2025
Kushangiliana
Novemba 2025


11:53

Kushangiliana

Ni Bwana pekee anafahamu ukomo na uwezo wetu binafsi, na kwa sababu ya hilo, ni Yeye pekee aliyestahili kikamilifu kuhukumu utendaji wetu.

Hivi karibuni nilisoma juu ya uzoefu ulionigusa kwa kina. Ulitokea kwenye Shindano la Riadha na Michezo ya Ndani ya Marekani—shindano la wazee.

Mmoja wa washiriki kwenye tukio la mita 1,500 alikuwa Orville Rogers mwenye miaka 100. Mwandishi anaandika:

“Mwanzishaji alipotoa ishara, wakimbiaji walipiga mbio, Orville akiwa karibu kabisa na mwisho, ambapo alibaki peke yake kwa muda wote wa mbio akiburuza miguu taratibu. [Wakati] mkimbiaji wa mwisho pembeni ya Orville alipomaliza, Orville bado alikuwa na mizunguko miwili na nusu ya kukamilisha. Takriban watazamaji 3,000 waliketi kwa utulivu wakimtazama akizunguka taratibu—kwa ukamilifu, kimya kimya na peke yake.

“[Lakini] alipoanza mzunguko wake wa mwisho, umati ulisimama wima, wakishangilia na kupiga makofi. Wakati alipofikia sehemu ya kuhitimisha, umati ulikuwa ukipiga kelele za shangwe. Kwa ushangiliaji wa kutia moyo wa maelfu ya watazamaji, Orville alivuta pumzi yake yote ya akiba. Umati ulilipuka kwa shangwe pale alipovuka mstari wa mwisho na alikumbatiwa na washindani wake. Orville kwa unyenyekevu na shukrani aliwapungia umati na kutembea kutoka uwanjani akiwa na rafiki zake wapya.”

Hizi zilikuwa mbio za tano za mashindano ya Orville, na kwenye kila tukio lililopita alishika pia nafasi ya mwisho. Baadhi wangejaribiwa kumhukumu Orville, wakidhani kwamba hakupaswa kushindana katika umri wake—kwamba hakustahili kuwa uwanjani kwa sababu alifanya matukio yake yawe marefu sana kwa kila mtu mwingine.

Lakini japokuwa siku zote alikuwa wa mwisho, Orville alivunja rekodi tano za ulimwengu siku hiyo. Hakuna aliyemtazama angeamini hilo lingewezekana, lakini si watazamaji wala washindani wenzake walikuwa majaji. Orville hakuvunja sheria yoyote, na viongozi hawakushusha kiwango chochote. Alikimbia mbio zilezile na kutimiza vigezo sawa kama washindani wengine wote. Lakini kiwango chake cha ugumu—katika hali hii, umri wake na uwezo wa kimwili wenye ukomo, vilizingatiwa kwa kumweka katika kipengele cha wenye umri wa miaka 100+. Na katika kipengele hicho, alivunja rekodi tano za ulimwengu.

Kama vile Orville alivyobeba ujasiri wa kuingia kwenye uwanja ule kila mara, inahitaji ujasiri mkubwa kwa baadhi ya dada zetu na kaka zetu kuingia kwenye changamoto za maisha kila siku, wakijua wanaweza kuhukumiwa pasipo haki hata ingawa wanafanya kila wanaloweza dhidi ya vikwazo vya kumfuata Mwokozi na kuheshimu maagano yao na Yeye.

Popote tunapoishi ulimwenguni, licha ya umri wetu, ni hitaji la msingi la mwanadamu kwetu sote kuhisi hisia ya kuwa sehemu ya, kuhisi kwamba tunatakiwa na kuhitajika na kwamba maisha yetu yana lengo na maana, licha ya hali zetu na ukomo wetu.

Kwenye mzunguko wa mwisho wa mbio, umati bila kuchoka ulimshangilia Orville, wakimpa nguvu ya kuendelea kukimbia. Haikujalisha kwamba alimaliza wa mwisho. Kwa washiriki na umati, hili lilikuwa zaidi ya shindano. Katika njia nyingi, huu ulikuwa mfano wa kupendeza wa upendo wa Mwokozi katika matendo. Wakati Orville alipomaliza, wote walifurahia pamoja.

Kama vile Mashindano ya Riadha, mikusanyiko yetu, na familia zinaweza kuwa mahala pa kusanyiko ambapo tunashangiliana—jumuiya ya maagano inayotiwa ari kwa upendo wa Kristo kwa kila mmoja—inayosaidiana kushinda changamoto zozote zinazotukabili, tukipeana nguvu na kuhimizana bila kuhukumiana. Sote tunahitajiana. Nguvu ya kiungu hutokana na umoja, na ndiyo maana Shetani ana nia ya kututenganisha.

Kwa bahati mbaya, kwa baadhi yetu, kuhudhuria kanisani nyakati zingine inaweza kuwa jambo gumu kwa sababu kadha wa kadha. Yaweza kuwa mtu anapambana na maswali ya imani au mtu ana wasiwasi au msongo wa mawazo. Yaweza kuwa mtu kutoka nchi tofauti, au mbari, au mtu mwenye uzoefu tofauti wa maisha au jinsi ya kuona mambo ambaye anahisi yuko tofauti na wengine. Yaweza kuwa wazazi waliokosa usingizi na wanaopambana na hekaheka za malezi ya watoto wadogo au mtu ambaye ni mseja katika mkusanyiko uliojaa wanadoa na familia. Yaweza kuwa pia mtu anajipa ujasiri wa kurudi baada ya miaka mingi ya kuwa mbali au mtu mwenye hisia za hofu kwamba hawastahili na kamwe hawatakuwa sehemu ya.

Rais Russell M. Nelson alisema: “Kama wanandoa katika kata yako wakitalikiana, au mmisionari akirejea nyumbani mapema, au kijana akiwa na wasiwasi na ushuhuda wake, hawahitaji hukumu yako. Wanahitaji kupata upendo msafi wa Yesu Kristo unaoakisiwa katika maneno na matendo yako.”

Uzoefu wetu kanisani umekusudiwa kutoa miunganiko muhimu na Bwana na kila mmoja wetu ambayo inahitajika sana kwa ajili ya ustawi wetu kiroho na kihisia. Yenye asili katika maagano tunayofanya na Mungu, tukianza na ubatizo, ni jukumu letu la kupendana na kujaliana kama washiriki wa familia ya Mungu, washiriki wa mwili wa Kristo, na si tu kuweka vema ndani ya kisanduku cha mambo tunayotarajia kufanya.

Upendo kama wa Kristo na kujaliana ni mambo ya juu na matakatifu. Upendo msafi wa Kristo ni hisani. Kama Rais Nelson alivyofunza, “Hisani hutusukuma ‘kubebeana mizigo’ [Mosia 18:8] badala ya kurundikiana mizigo juu ya kila mmoja.”

Mwokozi alisema, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” Na Rais Nelson aliongeza: “Hisani ni tabia ya msingi ya mfuasi halisi wa Yesu Kristo.” Ujumbe wa Mwokozi uko wazi: wanafunzii Wake wa kweli hujenga, huinua, huhamasisha, hushawishi na kutia moyo. … Jinsi tunavyozungumza na wengine na kuhusu wengine … ni muhimu sana.”

Fundisho la Mwokozi juu ya hili ni rahisi sana. Limefupishwa katika Sheria ya Dhahabu: Watendee wengine vile ambavyo wewe ungetaka utendewe. Jiweke kwenye nafasi ya mtu yule na watendee jinsi ambavyo wewe ungetaka utendewe ikiwa ungekuwa kwenye nafasi yao.

Kutenda kama Kristo kwa wengine huenda mbali zaidi ya familia zetu na mikusanyiko yetu. Kunawajumuisha akina dada na kaka zetu wa imani zingine au wasio na imani kabisa. Kunawajumuisha akina kaka na dada zetu kutoka nchi zingine na tamaduni zingine, vile vile wale wa mrengo mwingine kisiasa. Sisi sote ni sehemu ya familia ya Mungu, na Yeye anawapenda watoto Wake wote. Yeye anatamani kwamba watoto Wake wampende Yeye na pia wapendane.

Maisha ya Mwokozi yalikuwa mfano wa kupenda, kukusanya, na kuinua hata wale ambao jamii iliwahukumu kama waliokataliwa na wachafu. Mfano Wake ndiyo tulioamriwa kuufuata. Tuko hapa kukuza sifa kama za Kristo na hatimaye tuwe kama Mwokozi wetu. Injili Yake si injili ya kuweka vema; ni injili ya kuwa—kuwa kama Yeye alivyo na kupenda kama Yeye anavyopenda. Yeye anatutaka tuwe watu wa Sayuni.

Nilipokuwa mwishoni mwa miaka ya 20, nilipitia kipindi cha msongo wa mawazo, na katika kipindi hicho, ilikuwa kana kwamba uhalisia kwamba Mungu yupo ulikuwa umepotea. Siwezi kuelezea hisia kwa ukamilifu zaidi ya kusema tu kwamba nilihisi kupotea kabisa. Tangu nikiwa mtoto, daima nilikuwa nimejua kwamba Baba yangu wa Mbinguni alikuwepo na kwamba ningeweza kuzungumza Naye. Lakini kipindi hicho, sikujua tena ikiwa kulikuwa na Mungu. Sikuwahi kupitia chochote kama hicho kabla katika maisha yangu, na ilikuwa kama msingi wangu wote ulikuwa ukiporomoka.

Kama matokeo, ilikuwa vigumu kwangu kuhudhuria kanisani. Nilienda, lakini ilikuwa kwa sehemu tu kwa sababu niliogopa kubandikwa jina la “asiyeshiriki kikamilifu” au “asiye mwaminifu sana,” na nilihofia kuwa mtu wa kufuatiliwa na mtu mwingine. Kile hasa nilichokihitaji wakati ule kilikuwa kuhisi upendo wa dhati, ulelewa wa dhati, na usaidizi kutoka kwa wale walio karibu nami, si hukumu.

Baadhi ya mawazo niliyohofia watu wangekuwa nayo kuhusu mimi, mimi mwenyewe nimeyawaza kuwahusu wengine wakati wao walipokosa kuhudhuria kanisa kila mara. Uzoefu binafsi mchungu ulinifunza baadhi ya masomo ya thamani kuhusu kwa nini tumeamriwa kutohukumu pasipo haki.

Je, kuna wale kati yetu wanaoteseka kimya kimya, wakihofia wengine kujua mapambano yao yaliyofichika kwa sababu hawajui mwitikio utakuwaje?

Ni Bwana pekee ajuaye kikamilifu kiwango cha ugumu ambacho kupitia hicho tunakimbia mbio zetu za maisha—mizigo, changamoto, na vikwazo vinavyotukabili ambavyo mara nyingi wengine hawavioni. Ni Yeye pekee anaelewa majeraha ya kubadili maisha na wasiwasi ambao baadhi yetu tumeupata katika kipindi kilichopita ambao bado unatuathiri sasa.

Mara nyingi hata tunajihukumu wenyewe kwa ukatili, tukidhani tunapaswa kuwa mbali sana kwenye mbio. Ni Bwana pekee anafahamu ukomo na uwezo wetu binafsi, na kwa sababu ya hilo, ni Yeye pekee anayestahili kikamilifu kuhukumu utendaji wetu.

Akina dada na akina kaka, hebu tuwe kama wale watazamaji katika hadithi na kushangiliana katika safari yetu ya ufuasi bila kujali hali zetu! Hilo halituhitaji tuvunje sheria au kushusha viwango. Hakika ni amri ya pili iliyo kuu—kuwapenda jirani zetu kama nafsi zetu. Na kama Mwokozi wetu alivyosema, “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo … mlinitendea mimi,” kwa mema au mabaya. Yeye pia ametuambia, “Kama hamna umoja ninyi siyo wangu.”

Kutakuwa na nyakati katika maisha ya kila mmoja wetu ambapo tutakuwa watu tunaohitaji usaidizi na kutiwa moyo. Hebu tuweke ahadi sasa ya daima kufanya hivyo kwa kila mmoja. Tunapofanya hivyo, tutajenga umoja mkuu na kuruhusu nafasi kwa ajili ya Mwokozi kufanya kazi Yake takatifu na kumbadilisha kila mmoja wetu.

Kwa kila mmoja wenu anayeweza kuhisi amebaki nyuma katika mbio hizi za maisha, safari hii ya duniani, tafadhali endelea kusonga. Ni Mwokozi pekee anayeweza kuhukumu ni wapi unapaswa kuwa katika wakati huu, na Yeye ni mwenye huruma na mwenye haki. Yeye ni Mwamuzi Mkuu wa mbio za maisha, na ni Yeye pekee anaelewa kikamilifu kiwango cha ugumu ambacho kupitia hicho unakimbia au kutembea au kuburuza miguu. Yeye atazingatia ukomo wako, uwezo wako, uzoefu wako wa maisha, na mizigo iliyojificha unayoibeba, vilevile matamanio ya moyo wako. Wewe vilevile kiuhalisia unaweza kuwa umevunja rekodi za kiishara za dunia. Tafadhali usipoteze tumaini. Tafadhali endelea kusonga! Tafadhali baki! Wewe ni wa mahala hapa! Bwana anakuhitaji, na sisi tunakuhitaji!

Popote unapoishi ulimwenguni, bila kujali ni mbali kiasi gani, tafadhali daima kumbuka kwamba Baba yako wa Mbinguni na Mwokozi wako wanakujua na kukupenda kikamilifu. Wewe kamwe haujasahaulika Kwao. Wanataka kukuleta nyumbani.

Weka macho yako kwa Mwokozi. Yeye ni fimbo yako ya chuma. Usimwache Yeye. Ninashuhudia kwamba Yeye yu hai na wewe unaweza kumtumaini Yeye. Ninashuhudia pia kwamba Yeye anakushangilia.

Na wote tufuate mfano wa Mwokozi na kushangiliana, ni sala yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Jeffrey C. Strong, ulinganifu binafsi; imetumiwa kwa ruhusa.

  2. Moja ya vipaumbele vya urais wetu imekuwa ni kwa akina dada kupata hisia ya kuwa sehemu ya, wanapokuwa kanisani na hasa kwenye Muungano wa Usaidizi. Nimepata nafasi nyingi za kusoma barua na kusikia uzoefu ambao umenihuzunisha kwa kiasi kikubwa.

  3. Ona 1 Wakorintho 12:26.

  4. Ona Henry B. Eyring, “Mioyo Iliyofumwa kama Kitu Kimoja,” Liahona, Nov. 2008, 68–71; ona pia Ulisses Soares, “Wamoja katika Kristo,” Liahona, Nov. 2018, 37–39; “One in Christ” (video), Gospel Library.

  5. Ona 3 Nefi 11:29.

  6. Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” Liahona, Mei 2023, 100. Katika hubiri hilohilo, alisema kwamba “mabishano humfukuza Roho—kila mara.”(ukurasa wa 100). Ninaweza kuongeza kwamba mawazo ya hukumu kuhusu wengine yanaweza kumfukuza roho vilevile. Tunapowadharau wengine kwa mawazo ya kukosoa, huo ni ushahidi wa kiburi, na Rais Jeffrey C. Strong, amesema kwamba “kiburi ni adui mkubwa wa umoja” (“Our Hearts Knit as One,” 70).

  7. Ona J. Anette Dennis, katika “Njooni na Mchukue Nafasi Yenu kama Wanawake wa Maagano” (mahubiri yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Wanawake huko Chuo Kikuu cha Brigham Young, Mei 1, 2024), Gospel Library; ona pia Mosia 18:8–10.

  8. Ona 1 Wakorintho 12:14–26.

  9. Ona Moroni 7:47.

  10. Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” 101; msisitizo umeongezwa.

  11. Yohana 1:35; msisitizo umeongezwa.

  12. Ona Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” 100, 99.

  13. Ona Mathayo 7:12.

  14. Tunapomfuata Mwokozi na kutamani kuwa kama Yeye, tutajitahidi kumwona kila mtu jinsi Yeye anavyowaona, na tunapoendelea kusali kwa ajili ya kipawa cha hisani, hisia za dhati za upendo na kujali zinaweza hatimaye kukua ndani ya mioyo yetu. Tutakuza tamanio la “kujenga, kuinua, kuhimiza, kushawishi, na kuvuvia” wengine, si kwa hisia ya jukumu bali kwa sababu tunapiga hatua kidogo kidogo kuwa kama Mwokozi wetu (Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” 100). Kuhudumu kama Kristo kwa wengine kutakuwa sehemu ya utu wetu, si kile ambacho sisi tunafanya.

  15. Ona Mosia 23:15.

  16. Ona, kwa mfano, Mathayo 9:10–13; Marko 1:40–42; Luka 8:43–48; 14:13–14; Yohana 4:7–26; 5:2–9; 8:3–11.

  17. Ona 3 Nefi 27:27; ona pia Robert C. Gray, “Kujichukulia Juu Yetu Jina la Yesu Kristo,” Liahona, Nov. 2018, 97–100.

  18. “Suluhisho pekee la kudumu kwenye tofauti zinazotugawa ni kwa sisi sote kufuata mafundisho ya Mwokozi wetu na kuwa kidogo kidogo kama Yeye alivyo” (Dallin H. Oaks, katika Joel Randall, “Following Christ Is ‘a Continuous Commitment and Way of Life,’ President Oaks Teaches European Saints from Belgium,” Church News, Tuesday, July 14, 2025).

  19. Ona Dallin H. Oaks, “Changamoto ya Kuwa,” Liahona, Jan. 2001, 40–43.

  20. Ona Yohana 13:34.

  21. “Wito wa ufafanuzi kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni kujitahidi kuwa watu wa Sayuni ambao wana moyo mmoja na nia moja na wanaoishi katika haki” (Quentin L. Cook, “Mioyo Iliyounganishwa Pamoja katika Umoja na Haki,” Liahona, Nov. 2020, 21).

  22. Ona J. Anette Dennis, “Why I Choose to Stay” (mahubiri yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Wanawake huko Chuo Kikuu cha Brigham Young Mei 2, 2024), Gospel Library.

  23. Ona Tafsiri ya Joseph Smith, Mathayo 7:1–2 (katika Mathayo 7:1, tanbihi a); Alma 41:14.

  24. Ona J. Anette Dennis, “Nira Yake ni Laini na Mzigo Wake ni Mwepesi,” Liahona, Nov. 2022, 80–81.

  25. Ona Alma 7:11–12.

  26. Ona Mathayo 22:36–40.

  27. Mathayo 25:40

  28. Mafundisho na Maagano 38:27.

  29. Ona Zaburi 145:8–9; Waefeso 2:4–5.

  30. Ona Tamara W. Runia, “Toba Yako Haimchoshi Yesu Kristo; Inaongeza Shangwe Yake,” Liahona, Mei 2025, 91.

  31. Ona Mafundisho na Maagano 137:9.

  32. Ona Warumi 8:38–39.

  33. Ona pia Patrick Kearon, “Kusudi la Mungu Ni Kukuleta Nyumbani,” Liahona, Mei 2024, 87–89.

  34. Ona Yohana 1, kichwa cha habari cha sura na mstari wa 1; 1 Nefi 11:24–25.

  35. Ona Jeffrey R. Holland, “Kesho Bwana Atafanya Miujiza Miongoni Mwenu,” Liahona,, Mei 2016, 127.