na kaka, asanteni kwa kujitoa kwenu kwa uaminifu kuja kwa Yesu Kristo kwa nyakati hizi zenye changamoto. Ninyi ni wa kusitajabisha; ni warembo; kila mmoja ni mtoto wa Mungu. Ni sala yangu kuwa tutaweza kutambua msukumo wa Roho Mtakatifu kila tunapotaka kuwa na kuwasaidiana kila mmoja kuwa wafuasi wa Yesu Kristo waliojitoa na kuhisi shangwe Yake tunapoabudu katika nyumba ya Bwana.
Rais Russell M. Nelson ameshauri: “Sasa ni wakati wako na mimi wa kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Sasa ni wakati wa kufanya ufuasi wetu kuwa kitu cha kipaumbele. Katika ulimwengu uliojaa vivuruga mawazo vya kuleta kizunguzungu, tunawezaje kufanya hili?
Alitoa jibu: “Kuabudu hekaluni mara kwa mara kutatusaidia. Katika nyumba ya Bwana, tunafokasi kwa Yesu Kristo. … Tunakuja kumjua Yeye. … Kila mtafutaji wa dhati wa Yesu Kristo atampata hekaluni.”
Hivyo, tunakuwa vipi na kuwasaidia wengine kuwa wafuasi wa Yesu Kristo waliojitoa na kuhisi shangwe yake tunapoabudu katika nyumba ya Bwana? Tunamhudumia yule mmoja. Kuhudumu katika njia ya Mwokozi kunajumuisha huruma, wema, uvumilivu na upendo usiohukumu. Tunapomhudumia yule mmoja, tunamwalika huyo mmoja kuja Yesu Kristo na kuabudu katika nyumba ya Bwana kupokea nguvu Zake za kuokoa. Kwa maneno mengine, tunasaidiana kila mmoja kuwa wanafunzi waliojitoa tunapomhudumia yule mmoja katika njia zinazoelekeza katika nyumba ya Bwana.
Tunajifunza kutoka kwa Yesu Kristo nguvu za kumhudumia yule mmoja kwa upendo na bila kuhukumu. Unamkumbuka mwanamke Msamaria kisimani. Mwanamke huyu huenda alijihisi asiye wa thamani, mpweke, aliyekata tamaa na asiyeonekana. Yawezekana alihisi asiyekuwa sehemu ya watu. Katika maisha yake yote amekuwa na wanaume watano, na mwanaume aliyekuwa akiishi naye hakuwa mme wake. Wengine huenda walimhukumu isivyo haki bila kujua hali ya maisha yake. Huenda hii ikawa sababu ya kuja kisimani peke yake wakati wa jua kali la siku. Na bado, alikuwa mwanamke wa kwanza ambaye Yesu Kristo alimtangazia kuwa Yeye ni Masiya. Kwa Yesu, mwanamke huyu alikuwa ni binti wa Mungu.
Yesu Kristo alimfundisha mwanamke huyo kwamba kupitia Kwake mtu anaweza kupokea uzima wa milele kwa kunywa maji ya uzima. Alitamka, “walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi … hataona kiu milele; bali [yatakuwa] chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.”
Mwanamke wa Samaria alihisi upendo wa Mwokozi na kupokea ushuhuda kupitia Roho kwamba alikuwa Masiya. Baada ya ushuhuda huu, alirudi mjini na kuwaalika wengine kuja na kuona, na wengi waliamini kwamba Yesu “hakika ni Kristo, Mwokozi wa dunia.” Yesu alimhudumia yule mmoja kwa upendo, matokeo yake, wengine walikuwa wafuasi wake waliojitoa.
Tunajifunza nguvu za uhudumiaji kwa yule mwenye upendo wa dhati kutoka kwa Mitume wa Kristo Petro na Yohana. Unamkumbuka mtu mmoja, aliyekuwa kilema tangu kuzaliwa kwake akilala kila siku kwenye lango la hekalu akiomba hela. Mwanaume huyu huenda alijihisi sio wa muhimu, mpweke, aliyekata tamaa, na asiyeonekana. Yawezekana alihisi kutokuwa sehemu ya watu.
“Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.”
Petro alimshika mwanaume kwa mkono wake wa kuume, akamwinua juu, na mwanaume yule akafanywa mzima. Mara tu baada ya muujiza, mwanaume akaingia ndani ya hekalu pamoja na Petro na Yohana, “akitembea, akirukaruka, na kumsifu Mungu” Petro na Yohana walimhudumia yule mmoja katika njia ambazo zilielekeza katika nyumba ya Bwana, na mwanaume huyu akawa mwanafunzi aliyejitoa wa Yesu Kristo.
Rafiki zangu, zimekuwepo nyakati katika maisha yangu ambapo nami nilijihisi asiyefaa, mpweke, kukata tamaa na kutoonekana. Nimehisi kama kutokuwa sehemu ya watu. Nimekuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho tangu nilipokuwa na umri wa miaka 19. Mwaka mmoja baadaye,nilikubali wito wa kutumika kama mmisionari kijana, ingawa kulikuwa na mengi ambayo nilikuwa bado sijajifunza kuhusu Historia ya Kanisa.
Mapema katika huduma yangu ya misioni, nilijifunza kwamba kulikuwa na kipindi kwamba wale Weusi wenye asili ya Afrika hawakuruhusiwa kufurahia baraka zote za kuabudu katika nyumba ya Bwana. Kulijua hili kwa mara ya kwanza kuliniletea hisia za hasira, kuchanganyikiwa, mashaka na woga. Hisia hizi zilikuwa kubwa mno kwamba uwezo wangu wa kumtambua Roho Mtakatifu ulipotea kwa kipindi fulani.
Kwa bahati nzuri, nilikuwa na mmisionari mwenza mzuri, Kevin Vick, aliyenihudumia kwa upendo, uvumilivu na upole. Kila usiku alipokuwa akishuhudia hisia zangu za mashaka na kutokuwa na hakika, angesema tu kwa kijana Mzee Johnson, “nakupenda.” Baada ya wiki mbili, nilijiruhusu mwenyewe kuhisi upendo wa Kevin. Nilipata ujarisi wa kusali kwa Baba wa Mbinguni katika jina la Yesu Kristo. Kadiri nilivyosali, nilivutwa kwenye mlango wa 6 wa Mafundisho na Maagano, mistari ya 21–23, iliyosema:
“Tazama, Mimi ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. … Mimi ni nuru ing’aayo gizani. …
“… Rejesha mawazo yako juu ya usiku ule uliponililia katika moyo wako, kwamba uweze kujua ukweli wa mambo haya.
“Sikusema amani akilini mwako kuhusiana na jambo hili? Ni ushahidi gani mkubwa zaidi unaoweza kupata kuliko kutoka kwa Mungu?”
Nilipokuwa nikisoma, nilikumbuka. Nilikumbuka siku niliyofunga na kusali kujua kwamba kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu, na kwamba Joseph Smith ni Nabii wa Urejesho. Nilikumbuka maagano niliyofanya kwenye nyumba ya Bwana ambayo yaliniunganisha kwa Yesu Kristo katika njia ya kibinafsi na ukaribu. Nilihisi upendo wa Mwokozi, huruma Yake, na hakikisho Lake kuwa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme Wake hapa duniani na ni muhimu kutuandaa sisi kwa Ujio Wake wa Pili. Kwa sababu nilikumbuka, niliweza tena kumtambua Roho Mtakatifu na kuelewa kabisa kwamba Yesu ndiye Kristo na mimi ni mfuasi Wake.
Wakati mwingine tutakuwa na maswali yasiyo na majibu na hisia za kuwa wasio na umuhimu, kukata tamaa, wapweke, na wasioonekana. Hata hivyo, rafiki zangu, tunapaswa kusonga mbele kwa imani katika Yesu Kristo na kukumbuka maneno yake:
Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”
Mimi ni shahidi wa uhalisia huu na baraka zilizoahidiwa za Mwokozi.
Kwa hiyo, tunaweza kufanya nini ili kuhakikisha kuwa huduma yetu kwa yule mmoja katika njia ya Mwokozi inakuwa inafaa zaidi? Kuishi mafundisho ya Kristo kutatusaidia. Kuishi mafundisho ya Kristo kama Rais Nelson alivyoelezea “kunaweza kuzalisha mzunguko imara zaidi, ukitengeneza kasi ya kiroho katika maisha yetu.”
Kadiri tunavyojitahidi kuishi sheria za juu za Yesu Kristo … Mwokozi anatuinua juu ya mvuto wa ulimwengu huu ulioanguka kwa kutubariki kwa hisani kuu, unyenyekevu zaidi, ukarimu zaidi, wema zaidi, nidhamu binafsi, amani na pumziko.”
“Msukumo [huu wa kiroho] unaozalishwa kwa kuishi mafundisho ya Kristo” kama anavyoelezea Mzee Dale G. Renlund, “si tu hutoa nguvu kwa ajili ya badiliko la asili yetu ya kiungu kuwa hatma yetu ya milele, bali pia hutuhamasisha kuwasaidia [kuwahudumia] wengine katika njia zifaazo.” Mzee Renlund anatukumbusha kwamba “kazi ya Mwokozi ni kuponya [kutufanya wazima]. Kazi yetu ni kupenda—kupenda na kuhudumia katika njia ambayo wengine wanavutwa karibu na Yesu Kristo.”
Uwezo wetu wa kuishi mafundisho ya Kristo utaboreshwa kwa kujifunza kwetu kitabu cha Mormoni kila siku na kupokea sakramenti kila wiki. Rais Nelson alitamka kwamba Kitabu cha Mormoni “hufundisha mafundisho ya Kristo … [na] hutoa uelewa kamili na wenye nguvu juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo unaoweza kupatikana sehemu yoyote.” Ninakipenda kitabu hiki. Na kwa maombi kupokea ibada ya sakramenti kila wiki huongeza uelewa wetu juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo na kutoa utakaso wa kiroho, faraja na nguvu za uungu katika maisha yetu. Kumbuka,”katika ibada za [ukuhani], nguvu za uungu zinadhihirishwa,” na nguvu hizi ambazo huja kutoka kwa Yesu Kristo, huimarisha matamanio yetu na uwezo wetu wa kumhudumia yule mmoja.
Kujifunza kwangu Kitabu cha Mormoni na kupokea sakramenti hupunguza hisia za kukatishwa tamaa, huongeza azimio langu la kumhudumia yule mmoja katika njia ya Mwokozi, na husaidia kufanya uanafunzi wangu kuwa kipaumbele changu cha juu.
Rafiki zangu, naahidi kwamba kadri tunavyoishi mafundisho ya Yesu Kristo na kumhudumia yule mmoja katika njia ambayo huongoza katika nyumba ya Bwana, tutasonga mbele kwa imani katika Yesu Kristo hata katikati ya maswali yasiyojibika na hisia za kutokuwa wa muhimu, upweke, kukata tamaa na kutoonekana. Tutamwalika kila mmoja kuja kwa Yesu Kristo na kuabudu katika nyumba ya Bwana ili kupokea nguvu Zake okozi na upendo. Katika nyumba ya Bwana, “tutahisi huruma ya [Mwokozi]. Tutapata majibu ya maswali yetu magumu. Na tutaweza kuelewa zaidi shangwe ya injili Yake.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.