Uelekeze Moyo Wako kwa Yesu Kristo: Zawadi Takatifu ya Muziki wa Watoto
Nyimbo za Watoto ni mahubiri kwa wanafunzi wa Yesu Kristo, shuhuda kwenye ukweli wa injili iliyorejeshwa, na sala zilizofanywa kuwa muziki.
Moja ya baraka zangu kwa Watoto ni kwamba moyo wangu umejifunza kupenda watu wa lugha nyingi ambazo mimi sizizungumzi. Nimepata shangwe katika kuunganika na Watakatifu wenzangu kupitia lugha moja ya muziki mtakatifu. Na hususan kupitia nyimbo rahisi za Watoto, Roho Mtakatifu amevuka vizuizi vya lugha na kuujaza moyo wangu kwa minong’ono Yake. Katika sauti za watoto, upendo wa Mungu na Mwanaye, Yesu Kristo, umetangazwa katika ukweli msafi, unaopenya.
Ingawa sikukulia Darasa la Watoto, Roho amenifunza kwa haraka utakatifu wa nyimbo zake, na zimekuwa sehemu ya kuabudu kwangu binafsi. Nyimbo za Watoto zimebeba ushawishi mtakatifu katika maisha yangu na zimeiinua nafsi yangu, zimenifunza kweli za milele, na kunileta karibu na Mwokozi na injili Yake.
Rais Dallin H. Oaks aliwahi kufunza kwamba “Kuimba nyimbo za dini ni njia mojawapo bora za kujifunza mafundisho ya injili iliyorejeshwa.” Maneno hayo ni kweli kwetu sote lakini ni kweli hususan kwa watoto. Muziki wa Watoto ni moja ya nyenzo za upendo za Mungu kwa ajili ya kupanda mbegu za ushuhuda ndani ya mioyo ya wanafunzi wadogo wa Mwokozi. Wazazi, viongozi, na walimu hutoa virutubisho kwa mbegu hiyo pale wanaposhuhudia na kualika shuhuda za watoto juu ya yote wanayoyajua kuhusu Baba wa Mbinguni, Mwanaye, Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu.
Katika miaka hii kadhaa ya mwisho ya huduma yangu, nimetumia muda kuimba na kujifunza muziki wa Watoto wakati nikitafakari maswali kadhaa:
-
Ni kwa jinsi gani nyimbo za Watoto zilizoimbwa utotoni huwa lugha ya kiroho watoto wanayoitumia kushuhudia kwa kipindi cha maisha yao yote?
-
Ni kwa jinsi gani kuimba kweli za injili huwasaidia watoto wamkumbuke Bwana kama sehemu ya agano lao na kuwaandaa kwa ajili ya ibada Zake?
-
Na ni kwa jinsi gani nyimbo za Watoto husaidia kuandika sheria ya Mungu juu ya mioyo ya wanafunzi hawa wadogo?
Wakati Darasa la Watoto lilipoanza mnamo 1878, Rais wake Mkuu wa kwanza, Aurelia Spencer Rogers, alisema “kuimba kulikuwa muhimu.” Muziki daima umekuwa kiini cha kuwafundisha watoto injili. Nyimbo za Watoto zinaweza kuwa lugha ya kwanza ya kiroho ya mtoto kwa sababu mapigo yake rahisi, ya kukumbukwa hutoa sauti kwenye kweli za injili. Nyimbo hizi hubeba nguvu ya kubaki kwa watoto kwa maisha yote, zikiwa sehemu ya uanafunzi wao na njia asilia kwao kushuhudia juu ya Mwokozi.
Kufundisha Mafundisho ya Yesu Kristo Kupitia Wimbo
Nyimbo za Watoto zinaweza pia kuwa nyenzo zenye nguvu za kufundisha mafundisho. Baadhi ya nyimbo husimulia hadithi za maisha na huduma ya Mwokozi. Zingine hufundisha kuhusu sifa Zake, kama vile imani Yake, tumaini Lake, na hisani Yake. Na nyimbo takatifu zaidi hushuhudia juu ya Upatanisho Wake usio na mwisho na upendo unaotiririka kutokana na tendo hilo la wokovu.
Nabii wa Bwana, Rais Russell M. Nelson, amefundisha: “[Muziki] unaweza kutoa ushawishi endelevu kwa wema kuanzia wanapokuwa wadogo. … Una nguvu ya kutoa lishe ya kiroho. Unayo nguvu ya uponyaji. Unayo nguvu ya kuwezesha kuabudu; kuturuhusu tutafakari juu ya Upatanisho na Urejesho wa injili ya [Mwokozi] na kanuni zake za kuokoa na ibada za kuinua. Muziki una nguvu kwa ajili yetu kuelezea mawazo ya sala na kutoa ushuhuda wa kweli takatifu.”
Kama wazazi, viongozi, na walimu, juhudi zetu hujumuisha kuwasaidia watoto wafikie baraka hizi zilizoahidiwa kwa kufundisha kwa kusudi kweli za injili katika muziki. Rais Nelson pia alifundisha kwamba “watoto wanaweza kujifunza mafundisho wakati wanapojifunza kuimba kama vile wanavyoweza kujifunza mafundisho darasani.” Nyimbo hizi zinaweza kutoa hazina ya mahubiri yaliyojaa imani ambayo huwaelekeza watoto kwa Mwokozi na kuwasaidia kukuza kujitolea kwenye injili yake.
Maandiko yanafundisha kwamba wimbo wa mwenye haki unaotoka moyoni humfurahisha Mwokozi. Ninaweza tu kujiuliza juu ya shangwe ambayo sauti za wanafunzi wadogo wa Bwana huleta. Ninajua nyimbo zao za sala hufika mbinguni kama madhihirisho ya imani ambayo humwalika Roho Mtakatifu kuthibitisha kweli za milele na kwa utulivu na taratibu kuwaalika wengine kukubali wito kutoka kwa Mwokozi wetu wa kumfuata Yeye na kuja nyumbani. Kama vile Mzee Henry B. Eyring alivyotukumbusha, ni katika nyakati hizo za kumhisi Roho ambapo tunapata ushahidi wa Upatanisho wa Mwokozi ukifanya kazi katika maisha yetu.
Kuandika Ukweli juu ya Moyo
Muziki wa watoto unaweza kuwa muujiza unaobebwa kwenye tao la maisha yote ya uanafunzi ambayo watoto wetu watayaishi. Wimbo ulioimbwa katika umri wa miaka sita una nguvu ya kubaki nasi—na unaweza kurudi miongo mingi baadaye katika nyakati za maamuzi, jaribu, huzuni, au shangwe. Pengine katika miaka yetu ya baadaye, maneno ya “Nitafuata Mpango wa Mungu” yanaweza kuwa nanga ya kiroho inayorudia ushahidi wa Mtume Paulo wa uhakika wa ahadi za Mungu kwetu. Au yanaweza kutukumbusha kwamba kwa sababu Mungu hutimiza ahadi zake, maagano Yake hutoa faraja kuu na mahala pa kimbilio na kutualika tuweke tumaini letu na hakikisho imara juu ya Yesu Kristo na nguvu Yake ya upatanisho.
Waumini watu wazima ulimwenguni kote, katika nyakati za magumu, mara nyingi hukumbuka na kugeukia nyimbo za Watoto walizojifunza wakiwa wadogo. Kwa wengi, nyimbo hizi ziliimarisha usanifu wa mwanzo wa imani yao katika Yesu Kristo na mara nyingi zilikuwa mahala pa kwanza ambapo uongofu kwenye injili Yake ulianzia. Wazazi, viongozi, na walimu walistawisha imani hiyo kwa miaka mingi kwa kufundisha, kuimba, na kushuhudia kwa watoto kwa uangalifu.
Dada mmoja alishiriki nami kwamba alithamini muziki wa watoto, na baada ya miaka 20 anaukumbuka kwa kuchochea uongofu wake endelevu kwenye injili ya Yesu Kristo. Muumini mwingine alishuhudia kwamba Darasa la Watoto lilipanda mbegu ya haradali ya imani wakati alipokuwa mdogo na ilikuwa sababu ya yeye kuweza kurejea kwenye Kanisa la Bwana akiwa na miaka 30. Mwokozi aliahidi, “Mfariji … atawafundisha mambo yote, na kuwakumbusha mambo yote.” Muziki wa Watoto unaweza kuwa njia ambayo kwayo ahadi inatimizwa.
Wimbo mwingine pendwa wa Watoto huvuta nguvu ya imani rahisi na ushuhuda wa kudumu:
Watoto wanapoimba, wanaelezea tamanio la mwanafunzi na kujifunza mpangilio wa kuishi maagano. Roho anaweza kutumia muziki kufunga kweli za milele kwenye mioyo yao yenye upendo. Na baada ya muda, watoto wanaweza kuchagua kutuni na kugeuza mioyo yao na maisha yao kumwelekea Yesu Kristo kwa kufanya na kushika maagano matakatifu na Yeye.
Kukumbuka Maagano Yetu na Kujitayarisha kwa ajili ya Ibada
Muziki mtakatifu unaweza kusaidia kuandika mafundisho ya Kristo ndani ya nafsi na kutuandaa kupokea ibada Zake. Unaunganisha mafundisho ya Mwokozi kwenye kumbukumbu yetu na kumbukumbu hiyo kwenye uanafunzi wetu Kwake.
Kama viongozi wa Watoto, tunayo fursa na jukumu takatifu la kuhakikisha kwamba muziki katika Darasa la Watoto unafunzwa kwa shangwe, kwa uelewa wa mafundisho, na kwa Roho. Hii hujumuisha kuwaalika watoto wagundue kile wanachohisi pale wanapoimba na kuwasaidia watambue kwamba hisia hizo huja kutoka kwa Roho Mtakatifu. Juhudi hizi husaidia kuwaandaa watoto wetu kwa ajili ya ibada takatifu, kama vile ubatizo na uthibitisho, vilevile kuvuvia kumbukumbu yao ya maagano wakati wanapofanya upya ahadi zao kwa Mungu mara kwa mara.
Katika Karamu ya Mwisho, baada ya Mwokozi kuanzisha sakramenti, Mathayo anaandika kwamba “nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.” Kila wiki, waumini waliobatizwa na kuthibitishwa wa Kanisa la Bwana lililorejeshwa, ikiwa ni pamoja na watoto wadogo waliobatizwa wa miaka minane, hujitayarisha kupokea sakramenti ya Bwana. Kupitia kuimba muziki mtakatifu, mkusanyiko wa watoto wa Mungu hupewa fursa ya kuiandaa mioyo yao kwa ajili ya ibada takatifu ya kujichukulia juu yao wenyewe jina Lake, daima kumkumbuka, na kushika amri Zake.
Ushuhuda wa Hitimisho
Marafiki wapendwa, ninashuhudia kwamba nyimbo za Watoto hufundisha kweli za milele na mafundisho ambayo hutuongoza kwa Yesu Kristo na injili Yake. Ninawaalika mzingatie ni kweli zipi za Watoto zimeandikwa ndani ya mioyo yenu kupitia mafundisho rahisi ya nyimbo hizi na kushuhudia kweli hizo kwa wanafunzi wadogo wa Mwokozi pale mnapowafundisha habari njema ya injili kupitia wimbo.
Ninajua kwamba Mungu Baba yetu, katika upendo Wake usio na mwisho, alimtuma Mwanaye Mpendwa duniani kutufundisha, kutuonesha njia, na kutukomboa kupitia upatanisho.
Ninajua kwamba maisha na huduma ya Mwokozi ni halisi na binafsi. Maandiko yamejaa hadithi za uponyaji Wake, ukarimu Wake, na miujiza Yake.
Ninajua kwamba Baba wa Mbinguni anasikia na anajibu sala za dhati za watoto Wake, bila kujali umri wao, hali, au lugha yao. Anasikia sala za utulivu za kusihi za mioyo yetu.
Ninashuhudia kwamba katika Gethsemane, Yesu Kristo alibeba uzito wa dhambi zetu, huzuni, na maumivu. Alikuwa radhi kuteseka kwa sababu ya upendo Wake kwetu na kufanya iwezekane sisi kusamehewa na kurejea nyumbani.
Ninajua kwamba sisi ni watoto halisi wa Mungu, tulioumbwa katika mfano Wake, tuliovikwa uwezekano wa kiungu, na kualikwa kurejea kuishi Naye ikiwa tutachagua kumfuata Yesu Kristo.
Ninajua kwamba Yesu Kristo ni mfano wetu mkamilifu, na kadiri tunavyomfuata kwa kuhudumu, kusamehe, na kuwapenda wengine, tunakuwa zaidi kama Yeye siku hadi siku.
Na ninajua kwamba mahekalu matakatifu ya Bwana ni nyumba Zake hapa duniani. Ndani ya nyumba hizo, tunafanya maagano matakatifu, tunapokea baraka za milele, na kujifunza zaidi juu Yake na kuhisi zaidi uwepo Wake. Hekaluni ni mahali pa kujifunza, amani, na maandalizi kwa ajili ya maisha yetu.
Ninashuhudia kwamba juhudi tunazozifanya za kufundisha na kuimba nyimbo hizi za Watoto kwa watoto wetu si tu sehemu nzuri ya utamaduni wa dini yetu. Ni mahubiri kwa wanafunzi wa Yesu Kristo, shuhuda kwenye ukweli wa injili iliyorejeshwa, na sala zilizofanywa kuwa muziki. Muziki mtakatifu unaweza kuangaza Nuru ya Kristo kwa wasikilizaji na unaweza kuimimina ndani ya moyo wa mwimbaji. Wapendwa marafiki, Yesu bado anatuhitaji tushiriki ushawishi wake. Nashuhudia hivi, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.