Upendo wa Yesu Kristo wa Kulipia Dhambi
Uponyaji na msamaha vinapatikana katika utimilifu wake katika upendo wa Yesu Kristo wenye kulipia dhambi.
Ninaeleza upendo wangu kwa Rais Russell M. Nelson na shukrani zangu kwa ushawishi usio kifani aliokuwa nao kwa kila mmoja wetu. Na kwetu sisi sote, ninamshukuru Mungu kwa kuyatunza na kuyakuza maisha mema ya Rais Dallin H. Oaks.
Kwa kila mwaka unaopita, ninajisikia upendo mkubwa kwa ajili ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo, na kwa Upatanisho Wake wenye rehema. Dhabihu Yake kuu, yenye kuhakikisha ushindi dhidi ya mauti na dhambi, ndiyo matokeo yenye mchango mkubwa katika historia yote ya mwanadamu. Kuelewa zawadi Yake ya kiungu kwangu mimi ni kilele cha wazi cha mafunzo ya kimbingu ambayo yataendelea hata baada ya kaburi.
Huruma ya Mwokozi yenye nguvu katika kusamehe dhambi na katika uponyaji wa majeraha yaliyo sababishwa na dhambi za wengine ni dhihirisho kuu zaidi la kimuujiza la upendo wa Mungu.
Hamu yangu ni kutoa tumaini kwa wale wanao tafuta msamaha wa dhambi zilizo kubwa na kutoa faraja kwa wale wanao tafuta uponyaji kutokana na majeraha machungu zaidi yaliyo sababishwa na dhambi kubwa za watu wengine.
Uponyaji na msamaha vinapatikana katika utimilifu wake katika upendo wa Yesu Kristo wenye kulipia dhambi.
Imani katika Yesu Kristo
Kama umetenda dhambi kubwa na uko katika mchakato wa kutubu au unayo hamu ya kutubu kikamilifu na kuhisi shangwe isiyo elezeka ya msamaha, tafadhali jua kwamba muujiza huu unakusubiria wewe. Mwokozi kwa mwendelezo anaita, “Njooni kwangu.”
Kuimarisha imani yako katika Mwokozi wetu, Yesu Kristo, kutahuisha kutamani kwa nafsi yako kumjua Yeye, kuamini katika Yeye, na kuuweka moyo wako Kwake. Enoshi aliomba msamaha kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, “Bwana, je, inafanywa vipi? Bwana akamjibu, “Kwa sababu ya imani yako katika Kristo, ambaye wewe hujamwona kamwe wala kumsikia.”
Na Moroni aliongeza, “Ikiwa mtajinyima ubaya wote na kumpenda Mungu na mioyo yenu, akili, na nguvu zenu zote, basi neema Yake inawatosha.”
Kugeuka kutoka dhambini, kugeuka kumwelekea Mungu, na kuimarisha imani yako katika Yesu Kristo ni mwanzo mzuri. Kwa unyenyekevu kukabidhi mapenzi yako kwa Mungu ikijumuisha kukiri dhambi zako kubwa kwa askofu wako au rais wa tawi, lakini msamaha wako kamili huja kutoka kwa Mwokozi. Msamaha ni zawadi ya kiungu inayotolewa kupitia neema ya Yesu Kristo.
Uaminifu
Hamu ya kweli ya kurudi kwa Mungu inaambatana na dhamira ya dhati ya kuwa mwaminifu kiukamilifu kwa Baba yako wa Mbinguni, kwako wewe mwenyewe, na wale ulio waumiza, na kwa kiongozi wako wa ukuhani. Baba yako wa Mbinguni hufurahia katika azimio lako la kuja Kwake kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka. Kuwa na roho iliyopondeka ni kwa unyenyekevu kujiweka wewe mwenyewe katika mikono ya Mungu; kuwa na moyo uliovunjika huleta kile Mtume Paulo alikielezea kama “huzuni ya kiungu,” ni hamu ya kina ya nafsi ya kurudi Kwake kwa gharama yo yote.
Kurejesha Kilichovunjika
Hamu yako hukuelekeza kwenye kutaka kurekebisha kile ulichovunja. Lakini, kwa kutambua kuwa baadhi ya mambo hayapo katika uweza wako wa kuyarekebisha, unasali kwa dhati kwamba Bwana, kupitia neema Yake, atasaidia kuwaponya wale walioumizwa kama matokeo ya matendo yako.
Athari za dhambi kubwa kwa watu wengine mara nyingi ni ngumu sana kuzishinda. Je, unafuata mfano wa wana wa Mosia, ambao “wakijibidiisha wakijitahidi kuponya majeraha yote waliyofanya”? Zungumza na wale unao waheshimu kuhusu kile ambacho yawezekana hukioni.
Nilipokuwa nikiandaa mahubiri haya, nilipokea barua pepe nisiyotarajia kutoka kwa mtu fulani aliye katika mchakato wa kutubu na anatamani kurudi Kanisani. Mke wake wa zamani bado alikuwa anateseka kutokana na “kupotea kwa ndoa [yao] ya milele, [magumu pamoja na watoto], kupotea kwa usalama wa kifedha, … kuto [kuweza] kumudu gharama za maisha, [na] hisia zenye kukaba roho za kusalitiwa.”
Alishiriki na mimi jinsi kiongozi wake wa ukuhani “alivyojisikia kuvutiwa [kumwomba] kwa sala kufikiria nini [zaidi angeweza kufanya kwa ajili ya mke wake wa zamani na watoto].” Kwa ruhusa yake ninashiriki sehemu ya barua pepe yake:
“[Kwanza] nilifikiri [pesa] niliyoiacha katika tamko langu la talaka ilikuwa zaidi ya ukarimu, lakini rais wangu wa tawi alinihimiza kufunga na kusali kuhusu hilo.
“Mwanzoni, nilipambana na wazo la kurejesha zaidi. Kwa vile dhambi zangu hazikuwa za kifedha, nilijiuliza ‘kurejesha kwa ukarimu’ hasa maana yake ni nini … [lakini] punde niligundua haikuwa tu kuhusu pesa.
“Viongozi wangu wa ukuhani walikutana na [mke wangu wa zamani] na watoto wangu walikuwa bado wanapambana na hawajapona.”
“Lengo langu jipya lilikuwa ni kusonga mbele kwa imani. … Nilielezea tu hamu yangu ya kusaidia lakini bila masharti kwenye jambo hilo. … Niliamua [kumtumia mke wangu wa zamani kiasi maalumu] kutoka kila mshahara ninaolipwa, ambacho kilikuwa sehemu kubwa ya mshahara wangu. Kabla tu ya kufanya malipo yangu ya kwanza, Bwana [alishawishi akili yangu kwamba nilihitajika] kutoa [mara mbili ya kiasi kile].
“Nimejifunza kwamba urejeshaji siyo tu kuhusu pesa. Ni kuhusu kwa unyenyekevu kuyatoa kwa dhati maisha yetu kwa Bwana. … Pesa ni kwa ajili ya kusaidia kufidia kile nilichokichukua kutoka kwa familia yangu kwa sababu ya chaguzi zangu mbaya. Ni kuhusu kufanya na kutimiza ahadi pasipo kutarajia cho chote kama malipo na kumsaidia yeye asihofu kuhusu malipo ya bili ili aweze kumtafuta roho.”
Jitihada zako za kurejesha kile ulicho kivunja yawezekana zisihusiane na pesa, lakini kadiri kwa unyenyekevu unaposhauriana na Bwana, unaweza kuona kuna la zaidi unaloweza kufanya.
Idhini ya Kiungu Kidogo Kidogo
Unapotafuta msamaha wa Bwana, kuwa na subira, unapongojea idhini Yake kamili. Zingatia andiko hili:
“Wao … walijinyenyekeza wenyewe katika vina vya unyenyekevu; na … walimlilia Mungu sana; ndiyo, hata siku yote. … [Lakini] Bwana alikuwa mzito kusikia kilio chao kwa sababu ya maovu yao.”
“Hata hivyo Bwana alisikia vilio vyao, na kuanza … kupunguza mizigo yao; … na … wakaanza kufanikiwa kidogo kidogo.”
Kuwa mvumilivu Bwana anapokupa baraka Zake na idhini Yake kidogo kidogo.
Katika wakati wa Bwana, utahisi sauti ya Bwana ikikuambia, “Vitu hivi visikusumbue tena.” Siku moja, kadiri unavyoendelea kumgeukia Mwokozi, Baba Yako wa Mbinguni “ataondolea mbali hatia kutoka [moyoni mwako], kupitia neema ya Mwanawe.”
Kujeruhiwa na Kuteseka
Kwa wewe ambaye umejeruhiwa pasipo haki na dhambi kubwa za wengine, ninatamani kushiriki upendo na huruma ya Mwokozi, faraja Yake na amani.
Huzuni ambayo umeihisi, kuvunjika moyo, upotevu, hisia za kuchosha za usaliti, zenye kuangusha maisha yako kama ambavyo umefikiria kuwa hivyo—ninakupeni hakikisho langu la dhati, kuwa huyu Mwokozi anakujua na anakupenda. Mfikie Yeye. Yeye ni faraja na nguvu yako; Yeye atakutumia malaika Wake ili wakubebe. Lini uchungu wako utatoweka, huzuni yako kunyamazishwa, kumbukumbu zisizotakiwa kusahaulika? Mimi sijui. Lakini hili nalijua: Yeye anao uweza wa kuleta uzuri kutoka katika majivu ya mateso yako.
Wapendwa Kaka zetu na dada zetu wa Grand Blanc, Michigan, kwa imani yao katika Yesu Kristo isiyotishika, na kwa ujasiri wao na kutokuwa kwao na ubinafsi, wamepokea na watapokea, katika wiki na miezi ijayo, wingi wa upendo na neema ya Mwokozi isiyo linganishwa.
Unapoendelea kuweka kuamini kwako katika Yeye, mawingu ya kiza na kwikwi za kuonyesha huzuni usiku zitabadilishwa kuwa maporomoko ya ghafla ya machozi ya shangwe na amani katika mwangaza wa asubuhi. “Huzuni yako itageuzwa kuwa shangwe. … Na shangwe yako hakuna mtu atakayeitwaa kutoka kwako.” Wakati huo utakuja. Nashuhudia kwamba utakuja.
Upendo wa Yesu Kristo wenye kulipia dhambi unaweza kupatikana katika hali ngumu sana, lakini sisi sote kwa kiasi kisichobadilika tunahitaji neema ya Mwokozi wetu ya kulipia dhambi. Rais Dallin H. Oaks amefundisha: “Kwa sababu ya uzoefu Wake wa kulipia dhambi katika maisha ya duniani, Mwokozi wetu anaweza kufariji, kuponya, na kuimarisha wanaume wote na wanawake wote kila mahali, lakini mimi naamini Yeye hufanya hivyo kwa wale tu ambao wanamtafuta Yeye na kuomba msaada Wake. Mtume Yakobo alifundisha: ‘Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza’ (Yakobo 4:10). Tunastahili baraka hiyo tunapoamini katika Yeye na kuomba msaada Wake.”
Mzee Robert E. Wells
Nilipokea ruhusa kutoka kwa rafiki yangu kipenzi Mzee Robert E. Wells, Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka aliyepumzishwa na kubaki na heshima hiyo, sasa ana miaka 97, ameniruhusu kushiriki uzoefu wake huu wa zaidi ya miaka 60 iliyopita.
Wakati akiishi huko Paraguai mwaka 1960 na akiwa ameajiriwa kama mfanya kazi wa kimataifa wa benki, Robert Wells, wakati huo akiwa na umri wa miaka 32, na mke wake, Meryl, wote wawili walikuwa marubani katika ndege mbili tofauti, wakiruka kutoka nyumbani Uruguay kwenda Paraguay. Wakiyakabili mawingu mazito, Robert na Meryl walipoteana kimawasiliano ya kuona na ya radio wao kwa wao. Robert kwa haraka akatua, ambapo aligundua kwamba ndege ya mke wake ilikuwa imedondoka. Si mke wake wala wale marafiki wawili walioruka pamoja na mke wake hakuna aliyenusurika. Watoto wake nyumbani huko Asunción, walikuwa wa umri wa miaka saba, mitano , na miwili.
Mzee Wells alizungumzia juu ya huzuni yake:
“Maneno milele hayatatosha kuelezea huzuni iliyo vimba ndani yangu, ikimaliza hisia zangu na kutia ganzi fahamu zangu. Machozi ya huzuni ya ndani kabisa hayakukoma kutiririka. Kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, akili yangu ilipokuwa ikijaribu kushughulikia uhalisia wa kifo cha mke wangu, nilijikuta nikipitia hisia za hatia kubwa ya kujihisi niliwajibika kwa kudondoka kwa ndege hiyo.”
Robert alijilaumu mwenyewe kwa kutohakikisha ukaguzi wa kina wa ndege hiyo na kwa kutompa mke wake maelekezo mazuri zaidi ya vifaa vya kurusha ndege. Alihisi alikuwa na hatia ya uzembe.
Robert alisema:
“Akili yangu iliingia katika giza lenye kudunduwaza. … Nilikuwepo tu—[kwa ajili ya watoto,] na siyo zaidi.”
“Mimi … nilipoteza hamu yangu ya kuendelea.”
Baada ya muda, Robert alibarikiwa kwa kupitia tukio hili la kina la kiroho. Alisimulia:
“Jioni moja, karibia mwaka mmoja baadaye, wakati nimepiga magoti kusali, muujiza ulitokea. Wakati nikisali na kumsihi Baba wa Mbinguni, nilihisi kama vile Mwokozi alikuja pembeni yangu na nikasikia sauti ya kuweza kusikika ikisema maneno haya nafsini mwangu na masikioni mwangu: ‘Robert, dhabihu yangu ya kulipia dhambi ililipia dhambi zako na makosa yako. Mke wako anakusamehe. Marafiki zako wanakusamehe. Nitainua mzigo wako. …’
“Kutokea muda huo, mzigo wa hatia [na kukata tamaa] kwa mshangao viliinuliwa kutoka kwangu. Nilikuwa nimeokolewa! Mara moja nilielewa nguvu yenye kuzingira ya Upatanisho wa Mwokozi na … kwamba ilitumika moja kwa moja kwangu. …’ Mimi …nilipitia nuru na shangwe ambayo kamwe sikuwahi kuijua hapo kabla. … Nilikuwa nimepatiwa zawadi ambayo sikuifanyia kazi—zawadi ya neema ya Bwana. … Sikuistahili—sikuwa nimefanya lo lote la kustahili hiyo, lakini hata hivyo Yeye alinipatia.”
Akina kaka na akina dada, na kila mmoja wetu “atakaswe katika Kristo kwa neema ya Mungu, kupitia kumwagwa kwa damu ya Kristo, … [ili mpate kuwa] watakatifu pasipo mawaa.”
Ninashuhudia juu ya upendo, rehema, na neema ya Mwokozi na Mkombozi wetu. Yeye yu hai. Sisi ni Wake; sisi ni watoto wa agano. Kadiri tunavyoamini katika Yeye, kumfuata Yeye, na kumtumainia Yeye, Yeye atatuinua kutoka kwenye huzuni yetu na dhambi zetu. Kisha, kupita maisha haya ya duniani, katika nyumba ya Baba Yake, tutaishi pamoja na Yeye milele na milele. Katika jina la Yesu Kristo, amina.