Jina Ambalo Ninyi Mnaitwa
Inamaanisha nini kuitwa kwa jina la Kristo?
Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba kama Bwana angezungumza nasi moja kwa moja, kitu cha kwanza ambacho angehakikisha tunaelewa ni utambulisho wetu wa kweli: sisi ni watoto wa Mungu, watoto wa agano, na wanafunzi wa Yesu Kristo. Jina jingine lolote hatimaye litatuangusha.
Nimelijua hili wakati mwanangu mkubwa alipopata simu yake ya kwanza ya mkononi. Kwa shauku kubwa, alianza kuingiza majina ya familia yake na marafiki kwenye orodha ya mawasiliano yake. Siku moja, niliona kuwa mama yake alikuwa akipiga simu. Kwenye skrini kulionekana jina la “Mama.” Huo ulikuwa uchaguzi wa busara na adhimu—na, nitakiri, ni ishara ya heshima kwa mzazi bora katika nyumba yetu. Kiuhalisia, nilikuwa na hamu ya kujua. Je, mimi alinipa jina gani?
Nilitafuta kwenye orodha ya mawasiliano yake, nikidhania kwamba kama Wendi alikuwa “Mama,” lazima nitakuwa “Baba.” Sikuwepo. Nilipekua “Dad.” Bado halipo. Hamu yangu ya kujua iligeuka kuwa mashaka kiasi. “Je, ananiita ‘Corey’?” Hapana. Katika jitihada yangu ya mwisho, nilifikiri, “Sisi ni wacheza soka—pengine ananiita ‘Pelé.’” Matamanio ya kufikirika. Mwisho, nilipiga namba yake mimi mwenyewe, na maneno mawili yakatokea kwenye skrini yake: “Siyo Mama”!
Akina kaka na akina dada, ni kwa jina gani ninyi mnaitwa?
Yesu aliwaita wafuasi Wake kwa majina mengi: Wanafunzi. Wana na mabinti. Watoto wa manabii. Kondoo. Marafiki. Nuru ya Ulimwengu. Watakatifu. Kila moja ya majina haya linabeba umuhimu wa milele na linasisitiza uhusiano binafsi na Mwokozi.
Lakini miongoni mwa majina haya moja linainuka juu zaidi ya mengine—na hilo ni jina la Kristo. Kwenye Kitabu cha Mormoni, kwa nguvu Mfalme Benjamini alifundisha:
“Hakuna jina lingine ambalo kwalo huleta wokovu; kwa hivyo, ningependa mjivike juu yenu jina la Kristo. …
“Na itakuwa kwamba ye yote atakayefanya hivi atakuwa katika mkono wa kulia wa Mungu, kwani atajua jina ambalo anaitwa; kwani ataitwa kwa jina la Kristo.”
Wale wanao jichukulia juu yao wenyewe jina la Kristo wanakuwa wanafunzi na mashahidi Wake. Katika kitabu cha Matendo, tunasoma kwamba baada ya Ufufuko wa Yesu Kristo, mashahidi walio chaguliwa na Mungu waliamriwa kuhubiri na kushuhudia kwamba ye yote atakaye amini katika Yesu Kristo, kubatizwa, na kumpokea Roho Mtakatifu atapokea ondoleo la dhambi. Wale walio pokea ibada hizi takatifu walikusanyika pamoja na Kanisa, wakawa wanafunzi, na waliitwa Wakristo. Kitabu cha Mormoni pia kinawaelezea waumini wa Kristo kama Wakristo na watu wa maagano kama “watoto wa Kristo, wana, na mabinti zake.”
Inamaanisha nini kuitwa kwa jina la Kristo? Inamaanisha kufanya na kushika maagano, daima kumkumbuka Yeye, kushika amri Zake, na kuwa “tayari … kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika mambo yote.” Inamaanisha kusimama pamoja na manabii na mitume wanapopeleka ujumbe wa Kristo kote ulimwenguni—pamoja na mafundisho yake, maagano, na ibada zake. Pia inamaanisha kuwahudumia wengine ili kusaidia kupunguza mateso na kuwa nuru na kuleta tumaini katika Kristo kwa watu wote. Kama ilivyo, huu ni mchakato wa maisha yote. Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba “tunafikiria kwamba hiki ni kituo ambacho hakuna mwanadamu aliye wahi kufika kwa mara moja.”
Kwa sababu safari ya uanafunzi inachukua muda na juhudi iliyojengwa “mstari juu ya mstari kanuni juu ya kanuni,” ni rahisi kumezwa kwenye majina ambayo ulimwengu hutupatia. Haya yana thamani ya muda tu na hayatatosheleza kama yalivyo. Ukombozi na mambo ya milele “huja tu katika na kupitia kwa Masihi Mtakatifu.” Kwa hiyo, kufuata ushauri wa kinabii wa kufanya uanafunzi kuwa kipaumbele hufaa na ni busara, hususani katika zama za sauti za ushindani na ushawishi. Hili lilikuwa kiini cha ushauri wa Mfalme Benjamini aliposema, “Ningetaka kwamba mkumbuke kudumisha jina [la Kristo] liandikwe daima katika mioyo yenu, … kwamba msikie na kujua sauti ambayo ninyi mtaitwa, na pia, jina ambalo yeye atawaita.”
Nimeliona hili katika familia yangu mwenyewe. Martin Gassner Babu wa baba yangu alibadilika milele kwa sababu ya rais wa tawi mnyenyekevu alipojibu wito wa Mwokozi. Huko Ujerumani katika mwaka 1909, nyakati zilikuwa ngumu, na fedha ilipatikana kwa shida sana. Martin alifanya kazi kama mhunzi katika kiwanda cha kutengeneza mabomba. Kwa ridhaa yake mwenyewe, siku nyingi za malipo ziliishia kwenye kulewa, kuvuta sigara na kulipia vileo baa. Mke wake mwishowe alimuonya kwamba kama hatabadilika, yeye angeondoka.
Siku moja, Martin akielekea baa alikutana na mfanyakazi mwenzake akiwa na kipeperushi cha kidini kilichokunjwa mkononi. Alikuwa amekiokota mtaani na alimwambia Martin kwamba alihisi kitu tofauti baada ya kukisoma kipeperushi hicho chenye jina Was wissen Sie von den Mormonen?, au Je, unajua nini kuhusu Wamormoni? Nina uhakika jina hilo limebadilishwa
Kulikuwa na anuani iliyoandikwa nyuma yake, kiasi cha kutosha tu kuelezea mahali kanisa lilipokuwa. Umbali wa kanisa lilipo ni mrefu kidogo, lakini waliguswa na kile walichosoma na wakaamua kupanda treni Jumapili ile ili kuchunguza. Walipofika, aliona kwamba anuani ile haikuwa ya kanisa walilotegemea, lakini ni nyumba ya kuhifadhi maiti. Martin alisita—kwa sababu kwa kweli, kanisa ndani ya nyumba ya kuhifadhi maiti ilionekana kama ni kitu kisichowezekana.
Lakini ghorofani kwenye ukumbi wa kukodi, walikuta kikundi kidogo cha Watakatifu wamekusanyika. Mwanaume mmoja aliwaalika kwenye mkutano wa kutoa ushuhuda. Martin aliguswa na Roho na alivutiwa sana na wepesi na shuhuda hizo za dhati kwamba naye akatoa ushuhuda wake. Na ilikuwa hapo, pale mahali pasipo kuwa pa kawaida, kwamba alisema tayari alikuwa amejua lazima ni kweli.
Baada ya hapo, mtu alijitambulisha kama rais wa tawi na kuuliza kama wangerudi tena. Martin alilelezea kwamba alikuwa akiishi mbali na hakuweza kumudu gharama za usafiri za kila wiki. Rais wa tawi kwa urahisi alimwambia, “Nifuate.”
Walitembea mitaa michache kuelekea kiwanda kilichoko jirani mahali ambapo rafiki wa rais wa tawi alikuwa akifanya kazi. Baada ya maongezi mafupi, Martin na rafiki yake wakapata ajira. Kisha, rais yule wa tawi akawaongoza kwenye nyumba za makazi za kupanga na akapata nyumba kwa ajili ya familia zao.
Haya yote yalitokea ndani ya saa mbili. Martin na familia yake walihamia wiki iliyofuata. Miezi sita baadaye walibatizwa. Mwanaume ambaye awali alitambulika kama mlevi asiye na matumaini alikuja kuwa mwenye ari kwenye imani yake mpya kwamba watu wa mji walianza kumuita, pengine siyo kwa mapenzi sana, “kuhani.”
Kuhusu jina la rais wa tawi, siwezi kuwambieni jina lake—utambulisho wake umepotea kitambo. Lakini mimi ninamuita mwanafunzi, balozi, Mkristo, Msamaria mwema, na rafiki. Ushawishi wake bado unasikika miaka 116 baadaye, na mimi nasimama mabegani mwa uanafunzi wake.
Kuna usemi kwamba unaweza kuhesabu mbegu ndani ya tufaha, lakini huwezi kuhesabu matufaha yanayotokana na ile mbegu moja. Mbegu iliyopandwa na rais wa tawi imezaa matunda yasiyo na idadi. Asingeweza kujua kwamba miaka 48 baadaye, vizazi kadhaa vya familia ya Martin pande zote za pazia wangeunganishwa katika Hekalu la Bern Uswizi.
Pengine mahubiri makuu zaidi ni yale ambayo hatutawahi kuyasikia lakini yale tunayoona katika ukimya, matendo yasiyo jitanguliza na kazi tunazo ziangalia katika maisha ya watu wa kawaida ambao, wanajaribu kuwa kama Yesu, wakizunguka huku na huko wakitenda mema. Kile alichofanya rais huyu wa tawi mkarimu hakikuwa sehemu ya orodha ya mambo yake ya kufanya. Alikuwa tu akiishi injili kama inavyoelezwa katika kitabu cha Alma: “Hawakuwafukuza … wale walio kuwa na njaa, au wale walio kuwa na kiu, au wale waliokuwa wagonjwa, … walikuwa wakarimu kwa wote, wazee na vijana, … wanaume na wanawake.” Na, hoja tusiyo paswa kuipuuzia, hawakumfukuza ye yote “iwe wa nje ya kanisa au ndani ya kanisa.”
Wale wanao jichukulia juu yao wenyewe jina la Kristo wanatambua, kama Joseph Smith alivyosema “mtu aliyejaa upendo wa Mungu, hatosheki na baraka za familia yake pekee, bali huenda ulimwenguni kote, akijitahidi kubariki jamii yote ya binadamu.”
Hivi ndivyo Yesu alivyoishi. Ukweli ni kwamba, Yeye alifanya mengi sana kiasi kwamba wanafunzi Wake hawakuweza kuandika yote. Mtume Yohana aliandika: “Kuna na mambo mengi ambayo aliyafanya Yesu, ambayo, yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.”
Acheni tujitahidi kufuata mfano wa Kristo, tukitenda mema na tukifanya uanafunzi kipaumbele cha maisha yote ili kwamba kila wakati tunapo zungumza na wengine, waweze kuhisi upendo wa Mungu na nguvu za uthibitisho za Roho Mtakatifu. Ndipo tunaweza kuungana na babu wa baba yangu na mamilioni ya wanaume na wanawake wengine ambao wametamka, kama mwanafunzi Andrea, “Tumemwona Masihi.”
Hatimaye, utambulisho wetu haubainishwi na ulimwengu. Lakini uanafunzi wetu unabainishwa kwa ibada tunazopokea, maagano tunayoshika, na upendo tunaoonyesha kwa Mungu na jirani kwa kutenda tu mema. Kama Rais Nelson alivyofundisha, sisi sote ni watoto wa Mungu, watoto wa agano, wanafunzi wa Yesu Kristo.
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo yu hai na amesha tukomboa. Yeye ndiye Yule aliyesema, “Nimekuiteni kwa … jina; ninyi ni wangu.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.