Mkutano Mkuu
Heri Wapatanishi
Mkutano mkuu wa Oktoba 2025


13:16

Heri Wapatanishi

Upatanishi bado unaanzia mahala pa muhimu zaidi—ndani ya mioyo yetu. Kisha nyumbani na kwenye familia.

Karibuni kwenye mkutano mkuu. Tunashukuru jinsi gani kwa kukusanyika.

Tunapotazamia matangazo haya ya mkutano, tunafahamu vyema juu ya wiki zilizotangulia hili. Tunatambua kwamba mioyo mingi inaomboleza kwa upotevu, na baadhi wanahisi kutokuwa na uhakika kunakosababishwa na vurugu au majanga kote ulimwenguni. Hata watu wacha Mungu waliokusanyika katika sehemu takatifu—ikijumuisha kanisa takatifu katika Michigan—wamepoteza maisha yao au wapendwa wao. Ninazungumza kutoka ndani ya moyo wangu, nikitambua kwamba mingi ya mioyo yenu imelemewa na kile ambacho ninyi, familia zenu, au ulimwengu wetu umepitia tangu mkutano mkuu uliopita.

Kapernaumu Galilaya

Vuta taswira pamoja nami kwamba wewe ni kijana katika Kapernaumu, kando ya Bahari ya Galilaya, wakati wa huduma ya Yesu Kristo. Taarifa zinasambaa kuhusu rabi—mwalimu—ambaye ujumbe wake unawavuta wengi. Majirani wanapanga kusafiri kwenda mlima ulio mkabala na bahari ili kumsikiliza.

Unaungana na wengine kutembea katika njia yenye vumbi ya Galilaya. Unapofika, umati mkubwa uliokusanyika kumsikiliza huyu Yesu unakushangaza. Baadhi wananong’ona kwa upole, “Masiya.”

Unasikiliza. Maneno Yake yanaugusa moyo wako. Kwenye matembezi marefu ya kurudi nyumbani, unachagua ukimya badala ya mazungumzo.

Unatafakari mambo ya kustaajabisha—mambo ambayo ni zaidi hata ya sheria ya Musa. Alizungumza kuhusu kugeuza shavu lingine na kuwapenda maadui zako. Aliahidi, “Heri wapatanishi: maana hao wataitwa wana wa Mungu.”

Katika uhalisia wako, kadiri unavyohisi uzito wa siku ngumu—kutokuwa na uhakika na hofu—amani inaonekana kutofikika.

Hatua zako zinaongezeka; unafika nyumbani umechoka sana. Familia yako inakusanyika; baba yako anauliza, “Tuambie kile ulichosikia na kuhisi.”

Unashiriki kwamba Alikualika kuacha nuru yako iangaze mbele za watu, kutafuta haki hata wakati unapoudhiwa. Sauti yako inatetemeka unaporudia, “Heri wapatanishi: maana hao wataitwa wana wa Mungu.”

Unauliza, “Ninaweza kweli kuwa mpatanishi wakati ulimwengu upo katika vurugu, wakati moyo wangu umejaa hofu, na wakati amani inaonekana kutofikika?”

Baba yako anamtazama mama yako na kujibu kwa upole, “Ndiyo. Tunaanzia mahali pa muhimu zaidi—ndani ya mioyo yetu. Kisha kwenye nyumba na familia zetu. Tunapofanya mazoezi huko, upatanishi unaweza kusambaa kwenye mitaa na vijiji vyetu.

Peleka Mbele Miaka 2,000

Peleka mbele miaka 2,000. Hakuna haja ya kuvuta taswira—huu ni uhalisia wetu. Ingawa mashinikizo yanayohisiwa na kizazi chipukizi cha leo ni tofauti na yale ya kijana katika Galilaya—ubaguzi, ukosefu wa dini, visasi, hasira barabarani, jeuri, na mashambulizi kwenye mitandao ya kijamii—vizazi vyote viwili vinakabiliana na tamaduni za migogoro na mashinikizo.

Kwa shukrani, wavulana na wasichana wetu kadhalika wameletwa kwenye nyakati zao za Mahubiri ya Mlimani: seminari, mikutano ya Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, na Njoo, Unifuate. Hapa wanapokea mialiko sawa ya kudumu kutoka kwa Bwana: kuacha nuru yao iangaze mbele za watu, kutafuta haki hata wakati wanapoudhiwa, na kuwapenda maadui zao.

Wanapokea pia maneno ya kutia moyo kutoka kwa manabii walio hai wa Urejesho: “Wapatanishi Wanahitajika.” Kuwa na maoni tofauti bila kuwa adui. Badilisha ubishi na kiburi kwa msamaha na upendo. Jenga madaraja ya ushirikiano na uelewa, si kuta za chuki au ubaguzi. Na ahadi ileile: “Heri wapatanishi: maana hao wataitwa wana wa Mungu.”

Mioyo ya kizazi chipukizi cha leo imejaa ushuhuda wa Yesu Kristo na tumaini kwa ajili ya siku zijazo. Na bado wao pia wanauliza, “Ninaweza kweli kuwa mpatanishi wakati ulimwengu upo katika vurugu, moyo wangu umejaa hofu, na amani inaonekana kutofikika?”

Jibu imara kwa mara nyingine ni ndiyo! Tunayakubali maneno ya Mwokozi: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa. … Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”

Upatanishi bado unaanzia mahala pa muhimu zaidi—ndani ya mioyo yetu. Kisha nyumbani na kwenye familia. Tunapofanya mazoezi huko, upatanishi utasambaa katika ujirani na jumuiya zetu.

Hebu tuzingatie zaidi maeneo haya matatu ambapo Mtakatifu wa Siku za Mwisho wa leo “anakuwa mpatanishi .

Upatanishi Ndani ya Mioyo Yetu

Kwanza ni ndani ya mioyo yetu. Kipengele cha wazi cha huduma ya Kristo kinaelezea jinsi watoto walivyovutiwa Naye. Hapo ndipo kidokezo kilipo. Kutazama ndani ya moyo msafi na usio na hatia wa upatanishi wa mtoto inaweza kuwa uvuvio kwa mioyo yetu. Hivi ndivyo watoto kadhaa wa umri wa Msingi walivyojibu “Inaonekanaje kuwa mpatanishi?”

Ninashiriki majibu yao moja kwa moja kutoka mioyoni mwao! Luke alisema, “Daima wasaidie wengine.” Grace alishiriki jinsi ilivyo muhimu kusameheana, hata wakati ambapo haionekani kuwa sawa. Anna alisema, “Nilimwona mtu ambaye hana wa kucheza naye, hivyo nilienda kucheza naye.” Lindy alisema kwamba kuwa mpatanishi ni kuwasaidia wengine. “Kisha unasongesha hilo mbele. Litaendelea mbele tena na tena.” Liam alisema, “Usiwe mkorofi kwa watu, hata kama wao ni wakorofi kwako.” London alisema kwa msisitizo, “Ikiwa mtu anafanya mzaha au ni mkorofi, unasema, ‘Tafadhali acha.’” Trevor alisema, “Ikiwa kuna donati moja imebaki na wote mnaitaka, mnagawana.”

Majibu ya watoto hawa ni ushahidi kwangu kwamba sote tumezaliwa na tabia ya asili ya kiungu ya ukarimu na huruma. Injili ya Yesu Kristo hukuza na kufuma pamoja tabia hizi za kiungu, ikijumuisha upatanishi, ndani ya mioyo yetu, zikitubariki katika maisha haya na yajayo.

Upatanishi Nyumbani

Pili, kujenga upatanishi ndani ya nyumba zetu kwa kutumia mpangilio wa Bwana kushawishi mahusiano kati yetu: ushawishi, uvumilivu, upole, ukarimu, unyenyekevu na upendo usio unafiki.

Hapa kuna hadithi ya kuvutia inayoelezea jinsi familia moja ilivyofanya upatanishi kuwa lengo la pamoja, wakifanyia kazi kanuni hizi.

Watoto katika familia hii walikuwa wakipata shida katika uhusiano wao na mtu ambaye tabia yake mara nyingi ilikuwa hasira, kujikweza, na ukali. Watoto, wakiumizwa na kukasirishwa, walianza kujiuliza ikiwa njia pekee ilikuwa ni kuiga tabia zilezile za roho ya ukatili.

Jioni familia ilizungumza kwa uwazi pamoja kuhusu hali ile na madhara yake. Na kisha wazo likaibuka—si tu suluhisho bali jaribio.

Badala ya kujibu kwa ukimya au kisasi, watoto wangefanya jambo lisilotarajiwa: wangejibu kwa ukarimu. Si tu kujizuia kwa upole bali utoaji wa makusudi, kutoka moyoni wa maneno ya ukarimu na matendo ya kujali, bila kujali malipo yake. Wote walikubali kujaribu kwa muda fulani, ambapo baadaye wangekutana tena na kujadili.

Ingawa baadhi mwanzoni walisita, walijikita kwenye mpango kwa moyo wa dhati.

Kilichotokea baadaye kilikuwa cha kustaajabisha.

Uadui ulianza kupungua. Tabasamu zikachukua nafasi ya hasira. Mtu mzima yule, aliyekuwa adui na mkali, alianza kubadilika. Watoto, wakipewa nguvu na uchaguzi wao wa kuongoza kwa upendo, walipata shangwe katika badiliko. Badiliko lilikuwa kubwa kiasi kwamba mkutano wa ufuatiliaji uliopangwa haukuhitajika. Ukarimu ulikuwa umefanya kazi yake ya kimya kimya.

Baada ya muda, miunganiko ya kweli ya urafiki ilijengwa, ikimuinua kila mmoja. Ili kuwa wapatanishi, tunawasamehe wengine na kwa makusudi kuwainua wengine badala ya kuwashusha chini.

Upatanishi kwenye Jumuiya Zetu

Tatu, upatanishi kwenye jumuiya zetu. Katika miaka ya dhiki ya Vita ya Pili ya Dunia, Mzee John A. Widtsoe alifundisha: “Njia pekee ya kujenga jumuiya yenye amani ni kuwajenga wanaume na wanawake wenye upendo na wapatanishi. Kila mmoja, kwa fundisho hilo la Kristo … anashikilia mikononi mwake amani ya ulimwengu [mzima].”

Hadithi ifuatayo inaelezea kwa uzuri mstari huo.

Miaka kadhaa iliyopita, wanaume wawili—imamu wa Kiislamu na Pasta wa Kikristo kutoka Nigeria—walisimama pande mkabala za mgawanyo mchungu wa kidini. Kila mmoja alikuwa ameteseka sana. Na bado, kupitia nguvu ya uponyaji ya msamaha, walichagua kutembea pamoja.

Pasta James Wuye na Imamu Muhammad Ashafa

Imamu Muhammad Ashafa na Pasta James Wuye walikuwa marafiki na washirika ambao hawakutarajiwa wa amani. Kwa pamoja walianzisha kituo kwa ajili ya upatanishi wa mchanganyiko wa dini. Sasa wanawafundisha wengine kubadilisha chuki kwa tumaini. Wakiwa wameteuliwa mara mbili kwa ajili ya Tuzo ya Amani ya Nobel, hivi karibuni wamekuwa wapokeaji wa uzinduzi wa Tuzo ya Amani ya Jumuiya ya Madola.

Maadui hawa wa zamani sasa wanasafiri bega kwa bega kujenga kile kilichovunjika, ushahidi hai kwamba mwaliko wa Mwokozi wa kuwa wapatanishi si tu unawezekana—bali pia una nguvu.

Tunapopata kuujua utukufu wa Mungu, ndipo, “hatutakuwa na nia ya kuumizana, bali kuishi kwa amani.” Katika mikusanyiko yetu na jumuiya, na tuchague kutazamana kama watoto wa Mungu.

Mpango wa Wiki Moja wa Mpatanishi

Kwa ufupi, ninatoa mwaliko. Upatanishi unahitaji tendo—tendo hilo laweza kuwa lipi, kwa kila mmoja wetu, kuanzia kesho? Je, unaweza kuzingatia mpango wa wiki moja, wenye hatua tatu wa mpatanishi?

  1. Nyumba isiyo na mabishano: Wakati mabishano yanapoanza, tulia na anza upya kwa maneno na matendo ya ukarimu.

  2. Kujenga maelewano mtandaoni: Kabla ya kuposti, kujibu, au kutoa maoni mtandaoni, uliza, Je hili litaleta maelewano? Ikiwa halileti, acha. Usitume. Badala yake, shiriki wema. Tangaza amani mahala pa chuki.

  3. Rekebisha na unganisha tena: Kila mwanafamilia angeweza kutafuta uhusiano uliovunjika ili kuomba msamaha, kuhudumu, kurekebisha, na kuunganisha.

Hitimisho

Imekuwa miezi kadhaa tangu nilipohisi msukumo usioepukika ulioongoza kwenye ujumbe huu: “Heri Wapatanishi.” Katika kuhitimisha, naomba nishiriki misukumo ambayo imekuja moyoni mwangu kwa kipindi hiki.

Upatanishi ni sifa kama ya Kristo. Wapatanishi nyakati zingine wanaitwa washamba au dhaifu—katika hali zote. Lakini bado, kuwa mpatanishi si kuwa dhaifu bali ni kuwa imara katika njia ambayo ulimwengu hauielewi. Upatanishi huitaji ujasiri na mwafaka lakini hauhitaji dhabihu ya kuvunja maadili. Upatanishi ni kuongoza kwa moyo mkunjufu, si kukataa mawazo mapya. Ni kufikiana kwa mikono iliyonyooshwa, si ngumi zilizokunjwa. Upatanishi si jambo jipya, la moto kutoka kwenye mashine. Lilifundishwa na Yesu Kristo Mwenyewe, kwa wale walio kwenye Biblia na Kitabu cha Mormoni. Upatanishi tangu hapo umefundsihwa na manabii wa siku za leo tangu siku za mwanzo za Urejesho hata hivi leo.

Tunatimiza jukumu letu la kiungu kama watoto wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo kadiri tunavyojitahidi kuwa wapatanishi. Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo, ambaye ni Mfalme wa Amani, Mwana wa Mungu aliye hai, katika jina la Yesu Kristo, amina.