Mwangaza wa Jua katika Dhoruba Zangu
Baada ya bibi yangu kufariki, nilifikiria kuhusu kumaliza maisha yangu mwenyewe. Lakini kuutegemea mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni kulinisaidia niendelee.
Picha na Niel Kabiling
Mambo! Mimi ni Honey Grace. Nina umri wa miaka 17 tu. Ninaishi Iloilo, huko Ufilipino!
Kumpoteza Bibi Yangu
Hivi karibuni, nilipitia kitu kigumu sana. Baba na mama yangu wametengana, na mama yangu anafanya kazi nje ya nchi. Nilikua na bibi yangu—yeye ndiye aliyenitambulisha kwenye injili na Kanisa. Lakini mwaka huu, alifariki bila kutarajia.
Alikuwa mtu wa mwisho niliyewahi kufikiria kuwa angekufa. Wakati mwingine nilidhani ningekufa kabla yake kwa sababu alikuwa na afya nzuri sana! Kamwe hakuwahi kuonyesha udhaifu na daima alikuwa na nguvu mbele yangu. Sikuwahi kufikiria maisha yangu bila yeye.
Kuelewa Mpango
Baada ya kufariki, wakati mwingine nilitamani ningekufa pia. Nilikuwa na mawazo kuhusu kumaliza maisha yangu mwenyewe. Lakini punde nilienda kwenye shughuli ya vijana wa kigingi ambapo tulikuwa na somo kuhusu mpango wa wokovu.
Nilijua kuhusu mpango wa wokovu, lakini labda uelewa wangu juu yake ulikuwa kidogo umegubikwa na mawingu kwa sababu ya kile kilichomtokea bibi yangu. Nilipokuwa nikisikiliza, niliwaza, “nimesahau baraka za dhabihu ya Yesu Kristo kwa ajili yangu.”
Nilitambua kwamba Yesu Kristo alikufa ili kiniokoa mimi. Sipaswi kumaliza maisha yangu kwa sababu ya matatizo ninayokuwa nayo. Mpango wa furaha unanipa tumaini kwamba ninaweza kumwona bibi yangu tena siku moja, kwa sababu maisha hayaishii tunapokufa. Ninahitaji kuendelea kumfuata Mwokozi ili niweze kumwona tena.
Kupata Nguvu Hekaluni
Baada ya bibi yangu kufariki, binamu yangu alihamia kwangu na akawa mlezi wangu. Binamu zangu ni marafiki zangu wa dhati, lakini badiliko lilikuwa bado gumu sana. Ilinibidi nijifunze kufanya kazi zote ambazo bibi yangu alikuwa akifanya. Ilinibidi nijiamshe mwenyewe kwenda shuleni na kuitunza nyumba.
Askofu wangu daima alikuwa akizungumza kuhusu kujitegemea, hivyo basi nilifanya utafiti kuhusu hilo katika Gospel Library. Ilinisaidia kujifunza kusimama kwa miguu yangu miwili.
Mimi pia bado nina mawasiliano na baba yangu. Siku moja, tulikuwa na mabishano. Mabishano hayo kwa kweli yalinisumbua sana, lakini ghafla kulikuwa na nafasi ya vijana kwenda safari ya hekaluni. Nilipokuwa hekaluni, nilihisi amani. Sikufikiria kuhusu matatizo nyumbani. Sikufikiria kuhusu hasira niliyokuwa nayo kwa baba yangu. Nilifikiria juu ya mambo ambayo ningeweza kufanya ili kumsaidia yeye. Nilifikiria kuhusu kuwa mfano mzuri. Nilifikiria kuhusu mambo ya milele, kuhusu kuunganishwa na wazazi wangu hekaluni siku moja. Niliamua kusema samahani kwa baba yangu kwa kupigana naye.
Mwokozi pamoja na Watoto, na Michael Malm
Kumtegemea Mwokozi Wangu
Nimejifunza daima kufokasi juu ya Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni. Ninapata nguvu yangu kutoka Kwao, na ninakumbuka kwamba Wao wananilinda.
Kuelewa mpango wa wokovu, hasa Upatanisho wa Mwokozi, kulinisaidia kushinda mawazo yangu ya kujiua. Hunisaidia kuhisi amani katika kuishi. Hunipa matumaini kwamba ninaweza kukutana tena na bibi yangu upande mwingine wa pazia siku moja.
Yesu Kristo ndiye tumaini la kuendelea na maisha yangu ingawa nina changamoto nyingi. Upendo wake kwa ajili yangu kamwe hauishi. Yeye ni mwangaza wa jua katika maisha yangu. Kunapokuwa na dhoruba au mvua, Yeye yupo pale. Yeye ni Mwokozi wangu. Yeye ni nyumba yangu. Yeye ni maisha yangu. Yeye ananifanya niendelee. Yeye ni mojawapo ya sababu ninapenda kuishi.
Mwandishi anaishi Cagayan, Ufilipino