Yesu Kristo na Mwanzo Wako Mpya
Sisi sote tunaweza kuwa na mwanzo mpya kupitia Yesu Kristo na kwa sababu ya Yesu Kristo. Hata wewe.
Maandiko Yanaeleza kwa Uchache: Yesu Alizunguka Huko na Huko, Akitenda Kazi Njema
Yesu “alizunguka huko na huko akitenda kazi njema.” Tunasoma maelezo hayo pungufu katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Ni maelezo pungufu kiasi gani! Hakika Yesu alitenda kazi njema! Yeye ni kiini hasa—na chanzo—cha wema! Alijitolea maisha Yake yote kutenda mema. Yeye ni “mwenye rehema na hisani, mvumilivu na mwenye utele,” wema usio na mwisho na rehema ya milele.
Jaribio lolote la kuelezea au kufanyia muhtasari wema Wake na rehema Yake ingekuwa ni maelezo pungufu. Kwa kweli, kama Mtume Yohana alivyojaribu kueleza, kama tungejaribu kurekodi kila uthibitisho wa wema wa Mwokozi, “hata ulimwengu wenyewe usingeweza kubeba vitabu ambavyo vinapaswa kuandikwa.”
Yesu Kristo Anatoa Mwanzo Mpya Kwa kila Mmoja wetu
Mifano mahususi tuliyonayo iliyohifadhiwa katika maandiko kuhusu Yesu “akifanya mema” inatufanya tuwe na hofu na kushangazwa, hasa tunapofikiria jinsi ambavyo ingekuwa kuwa pale, kushuhudia miujiza Yake, kupokea mafundisho Yake, na kupata uponyaji Wake. Alizungumza na waliokataliwa katika jamii, aliwagusa wagonjwa na wasafi, Alileta faraja kwa waliochoka, Alifundisha ukweli wa kukomboa, na Aliwaita wenye dhambi watubu. Kwa kila mwenye ukoma, mtu kipofu, na mwanamke mzinzi; kwa viwete, viziwi, na mabubu; kwa kila mama mwenye huzuni, baba mwenye kukata tamaa, na mjane anayepitia majonzi; kwa waliohukumiwa, waliofedheheshwa, na walioteseka; kwa wafu katika mwili au wafu katika roho, kile alichofanya ni kutoa mwanzo mpya. Ndiyo, maelezo mengine pungufu!
Kila kitu alichosema na kufanya kilitoa mwanzo mpya kwa kila mmoja wao aliowaponya, kuwabariki, kuwafundisha, na kuwaondolea dhambi. Hakujiweka mbali nao, na hakika hatajiweka mbali nawe. Fikiria katika wakati huu kusikia maneno yoyote ya kuleta uzima kutoka Kwake:
“Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”
“Wala mimi sikuhukumu: enenda zako; wala usitende dhambi tena.”
“Binti, imani yako imekuponya: enenda zako kwa amani.”
Maneno ya Mwokozi kwa watu hawa yalikuwa mafupi, lakini pamoja nayo alichora upeo mpya mkubwa wa msamaha, uponyaji, urejesho, amani, na uzima wa milele. Na habari njema ni kwamba, Yeye anatoa mwanzo mpya sawa kwako na kwangu. Sisi sote tunaweza kuwa na mwanzo mpya kupitia Yesu Kristo na kwa sababu ya Yesu Kristo. Hata wewe. Mwanzo mpya upo katikati ya mpango wa Baba kwa watoto Wake. Hili ni Kanisa la mwanzo mpya! Hili ni Kanisa la mwanzo msafi!
Hili ni Kanisa la Mwanzo Mpya
Kwa ubatizo wa maji na Roho, sisi “tumezaliwa mara ya pili” na kuweza “kutembea katika upya wa maisha.” Ni matumaini kiasi gani yanayoletwa na mwanzo mpya kwa yule aliyehangaika chini ya mzigo wa dhambi au kuteseka kutokana na athari za maisha yaliyojaa matatizo na mahusiano yasiyofanya kazi? Yesu hakuwa na haja ya msamaha wa dhambi Yeye Mwenyewe au mwanzo mpya katika maisha, lakini alibatizwa, akionyesha kwetu kwa uwazi njia ya mwanzo mpya aliyoiweka kwa kila mmoja wetu.
Na mwanzo wetu mpya hautokei mara moja tu. Tuna tabia ya kufikiria kwamba ubatizo wetu ni nafasi yetu moja tu ya mwanzo mpya. Sio hivyo. Hatuna nafasi moja tu. Mwanzo huu mpya unaweza kutokea kila siku! Na kwa hakika kila wiki tunakula kipande kidogo cha mkate na kunywa kikombe kidogo cha maji katika kumbukumbu ya zawadi ya Mwokozi wetu mkamilifu, ambaye alikufa kwa kusudi maalum la kutupa mwanzo mpya kadiri tunavyohitaji! Yesu anatupa mwanzo mpya kadri tunavyohitaji.
Kwa kuweka ahadi na kufurahia katika maisha mapya katika Kristo, tunaweza kuwa “kiumbe kipya,” ambapo vitu vya zamani vinapita na vitu vyote vinakuwa vipya. Ni nafuu kiasi gani ambayo aina hii ya mapambazuko mapya inaleta kwa nafsi inayojaribu, kwa kuendelea kuchagua imani katika nguvu ya Mwokozi wetu ya kuponya na kurekebisha, licha ya vikwazo vinavyotisha vya kuishi katika ulimwengu ulioanguka? Mwokozi hakuwahi kukata tamaa katika ahadi Yake ya kutimiza mapenzi ya Baba na kukamilisha huduma Yake ya upatanisho wa kiungu, hata kupitia maumivu ambayo yalimsababishia kutetemeka, kutokwa na damu kwenye kila kinyweleo, kuteseka mwili na roho, na kuomba kikombe chenye uchungu kiondolewe. Tena, Yeye alikuwa akionyesha kwetu jinsi ya kuvumilia kwa uaminifu.
Kwa kila agano tunalofanya na kila juhudi tunayotoa ili kulihifadhi, tunaweza kupokea “moyo mpya” na kipimo kamili cha “roho mpya.” Polepole, kadiri tunavyokaribisha wema Wake katika mioyo yetu na kufukuza mawazo hasi katika akili zetu, tunakuwa watu Wake kwa kuwa kiuhalisia tunamfanya Yeye kuwa Mungu wetu. Yesu anataka sana kuwa Mkuu wetu na Mchungaji wetu na Mfalme wa Amani, na tunaweza kuchagua kumfanya hivyo ndani ya mioyo na akili zetu.
Mwanzo Mpya kwa Jinsi Tunavyoiangalia Toba
Toba inafungua mlango wa mwanzo wetu mpya, mwanzo msafi, na nafasi za pili. Mafundisho ya mpendwa wetu Rais Russel M. Nelson yameondoa dhana potofu kuhusu zawadi ya kiungu ya toba, na nadhani hatimaye tunaanza kuielewa.
Ni furaha kusikia vijana wetu wakielezea maana ya toba kwao. Hivi karibuni nilisikia msichana akisema, akiwa na tabasamu usoni mwake, “Ninapofikiria toba, toba ya kila siku, nahisi furaha na matumaini makubwa. Ninahisi upendo na furaha ya Baba yangu wa Mbinguni na Mwokozi wangu. Siogopi kumjia Baba wa Mbinguni katika sala na kuomba msaada wake kwa chochote ninachokutana nacho. Najua Hawanilengi kunikamata nikifanya kosa. Mikono yao iko wazi sana. Kwangu mimi hii ndiyo toba,” alisema. Huyu msichana anaelewa kwamba kwa sababu ya Yesu Kristo, anaweza kuwa na mwanzo mpya!
Mwanzo Mpya kwa Kila Mmoja, Kila Wakati
Je, unahitaji mwanzo mpya? Je, unaweza kuwa na mwanzo msafi, hata wewe? Fikiria kuhusu watu ambao Mwokozi aliwahudumia—watu ambao aliwafundisha, aliwaponya, aliwafufua, aliwasamehe, na aliwarejesha. Je, alikuwa anawachagua kutoka kwenye daraja fulani la kiuchumi au asili fulani? Je, alikuwa anawatofautisha kati ya wema na wenye dhambi? Je, alikuwa anawachagua watu kwa sababu walistahili zaidi au walipendwa zaidi? Hapana.
Baadhi walikuja Kwake kwa imni kubwa, wakiamini katika nguvu Zake za kuponya—kwa mfano, mwanamke mwenye kutokwa na damu, mwanajeshi wa Kirumi ambaye mtumishi wake alikuwa akifa, mwenye ukoma, Yairo, au Bartimayo kipofu. Kila mmoja wao aliweka imani yao njiani, wakitumaini kwamba wema na uwezo wa rabi kutoka Nazareti utaweza kubadilisha maisha na matarajio yao. Na Yeye alifanya hivyo. Yeye aliacha uponyaji Wake uendelee.
Lakini Yesu pia aliiwabariki wale waliokuwa na imani haba, kama baba wa mtoto mgonjwa aliyepaza sauti, labda kama ambavyo wewe umepaza sauti, “Bwana, ninaamini; nisaidie kutokuamini kwangu.” Na alimimina rehema hata kwa wale ambao hawakumtafuta kabisa, kama vile mwanamke aliyekamatwa kwenye uzinzi, mjane wa Naini, mtu mlemavu katika bwawa la Bethzatha, na mtu aliyezaliwa kipofu. Je, umemhisi akifanya mema katika maisha yako hata wakati ambapo hujamtafuta au kumfuata?
Kwa kila mmoja wa wahusika kwenye maandiko, na kwa wote ambao wangesikiliza na kujibu, aliwapa mwanzo mpya, iwe maisha mapya yaliyosamehewa dhambi, au maisha mapya yaliyoponywa ugonjwa au maisha mapya yaliyofufuliwa kutoka kifo.
Hii inamaanisha nini kwako na kwangu? Wema wake na rehema na upendo wake havina mipaka. Mwanzo mpya uko katikati ya mpango wa Baba! Mwanzo msafi ni dhamira ya Mwana! Mchana mpya, sura mpya, na fursa mpya ni kiini kirahisi cha habari njema ya injili!
Hivyo, je, umekuwa mbali sana na maagano yako kiasi cha kutostahili kupokea mwanzo mpya? Hapana. Je, umefanya hiki au kile mara nyingi kiasi cha kutostahili nafasi nyingine? Hapana. Je, umepotoka mbali na Kristo kiasi cha kutoweza kuandika hadithi mpya kuanzia hapa na kuendelea? Hapana. Adui pekee ndiye anaye nufaika na wazo kwamba umezama. Haujazama.
Na mwanzo mpya ni zaidi ya dhambi zetu na makosa. Kupitia wema na neema ya Mwokozi, tunaweza kupata mwanzo mpya ambao unaleta mabadiliko katika mitazamo ya zamani, tabia mbaya, hisia za hasira, mitazamo hasi, hisia za kutokuwa na nguvu, na tabia za kulaumu wengine na kuepuka uwajibikaji binafsi. Unaweza kweli kubadilisha mambo kuhusu wewe mwenyewe ambayo yamekuwa yakikukandamiza kwa miaka. Unaweza kuanza tena kupitia uweza wa Bwana wa mwanzo mpya. Hajawahi kuchoka kutupa mwanzo mpya.
Kwa wale wanaotaabika na dhambi ileile au kushindwa kulekule mara kwa mara, endelea mbele. Hajakuwekea kizuizi mbele yako. Hajaweka kikomo kwenye nafasi zako za pili. Endelea mbele. Endelea kujitahidi. Tafuta msaada kutoka kwa wale wanaokuzunguka. Na utumaini katika mwanzo mpya ambao uko kwako kila wakati unapomrudia Baba yako katika uaminifu wa moyo. Tuache kutenda dhambi kwa makusudi, kurudia rudia bila kuzingatia, na uasi wa kiburi nyuma yako ambapo kinapaswa kuwa. Huna haja ya kuwa kama ulivyokuwa zamani. Pokea mwanzo wako mpya, nafasi yako ya pili au ya tatu au ya nne—au ya mia—iliyotolewa kwako kupitia damu ya ukombozi ya Yesu Kristo.
nina shukrani kupita maelezo kwa mwanzo mpya niliopewa na kwa mingine mingi ambayo bado nitapewa.
Hitimisho
Mwokozi wetu alitoa maelezo ya mwisho ambayo bila hayo kusingekuwa na sababu ya tumaini au furaha siku hii. Baada ya maumivu ya Gethsemane na mwishoni mwa msalaba wenye mateso, alisema tu, “Imekwisha.” Unabii wa Kimasihi ulikamilika, na malipo kamili ya deni la dhambi na mateso ya wanadamu yalikuwa yamelipwa. Alitangaza “imekwisha” dhabihu Yake isiyo na mwisho na ya milele. Hata hivyo, Upatanisho Wake haungekamilika hadi Yeye Mwenyewe alipopata uzoefu wa maisha mapya siku ya tatu, ule mwanzo mpya kama kiumbe aliyetukuka, aliyefufuka kupitia nguvu ya Baba.
Kwa sababu mara zote Alifanya vitu ambavyo vilimpendeza Baba Yake, na kwa sababu “Aliteseka kwa mapenzi ya Baba katika vitu vyote,” wewe na mimi tunaweza kuwa na mwanzo mpya. Pokea mwanzo wako mpya, hata leo, sasa hivi. Yesu Kristo ni Mwanzilishi na Mtimizaji wa imani yetu, akiandika aya nyingi mpya pamoja nasi. Yeye ni Mwanzo na Mwisho—mwisho wa aibu zetu na mateso, na mwanzo wa maisha mapya ndani Yake, akituruhusu kuacha yaliyopita na kuanza tena kwa alfajiri mpya kadiri tunavyohitaji. Kwa hakika “wema na rehema Zake zitatufuata siku zote za [maisha yetu].” Katika jina la Yesu Kristo, amina.