Mkutano Mkuu
Nenda na Ukatende Vivyo Hivyo
Mkutano mkuu wa Oktoba 2025


10:28

Nenda na Ukatende Vivyo Hivyo

Ningependa kuangazia wale wamisionari waliopangiwa kazi ya kutoa huduma. Wao ni mifano kwetu.

Wakati Mwokozi alipokuwa akisafiri kupitia Bethsaida, baadhi ya watu walimleta mtu asiyeona Kwake. Pengine walikuwa wakitarajia kuona muujiza papo hapo. Mwokozi “alimchukua yule mtu asiyeona kwa kumshika mkono, na kumwongoza nje ya mji” ili kumponya kwa faragha. Mwanzoni, uponyaji ulionekana kuwa usio wa ufanisi sana. Yule mtu “akatazama juu, na akasema, ninaona watu kama miti ikitembea.” Yesu, kwa huruma, “aliweka mikono yake tena juu ya macho yake, na kumfanya aangalie juu.” Na kwa ule mguso wa ziada wa mikono ya Mwokozi, mtu yule asiyeona sasa “aliona … wazi kabisa.”

Huu ni mfano mmoja tu wa jinsi maisha ya Mwokozi yanavyofahamika kwa vitendo vya unyenyekevu vya huduma. Anatukumbusha kwamba Yeye “hakuja kutumikiwa, bali kutumikia” na kisha anatualika kufuata mfano Wake kwa kwenda maili ya ziada, tukitoa kwa wale wanaotuomba, na kuwapenda jirani zetu. Yeye alipoulizwa, “Na jirani yangu ni nani?” Kristo alishiriki mfano wa Msamaria mwema kwa wito wa “nenda, na ukatende vivyo hivyo.”

Wamisionari wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni mfano wa siku za sasa wa Msamaria mwema ambao Kristo anatualika sisi tuwe. Ningependa kuangazia wale wamisionari walio pangiwa kazi ya kutoa huduma. Wao ni mifano kwetu sisi wa jinsi huduma (1) inavyofungua mioyo kwa injili ya Yesu Kristo, (2) inavyoruhusu sisi sote kutumikia bila kujali hali zetu, na (3) inavyoleta nguvu ya Kristo ndani ya maisha yetu.

Kwanza, Huduma Inafungua Mioyo kwa Injili ya Yesu Kristo

Karibia mwaka wa 91 K.K, Amoni, Mmisionari wa Kitabu cha Mormoni, alijitambulisha mwenyewe kwa Mfalme Lamoni kwa kusema, “Ninatamani kuishi miongoni mwa watu hawa kwa muda; … [nami] nitakuwa mtumishi wako.” Kwa sababu ya huduma yake kwa mfalme, Amoni alipewa fursa ya “kuzungumza kwa ujasiri, …na kumwambia [Mfalme Lamoni] … kwa uwezo gani” yeye alitenda huduma yake. Katika majibu, mfalme aliahidi kwamba “lo lote [Amoni] atakalotaka … [mfalme ange]mpatia.” Ombi pekee la Amoni lilikuwa kwamba mfalme asikilize ujumbe wa injili ya Yesu Kristo. Matokeo ya huduma ya Amoni ilikuwa “maelfu ya roho [zililetwa] kwenye toba.”

Katika siku yetu, huduma inaendelea kuwaongoza wengine kwenye injili. Dada Bevan alikuwa anahudumu kama mmisionari wa kufundisha wakati alipoanza kupitia matatizo ya kiafya yaliyomhitaji yeye kurudi nyumbani kwa ajili ya matibabu. Badala ya kupumzishwa, yeye aliweza kuendelea kuhudumu kama mmisionari wa kutoa huduma akitokea nyumbani.

Wakati wakitembelea bustani, Dada Bevan pamoja na rafiki yake walishawishiwa kuzungumza na mama akiwa na watoto wadogo wanne, lakini walisita mpaka ile familia ikaondoka. Siku iliyofuata, walirudi kwenye ile bustani, wakisali kwamba familia hii ingekuwa pale. Kwa muujiza, mama yule alikuwa amekaa mahali pale pale kama siku ya jana. Wakati huu Dada Bevan na rafiki yake walimwendea yule mama, wakapata kumjua, na wakagundua kwamba alikuwa na haja ya msaada wa kimwili. Walitoa ule msaada na kisha wakamwalika kujifunza kuhusu injili.

Kwa sababu ya huduma hiyo na mwaliko, mama huyu na mtoto wake mkubwa walibatizwa, wakifuatiwa na mtoto aliyefuatia kwa ukubwa mwaka mmoja baadaye. Bado waumini hai hadi leo hii. Dada Bevan alijua uzoefu wake ulishawishiwa kiungu, na “ilithibitika [kwake] kwamba [yeye] alikuwa mahali pale pale Mungu alipohitaji [yeye] awepo.”

Kama Amoni na Dada Bevan, tunapo wahudumia wengine, sisi “tunaonyesha mfano mwema kwao” na wanatamani kujua “sababu ya tumaini lililoko ndani yetu [sisi].”

Yesu anatualika “nendeni, nanyi mkatende vivyo hivyo.”

Pili, Huduma Inaturuhu Kutumikia Bila Kujali Hali Zetu

Rais Russell M. Nelson alitoa wito juu ya “kila mvulana mwenye kustahili, anayeweza ili kujiandaa kwa ajili ya na kuhudumu misheni” na kwa kila msichana anayeweza “kusali ili kujua kama Bwana angependa [yeye] ahudumu misheni.” Aliahidi kwamba “uamuzi wako wa kuhudumu misheni, iwe ya kufundisha au misioni ya kutoa huduma, utakubariki wewe na wengine wengi.” Misheni za kutoa huduma zimebadilisha maana ya neno weza. Sasa kila mvulana mwenye kustahili na msichana anayetamani kuhudumu kama mmisionari kwa ajili ya Bwana anaweza kufanya hivyo, isipokuwa wachache sana.

Mze Holgado ni mfano wa kuwa na uwezo wa kuhudumu bila ya kujali hali binafsi. Yeye alizaliwa na maradhi ya kurithi yasiyo ya kawaida, ambayo yalimtenga na kuhudumu kama mmisionari wa kufundisha. Mzee Holgado aliitwa kama mmisionari wa kutoa huduma na alijitolea kufanya kazi katika ghala ya askofu, mahali ambapo aliwasaidia wengine kupata msaada walio hitaji. Yeye alipanga safu, aliweka mboga katika maboksi, na kuvunja maboksi ya kadibodi.

Mzee Holgado alipokuwa akizungumza katika mkutano wa sakramenti baada ya misheni yake, alishiriki kwamba “Mungu anahitaji wamisionari wa kutoa huduma. Anahitaji watu wa kuwapenda na kuwahudumia wengine. Watu hawa hupanga karatasi za maliwato, kupakia brokoli kwenye mifuko, kujenga samani, na ni watu walio wema kwa watu.”

Huhitaji kupangiwa kazi ya kuhudumu au kuvaa tagi ya jina ili kufanya yaliyo mema. Kila tendo la huduma hutambuliwa na Mwokozi. Sisi sote tunaweza kuwasaidia wengine kuja kwa Kristo kwa kuhudumu kwa upendo wa ukarimu. Sisi sote tunaweza kutumikia katika jina la Kristo kwa yule mmoja kupitia uweza wa Roho Mtakatifu na kuishi kama mifano ya imani katika Yesu Kristo. Huduma inaturuhusu sisi kujiwasilisha wenyewe kama dhabihu inayo ishi ambayo inakubalika kwa Mungu.

Yesu anatualika “nendeni, nanyi mkatende vivyo hivyo.”

Tatu, Huduma Huleta Nguvu za Kristo Ndani ya Maisha Yetu

Mmisionari kijana aliyepewa uhamisho kutoka jukumu la kufundisha kuwa jukumu la kutoa huduma alipambana na baadhi ya changamoto binafsi ambazo zilimwacha akihitaji nguvu ya Kristo ya uponyaji. Huduma iliyowekwa wakfu ilileta nguvu hiyo ndani ya maisha yake. Yeye alisema, “Nilihisi kwamba wakati nilipokuwa nikipambana, niliweza kumhisi Kristo akininyanyua juu. Kuna kitu fulani maalumu kuhusu kumwona Yeye akiwabariki watu kupitia stoo ya chakula, ndani ya hekalu, na kupitia injili Yake.”

Mzee huyu alianza kuhisi shangwe ya kina, na hamasa mpya aliyoigundua ilimbariki yeye na familia yake yote. Roho aliingia ndani ya nyumba yao kwa wingi sana, walihudhuria hekaluni pamoja zaidi mara kwa mara, na Kristo akawa fokasi kuu katika familia yao. Mmisionari huyu anaamini kwamba Kristo aliokoa maisha yake na aliibariki familia yake kupitia huduma.

Rais Nelson alifundisha, “Utayari wa kuhudumu na kuwaimarisha wengine vinasimama kama ishara ya utayari wa mtu kuponywa” kwa nguvu za Mwokozi zenye kukomboa.

Yesu anatualika sisi “nendeni, nanyi mkatende vivyo hivyo.”

Wamisionari wa Kutoa Huduma ni Mifano ya Wanafaunzi wa Yesu Kristo Walio Wekwa Wakfu.

Wakati wewe au mshiriki wa familia anapobarikiwa kupata wito kama mmisionari wa kutoa huduma, huo ni wakati wa kushangilia. Familia yako sasa itakuwa na mwakilishi wa Bwana Yesu Kristo aliyesimikwa akiishi ndani ya nyumba Yenu. Hiyo itawabadilisha ninyi nyote kuwa wema. Hakupaswi kuwa na kubeza katika wito wo wote wa kuhudumu. Tunaimba, “Nitakwenda utakako” na “Nitakuwa utakacho.” Hii ni fursa ya kuonyesha kwa hakika tunamaanisha kile tunachosema!

Kwenu ninyi nyote mnaohudumu, na mahususi kwa wamisionari vijana 4,000 mnaotoa huduma, sisi tunawapenda! Kama wamisionari wa kufundisha ni vinywa vya Bwana, basi ninyi wamisionari wa kutoa huduma ni mikono ya Bwana, na siyo wamisionari wa daraja la pili. Kila mmoja wenu ni muhimu sana katika kukusanya Israeli. Rais Nelson alifundisha kwamba “wakati wo wote tunapofanya kitu cho chote ambacho kinamsaidia mtu yeyote … kufanya na kushika maagano yao na Mungu, tunasaidia kukusanya Israeli.”

Ninyi wamisionari wa kutoa huduma mnakusanya Israeli katika njia nyingi, na huduma yenu inabadilisha maisha. Mara nyingi wewe hujui mnufaika wa huduma yako ni nani, lakini Mungu anajua. Daima kumbuka kwamba “kadiri [umhudumiavyo] mmoja wa wadogo hawa, … [umemhudumuia Yeye].” Tunasikia sauti zenu mnapojitolea kwenye vituo vya huduma vya Kanisa; tunaona tabasamu zenu mnaposaidia katika vikundi vya jumuiya na tunahisi nuru yenu mnapohudumu katika mahekalu. Mnawalisha wenye njaa, mnawavisha walio uchi, na mnawapa kinywaji wenye kiu.

Sisi sote tunahitaji kwenda, na kutenda vivyo hivyo.

Huduma ni Damu ya Uhai wa Wanafunzi wa Kristo.

Huduma inayo nguvu ya kufungua mioyo kwa ajili ya injili na inaturuhusu sisi sote kutoa nafsi yetu yote kwa Kristo. Huibadilisha mioyo yetu ili iwe kama Yeye, na katika mchakato, tunawainua wengine. Rais Nelson wakati mmoja alisema, “Katika ulimwengu huu uliopigwa kwa uozo wa kiroho, je, inawezekana watu … wakafanya tofauti?” Jibu lake: “Ndiyo! … ‘Watu wa agano wa Mungu, … waliovikwa silaha … na nguvu za Mungu katika utukufu mkuu’ … wanaweza kuinua maisha ya wanadamu wote.” Kupitia huduma tunabadilisha mioyo—na huu ulimwengu.

Kristo “alizunguka huko na huko akitenda wema.” Aliwatumikia wagonjwa, alirejesha uoni kwa vipofu, na kuwatembelea walio kataliwa. Alipika vyakula, alisaidia katika sherehe za harusi, na akawalisha maelfu wenye njaa. Tunapohudumu katika jina la Kristo kwa yule mmoja, tunazidi kuwa watakatifu na wenye kustahili zawadi ya uzima wa milele. Yesu Kristo yu hai. Yeye ni Mwokozi wangu na wako. Yeye ni Mkombozi wetu. Yeye ni mfano wetu mkuu wa utumishi. Ninakualikeni kila mmoja wetu twende, na tutende vivyo hivyo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Marko 8:22-26.

  2. Mathayo 20:28.

  3. Ona Mathayo 5:41.

  4. Ona Mathayo 5:42.

  5. Ona Mathayo 22:39.

  6. Ona Luka 10:29–37.

  7. Kwa taarifa juu ya wamisionari vijana na jinsi ya kutuma maombi ya kuhudumu, tafadhali tembelea ChurchofJesusChrist.org/service-missionary.

  8. Alma 17:23, 25.

  9. Ona Alma 17:31–39; 18:9–10, 20.

  10. Alma 18:21.

  11. Ona Alma 18:22.

  12. Alma 26:22.

  13. Dada Bevan alihudumu misheni ya kufundisha katika Misioni ya Florida Tampa na misheni ya kutoa huduma katika Misioni ya Orem Utah.

  14. Mahojiano binafsi na Janae Bevan yalifanyika Juni 10, 2025. Hadithi na nukuu zimetumiwa kwa ruhusa.

  15. Alma 17:11.

  16. 1 Petro 3:15.

  17. Russell M. Nelson, “Kuhubiri Injili ya Amani,” Liahona, Mei 2022, 6.

  18. Nina shukrani kwa Dada Amy A. Wright, Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Watoto, ambaye amefundisha kanuni hii kwa upana.

  19. Rubinstein-Taybi syndrome.

  20. Usaili binafsi pamoja na Perla García, binti wa Ricardo García. Hadithi na nukuu zimetumiwa kwa ruhusa.

  21. Maelezo ya dhumuni la Mmisionari wa kutoa huduma “Kuwasaidia wengine kuja kwa Kristo kwa kuhudumu kwa ukarimu wa upendo kama ambavyo Mwokozi angefanya. Minister in His name to the one through the power of the Holy Ghost and live as an example of faith in Jesus Christ, repentance, covenant keeping with God, and enduring to the end” (Missionary Standards for Disciples of Jesus Christ—Service Missionaries, 1.0, Gospel Library).

  22. Ona Warumi 12:1

  23. Mahojiano binafsi na Jordan Fry yalifanyika Juni 12, 2025. Hadithi na nukuu zimetumiwa kwa ruhusa.

  24. Russell M. Nelson, “Yesu Kristo—Mponyaji Mkuu,” Liahona, Nov. 2005, 87.

  25. Mnamo Julai 2022, Dada Evanson na mimi tulikuwa tukihudumu kama viongozi wa Misioni ya Utah Orem. Pamoja na misioni nyingine tisa ulimwenguni, tulipewa heshima ya kushiriki katika mradi wa majaribio ambapo ilishirikisha wamisionari vijana wa kutoa huduma katika misioni yetu. Baada ya mkutano wetu wa kwanza, niliandika katika shajara yangu, “Usiku wa leo tulikuwa na mkutano wa kipekee. Tulikutana na wamisionari wapya 140 pamoja na wazazi wao. Ukumbi wa kanisa na ukumbi wa mazoezi ya viungo vilijaa kabisa, tulikuwa na mkutano ulio jawa na Roho, wenye nguvu wa kuwakaribisha wamisionari wa kutoa huduma ndani ya Misioni ya Utah Orem. Tulizidiwa na hisia za upendo tulio nao kwao. Wote wako tayari kuhudumu. Ilikuwa ni asubuhi nzuri. Hali za wamisionari hawa ni mtambuka kutoka wamisionari wa zamani wa kufundisha wanao jitazamia kupona kutokana na majeraha hadi wamisionari wasio ongea wakitumia viti mwendo. Baada ya mkutano ule, Dada Evanson aliniambia, “Sasa misioni yetu inaonekana imekamilika.

  26. Ona David A. Bednar, “Tumeitwa Kazini,” Liahona, Mei, 2017, 67–70.

  27. “Nitakwenda Utakako,” Nyimbo za Dini, no. 154.

  28. Ona Mathayo 23:11.

  29. Russell M. Nelson, “Acha Mungu Ashinde,” Liahona, Nov. 2020, 92–93.

  30. Mathayo 25:40

  31. Ona Matthayo 25:34–36.

  32. Ona Omni 1:26.

  33. Russell M. Nelson, “Personal Preparation for Temple Blessings,” Liahona, Julai 2001, 39.

  34. Matendo 10:38.

  35. Ona Marko 1:30–31.

  36. Ona Marko 8:22–26.

  37. Ona Luka 19:1–10.

  38. Ona Yohana 21:9.

  39. Ona Yohana 2:1–10.

  40. Ona Yohana 6:5–13.

  41. Ona Mathayo 25:34; Warumi 12:1.