Mkutano Mkuu
Mpatanishwe kwa Mungu
Mkutano mkuu wa Oktoba 2025


10:22

Mpatanishwe kwa Mungu

Kupatanishwa huku na Mungu, kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, kunatuongoza kwenye imani isiyoyumba.

Wakati ninaposoma maandiko, nakutana na maneno yanayonivutia sana, hasa kwa sababu yana maana maalum kutokana na uzoefu niliopata katika maisha yangu. Nilitumia ujuzi wangu kufanya kazi kama mhasibu wa utafiti. Kwa kumbukumbu hizo, neno patanisha limenivutia nikiwa ninasoma maandiko. Kazi yangu ilikuwa kupatanisha kiasi kilichoripotiwa na rekodi za kifedha kwa kutumia ujuzi wa uhasibu, ukaguzi, na uchunguzi. Kwa maneno mengine, lengo langu lilikuwa ni kupanga ripoti za kifedha na hati za kifedha ili kuhakikisha usahihi na uhalali. Nilifanya jitihada kubwa kutatua tofauti, na ilikuwa kawaida kwamba muda mwingi ulitolewa kutatua hata tofauti ndogo sana.

Mtume Paulo aliwasihi Wakorintho “wapatanishwe na Mungu.” Kupatanishwa na Mungu ina maana ya kurudishwa katika ushirikiano na Mungu, au kurejesha uhusiano na Mungu ambao umezuiliwa au umevunjika kwa sababu ya dhambi zetu au matendo yetu. Kwa maneno rahisi, kupatanishwa na Mungu inamaanisha kufanya mapenzi na matendo yetu yalandane na mapenzi ya Mungu au, kama alivyofundisha Rais Russell M. Nelson, kumruhusu Mungu ashinde katika maisha yetu.

Kama ilivyofundishwa katika maandiko, tuko huru kujitendea, “kuchagua njia ya kifo kisicho na mwisho au njia ya uzima wa milele.” Lakini ikiwa hatutakuwa na bidii, uhuru huu wa kutenda kwa ajili yetu wenyewe unaweza kusababisha kupoteza uhusiano na mapenzi ya Mungu.

Nabii Yakobo alifundisha kwamba tunapokuwa katika hali ya kutokuelewana au kukosa uhusiano mzuri na Mungu, njia pekee ya kupata upatanisho ni “kupatanishwa na [Mungu] kupitia upatanisho wa Kristo.” Tunapaswa kutambua kwamba kupatanishwa kunategemea rehema, ikimaanisha kwamba tendo la neema la Kristo la dhabihu linafanya upatanisho uwezekane.

Unapotafakari maisha yako mwenyewe, fikiria kuhusu wakati ulipohisi uko mbali na Baba wa Mbinguni kwa sababu ulikuwa umesonga mbali Naye. Kwa mfano, labda umepunguza kidogo bidii katika sala zako Kwake au katika kutii amri Zake. Kama ambavyo tunachagua kujitenga na Mungu, lazima tuchague juhudi za kupatanishwa. Bwana alisisitiza majukumu yetu pale Aliposema, “Sogeeni karibu nami na mimi nitasogea karibu na nyinyi; nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata; ombeni, nanyi mtapewa; bisheni, nanyi mtafunguliwa.”

Mwokozi anatusaidiaje turudishe na kupatanisha uhusiano huu muhimu? Kwangu mimi, ninapiga hatua kubwa katika safari yangu ya kujipatanisha na Mungu ninapofuata ushauri uliofundishwa na Rais Nelson na kutubu kila siku. Sababu ni kwamba kujipatanisha kunamaanisha kurejesha uhusiano uliovunjika, hasa kati ya Mungu na wanadamu, kwa kuondoa kizuizi cha dhambi.

Moja ya mapatanisho makubwa tuliyosoma kwenye maandiko ni ule wa Enoshi. Kitu katika maisha yake kilikuwa hakiko sawasawa na Mungu. Alionyesha kutegemea Upatanisho wa Yesu Kristo ili kuweza kujipatanisha na Mungu. Alieleza tamanio lake la kutubu, unyenyekevu wake, umakini wake, na ari yake. Kujipatanisha kwake na Mungu kulithibitishwa ilipokuja sauti ikamwambia, “Enoshi, dhambi zako zimesamehewa, na utabarikiwa.” Enoshi alitambua athari ambazo kutubu na kujipatanisha vilikuwa navyo kwake pale aliposema, “Na mimi, Enoshi, nilijua kwamba Mungu hawezi kusema uongo; kwa hivyo, dhambi zangu zilifutiliwa mbali.”

Kujipatanisha hakutuletei tu faraja kutokana na hisia za hatia bali pia amani ndani yetu na amani kwa wengine. Kunaponya mahusiano, kunalainisha mioyo, na kuimarisha ufuasi wetu, kukileta kujiamini zaidi mbele ya Mungu. Kile kinachonipa matumaini makubwa na ujasiri kwangu ni tunda lingine la upatanisho lililoelezewa na Enoshi wakati aliposema, “Na baada ya mimi, Enoshi, kusikia maneno haya, imani yangu ilianza kuwa thabiti katika Bwana.”

Nilipokuwa mvulana mdogo, babu yangu kwa mama alikuwa na shamba kubwa la cheri. Nilikuwa na fursa ya kufanya kazi kwenye shamba, hasa wakati wa majira ya joto wakati wa mavuno ya cheri. Kama mvulana mdogo sana, niligundua kwamba kiwango cha kushiriki kwangu kilikuwa kupokea ndoo na kisha kutumwa juu ya mti kuchukua cheri.

Mavuno ya cheri yalibadilika sana wakati babu yangu aliponunua mashine iitwayo kitikisa cheri. Mashine hii inachukua shina la mti na kulitikisa, na kufanya cheri kuanguka kutoka kwenye mti hadi kwenye nyavu zinazotumika kukusanya cheri. Niligundua kuwa wakati kitikisa kinapoanza kutikisa mti, karibu cheri zote zilikuwa zinaanguka kutoka mtini ndani ya sekunde. Pia niligundua kuwa haikujalisha ikiwa mti unatikiswa kwa sekunde 10 au dakika moja kamili, cheri zingine hazingeanguka. Kweli zilikuwa haziwezi kutikiswa.

Kuangusha cheri kutoka kwenye mti kunawezekana kwa sababu ya kuachiwa kwa ethilini. Homoni hii inasababisha tabaka la seli kati ya shina la cheri na mti kuwa dhaifu. Hivyo, shina la cheri iliyoiva linafunguka kwa urahisi kutoka kwenye mti kwa sababu ya muunganiko ulio dhaifu.

Katika maandiko, tunajifunza kwamba Shina la Yese ni mfano wa Masihi, Yesu Kristo, ambaye alitabiriwa kuja kutoka katika ukoo wa Yese, baba wa Mfalme Daudi. Kama vile ethilini inavyoshindwa kuunganisha shina la cheri iliyoiva, kutokuwa na utii, shaka, na hofu vinaweza kudhoofisha muunganiko wetu na shina la Yese, au Yesu Kristo, na kuturuhusu kutingishwa kirahisi na kutenganishwa Naye. Kadri tunavyoweza kuwa waaminifu, lazima tujilinde dhidi ya kufanywa dhaifu kwa muunganiko wetu na Yesu Kristo.

Katika Mafundisho na Maagano, hata waaminifu wanapewa onyo: “Lakini kuna uwezekano kwamba binadamu anaweza kuanguka kutoka katika hali ya neema, na kujitenga kutoka kwa Mungu aliye hai.” Bwana anaendelea, “Ndiyo, … na hata wale waliotakaswa wachukue tahadhari vile vile.” Kuepuka kuanguka, Bwana alishauri, “Kwa hiyo kanisa na lichukue tahadhari, na kusali daima, wasije wakaanguka majaribuni.”

Mtu anaweza kulinganisha hali ya kutikiswa kwa urahisi na kile ambacho maandiko yanakielezea kama kuwa tayari kuangamia kwa madhara yanayotokana na vitendo. Kifungu hiki pia kinaweza kutumika kwa njia pana kuashiria hali ya kuzorota, ubovu, au upungufu ambao unafanya kitu kuwa rahisi kuvunjika au kuharibiwa.

Huku kuiva kunawakilisha nini? Je, ina maana kwamba tunaweza kufikia hatua ambapo hatuwezi kubadilika? La, nadhani ina maana kwamba tunaweza kufikia wakati ambapo hatutaki kubadilika. Kinyume cha kuwa tayari kwa maangamizo ni kufanya mambo ambayo yataimarisha muunganiko wetu na Yesu Kristo. Kama ilivyoelezwa, toba ilimwongoza Enoshi kwenye hatua ya imani isiyoyumbishwa. Kuna nguvu katika toba—toba ya kawaida, ya haraka, na ya mara kwa mara. Kama Rais Nelson alivyotufundisha: “Hakuna kinacholeta uhuru zaidi, cha kiungwana zaidi, au cha muhimu zaidi kwa ukuaji wetu binafsi kuliko ilivyo fokasi yetu ya kila siku, kwenye toba.”

Mbali na toba, nabii Yakobo alifundisha kwamba kuwa na ufahamu wa mkono wa Mungu katika maisha yetu, kutafuta na kupokea ufunuo, na kumsikiliza Mungu anapozungumza kunatusaidia kutufanya tusitikisike. Yakobo pia alifundisha, “Kwa hivyo, tunawachunguza manabii, na tunayo mafunuo mengi na roho ya unabii; pamoja na mashahidi hawa wote tunapokea tumaini, na imani yetu haiwezi kutingishwa.” Kusikiliza na kutenda kulingana na maneno na mialiko ya manabii na mitume kunaweza kutujaza kwa tumaini, ujasiri, na nguvu, na hivyo kupelekea imani yetu isitetereke.

Nimejifunza kuwa, matamanio ya kupatanishwa na Mungu yanapaswa kuambatana na matamanio ya kutubu. Kutubu na kupata baraka za Upatanisho wa Yesu Kristo huongoza kwenye imani isiyotetereka. Imani isiyotetereka huongoza kwenye tamanio la kupatanishwa na Mungu daima. Hii ni mifumo iliyo katika duara, au ya kujirudia rudia.

Akina kaka na akina dada, ninawaalika kupatanishwa na Mungu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Ninashuhudia kwamba kufanya na kushika magano kunafanya muunganiko wetu na Mwokozi kuwa imara, hivyo kuepuka kuwa tayari kwa maangamizo. Ninashuhudia kwamba kupatanishwa huku na Mungu, kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, kunatuongoza kwenye imani isiyoyumba.

Ninajua Baba wa Mbinguni anatupenda mimi na wewe, na alimtuma Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, kuwa Mwokozi, Mkombozi, na mpatanishi wetu. Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo na ninafanya hivi katika jina la Yesu Kristo, amina.