“Wiki Takatifu ya Mia,” Rafiki, Machi. 2026, 12–13.
Mia Wiki Takatifu
Kila siku hutusaidia kumkumbuka Yesu Kristo.
Hadithi ya kweli kutoka Marekani.
Tulianza kujiandaa kwa ajili ya Pasaka wiki moja mapema! Baba alisema wiki kabla ya Pasaka huitwa Wiki Takatifu. Mama alisema kutakuwa na mambo ya kushangaza kidogo kwenye meza ya jikoni kila siku. Kila mmoja wetu angetusaidia kumkumbuka Yesu Kristo. Nitaandika kuhusu yote katika shajara yangu!
Siku ya kwanza, tulikuta majani yaliyotengenezwa kwa karatasi.
Mama na Baba walisoma hadithi ya Jumapili ya Matawi kutoka kwenye maandiko. Wakati Yesu Kristo alipokwenda Yerusalemu, watu walipunga matawi ya mitende na kupiga kelele, “Hosana!”
Lucy, dada yangu, alishikilia picha ya Yesu akiwa juu ya punda. Sisi wengine tulipunga matawi yetu ya karatasi. Nilihisi furaha nikifikiria nilikuwa nikimkaribisha Yesu.
Siku ya pili, tulikuta mfuko wa takataka.
Yesu alifadhaishwa kwamba watu walikuwa wakiuza vitu hekaluni, hivyo Aliwatoa nje. Tuliokota taka nje ya vichaka kuzunguka kanisa. Nina furaha kwamba tungeweza kusaidia kuitunza nyumba ya Mungu!
Siku ya tatu, tulikuta udongo wa mfinyanzi.
Mama alisoma masimulizi ambayo Yesu Kristo alikuwa amewaambia watu. Tulisikiliza na kutumia udongo kutengeneza vitu kutoka kwenye hadithi. Lucy alitengeneza kondoo kwa sababu Yesu ndiye Mchungaji Mwema. Nilitengeneza taa ndogo ya mafuta. Ilinisaidia kukumbuka kuweka moyo wangu ukiwa umejaa imani.
Mnamo siku ya nne, tulikuta mdalasini.
Baba alituambia kuhusu jinsi Mariamu alivyompa Yesu Kristo mafuta maalumu kwa ajili ya miguu Yake. Harufu yake ilijaza nyumba yote.
Hatukuwa na mafuta haya maalum. Badala yake, tulitumia mdalasini kutengeneza kiburudisho. Mama alisema kwamba wakati tuliponusa harufu ya mdalasini wakati kiburudisho kikiokwa, tunapaswa kutafakari ambacho tungeweza kumpa Yesu.
Katika siku ya tano, tulikuta mishumaa.
Tuliwawasha mishumaa na kuimba wimbo, kama vile Yesu Kristo na wanafunzi Wake walivyoimba kwenye Karamu ya Mwisho. Tulikula mkate na kunywa sharubati ya zabibu ili kukumbuka sakramenti ya kwanza. Pia tulikuwa na komamanga ili kutukumbusha juu ya damu ya Yesu, na mizeituni kutukumbusha bustani ya Gethsemane.
Wakati tukila, muungurumo wa radi ulisikika nje. Nilijihisi salama na mwenye shukrani nikijua kwamba Yesu tayari amekabiliana na dhoruba ya giza.
Mnamo siku ya sita, tulikuta chombo cha kupandia maua.
Tulisoma kuhusu jinsi Yesu Kristo alivyokufa kwa ajili yetu. Kisha tukachukua chombo cha kupandia maua kilicho tupu na kwenda nacho bustanini na kukilaza kiubavu, kama mfano wa kaburi. Tuliweka udongo na vipande vya miamba kukizunguka lakini hatukuziba sehemu yake ya uwazi. Mama alitupatia kitu cha kuwakilisha mwili wa Yesu. Kwa unyenyekevu tulikifunika kwa kitambaa cheupe na kukiweka ndani ya chombo cha kupandia maua.
Japokuwa lilikuwa ni chombo tu cha kupandia maua, bado nilihisi huzuni kufunika sehemu yake ya uwazi kwa jiwe.
Siku ya saba, tulikuta karatasi zenye majina ya mababu zetu.
Mama alisema kwamba baada ya Yesu Kristo kufa, Alianzisha kazi ya umisionari katika ulimwengu wa roho. Kwa njia hiyo watu ambao hawakujifunza injili Yake duniani bado wangeweza kujifunza kuhusu Yeye. Katika mahekalu, tunaweza kubatizwa kwa niaba ya watu ambao hawakubatizwa kabla ya kufa.
Mimi na Lucy bado si wakubwa vya kutosha kuingia ndani ya hekalu, lakini tulisaidia kukata kadi za majina zilizochapishwa. Mama na Baba walifanya zamu kufanya kazi ya hekaluni kwa ajili ya watu walio kwenye kadi na kutembea kuzunguka viwanja vya hekalu pamoja nasi. hata kwa kuwa nje, hekalu lilikuwa kama mbingu ndogo.
Wakati wa Pasaka, tulikuta kaburi tupu.
Asubuhi ya Pasaka jiwe lililokuwa mbele ya chombo cha kupandia maua lilikuwa limeondolewa na kitambaa kilikuwa hakina kitu. Kulikuwa na kadi ambayo ilisema, Amefufuka!
Tayari nilijua kwamba Yesu Kristo ndiye sababu ya Pasaka. Baada ya kusherehekea Wiki Takatifu, ninahisi kama ninamjua Yeye vizuri zaidi pia.
Vielelezo na Melissa Kashiwagi. Inaweza kunakiliwa kwa matumizi ya Kanisa pekee.