“Mpango Mzuri Sana,” Rafiki, Machi. 2026, 4–7.
Mpango Mzuri Sana
Kabla ya sisi kuja duniani, Baba wa Mbinguni alikuwa na mpango mzuri sana kwa ajili yetu. Tungezaliwa na kujifunza na kukua duniani. Tungeweza kufuata njia Yake ya agano na kufanya chaguzi nzuri.
Baba wa Mbinguni alijua tungehitaji msaada. Alijua tungefanya chaguzi mbaya na kutenda dhambi wakati mwingine. Hatungeweza kurudi Kwake kama hatungekuwa wasafi.
Tulihitaji mtu maalum ili kutusaidia kuwa wasafi kutokana na dhambi zetu. Yesu Kristo alikuwa mzaliwa wa kwanza Mwana wa kiroho wa Baba wa Mbinguni. Alijitolea kuja duniani na kutuokoa kutokana na dhambi zetu.
Kwa mamia ya miaka, watu walimsubiri Yesu azaliwe. Hatimaye, nyota mpya iliangaza angani ili kuuambia ulimwengu Mwokozi alikuwa amekuja.
Yesu alipokua, Aliwafundisha watu injili. Alikuwa mkarimu na mwenye upendo. Aliwabariki watoto.
Alifundisha kwamba tunapaswa kumfuata Yeye na kuwatendea wengine kama ambavyo Yeye angewatendea wengine. Aliwaponya watu waliokuwa wagonjwa. Aliwarudisha watu kwenye uhai ambao walikuwa wamekufa.
Yesu alijua ulikuwa wakati wa muujiza Wake mkuu. Alienda kwenye Bustani ya Gethsemane na kusali. Aliyasikia maumivu ya dhambi zetu sisi sote na huzuni na magonjwa.
Baadhi ya watu walimkasirikia Yesu. Hawakupenda kile alichofundisha na hawakuamini kuwa Yeye alikuwa Mwana wa Mungu. Yesu alikamatwa na kupigiliwa misumari msalabani, ambapo alikufa.
Marafiki wa Yesu walihuzunika sana. Waliulaza mwili Wake kaburini na kuviringisha jiwe kubwa mbele ya mlango.
Siku tatu baadaye, baadhi ya wanawake walikwenda kaburini. Lile jiwe lilikuwa limeviringishwa mbali, na kaburi lilikuwa tupu. Mariamu Magdalena alianza kulia kwa sababu mwili wa Yesu haukuwepo. Mtu mkarimu karibu naye alimuuliza kwa nini alikuwa akilia. Wakati alipomwambia, mtu yule alimwita Mariamu kwa jina. Alimtazama na kuona kwamba Yeye ni Yesu! Alikuwa hai tena!
Wakati wa Pasaka tunasherehekea kile Yesu Kristo alichofanya kwa ajili yetu. Kwa sababu Aliteseka kwa ajili yetu, tunaweza kutubu na kuwa wasafi. Kwa sababu Yeye alifufuka, sisi pia tutaishi tena! Kwa sababu yake Yeye, sisi tunaweza kurudi kwa Baba wa Mbinguni na kuwa na familia zetu milele.
Vielelezo na Matt Sweeney Vinaweza kunakiliwa kwa matumizi ya Kanisa pekee.