Wakati Majaribu Yanapoonekana kuwa Makubwa Mno
Kuvunjika moyo ni sehemu ya maisha. Lakini kwa msaada, tunaweza kuyaona kupitia mtazamo wa Mungu.
Mlima Timpanogos ni mlima ulioko huko Utah, Marekani, ambao ni futi 11,000 (mita 3,353) juu ya usawa wa bahari na umejawa na msongamano wa maporomoko ya maji, kuta za miamba, majani na wanyamapori. Kusimama chini ya mlima kama huu kunaweza kukufanya ujihisi mdogo. Huwezi kukiona kilele au pande zake. Unaweza kuonekana mkubwa sana na usioweza kuondoleka.
Hata hivyo, safari ya dakika 10 kwa gari kutoka Mlima Timpanogos hukuruhusu kuuona tofauti. Kutoka kwenye mtazamo huu, unaweza kuona njia na barabara ambazo zimekatwa kupitia kwenye mlima huu. Hizi zinaonyesha kwamba watu wengine wamekuwepo hapa hapo awali na kwamba kuna njia salama hadi kileleni na kuuzunguka mlima huu.
Majaribu katika maisha yako hivi sasa yanaweza kuhisi vivyo hivyo. Kukabiliana na changamoto ngumu sana kunaweza kuhisi kama kutazama milimani na usiweze kuona kileleni au hata pande kuzunguka milima hiyo. Inaweza kuonekana mikubwa mno na labda haiwezekani kupita kufika upande wa pili. Majaribu hayo yanaweza hata kukufanya ujihisi mdogo, umechanganyikiwa, mwoga au mpweke.
Lakini hapa kuna kitu kingine cha kujaribu. Piga hatua nyuma na ujaribu kuona majaribu yako kwa mtazamo tofauti—mtazamo wa Mungu.
Kwa mtazamo huu, unaweza pia kutambua kwamba haujaachwa peke yako kutatua matatizo yako. Una Baba wa Mbinguni ambaye anakupenda na atakusaidia. Wengine, hususani Mwokozi, wamefanikiwa kupitia nyakati ngumu pia. Wanataka kukupa mwongozo unaouhitaji ili kushinda majaribu yako, hata yale makubwa sana.
Ni kwa Jinsi Gani Tunaweza Kubadili Mtazamo Wetu?
1 Fuata mpango wa Baba wa Mbinguni.
Yesu Kristo ndiye mfano wetu mkamilifu. Kanuni ambazo Yeye alifundisha ni rahisi, zenye nguvu na rahisi kueleweka. Je, hiyo inamaanisha kuwa daima ni rahisi kufuata? Hapana. Si mara zote. Lakini kila wakati tunapomfuata Yeye kwa imani, mtazamo wetu unaanza kubadilika. Tunaanza kuona changamoto kama fursa za kumfikia Mwokozi badala ya kuzitazama kama adhabu, mashimo au vizuizi vinavyotuweka mbali.
2 Mwombe Mungu akusaidie.
Mungu ni Baba yako wa Mbinguni. Yeye anakujua, anakupenda na yuko tayari kukusaidia wakati wowote unapoomba. Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba “mtazamo wa Bwana unapita hekima yenu ya duniani. Majibu Yake kwa sala zenu yanaweza kuwashangaza na yatawasaidia kufikiria selestia.”
Unaposali, Mungu anaweza kukusaidia uone mambo ambayo huwezi kuyaona kwa sasa. Yeye anaweza kukuongoza kupitia majaribu yako na hata kukupa amani na nguvu unapomfuata Yeye.
3Waombe wengine msaada.
Baba wa Mbinguni amewaweka watu wema katika maisha yako ambao wanaweza kukusaidia. Unapopambana na changamoto ambazo zinaonekana kuwa kubwa za kutisha mbele yako, fikiria kuzungumza na mwanafamilia anayeaminika, rafiki, kiongozi wa Kanisa au askofu wako.
Kumwomba mwenye ukuhani anayestahili kwa ajili ya baraka ya faraja na mwongozo ni njia nyingine nzuri ya kujiona mwenyewe na maisha kupitia mtazamo wa Mungu.
Kuona kwa Uwazi
Kama mlima mkubwa uliosimama katika njia yako, wakati mwingine majaribu yako yanaweza kuonekana kuwa makubwa sana. Lakini kadiri unavyoishi mpango wa Mungu na kumwacha Yeye na watu wengine wakusaidie, utaweza kuona changamoto zako kwa njia tofauti.
Unaweza kupiga hatua nyuma na kuona kwamba pale kuna njia ya kushinda majaribu yako. Yesu Kristo hutoa njia unayoweza kupita. Bila kujali ni majaribu makubwa kiasi gani yanayoweza kutokea, Mungu ni mwenye nguvu zaidi.