2025
Msaada na Mwongozo kwa ajili ya Wakati Wako Ujao
Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana ya Julai 2025


Msaada na Mwongozo kwa ajili ya Wakati Wako Ujao

Maisha hayafuati daima mipango yako, lakini kumtegemea Bwana kutabadilisha maisha yako kuwa bora.

mtu akiwa na alama za swali na nguzo ya alama

Wakati mwingine inaweza kuonekana kama ulimwengu umejaa mashaka. Unaweza kuwa unajiuliza ni nini kilichohifadhiwa kwa ajili ya siku zako zijazo. Nilihisi vivyo hivyo.

Mimi pamoja na wazazi wangu tulijiunga na Kanisa nilipokuwa na umri wa miaka 16. Wakati huo, nilikuwa mwenye aibu sana. Baada ya kujiunga na Kanisa, nilipata kujiamini. Nilijifunza kuhusu mimi ni nani, wapi ninatoka, kwa nini niko hapa na ninaenda wapi baada ya maisha haya.

Niligundua wakati huo kwamba hata kama sikujua kwa undani ni aina gani ya vitu ambavyo ningefanya katika maisha yangu, kulikuwa na msaada na mwongozo wa kuniongoza kwenye siku kubwa za usoni

Hilo pia ni kweli kwako wewe!

Mwongozo kutoka kwa Nabii

Nilikuwa na umri wa miaka 17 wakati nabii, Rais Spencer W. Kimball (1895–1985), alipotembelea Korea Kusini mwaka 1975. Nilimwona katika mkutano ambapo karibu vijana 400 wa Kikorea walikusanyika ili kusikia sauti yake.

Rais Kimball alishiriki jinsi alivyojifunza maandiko na kusali kila siku tangu alipokuwa mdogo. Alizungumza kuhusu umuhimu wa kuweka vipaumbele. Alisema tunapaswa kuhudhuria seminari, kujiandaa kwa ajili ya misheni na ndoa ya milele na kufanya kazi kuelekea wokovu. Pia alitoa ushuhuda wake.

Maneno ya nabii yaliangaza fikra zangu. Nilikuwa katika shule ya upili, lakini sikuwa napenda kufanya kazi za shule. Nilipenda michezo! Nilicheza soka wakati wowote nilipopata nafasi na mara nyingi nilicheza badala ya kujifunza. Sikuwa mwanafunzi mzuri. Baada ya kumsikiliza nabii, bado nilifurahia soka, lakini niliamua kuweka baadhi ya vipaumbele.

Ningefanya kadiri niwezavyo ili kujifunza. Ningehudumu misheni, kuunganishwa hekaluni, na kuwa na familia yenye furaha. Nilijua kwamba kama ningehitaji kuwa na kesho iliyo kuu sana, ningehitaji kumfuata nabii—bila kujali chochote.

Pamoja na fursa zote na changamoto zote utakazokabiliana nazo, utakuwa SAWA unapofuata mwongozo ambao manabii wanaoishi wanatoa.

Misheni Isiyo na Uhakika

Nilikuwa nimefanya ahadi ya kutumikia misheni, lakini pia kuna huduma ya lazima ya kijeshi nchini Korea Kusini. Baada ya shule ya upili, wavulana wengi waliingia jeshini, walitimiza huduma yao ya lazima, na mara moja wakatafuta elimu na kupata kazi. Ilikuwa vigumu kutoa miaka mingine miwili kwenye huduma ya umisionari. Kulikuwa na wazee wachache tu wa Kikorea wakati huo.

Nilipofika umri wa miaka 19, nilishika msimamo wangu na kujitayarisha na kutuma karatasi zangu za misheni. Niliitwa kuhudumu katika Misheni ya Korea Busan. Mwaka mmoja baadaye, niliandikishwa kuingia jeshini. Nilihuzunika sana kwamba ilinibidi kusitisha misheni yangu.

Nilipomaliza huduma yangu ya kijeshi miaka mitatu baadaye, nilihisi kwamba bado sijamaliza misheni yangu. Kila mtu aliniambia, “Wewe tayari umetumikia misheni. Bwana anaelewa hali yako, kwa hivyo kutumikia kwa mwaka mmoja tu ni SAWA.”

Nilimuuliza rafiki yangu mwema kutoka seminari kile ninachopaswa kufanya. Yeye alisema kwamba alijua ningetumikia mwaka mwingine wa misheni yangu. Uaminifu wake ulinipa ujasiri na uthibitisho wa kutumikia zaidi. Nilitumikia mwaka wa pili wa misheni yangu katika Misheni ya Korea Seoul. Wakati nilipomaliza, nilikuwa na umri wa miaka 25. Baadaye nilimuoa rafiki yule yule na tuliunganishwa katika Hekalu la Laie Hawaii.

Uzoefu huu ulinifundisha kwamba utakuwa sawa hata wakati mambo hayatokei jinsi ulivyoyasanifu. Wakati mipango na ono lako vinapoendana na mapenzi ya Bwana kwa ajili yako, Yeye atakusaidia katika maamuzi yako ya maisha.

Wakati Mkuu Ujao Unawezekana

Ingawa sikuwa na uhakika kama kijana ni aina gani ya maisha ningekuwa nayo, niligundua kwamba kuweka vitu vya kiroho kwanza ni ufunguo wa mafanikio—si tu katika maisha haya, bali pia katika maisha yajayo.

Ulipobatizwa, ulipokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Unapofokasi kwenye misukumo unayopokea, Roho Mtakatifu atakulinda na kukuongoza katika njia sahihi ya kwenda. Utahisi pia faraja na amani.

Unapojiandaa kwa ajili ya siku zako zijazo, kumbuka:

  • Kujifunza maandiko.

  • Kuendelea kusali.

  • Kumfuata nabii.

  • Siku zote umtegemee Bwana.

Nilipokuwa na umri wenu, nilijifunza kuhusu tabia na sifa za Mwokozi na jinsi ambavyo ningeweza kuwa zaidi kama Yeye. Yeye ni mkamilifu. Siwezi kikamilifu kuwa kama Yeye katika maisha haya, lakini ninajaribu kadiri niwezavyo, na nimekuwa bora katika kufanya hivyo.

Ninajua kwamba Yesu Kristo yu hai. Kwa sababu Yake, ninatumaini kubwa kwa ajili ya siku zijazo—na ninyi pia mnaweza!