Wanyenyekevu Hupiga Magoti Madhabahuni
Tunapofanya na kuheshimu maagano yetu, tunajifunga wenyewe kwa Mwokozi, kupokea ufikiaji mkubwa zaidi wa rehema Yake, ulinzi Wake, utakaso, uponyaji na pumziko.
Asanteni, kwaya, kwa ushuhuda wenu kupitia wimbo huo mpya.
Wimbo mpya wa sakramenti “Bread of Life, Living Water” huijaza nafsi yangu. Mstari mmoja katika wimbo unasema, “Sasa naja mbele ya madhabahu, nikimtolea moyo wangu uliovunjika.”
Uelewa wangu wa maneno hayo uliongezeka mara baada ya familia yetu kuondoka Newbury Park, California, kuhudumu katika Misioni ya Utah Ogden mwaka wa 2015. Nilipokea mwaliko wa kuzuru Kambi ya Jeshi la Anga ya Hill huko Layton, Utah. Sikuwa nimewahi kuwa kwenye kituo cha kijeshi, wala sikuwa nimekutana na kasisi wa kijeshi au wanaume na wanawake wanaofanya kazi ili kuandaa usalama na ulinzi kwa nchi yao.
Kasisi Harp, kama maelfu ya makasisi wengine wa hiari na kitaaluma wanaotumikia katika magereza yetu, hospitali, na vituo vya kijeshi kote ulimwenguni, alikuwa mfano wa kuigwa na aliniinua. Eneo letu la mwisho kwenye kituo hicho ilikuwa sehemu ya ibada. Nilimuuliza kasisi huyo ikiwa alitoa huduma kwa watu wote waliotamani kutafakari, kusali, kuwaza na kuabudu. Alikwenda kwenye ukuta wa mbele wa kanisa na kuvuta msalaba kutoka nyuma ya mapazia. Alisema alitumia msalaba huo kwa ibada za Kiprotestanti na Kikatoliki. Niliuliza alitumia nini kwa ndugu na dada zetu Wayahudi, na akaenda upande mwingine wa ukuta wa mbele na kuchomoa Nyota ya Daudi.
Kisha nikauliza, “Unafanya nini kwa ajili ya ibada za Watakatifu wa Siku za Mwisho?” Alisukuma alama hizo mbali na kuelekeza kwenye madhabahu kubwa ya mbao iliyokuwa katikati ya kanisa hilo. Alisema kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hutayarisha na kubariki mkate na maji kwenye madhabahu. Niliuliza ikiwa madhabahu hiyo kubwa iliyoonekana kuwa thabiti iliondolewa kabla ya ibada za ndugu na dada zetu Wayahudi, Waislamu, Wakatoliki au Waprotestanti. Alisema kuwa madhabahu hubakia hapo, kwa imani kadhaa kati ya hizo pia hutumia madhabahu kwa njia fulani.
Ibrahimu alijenga madhabahu, akamfunga Isaka, na alikuwa tayari kumtoa dhabihu mwanawe wa pekee, lakini mkono wake ulizuiwa, na akasema, kama vile Bwana alivyotangaza, “Mimi hapa”! Ni mara ngapi Yeye Mkuu au mmoja wa manabii Wake amejitolea kwa kusema, “Mimi hapa”?
Wakati wa Mahubiri Yake ya Mlimani, Mwokozi alitualika kupatana na kaka na dada zetu kabla hatujakaribia madhabahu. Paulo alifundisha kwamba “tumetakaswa” kwenye madhabahu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.
Nabii Lehi “aliacha nyumba yake … na vitu vyake vya thamani. … [Kisha] akajenga madhabahu … na kutoa sadaka … , na kumshukuru Bwana.”
Biblia na Kitabu cha Mormoni hutufundisha kumwabudu Mwana wa Mungu kwenye madhabahu. Kwa nini?
Wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa, walijenga na kuabudu kwenye madhabahu. Baada ya kutolewa kwenye Bustani ya Edeni na kuabudu kwa “siku nyingi,” malaika aliwatembelea na kuuliza swali kuu ambalo lingeweza kuulizwa kwa kila mmoja wetu: “Kwa nini unamtolea Bwana dhabihu?”
Adamu akajibu, “Sijui.”
Jibu la malaika kwa jibu la adamu la unyenyekevu ni la kushangaza: “Kitu … hiki ni mfano wa dhabihu ya Mwana Pekee wa Baba. … Kwa hiyo, nawe utafanya yale yote uyafanyayo katika jina la Mwana, nawe utatubu na kumlingana Mungu katika jina la Mwana milele yote.”
Meza ya sakramenti na madhabahu za hekalu huashiria dhabihu ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake usio na kikomo.
Tunapofanya na kuheshimu maagano yetu, kupokea ibada ya sakramenti kanisani na endaumenti na kuunganishwa hekaluni, tunajifunga wenyewe kwa Mwokozi, tukipata ufikiaji mkubwa zaidi wa rehema, ulinzi Wake, utakaso, uponyaji na pumziko.
Rehema na Ulinzi kupitia Maagano
Kama kijana wa umri wa miaka 15, nilimuomba baba yangu kama ningeweza kutohudhuria mkutano wa sakramenti—kwa Jumapili moja tu ya Januari kwa ajili ya mchezo maalum wa mpira wa Marekani. Alisema kwamba nilikuwa na umri wa kutosha kujifanyia uamuzi huo na akaniomba nifikirie shauri moja. Alisema, “Ukichagua kukosa sakramenti mara moja, ni rahisi kuchagua kuikosa tena.”
Kama Mwokozi ndiye kiunganishi kikuu, basi adui ndiye mtenganishaji. Yeye, Shetani, hutujaribu tujitenge na sehemu zetu za kuabudu zilizowekwa wakfu na kutoka kwenye ulinzi wa Yesu Kristo. Tunapomwabudu Mwokozi, tunapokea “uwezo wa kwenda kinyume na mtiririko wa asili wa kidunia.” Tunapotumia muda katika ushirika pamoja Naye, tuna ahadi ya “kukombolewa kutoka kwa Shetani.” “Kisha, tunaposhika maagano yetu, Yeye hutubariki kwa nguvu Yake ya kuimarisha.” Oh, jinsi ninavyothamini uzoefu wa kuwasiliana na Mwokozi kupitia maagano yaliyofanywa kwenye madhabahu takatifu.
Kukuza ufahamu wa Upatanisho wa milele wa Mwokozi mstari juu ya mstari, kanuni juu ya kanuni, hutoa chanjo ya kiroho dhidi ya hila za adui. Jaggi mmisionari kijana huko Mexico, Zuster Jaggi huko Ubelgiji, na wamisionari wengine kote ulimwenguni wana uwezekano mkubwa wa kuona marafiki zao wakidai baraka za ubatizo na kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu ikiwa marafiki zao wanahudhuria mkutano wa sakramenti ndani ya wiki ya kwanza ya toka wakutane nao.
Kijana huko Tonga au Samoa ana uwezekano mkubwa zaidi wa kuunganishwa katika nyumba ya Bwana kama wamejitayarisha kwa ajili ya na kupokea endaumenti zao baada ya kuhitimu masomo yao. Katika endaumenti, waumini wanaalikwa kuishi, kutii na kushika sheria tano ambazo huleta nguvu na ulinzi katika maisha yao. Tunapofanya maagano na Bwana, uhusiano baina yetu hufanyika. Tunaonyesha utiifu na upendo wetu Kwake. Nguvu na uwezo wetu huongezeka kwa kila ahadi iliyofanywa na kutunzwa.
Tafakari na Utakaso
Tunapopiga magoti kwa unyenyekevu na kiishara kwenye madhabahu za Bwana, ni fursa ya kutafakari, “kuchunguzwa kuhusu kiburi cha mioyo [yetu], … [kujinyenyekeza wenyewe] mbele za Mungu.” Kabla ya kwenda matembezini na marafiki zangu nikiwa kijana, mara nyingi mama yangu alisema, “Kumbuka wewe ni nani, na tafadhali nione wakati ukirejea nyumbani.” Mara kadhaa usiku nilishindwa kumuona kwa sababu nilichelewa kurudi nyumbani. Ninajuta kukosa muunganiko huo muhimu na Mama yangu.
Leo, ninatazamia kupata muunganiko pamoja na Baba wa Mbinguni. Katika mfumo wangu wa kila siku wa kuabudu, ninapiga magoti kusali, karibu na kitanda changu au kukusanyika na familia, na ninajiona nikipiga magoti kwenye madhabahu, nikitafakari na kuchunguza maisha yangu. Ninafikiria kuhusu sakramenti, hata vipande vizima vya mkate, vilivyomegwa na kuvunjwa kwa ajili yetu, kila kimoja kikiwa ni ishara ya mwili uliovunjika wa Mkombozi wetu. Ninakumbushwa kuhusu mafundisho ya Rais Dallin H. Oaks kwamba “kila kipande cha mkate ni cha kipekee, kama vile watu binafsi wanaoushiriki ni wa kipekee.” Ninapopiga magoti katika sala, ninafikiria jinsi ninavyoweza kumpa Mungu mapenzi yangu.
Mzee David A. Bednar alifundisha kwamba: “ibada ya sakramenti ni mwaliko mtakatifu na unaojirudia wa kutubu kwa dhati na kufanywa upya kiroho. Kitendo cha kushiriki sakramenti, ndani yake na katika kitendo chenyewe, hakiondoi dhambi. Lakini tunapojiandaa kwa dhamira na kushiriki katika ibada hii takatifu kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka, basi ahadi ni kwamba tunaweza daima kuwa na Roho wa Bwana pamoja nasi. Na kwa nguvu za utakaso za Roho Mtakatifu kama mwenzi wetu daima, twaweza daima kudumisha msamaha wa dhambi zetu.”
Wakati mimi na Amy tunatazama kwa karibu uzoefu wetu wa maisha, tunasherehekea zawadi ya upendo na dhabihu kamili ya Yesu Kristo. Pia tunaona jinsi ghadhabu ya kuzimu ilivyopunguzwa. Tunawezaje kushinda mitazamo ya hukumu, wasiwasi, mfadhaiko, saratani, kisukari, uonevu mtandaoni, utambulisho ulioibiwa, kupoteza mimba, kufiwa na mtoto, kaka na baba? Kwa sababu Yesu alichukua kikombe kichungu cha kutetemeka, kikombe cha ghadhabu—kwa ajili yangu, kwa ajili ya familia yangu, kwa ajili yetu sote!
Gethsemane, na Adam Abram, kwa heshima ya altusfineart.com © 2025
Kikombe “kichungu” alikunywa katika bustani ya Gethsemane na mateso Yake “yaliyozidi” pale msalabani Kalvari, huturuhusu kuwaweka wagumu, wenye jeuri, wenye fujo, wenye ghadhabu, na wanaotetemeka juu ya madhabahu za Bwana na “kutakaswa kwa kupokea Roho Mtakatifu;” siku zote.
Dada Patricia Holland alisema, “Ombi langu kuu kwako na kwangu mimi leo ni kwamba tujitoe kabisa, tujiweke kwenye madhabahu ya ahadi za Mungu na amani haijalishi tuko wapi na haijalishi tumefanya nini.”
Mahali pa Uponyaji na Pumziko
Tunapokuja madhabahuni, hatupati thawabu; tunajifunza kuhusu Mtoa Thawabu. Katika mafunzo hayo na kufungwa kimaagano huja uponyaji. Nefi alisema, “Amenijaza upendo wake, hata kwa kumaliza mwili wangu.” Na mpendwa Mkombozi wetu alitualika, “Je, hamtarudi kwangu sasa, na kutubu dhambi zenu, na kugeuka, ili niwaponye?”
Wakati mabinti zetu wakubwa wawili, Mackenzie na Emma, walipokuwa wadogo, moja ya hadithi yao pendwa ilikuwa The Chronicles of Narnia: The Lion, the Witch and the Wardrobe. Sote tulimpenda simba, Aslan. Moja ya usiku wetu wa kukumbukwa sana kusoma kitabu ilikuwa wakati simba mkuu alitoa maisha yake kwa ajili ya Edmund. Ni usiku wa kukumbukwa kwa sababu wazazi na mabinti walimwaga machozi wakati maisha ya simba yalichukuliwa kwenye Jedwali la Jiwe na Mchawi. Ni usiku wa kukumbukwa kwa sababu matumaini yaliendelea, licha ya janga hilo, hadi tukio la kushangaza lilipotokea. Vigelegele vya furaha vilitawala katika chumba kidogo cha kulala wakati Aslan alipofufuliwa na kusema, “Kama [Mchawi angejua maana ya kweli ya dhabihu], … [angejua] kwamba [ikiwa] mwathirika wa hiari ambaye hakufanya hila [angekufa] badala ya msaliti, Jedwali la [Mawe] lingepasuka, na kifo chenyewe kingeanza [kutoweka].”
Yesu Kristo huponya majeraha yote. Yesu Kristo anafanya iwezekane kuishi tena.
Katika hotuba yake ya mkutano mkuu wa Oktoba 2022, Rais Russell M. Nelson alielezea kikundi cha watalii kwenye matembezi ya wazi ya hekaluni. Mvulana mdogo alikuwepo. Rais Nelson alifundisha:
“Wakati kikundi kilipoingia katika chumba cha endaumenti, mvulana alionyesha kwa kidole madhabahu, mahali ambapo watu wanapiga magoti ili kufanya maagano na Mungu, na akasema, ‘Oh, ile ni nzuri. Hapa ni mahali pa watu kupumzika kwenye safari yao ya hekaluni.’
“… Inawezekana hakuwa na wazo kuhusu uhusiano wa moja kwa moja kati ya kufanya maagano na Mungu hekaluni na ahadi ya ajabu ya Mwokozi:
“Njooni kwangu, ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
“Jitieni nira yangu, na mkajifunze kwangu; … nanyi mtapata pumziko nafsini mwenu.
“‘Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi’ [Mathayo 11:28–30].msisitizo umeongezwa].”
“Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake,” hata hivyo Aliwaalika wanafunzi Wake, mimi na wewe, kwenye meza ya sakramenti kupumzika pamoja Naye hapo. Wakati “nafsi za wanyenyekevu hupiga magoti kwenye madhabahu” amani hujaa. Mikono ya Mwokozi wetu imenyoshwa; Meza yake imetandazwa. Njooni tumwabudu Mwana wa Mungu kwenye madhabahu zake takatifu Katika jina la Yesu Kristo, amina.