Mkutano Mkuu
Kujichukulia Jina la Yesu Kristo
Mkutano mkuu wa Oktoba 2025


13:22

Kujichukulia Jina la Yesu Kristo

Kadiri tunavyojitambua na kumkumbuka Yesu Kristo, ndivyo tunavyotaka zaidi kuwa kama Yeye.

Mwaka 2018, Chuo Kikuu cha Utah, kilianzisha uprofesa wa heshima uitwao “Kiti cha Urais cha Dkt. Russell M. Nelson na Dantzel W. Nelson katika Upasuaji wa Moyo na Kifua (Cardiothoracic Surgery)”—cardio, ikimaanisha moyo, na thoracic, ikimaanisha kifua. Hii inaheshimisha kazi muhimu ya Rais Nelson kama daktari wa upasuaji wa moyo na msaada aliopewa na marehemu mke wake, Dantzel. Uprofesa huu ulilipiwa na mfuko ulio sanifiwa ili udumu katika siku zijazo. Mtu aliye chaguliwa kwa aina ya uprofesa huu maarufu anapokea kutambuliwa, msaada wa mshahara na fedha za utafiti.

Dkt. Selzman pamoja na Rais Nelson

Daktari wa kwanza wa upasuaji wa moyo aliye chaguliwa kushikilia uprofesa huu alikuwa Dk. Craig H. Selzman, daktari mwenye umahiri wa upasuaji wa moyo ambaye si muumini wa Kanisa letu. Katika sherehe ya kutunza uprofesa huu kwa Dkt. Selzman, wageni wengi muhimu walihudhuria, wakiwemo Rais Nelson na mke wake Dada Wendy W. Nelson. Wakati wa mkutano, Rais Nelson alizungumza kwa kiasi kuhusu taaluma yake ya uanzilishi wa upasuaji wa moyo.

Kisha Dkt. Selzman alishiriki kile kilichomaanisha kwake kuteuliwa katika uprofesa huu. Alieleza kwamba siku nne zilizopita, baada ya siku ndefu kwenye chumba cha upasuaji, aligundua kwamba mmoja wa wagonjwa wake alihitaji kurudi kwenye upasuaji. Dkt. Selzman alikuwa amechoka na mwenye kukata tamaa, akijua kuwa angetumia usiku mwingine pale hospitali.

Dkt. Selzman akiwa pamoja na Dada na Rais Nelson

Jioni hii, Dkt. Selzman alikuwa na maongezi-ya-kubadilisha maisha yeye mwenyewe. Wakati huo, alifikiria, “Siku ya Ijumaa, nitateuliwa kwenye uprofesa unaoitwa kwa jina la Dkt. Nelson. Daima alijulikana kama mtu aliyedhibiti hisia zake, alimtendea kila mtu kwa heshima, na kamwe hakuwa na hasira. Sasa kwamba jina langu litakuwa limeunganishwa na lake, nahitaji kujaribu kuwa zaidi kama yeye.” Dkt. Selzman tayari alikuwa daktari wa upasuaji mahiri. Lakini alitaka kuwa hata bora zaidi.

Hapo awali, timu yake ya upasuaji inawezekana kuwa ilijua kuhusu uchovu wake na kukasirika kwake kwa sababu aliruhusu ionekane kupitia mtindo wake na sauti yake. Lakini katika chumba cha upasuaji usiku huo, Dkt. Selzman alifanya jitihada za kuwa mwangalifu sana ili kuwa mwenye msaada maalum na mwenye kuielewa timu yake. Alihisi kwamba ilileta tofauti na aliazimia kuendelea kujaribu kuwa zaidi kama Dkt. Nelson.

Dkt. Selzman amevaa pini ya RMN

Miaka mitano baadaye, Rais Nelson alichangia nyaraka zake za kitaaluma kwa Chuo Kikuu cha Utah. Watu mashuhuri kutoka Chuoni walikuja kumshukuru rasmi Rais Nelson. Wakati wa tukio hili, Dkt. Selzman alizungumza tena. Akitaja herufi za Rais Nelson, RMN, alisema, “Kuna maadili ya jamii katika ‘RMN’ ambayo sasa yanaenea katika Idara ya Upasuaji wa Moyo na Kifua katika Chuo Kikuu cha Utah.”

Katika hali za kukata tamaa, Dkt. Selzman alieleza, “ninafanya kile tunacho wafundisha wanafunzi wetu kufanya—fokasi, sahau, na fanya vyema kadiri unavyoweza. Maadili haya yanaishi ndani yetu kila siku. Tunawapa pini za kifuani kila mshiriki wa idara na kila mwanafunzi mpya. Chini ya pini kuna herufi hizi‘RMN.’ Maadili ya RMN ni ya msingi kwa mafunzo yetu; tunayafundisha kwa kila mtu. Dkt. Selzman alikuwa kwa makusudi ameboresha mtazamo wake na matarajio yake ya awali kwa sababu jina lake sasa lilikuwa limeunganishwa na lile la Rais Nelson.

Mfululizo huu wa matukio unao mhusisha Dkt. Selzman ulinifanya nijiulize, “Je, mimi nimebadilikaje tangu nimeunganisha jina langu na jina la Yesu Kristo? Je, nimechukua maadlil kama ya Kristo kama matokeo yake? Je, nimejaribu kwa dhati kuwa bora na kuwa zaidi kama Yeye?

Katika uzoefu wa Dkt. Selzman, tunaweza kuona angalau milingano mitano ya mchakato ambao tunajichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo. Ingawa mchakato huo unaanza na ubatizo, haukamiliki hadi pale tutakapo kuwa wasafi na watakatifu zaidi na kuwa zaidi kama Yeye.

Mlingano wa Kwanza ni utambulisho. Uteuzi wa Dkt. Selzman kwenye uprofesa wa Nelson uliunganisha jina lake na la Rais Nelson, na Dkt. Selzman aliaanza kujitambulisha pamoja na Rais Nelson. Tunapojichukulia juu yetu wenyewe jina la Yesu Kristo, tunaunganisha jina letu pamoja na Lake. Tunajitambulisha Naye. Tunafurahia kujulikana kama Wakristo. Tunamtambua Mwokozi na bila aibu tunasimama ili kuhesabiwa kama walio Wake.

Jambo linalohusiana kwa karibu na utambulisho ni mlinganisho mwingine—ukumbusho. Wakati Dkt. Selzman anapoingia ofisini kwake, macho yake yanavutwa kwenye medali aliyopokea alipochaguliwa kwenye uprofesa wa Nelson. Medali hii inamkumbusha kila siku kuhusu maadili ya RMN. Kwetu sisi, kushiriki sakramenti kila wiki kunatusaidia kumkumbuka Yesu Kristo kwa wiki nzima. Tunaposhriki sakramenti, tunafanya hivyo katika ukumbusho wa thamani ya gharama ambayo Yeye alilipa ili kutukomboa sisi. Tunafanya agano upya ili kumkumbuka Yeye, kutambua ukuu Wake na kuthamini wema Wake. Tunatambua tena na tena kwamba ni kwa neema Yake pekee tunaokolewa kutokana na kifo cha kimwili na kiroho.

Ukumbusho inamaanisha kwamba tunafuata ushauri uliotolewa na nabii Alma wa Kitabu cha Mormoni. Tunaacha “vitendo [vyetu] vyote viwe kwa Bwana, na po pote [tuendako, tuache] iwe kwa Bwana; … [tuache] mawazo [yetu] yote yaelekezwe kwa Bwana; … [na tuache] mapenzi ya [mioyo yetu] yawe juu ya Bwana milele.” Hata wakati tunapo jihusisha na mambo mengine, bado tunamkumbuka Yeye, kama tunavyo kumbuka majina yetu wenyewe, bila kujali kile kingine tunacho zingatia.

Ukuaji wa kukumbuka kile alichotufanyia Mwokozi ni mlingano wa tatu—kufuata mfano. Dkt. Selzman alianza kumuiga Rais Nelson na maadili ya RMN. Ninaamini kwamba maadili ya Rais Nelson ni dhihirisho tu la uanafunzi wake wa maisha yote kwa Yesu Kristo. Kwetu sisi, kadiri tunavyojitambua na kumkumbuka Yesu Kristo, ndivyo tunavyotaka kuwa zaidi kama Yeye. Kama wanafunzi wake, tunabadilika kuwa bora tunapo fokasi Kwake, zaidi ya tunapojitazama sisi wenyewe. Tunajaribu kuwa kama Yeye na kutafuta kubarikiwa kwa sifa Zake. Tunasali kwa bidii ili tujazwe na hisani, ule upendo msafi wa Kristo.

Kama Rais Nelson alivyofundisha mwezi Aprili: “Kadiri hisani inavyokuwa sehemu ya asili yetu, tutakosa hamu yaa kuwadhalilisha wengine. Tutaacha kuwahukumu wengine. Tutakuwa na hisani kwa wale wanaotoka katika hali zote za maisha. Hisani kwa watu wote … ni muhimu kwa ajili ya maendeleo yetu. Hisani ni msingi wa sifa ya uchamungu” Sambamba na hisani, tunatafuta, “kukuza, … na kupanua” zawadi nyingine za kiroho kutoka kwa Mwokozi, zikiwemo uadilifu, uvumilivu na bidii.

Kumuiga Yesu Kristo kunatuongoza kwenye mlingano wa nne—mfungamano na madhumuni Yake. Tunaungana Naye katika kazi Yake. Kama daktari wa upasuaji, Dkt. Nelson alijulikana kama mwalimu, mponyaji na mtafiti. Pini kwenye mkunjo wa koti kifuani inayotumika katika Kitengo cha Dkt. Selzman inasisitiza kazi hizi, zikionyesha maneno fundisha, ponya, na gundua. Kwetu sisi, sehemu ya kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo inahusisha kwa hiari, kwa kukusudia, na kwa shauku kufungamanisha malengo yetu na Yake. Tunaungana Naye katika kazi Yake wakati “tunapopenda, tunaposhiriki na tunapoalika.” Tunaungana Naye katika kazi Yake tunapowatumikia wengine, hasa wale walio katika hatari na wale ambao wamejeruhiwa, kuharibiwa au kupondwa na uzoefu wao wa duniani.

Kwa hiyo tunajichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo kwa ukamilifu zaidi kupitia utambulisho, ukumbusho, kuiga mfano na mfungamano. Kutenda haya manne yanatuongoza kwenye mlingano wa tano—uwezeshaji. Tunafikia nguvu na baraka za Mungu katika maisha yetu. Uprofesa wa Nelson unampa Dkt. Selzman utambulisho na fedha za msaada ambazo anazitumia kubadilisha utamaduni katika idara yake. Yeye anatumia hii “baraka ya nguvu” ili kuwasaidia watu wengine. Kwa njia hiyo hiyo, tunapojichukulia sisi wenyewe jina la Mwokozi, Baba yetu wa Mbinguni anatubariki kwa nguvu zake ili kutusaidia kutimiza misioni yetu katika maisha ya duniani.

Tunapofanya maagano ya ziada na Mungu, tunajichukulia juu yetu wenyewe kwa ukamilifu zaidi jina la Yesu Kristo. Kama matokeo yake, Mungu anatubariki zaidi kwa nguvu Zake. Kama Rais Nelson alivyofundisha: “Kila mtu anayefanya maagano katika visima vya ubatizo na hekaluni—na kuyashika—ameongeza ufikiaji wa nguvu ya Yesu Kristo. … “Thawabu ya kushika maagano na Mungu ni nguvu ya mbinguni … ambayo inatuimarisha sisi ili kustahimili majaribu, vishawishi na maumivu yetu ya moyo vyema zaidi.”

Tunakuwa wapokeaji zaidi kiroho. Tunakuwa na ujasiri zaidi wa kukabiliana na hali zisizowezekana. Tunaimarishwa zaidi katika azma yetu ya kumfuata Yesu Kristo. Kwa haraka zaidi tunatubu na kurudi Kwake pale tunapovunja sheria. Tunakuwa bora zaidi katika kushiriki injili Yake kwa nguvu Yake na mamlaka. Tunawasaidia wale walio katika shida bila ya kuwahukumu, bila kuwahukumu kabisa. Tunabakisha ondoleo la dhambi zetu. Tunakuwa na amani kubwa, na tunakuwa wenye shangwe zaidi kwa sababu daima tunaweza kushangilia. Utukufu wake utatuzunguka, na malaika Wake watakuwa na dhamana juu yetu.

Mwokozi anatualika, “Njooni kwa Baba katika jina langu, na katika wakati wake mtapokea utimilifu wake.” Ninawasihi kutenda haya. Njooni kwa Baba Yetu wa Mbinguni. Jichukulie juu yako jina la Yesu Kristo. Jitambulishe pamoja Naye. Daima mkumbuke Yeye. Jitahidi kuwa kama Yeye. Jiunge Naye katika kazi Yake. Pokea nguvu na baraka Zake katika maisha yako. Andika jina Lake moyoni mwako, kwa hiari na kwa kusudia. Hii inakupa wewe “hadhi” mbele za Mungu na kukustahilisha kwa ajili ya uombezi wa Mwokozi kwa niaba yako. Utakuwa mrithi aliyetukuka katika ufalme wa Baba yetu Mbinguni, mshirika wa urithi pamoja na Mzaliwa Wake wa Kwanza, Mwokozi wetu mpendwa na Mkombozi.

Yeye yu hai. Hakika ninajua hivyo. Yeye anakupenda. Yeye alitoa uhai Wake kwa ajili yako. Yeye anakusihi uje kwa Baba kupitia Kwake. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Pesa inatajwa kama endaumenti.

  2. Fanikio moja la kutia moyo ni kazi ya Rais Nelson katika kuunda mashine ya kwanza ya moyo na mapafu ya kupitisha damu iliyotumika katika upasuaji wa moyo.

  3. Rais Nelson aliripoti kwamba katika mafunzo yake ya upasuaji, daktari mmoja katika chumba cha upasuaji alikasirika na kurusha skalpeli ambayo ilitua katika kigasha cha mkono wa Rais Nelson. Rais Nelson alisema: “Uzoefu huu uliniachia mtazamo wa kudumu. Katika saa lile lile, nilijiahidi kwamba chochote kitokeacho katika chumba changu cha upasuaji, kamwe nisingepoteza nidhamu yangu ya hisia. Pia niliweka nadhiri siku hiyo ya kutorusha kitu chochote kwa hasira—iwe visu au maneno” (“Wapatanishi Wanahitajika,” Liahona, Mei 2023).

  4. Mchango huo ulijumuisha zaidi ya ripoti 7,000 za upasuaji, pamoja na karatasi za utafiti na maandiko mengine ya kitaaluma yaliyokusanywa wakati wa kazi ya kipekee ya matibabu ya Rais Russell M. Nelson.

  5. Watu kadhaa walimueleza Rais Russell M. Nelson, akiwemo Rais wa Chuo Kikuu cha Utah, Rais Taylor R. Randall, ambaye alimwita Rais Nelson kama mwanafunzi mwenye heshima kubwa zaidi wa Chuo Kikuu cha Utah.

  6. Neno ethos linaelezea “tabia, hisia, asili ya maadili ya kipekee, au imani zinazoongoza za mtu, kikundi, au taasisi” (Merriam-Webster.com Dictionary, “ethos”).

  7. Mnamo Januari ya 2018, mimi pamoja na mke wangu, Ruthu, tulihudhuria hafla ambayo DKt. Selzman aliteuliwa kwenye Upofesa wa Nelson. Miaka mitano baadaye, niliweza kudhuria tukio rasmi wakati Rais Nelson alipochangia nyaraka zake za kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Utah.

  8. Ona Moroni 7:48.

  9. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa kama “chukua” katika kifungu cha maneno “jichukulie jina la Kristo” humaanisha “kuinua” au “kubeba,” jinsi ambavyo mtu angebeba bendera inayomtambulisha mbebaji pamoja na mtu au kikundi (ona James Strong, The New Strong’s Exhaustive Concordance of the Bible [1984], Hebrew dictionary section, page 80, number 5375).

  10. Ona 2 Nefi 10:24; Moroni 10:32–33; Mafundisho na Maagano 76:69.

  11. Alma 37:36

  12. Dkt. Selzman amenukuliwa akisema: “Wakati wo wote unapoanza kuzungumzia huduma za afya na [Rais Nelson], anapata mng’aro kidogo katika jicho lake. … Ni ajabu kuona jinsi anavyokuwa na nguvu akizungumzia mambo hayo yote” (in Sydney Walker, “As President Nelson Turns 100, His Family and Associates Reflect on His Life and Legacy,” Church News, Sept. 7, 2024, thechurchnews.com). Binafsi nimeweza kuona “mng’aro wa huduma ya afya” katika macho ya Rais Russell M. Nelson, lakini hiyo si kitu kulinganisha na mng’aro alio nao anapomzungumzia Yesu Kristo.

  13. Ona Moroni 7:47–48.

  14. Russell M. Nelson “Kujiamini katika Uwepo wa Mungu,” Liahona, Mei 2025, 128, 128.

  15. Ona 1 Wakorintho 12:31; Mafundisho na Maagano 46:8.

  16. Russell M. Nelson, “Ushiriki wa Akina Dada katika Kukusanya Israeli,” Liahona,, Nov. 2018, 69.

  17. Ona Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023), 123–38.

  18. Ona Musa 1:39. Dhima ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni inaanza na, “Mimi ni mwana mpendwa wa Mungu na Yeye anayo kazi ya kufanywa na mimi. Dhima ya Wasichana inasema: “Kama mwanafunzi wa Yesu Kristo, ninajitahidi kuwa kama Yeye Alivyo. Ninatafuta na kufanyia kazi ufunuo binafsi na kuwahudumia wengine katika jina Lake takatifu (Maktaba ya Injili).

  19. Ona Dieter F. Uchtdorf, “Kazi ya Umisionari: Kushiriki kilichopo Moyoni Mwako,” Liahona, Mei 2019, Gary E. Stevenson, “Penda, Shiriki, Alika,” Liahona, Mei 2022.

  20. Mapema katika huduma yake ya duniani, Mwokozi alifafanua kusudi lake kwetu kwa kunukuu kutoka kwa Isaya: “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema, amenituma kuponya walio vunjika moyo, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa.” (Luka 4:18–19).

  21. Hata sala zetu kwa Baba yetu wa Mbinguni zitabadilika. Kama ilivyoelezwa katika ingizo la Kamusi ya Biblia “Sala”: ‘Wakristo wamefunzwa kusali katika jina la YesuKristo. “Tunaomba katika jina la Kristo wakati mawazo yetu yako katika mawazo ya Kristo na matakwa yetu ni matakwa ya Kristo —wakati maneno Yake yanapokaa ndani yetu (John 15:7). Ndipo sisi tunapoomba vitu ambavyo Mungu anaweza kutupatia. Sala nyingi hubaki bila kujibiwa kwa sababu haziko katika jina la Kristo hata kidogo; haziwakilishi kwa njia yo yote mawazo Yake, lakini zinatokana na uchoyo wa moyo wa binadamu”

  22. Ona Mafundisho na Maagano 109:26.

  23. Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022; msisitizo umeongezwa.

  24. Ona Mafundisho na Maagano 109:21-22. Kifungu cha maneno “wakati watu wako wakivunja sheria, yo yote miongoni mwa hizo” anatumia neno “wakati,” na siyo “kama.” Hii inapendekeza kwamba Mwokozi alitambua kwamba sisi sote tutavunja sheria, tutafanya makosa na kutenda dhambi. Lakini mpango ni kwamba “tutatubu haraka” ili “turejeshwe kwenye baraka” tulizo ahidiwa.

  25. Ona Yohana 16:33; Mosia 4:11; 18:26; Alma 36:2, 28–29; Etheri 7:27; Moroni 9:25.

  26. Ona Mafundisho na Maagano 109:22.

  27. Mafundisho na Maagano 93:19.

  28. Mormon alielezea kilichotokea kwa watu wake wakati Kristo alipokuwa hajihusishi na maisha yao. Watu wake “walikuwa wakati mmoja watu wa kupendeza, na walikuwa na Kristo kama mchungaji wao; ndiyo, walikuwa wanaongozwa hata na Mungu Baba. Lakini sasa, tazama, wanaongozwa na Shetani, hata vile vumbi litimuliwalo mbele ya kimbunga, au vile jahazi linavyo rushwaru shwa juu ya mawimbi, bila tanga wala nanga, au bila kitu cho chote cha kuiendesha; na vile ilivyo, ndivyo walivyo”(Mormoni 5:17–18). Pamoja na Mwokozi maishani mwetu, tumebarikiwa na nguvu, uthabiti, na mwelekeo.

  29. Mafundisho na Maagano 109:24.

  30. Ona Mafundisho na Maagano 45:3–5.

  31. Ona Warumi 8:17.