Injili ya Yesu Kristo: Sauti ya Kushangilia
Injili ya urejesho huleta dhumuni na shangwe kwako katika safari yako kuelekea uzima wa milele.
Nuru ya Tumaini, na Simon Dewey
Wakati nikihudumu kama kiongozi wa misheni huko Japan miaka kadhaa iliyopita, nilifanya usaili na mtu mmoja ambaye alikuwa amejiunga na Kanisa mwaka mmoja kabla na alikuwa akitafuta kupokea kibali cha hekaluni.
Wakati wa mazungumzo yetu, muumini huyu mpya alielezea jinsi alivyokuwa na shukrani kwa ajili ya baraka alizopokea katika mwaka tangu ubatizo wake. Kwangu mimi, alionyesha ujasiri wa agano unaotokana na uelewa wake wa injili, ambao ulikuwa umekita mizizi ndani yake. Alikuwa mwanafunzi mwongofu wa Yesu Kristo ambaye alipata mabadiliko makuu ya moyo (ona Mosia 5:2).
Kufuatia usaili huo, nilimwambia rais wa wilaya jinsi nilivyovutiwa sana kwamba wamisionari na waumini walikuwa wamempata, na kumlea kiroho, mtu bora kama huyu.
Nilishangazwa kujifunza kwamba wakati mtu huyu alipoanza kukutana na wamisionari na kuhudhuria kanisani, hakuwa na makazi na aliye katika hali zisizo na tumaini. Kujifunza injili kwa ndugu huyu na uongofu wake kwa kipindi cha miezi kadhaa kulipelekea mabadiliko yake ya kimiujiza, kumweka kwenye njia ya kujitegemea kiroho na kimwili na shangwe.
Injili ilimpa ndugu huyu picha iliyo wazi ya dhumuni la maisha yake. Kweli za wazi na za thamani za injili zilimletea majibu kwa maswali muhimu ya maisha ya duniani. Baraka kama hizo zipo sawa kwako na kwa watoto wote wa Mungu kupitia injili ya Yesu Kristo.
Dhumuni la Maisha
Injili ya Yesu Kristo imerejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith. Katika ushuhuda wake wa mwisho kwa Kanisa, Rais M. Russell Ballard (1928–2023), wakati huo–Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alisema:
“Sisi tunajua Mungu ni nani; tunajua Mwokozi ni nani kwa sababu tunaye Joseph. …
“… Tumebarikiwa kiasi gani kujua kile tunachojua kuhusu dhumuni letu katika maisha, kwa nini tuko hapa, kile tunachopaswa kujaribu kufanya na kutimiza katika maisha yetu ya kila siku.”
Kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ufahamu huo unajumuisha uelewa wa “mpango mkamilifu” wa Mungu wa wokovu, pia unajulikana kama “mpango mkuu wa furaha,” “mpango wa ukombozi,” na “mpango wa rehema” (Alma 42:8, 11, 15). Mpango wa Mungu huondoa dukuduku za maisha na shaka juu ya yajayo.” Muhimu na kitovu cha mpango huo na dhumuni la maisha ni “mafundisho ya Kristo.”
Kupitia injili, tunajua sisi ni watoto wa Mungu, tulioletwa duniani ili kujaribiwa na kutayarishwa kufufuka (ona Mafundisho na Maagano 76:39). Tunajua amri na tunafundishwa “kujua mema na maovu” (2 Nefi 2:5). Tunajua tuko hapa ili kupenda na kuhudumu na kwamba Mwokozi ametuita kuushinda ulimwengu na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo (ona Yohana 16:33).
Kile Joseph Smith alichokiita “sauti ya kushangilia ya Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo” kitatuimarisha wakati wa siku ngumu na kuleta maana na lengo kwetu sisi na wengine.
Utiifu na Baraka
Mungu ametupatia haki ya kujiamulia kimaadili ili kwamba tuweze kuwajibika kwa chaguzi zetu (ona Mafundisho na Maagano 101:78; ona pia 2 Nefi 2:16). Kama sehemu ya “upinzani katika vitu vyote” (2 Nefi 2:11), Shetani anaruhusiwa kutujaribu kutumia vibaya haki yetu ya kujiamulia.
Katika siku yetu, Bwana Yesu Kristo alimwita Nabii Joseph Smith “na alisema naye kutoka mbinguni, na akampa amri” (Mafundisho na Maagano 1:17). Bwana anaendelea kufunua amri Zake na mapenzi yake kwa manabii Wake leo kwa sababu Yeye anatamani kutuongoza kwenye furaha katika maisha haya na kwenye utukufu wa selestia katika maisha yajayo.
Mfalme Benjamini Anawahubiria Wanefi, na Gary L. Kapp
Kufundisha Mafundisho ya Kweli, na Michael Malm
Joseph Smith Akihubiri, na Sam Lawlor
Utiifu kwa amri za Mungu unapaswa kuja kutokana na kujitolea kwetu na upendo kwa ajili Yake. Bwana Yesu Kristo alitangaza, “Mkinipenda mtazishika amri zangu” (Yohana 14:15). Matokeo ya mwisho ya kuonyesha upendo wetu kwa Bwana kwa kutii amri Zake ni baraka ambazo huleta furaha na shangwe (ona Mafundisho na Maagano 130:20–21).
Kwa mtazamo ulio dhahiri juu ya asili na hatima yetu ya kiungu, tunajua kwamba “mambo yale yale yatakayofanya maisha [yetu] duniani kuwa bora inavyowezekana kuwa ndiyo mambo hayo hayo yanayoweza kufanya maisha [yetu] milele yote kuwa bora inavyowezekana kuwa!”
Shangwe katika Safari Yako
Mwongofu wa hivi karibuni mwenye furaha niliyekutana naye huko Japani miaka mingi iliyopita alipata injili ya urejesho ya Yesu Kristo kupitia bidii yake na ile ya wamisionari na waumini. Aligundua dhumuni lake na kupanua ono lake la mpango mkuu wa furaha, ambao ulimletea baraka na shangwe ambayo ilimwinua kimwili na kiroho.
Mzee Patrick Kearon wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili amefundisha:
“Kwa sababu ya mpango wa upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wa watoto Wake, na kwa sababu ya maisha ya ukombozi na misheni ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo, tunaweza—na tunapaswa—kuwa watu wenye shangwe zaidi duniani! Hata kama dhoruba za maisha katika ulimwengu wenye mashaka mara nyingi hutujia, tunaweza kujenga hisia inayokua na ya kudumu ya shangwe na amani ya ndani kwa sababu ya tumaini letu katika Kristo na uelewa wetu wa nafasi yetu wenyewe katika mpango mzuri wa furaha.”
Ninatoa shukrani zangu kwa ajili ya, na ushuhuda wa, injili ya urejesho ya Yesu Kristo na mpango mkuu wa furaha. Ninawaalika mpokee matunda ya injili na kuhisi furaha zaidi katika safari yenu kuelekea uzima wa milele.