Tangazo la Familia—Maneno kutoka kwa Mungu
Tangazo hili lina asili ya kiungu, hivyo lazima tulichukulie kwa unyenyekevu unaostahili maneno yanayotoka kwa Mungu.
Mkutano mkuu huu wa Oktoba 2025 unafanya kumbukizi ya miaka 30 ya tangazo la “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Kwa usanifu wa kiungu, tangazo hili, pamoja na maneno yake ya kiufunuo, lilitolewa ili “kudumisha na kuimarisha familia kama kitengo muhimu cha jamii.”
Kila mtu ni sehemu ya familia, iwe wewe ni mama, baba, binti, mwana, mjukuu, babu au bibi, shangazi, mjomba, kaka, dada au binamu. La muhimu zaidi, kila mmoja wetu ni, kama tangazo linavyoeleza, “mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni … [mwenye] asili na hatima ya kiungu.”
Wakati nilipoitwa kwenye utume huu mtakatifu mwaka 2015 nilishauriwa, “Tangazo hili sasa ni la kwako. Jina lako [akinyoshea kwa kidole kwenye maneno ‘Baraza la Mitume Kumi na Wawili’ katika kichwa cha habari] liko hapa. Lihisi na lifundishe kama wewe unalimiliki.”
Ninalipenda tangazo la familia. Nimelishuhudia kote ulimwenguni kutoka Afrika hadi Australia na kila mahali baina ya jukumu la familia katika mpango wa milele wa Mungu. Tangazo hili lina asili ya kiungu, hivyo lazima tulichukulie kwa unyenyekevu unaostahili maneno yanayotoka kwa Mungu.
Kumbukeni, akina kaka na akina dada, kama nilivyosema katika mkutano mkuu mmoja uliopita kutoka kwenye mimbari hii, “Maneno ni muhimu.”
Acha nikupeni baadhi ya chimbuko kuhusu tangazo hili kama ujumbe mkuu wa kile tunachoamini.
Mwaka 1994, mwaka mmoja kabla ya kuwasilishwa kwa tangazo, Akidi ya Mitume Kumi na Wawili walijadili jinsi ambavyo jamii na serikali zilivyokuwa zikijiondoa kutoka kwenye sheria za Mungu kwa ajili ya familia, ndoa na jinsia. “Lakini haya hayakuwa mwisho wa yale tuliyoyaona,” Rais Nelson baadaye alielezea. “Tuliweza kuona juhudi za jamii tofauti kuondoa viwango vyote na vizuizi kwenye shughuli ya kujamiiana. Tuliona mkanganyiko wa jinsia. Tuliweza kuona yote yakija.”
Wale Kumi na Wawili waliazimia kutayarisha waraka, tangazo rasmi, likitoa muhtasari wa msimamo wa Kanisa juu ya familia. Katika mwaka huo, Mitume hawa, waonaji walioitwa na Mungu, walitayarisha tamko kuhusu familia. Rais Dallin H. Oaks alikumbuka kwamba kwa sala walimgeukia Bwana kwa ajili ya “kile [wao] walichopaswa kusema na jinsi [wao] walivyopaswa kusema.” Waliuwasilisha kwa Urais wa Kwanza—Marais Howard W. Hunter, Gordon B. Hinckley na Thomas S. Monson kwa ajili ya mawazo yao.
Miezi michache tu baadaye mnamo Machi 1995, Rais Hunter alifariki na Rais Hinckley akawa Rais wa 15 wa Kanisa. Tangazo hilo likawa sasa katika mikono yake. Lini ingekuwa wakati sahihi kufanya tamko hili kwa Kanisa? Muda huo ulifika miezi sita baadaye.
Siku kadhaa kabla ya mkutano mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Septemba 23 ambao ulitangulia mkutano mkuu, Rais Hinckley na washauri wake walikutana katika kushauriana na Urais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi. Akina dada hawa, kama wale Mitume, wamekuwa wakizidiwa na uzito wa mashaka kuhusu wanawake na familia. Walikuwa wamefokasi kwenye mkutano unaokuja juu ya familia.
Rais Hinckley alikuwa amepangiwa kuhutubia wanawake hawa kwenye mkusanyiko huo. Yeye amekuwa akitafakari mwelekeo wa mahubiri yake. Mjadala huu ulivyoendelea, alitaja kwa jina tangazo hili lililoandaliwa hivi karibuni lakini bado halijatangazwa kwa umma “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Je, mkutano huu wa wanawake ulikuwa mazingira sahihi ya kufanya tamko la kimaamuzi kuhusu familia?
Rais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi Elaine Jack baadaye alielezea: “Sisi hatukujua Tangazo lile juu ya familia lilikuwa kitu gani kwa wakati ule. … [Sisi] tuliweza kulijua tu kwa kichwa cha habari, lakini tulihisi chochote juu ya familia … kingekuwa kitu chanya. … Nilijihisi chanya sana kwamba tulikuwa na washiriki wa Akidi ya Kumi na Wawili ambao walikuwa wakipokea ufunuo.”
Mkutano wa Muungano wa Usaidizi Jumamosi ile ulikuwa wa kihistoria. Rais Hinckley alitambulisha tangazo la familia kwa maneno haya muhimu: “Kwa maneno mengi ya ulaghai yanayochukuliwa kama ukweli, pamoja na udanganyifu mwingi kuhusiana na viwango na maadili, pamoja na vivutio vingi na vishawishi vya kuchukua pole pole uchafu wa ulimwengu, tumehisi kuonya na kuonya mapema … juu ya viwango, mafundisho na desturi zinazohusiana na familia ambazo manabii, waonaji,na wafunuzi wa Kanisa hili kwa kurudia rudia wameelezea kote katika historia yake.”
Kisha yeye akasoma lile tangazo kwa ukamilifu wake. Kama vile Bwana alivyosema, “Iwe ni kwa sauti yangu mwenyewe au kwa sauti ya watumishi wangu, yote ni sawa.”
Tangazo linaeleza, “Familia imeamriwa na Mungu.” Ninapenda uwazi wa maelezo hayo. Tangazo ni wito kwetu sisi kuishi duniani daima tukikumbuka uungu ulio ndani yetu na umilele ujao ulioko mbele yetu. Rais Nelson alifunza, “Wewe kiuhalisia ni mtoto wa Mungu. … Usifanye makosa kuhusu hili: Uwezekano wako ni wa kiungu. Kwa utafutaji wako kwa bidii, Mungu atakupatia taswira kidogo kidogo ya kile unachoweza kuwa.”
Lilipowasilishwa, tangazo hili halikufungamana na mitazamo ya wengi ulimwenguni. Siyo wakati huo. Siyo kwa sasa. Kuna wale ambao wanaona kasoro katika hili tangazo juu ya familia, ndoa na jinsia. Baadhi wanapendekeza Kanisa liliondoe, lifanye marejeo au hata kuliweka kando tangazo hili.
Tangazo hili juu ya familia ni, kama Rais Hinckley alivyoeleza, ni mafundisho, wapendwa kaka zangu na dada zangu. Kanuni hizi haziko nje ya hatua bali kikamilifu ndani ya hatua pamoja na njia za Bwana na njia Yake ya agano. Mafundisho ya tangazo hili yalifunuliwa na Bwana wetu Yesu Kristo kwa Mitume Wake wakati huo na sasa. Hili ni Kanisa Lake, Yeye ndiye aliyeweka ukweli ambao kwa ukweli huu sisi tunaishi.
Baadhi yenu mnaweza kuangalia tangazo na kusema, “Hii haifanyi kazi kwangu.” “Inaonekana haina maana.” “Familia yangu haionekani hivyo.” “Hainihusu.”
Kwa wale wenye mashaka, jueni kwamba wewe ni mtoto wa wazazi wa mbinguni, ni sehemu ya familia ya Baba wa Mbinguni. Hakuna mtu anayekujua vizuri zaidi au anayejali kwa kina zaidi kuhusu wewe kuliko Yeye anavyokujali. Mgeukie Yeye, mimina moyo wako Kwake, mtumainie Yeye na ahadi Zake. Unayo familia katika Mwokozi wako Yesu Kristo, ambaye anakupenda. Yeye alikuja duniani kulipia dhambi zetu na kubeba mzigo wa makosa yetu na zile siku mbaya sana. Yeye anaelewa kile unachokabiliana nacho na unavyohisi. Mgeukie Yeye, mtumainie Yeye atamtuma Roho Mtakatifu kuwa pamoja nawe, kukuinua na kukuongoza. Hisi upendo Wao ambao “umejimimina wenyewe katika mioyo ya watoto wa watu; … ni wa kupendeza zaidi ya vitu vyote … na inafurahisha zaidi kwa shangwe.”
Mitume wote wa Bwana wanakupenda sana. Tunasali kwa ajili yenu na tunaomba mwongozo wa Bwana kwa ajili yenu. Kaeni pamoja nasi. Mnaishi katika nyakati zenye changamoto ambapo yule adui anatafuta kuwafanya ninyi muwe wake. Msichotwe. Na kama umechotwa, rudi. Mikono yetu imenyoshwa kwako kama inavyofanya ile ya wengine wanao kupenda.
Tangazo linasema, “Wazazi wana jukumu takatifu la kuwalea watoto wao kwa upendo na kwa uadilifu.” Kitabu cha Mormoni kinatoa ushahidi wa pili kwenye ukweli huu. Katika aya ya kwanza ya mlango wa kwanza, tunasoma, “Mimi, Nefi, nikiwa nimezaliwa na wazazi wema.” Je, ni wangapi kati yetu tumeanza Kitabu cha Mormoni—na kuanza tena na tena—na katika mchakato huo tunaweka maneno yale katika kumbukumbu? Kuyatia moyoni.
Moja ya kauli yangu pendwa katika tangazo ni hii “Furaha katika maisha ya familia itapatikana kwa urahisi ikiwa imejegwa katika mafundisho ya … Yesu Kristo.”
Je, ni nani hapendi kuwa na furaha?
Na mafundisho ya Yesu Kristo ni nini? Tena, katika tangazo hili: “Imani, sala, toba, msamaha, heshima, upendo, huruma, kazi na shughuli nzuri za burudani.”
Je, ni maisha ya nani hayatakuwa bora zaidi kwa kutumia kanuni hizi muhimu? Hakuna ye yote kati yetu atakaye fanya kikamilifu; lakini tunaweza kufuata maneno ya hekima ya Rais Hinckley, “Fanya vizuri uwezavyo.”
Tunasoma katika tangazo, “Akina baba wataongoza … kwa upendo na haki,” na “akina mama kimsingi wanawajibika kuwalea watoto wao.” Kuongoza hakumaanisha kukandamiza na kulea hakumaanishi nafasi ya upili. Mungu amewapatia wanaume na wanawake nafasi tofauti lakini zilizo sawa ambazo zinakamilishana.
Acha nishiriki hadithi binafsi.
Mimi na mke wangu tulijifunza kufanya vyema zaidi katika kuwa wenza walio sawa baada ya siku moja mimi kuamua kufanya uamuzi muhimu pasipo kushauriana naye. Kitendo changu kilimshangaza, kilimshitukiza, na kumweka katika hali ngumu sana. Baadaye, aliweka mikono yake mabegani mwangu na kwa uthabiti alisema, “Ron, tafadhali, kamwe usinifanyie hivyo tena.” Tangu hapo tumekuwa vizuri sana kwenye ukurasa mmoja.
Tunapata katika tangazo la familia, “Akina baba na akina mama wanao wajibu wa kusaidiana kama wenza walio sawa.”
Sawa ni neno muhimu. Kwa miaka mingi, mimi na Dada Rasband tumefanya kazi pamoja katika kile tangazo linaelezea kama “majukumu yetu matakatifu,”. tumetengeneza ndoa iliyofungwa nira sawa. Kwa kuwa kila mmoja wa watoto wetu ameoa au kuolewa, Dada Rasband na mimi tumeendelea kuwashauri wao na wenza wao jinsi ya kuwa wenza walio sawa.
Tunapoishi angali macho yetu yakiwa kwenye utukufu wa Mungu, tunaheshimiana na kusaidiana. Mipangilio hii ya kiungu ya haki hutuongoza kwenye uimara wa maisha yetu binafsi, familia zetu na katika jamii.
Baba yetu wa mbinguni ametoa tangazo hili juu ya familia ili kusaidia kutuongoza sisi nyumbani Kwake ili kutusaidia kujifunza na kujawa na upendo, nguvu, dhumuni na uelewa wa milele. Kwa nafsi yangu yote, ninakusihi kuishi karibu na Yeye na Mwanawe Mpendwa. Ninakuahidi unapofanya hivi, Roho atakushawishi na kukuongoza na kukusaidia kuhisi moyoni mwako amani yao iliyoahidiwa ambayo “inapita uelewa wote.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.