Mkutano Mkuu
Manabii wa Mungu
Mkutano mkuu wa Oktoba 2025


11:8

Manabii wa Mungu

Kuisikiliza na kuitii sauti ya nabii ni muhimu kwenye kushikilia kila kitu kizuri hadi Ujio wa Pili.

Wapendwa vijana, ni kikao cha kupendeza cha mkutano wakati huu! Tayari tumewasikia Mitume hai watatu wa Yesu Kristo. Ni baraka kuu iliyoje! Na tutamsikia mmoja mwingine, Mzee Henry B. Eyring. Karamu ya kiroho inaendelea!

Nilipozungumza mwaka uliopita, tulijifunza jinsi ya kuukabili ulimwengu huu kupitia uzoefu wa Daudi kwa Goliati. Mnakumbuka yale mawe matano? Leo ninashiriki hadithi ya Agano la Kale niliyoisoma nikiwa na umri kama wenu, ambayo iliniacha nikitamani kuwa kama mhusika wake. Biblia haituambii jina lake, hivyo tutamwita mwanamke wa Shunemu kwa sababu hili ni jina la mji anakotoka.

Mwanamke akitengeneza mkate kwa ajili ya nabii

Siku moja, nabii Elisha alikuwa akipita Shunemu, na tunasoma kwamba palikuwepo “mwanamke mmoja mwenye cheo; naye [akamwalika] nabii aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia … kula chakula.” Nadhani nabii Elisha alikuwa na furaha sana kwa mwaliko wa kula katika nyumba ya yake! Alikuwa tayari amekwenda mara kadhaa wakati siku moja mwanamke alipomwambia mumewe, “Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu ni mtu mtakatifu wa Mungu..

Mwanamke anasema, “Sasa, ninaona.” Inaonekana alimwalika Elisha nyumbani kwake bila kujua alikuwa nabii; alipokea ushuhuda wake kupitia Roho Mtakatifu kwa kusikiliza kwa makini kile Elisha alichofanya na kufundisha. (Kumbukeni, hakukuwa na picha kipindi hicho! Hivyo ilikuwa vigumu kumtambua nabii kwa sura yake.)

Mwanamke akitayarisha chumba kwa ajili ya nabii

Lakini hadithi haikomei hapo. Siku moja, mwanamke akamwambia mumewe, “Tumfanyie chumba kidogo … na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.”

Mwanamke huyu mwaminifu alikuwa radhi kutengeneza chumba ndani ya nyumba yake ili kwamba nabii, akipita katika mji, angepata mahala pa kuishi!

Leo tunaweza kujifunza somo lenye nguvu kutokana na uzoefu huu.

Bwana alishuhudia kwa mwanamke wa Shunemu kwamba Elisha alikuwa nabii wa Mungu, na alitenda kwa kuifungua nyumba yake ili kumpokea.

Sisi pia tunaweza kupokea ushuhuda binafsi wa manabii wa Mungu leo na kuifungua mioyo yetu na akili zetu—nyumba yetu—kwa ujumbe ambao Baba yetu wa Mbinguni anao kwa ajili yetu katika siku hizi za mwisho.

Wapendwa vijana, ninawaalika mjiulize swali hili: Je, nina ushuhuda binafsi wa manabii wa Mungu walio hai?

Hebu tuanzie mwanzoni.

Nabii ni nani? Nabii ni mtu ambaye Mungu amemwita azungumze kwa niaba Yake. Wapo manabii duniani leo, kama vile ilivyokuwa katika nyakati za kale.

Manabii ni waonaji na wafunuzi. Hiyo humaanisha wanaweza kuona kile wengine wasichoweza kukiona, na wanaweza kutoa unabii wa matukio yajayo. Wanaweza pia kutuandaa dhidi ya majanga. Manabii hupokea amri na mafunuo kutoka kwa Bwana. Makala ya imani ya tisa inazungumza juu ya ufunuo unaoendelea katika siku hizi za mwisho. Inasema, “Tunaamini yale yote Mungu aliyoyafunua, na ambayo sasa anayafunua, na tunaamini kwamba bado Yeye atayafunua mambo mengi makuu na muhimu yahusuyo Ufalme wa Mungu.”

Mzee Gary E. Stevenson alisema, “Bwana anaendelea kufunua amri Zake na mapenzi yake kwa manabii Wake leo kwa sababu Yeye anatamani kutuongoza kwenye furaha katika maisha haya na kwenye utukufu wa selestia katika maisha yajayo.”

Manabii pia huitangaza injili na ni walimu wenye uvuvio na wajumbe wa Mungu kwa kila mmoja duniani.

Kila mshiriki wa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili ni nabii, mwonaji, na mfunuzi. Wakihudumu kama baraza chini ya maelekezo ya Bwana, wana mamlaka ya kutangaza na kufafanua mafundisho na kuweka sera kwa ajili ya Kanisa Lake. Kwa makini wanasali na kufanya shauri, kwani maamuzi ya akidi hizi lazima yatolewe kwa kauli moja. Kwa njia hii, Bwana anatuhakikishia kwamba mapenzi Yake yatatendeka.

Manabii wanashuhudia kumhusu Kristo—uwepo Wake, huduma Yake, na utakatifu Wake.

Ngoja tusome baadhi ya shuhuda za manabii ndani ya Kitabu cha Mormoni.

Abinadi alitangaza:

“Mungu mwenyewe atashuka miongoni mwa watoto wa watu, na atawakomboa watu wake.

“Na kwa sababu anaishi katika mwili ataitwa Mwana wa Mungu.”

Samweli Mlamani pia alishuhudia kwamba Yesu Kristo ni “Mwana wa Mungu, Baba wa mbingu na dunia, Muumba wa vitu vyote tangu mwanzo.”

Na nabii Moroni alisema, “Nimemuona Yesu, na … amenizungumzia uso kwa uso.”

Wakati Kristo alipowatembelea Wanefi, moja ya vitu vya mwanzo Yeye alivyofanya ilikuwa kuwaita Mitume kumi na wawili. Naye akawaambia watu, “Heri ikiwa mtasikiliza maneno ya hawa kumi na wawili ambao nimewachagua.”

Sasa, ngoja nishiriki maneno machache kwa wazazi au wanafamilia wengine wanaowalea watoto. Bwana mwenyewe aliwafundisha Adamu na Hawa kweli za mpango wa wokovu. Na kisha aliwaambia, “Ninakupeni amri, kuyafundisha mambo haya kwa uhuru kwa watoto wenu.”

Inamaanisha nini kufundisha kwa uhuru? Ni kujifunza kweli za injili, kuwa na ushuhuda binafsi wa kweli hizo, na kushiriki maarifa hayo kwa watoto wetu. Ni kuhimiza vyote, nyakati rasmi na zisizo rasmi za kufundisha. Ni kuishi kulingana na maarifa na ushuhuda huo.

Kitabu cha Mormoni kinawaelezea vijana mashujaa 2,060 kama “watu wa ukweli na wenye busara, kwani walikuwa wamefundishwa kutii amri za Mungu na kutembea wima mbele yake.” Wavulana hawa kwa uaminifu walimtii Helamani, ambaye kwa wakati huo alikuwa kiongozi wao wa jeshi na pia nabii wao, na walitambua kwamba mama zao walikuwa wameijaza mioyo yao kwa ukweli na imani.

Wazazi, katika ulimwengu huu ambapo kuna sauti nyingi na nyakati zingine kiza kinene, Mungu mwenyewe ametuamuru kuwalea watoto wetu katika nuru na kweli. Ametuamini kwa jukumu la kuwafundisha watoto wetu kweli za kuokoa za injili. Ikiwa tutashindwa kufanya hivyo, ulimwengu hautabeba jukumu hilo.

Wapendwa marafiki vijana, nina mwaliko kwa ajili yenu: Katika siku zinazokuja, ninawaalika mpige magoti, mfungue mioyo yenu, na msali kwa imani kwa Baba wa Mbinguni mkimuomba awathibitishie kwamba nabii na mitume Wake ni sauti Yake duniani leo.

Mwanamke Mshunami ametufunza kwamba tunaweza kuwa na ushuhuda huo kupitia Roho Mtakatifu. Ninawaahidi kwamba pale tunapojua kwamba wao ni wapakwa mafuta wa Mungu, maisha yetu yatakuwa rahisi licha ya changamoto zinazoendelea, kwani tutatii sauti yao kwa ujasiri, imani, na tumaini. Kuisikiliza na kuitii sauti ya nabii ni muhimu kwenye kushikilia kila kitu kizuri hadi Ujio wa Pili wa Mwokozi wetu.

Uovu wa ulimwengu unaongezeka, lakini Kanisa la Yesu Kristo na ufalme wake ni imara kuliko ilivyowahi kuwa. Sayuni inajivika mavazi yake mazuri, na enzi ya Kristo haitaanguka. Bwana anatutarajia kuwa imara katika shuhuda zetu, kuwa waliojaa imani, na kutubu kila siku. Mwokozi wetu, Yesu Kristo, anamtegemea kila mmoja wetu kuisongesha mbele kazi Yake.

Nabii Joseph Smith aliwahi kusema, “Ndugu, je, si lazima sisi tuendelee katika kazi hii iliyo kuu?” Hata hivyo, kwa kuwa ujumbe wangu ni mahususi kwa ajili yenu, vijana, ningependa kutumia neno vijana badala ya ndugu. Mpo tayari?

“[Vijana], je, si lazima sisi tuendelee katika kazi hii iliyo kuu? Twende mbele na siyo nyuma. Tuweni majasiri, [vijana]; na mbele, mbele kwenye ushindi! Acheni mioyo yenu ifurahi, na kuwa yenye furaha zaidi.

Nina shukrani kwa mwongozo na juhudi zilizowekwa wakfu za manabii walio hai. Ninatoa ushuhuda wangu wa unyenyekevu kwamba, waliitwa na Mungu ili kuendeleza, kuanzisha, na kuongoza ufalme wake duniani leo. Na itakuwa hivyo daima. Daima itakuwa kwamba Bwana anawachagua watumishi Wake. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Tafsiri ya Kihispania ya kirai hiki hutoa maana “kualikwa kwa kusisitiza.”

  2. 2 Wafalme 4:8.

  3. 2 Wafalme 4:9; msisitizo umeongezwa.

  4. 2 Wafalme 4:10.

  5. Ona Amosi 3:7.

  6. “Chini ya maelekezo ya Bwana, [Rais wa Kanisa] huliongoza Kanisa na ni mtu pekee duniani aliyepewa mamlaka ya kutumia funguo zote za ukuhani. … Anayo mamlaka ya kupokea ufunuo na kutangaza mapenzi ya Mungu kwa Kanisa lote” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 5.1.1.1, Gospel Library).

  7. Ona Mafundisho na Maagano 1:38.

  8. Gary E. Stevenson, “Injili ya Yesu Kristo: Sauti ya Sangwe,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2025, 5.

  9. Ona Mathayo 28:19–20; Mafundisho na Maagano 21:1, 4–5; 107:35.

  10. “Kila Mtume hushikilia funguo zote za ufalme na hutumia funguo hizo chini ya maelekezo ya Rais wa Kanisa” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 5.1.1.1).

  11. Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 5.1.1.1.

  12. Ona Mafundisho na Maagano 107:27–31.

  13. “Mitume Kumi na Wawili ni ‘mashahidi maalumu’ wa jina la Yesu Kristo. … Wanashuhudia kwa ulimwengu wote juu ya utakatifu Wake na uhalisia wa Ufufuko Wake …” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 5.1.1.1).

  14. Mosia 15:1–2.

  15. Helamani 14:12.

  16. Etheri 12:39.

  17. Akizungumza juu ya Kitabu cha Mormoni, Nabii Joseph Smith alifundisha: “Kitabu hiki pia kinatuambia kwamba Mwokozi alitokea kwenye bara hili baada ya ufufuo Wake; kwamba alipanda injili hapa katika utimilifu wake, neema, na nguvu, na baraka; na walikuwa na mitume, manabii, wachungaji, walimu, na wainjilisti; utaratibu ule ule, ukuhani ule ule, ibada zile zile, karama, nguvu, na baraka, kama zilizopatikana kwenye bara la mashariki” (History, 1838–1856, volume C-1 [2 November 1838–31 July 1842], 1282, josephsmithpapers.org).

  18. 3 Nefi 12:1; msisitizo umeongezwa.

  19. Musa 6:58; msisitizo umeongezwa.

  20. Ona Mafundisho na Maagano 68:25–28.

  21. “Tunapaswa kukamata kila fursa ya kushiriki mafundisho ya Yesu Kristo pamoja na watoto. Nyakati hizi za kufundisha ni za thamani na ni chache sana zikilinganishwa na juhudi zisizokoma za nguvu pinzani. Kwa kila saa inayotumiwa kuingiza mafundisho katika maisha ya mtoto, kuna masaa mengi ya upinzani yaliyojaa jumbe na picha zinazopinga au kupuuza kweli hizo za kuokoa.

    “Baadhi yenu mnaweza kufikiria kama inaweza kuwa bora kuwa karibu na watoto wenu kwa kuwa na burudani, au mnaweza kuuliza kama mtoto anaweza kuanza kuhisi kulemewa na mafundisho yenu. Badala yake, tunapaswa kuzingatia, ‘Kwa muda mfupi sana na fursa chache sana, ni maneno gani ya mafundisho ninayoweza kushiriki ambayo yatawaimarisha dhidi ya changamoto zisizoepukika kwenye imani yao?” Maneno unayoshiriki leo yanaweza kuwa yale wanayobeba pamoja nao, na leo punde itapita.” (Henry B. Eyring, “Rahisi Ni Mafundisho ya Yesu Kristo,” Liahona, Nov. 2024, 97).

  22. Kila kijana ni wa muhimu! (Ona Alma 57:6, 20).

  23. Alma 53:21; msisitizo umeongezwa.

  24. Ona Alma 56:44–48; 57:21.

  25. Ona Mafundisho na Maagano 93:40.

  26. Tunao pia mfano wa wazazi wa Enoshi, ambao walimlea “katika malezi na maonyo ya Bwana” (Enoshi 1:1) na kumfunza kuhusu “uzima wa milele, na shangwe ya watakatifu” (Enoshi 1:3). Enoshi aliijua hulka ya Mungu (ona Enoshi 1:6, 15, 17).

  27. Ona Mafundisho na Maagano 21:1–2, 4–6. “Wakati ulimwengu unasisitiza kwamba nguvu, mali, umaarufu na starehe za kimwili ndizo ziletazo furaha, hazileti! Haziwezi kuleta! Kile kinachozalishwa na vitu hivyo si chochote bali mbadala ulio tupu wa ‘hali ya baraka na yenye furaha ya [yule] anayetii amri za Mungu’ [Mosia 2:41].

    “Ukweli ni kwamba inachosha sana kutafuta furaha mahali ambapo huwezi kamwe kuipata! Hata hivyo, unapojifunga mwenyewe nira kwa Yesu Kristo na kufanya kazi ya kiroho inayohitajika kuushinda ulimwengu, Yeye na ni Yeye pekee, aliye na uweza wa kukuinua juu ya mvuto wa ulimwengu huu.

    “Sasa, ni kwa namna gani kuushinda ulimwengu kunabariki maisha yetu? Jibu liko wazi: Kuingia katika uhusiano wa agano na Mungu kunatufunga sisi Kwake katika njia ambayo inafanya kila kitu kuhusu maisha kiwe rahisi zaidi. Tafadhali msinielewe vibaya: Mimi sijasema kwamba kufanya maagano kunafanya maisha kuwa rahisi. Ukweli ni kwamba, tegemea upinzani, kwa sababu adui anataka wewe usigundue uweza wa Yesu Kristo. Lakini kujifunga mwenyewe nira na Mwokozi inamaanisha unapata kuzifikia nguvu Zake na uweza Wake wa kukomboa” (Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 97)

  28. Ona Etheri 8:26; Moroni 7:19–25.

  29. Ona Isaya 52:1.

  30. Ona Zaburi 125:1; Isaya 28:16.

  31. Mafundisho na Maagano 128:22; msisitizo umeongezwa.

  32. Ona Mafundisho na Maagano 1:30.

  33. Ona Makala ya Imani 1:5.