Mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya Familia
Mafundisho, ibada, na maagano ya hekaluni hubariki familia zote za dunia.
Vielelezo na Shawna Tenney
Hivi karibuni, mimi na Dada Uchtdorf tulihudhuria ubatizo wa mmoja wa vitukuu wetu. Tulipo tazama vizazi vingi kwa furaha wakisherehekea tukio hili, tulihisi shukrani kubwa kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya mpango Wake wa wokovu kwa ajili ya watoto Wake. Tulihisi ni kwa kiasi gani tangu mwanzo familia na maagano matakatifu vimekuwa muhimu Kwake.
Umuhimu huo unaweza kuonekana katika hadithi ya Agano la Kale ya Yakobo mwaminifu, ambaye alisafiri safari ndefu na yenye kutumia nguvu nyingi ili kutafuta mke, kuoa katika agano, na kuanzisha familia. Jioni moja, Yakobo alisimama ili kupumzika usiku huo lakini akapata mawe tu kwa ajili ya mto wake wa kulalia. Lazima alikuwa amechoka sana, kwa sababu bado aliweza kulala—na kuota ndoto.
Yakobo aliona “ngazi imewekwa juu ya nchi, na kilele chake kilifika mbinguni: na tazama malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya ngazi hiyo.
“Na, tazama, Bwana alisimama juu yake, na alisema, Mimi ndimi Bwana Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka” (Mwanzo 28:12–13).
Bwana kisha alifanya baadhi ya ahadi muhimu za agano kwa Yakobo—ahadi ambazo yeye pia alikuwa amefanya na baba na babu wa Yakobo, Isaka na Ibrahimu, ikijumuisha:
-
Ahadi kwamba Yakobo angekuwa baba wa “umati wa watu” (Mwanzo 28:3, 14).
-
Nchi ya ahadi kwa ajili ya vizazi vya Yakobo (ona Mwanzo 28:4, 13).
-
Ahadi kwamba kupitia Yakobo na “uzao wake familia zote za dunia zitabarikiwa” (Mwanzo 28:14; msisitizo umeongezwa).
Tukio la Yakobo lilikuwa takatifu sana kwamba alisema, “Kweli Bwana yupo mahali hapa. … Bila shaka hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni” (Mwanzo 28:16–17). Na hivyo, Yakobo akaita jina la mahali pale Betheli, ambalo linamaanisha “nyumba ya Mungu” (ona Mwanzo 28:19, tanbihi a).
Mahekalu ni zaidi kama ile ngazi aliyoiona Yakobo. Mafundisho, ibada, na maagano ya nyumba ya Bwana huunganisha mbingu na dunia. Maagano yangeweza kulinganishwa na vidato vya ngazi ambavyo hutusogeza karibu na Bwana. Na kupitia huduma yetu katika mahekalu matakatifu, tunabariki “familia zote za dunia—zilizopita, zilizopo, na za baadaye.”
Mtazamo wa Furaha wa Mbinguni
Mzee Bruce C. Hafen, mshiriki mstaafu wa Sabini aliyebaki na heshima hiyo, wakati mmoja alipokea simu kutoka kwa mhariri wa gazeti la habari la kitaifa ili kuzungumzia kuhusu kitabu ambacho kilitafiti historia ya imani kuhusu mbinguni katika dini tofauti.
“Waandishi waligundua kwamba umma unahisi njaa iliyoenea kwa ajili ya mbingu—familia za mbinguni,” Mzee Hafen alisema. Lakini “makanisa mengi ya Kikristo hutoa jibu dogo kwa njaa hii ya ndani”—isipokuwa moja: Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Katika Kanisa lililorejeshwa la Mwokozi, tunayo mahekalu matakatifu. Tuna ndoa ya milele, na mamlaka ya kuunganisha ambayo hubariki zaidi ya kifo cha kimwili. Tuna ahadi ya siku za usoni za milele na wapendwa wetu katika uwepo wa Baba na Mwana. Kutokana na haya yote, waandishi walihitimisha kwamba wazo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kuhusu mbinguni ni kamili zaidi—na, ningeongeza, la furaha zaidi.
Kama Rais Russell M. Nelson alivyofundisha, “Bwana … aliumba dunia ili kwamba tuweze kupata miili na kuunda familia. Alianzisha Kanisa Lake ili kuinua familia. Yeye hutoa mahekalu ili kwamba familia ziweze kuwa pamoja milele.”
Kuilinda Familia
Haipaswi kutushangaza kwamba kitu muhimu sana kwenye mpango wa Mungu kingekabiliwa na upinzani. Rais M. Russell Ballard (1928–2023) alisema, “Shetani anajua kwamba njia ya uhakika na yenye ufanisi zaidi ya kuvuruga kazi ya Bwana ni kupunguza ufanisi wa familia na utakatifu wa nyumba.”
Kujua kile tunachojua, tunapaswa kuwa miongoni mwa watetezi wenye bidii zaidi ulimwenguni wa familia.
Jinsi gani tunafanya hili?
Tunaweza kufanya “vitu vidogo na rahisi” (Alma 37:6) ambavyo vinaimarisha uhusiano wa kifamilia. Hii inajumuisha kufuata kanuni zilizo wekwa kwenye muhtasari katika tangazo la familia: “Imani, sala, toba, msamaha, heshima, upendo, huruma, kazi na shughuli nzuri za burudani.” Bila kujali hali ya familia yako ya sasa, unaweza kuonyesha kwa matendo yako kwamba uhusiano wa kifamilia una umuhimu wa milele kwako.
Kwa kuishi, kutetea, na kushiriki kweli za milele kuhusu familia, tunaweza kuwasaidia wengine kuona kwamba “familia ni kitovu cha mpango wa Muumba kwa ajili ya majaliwa ya milele ya watoto Wake” na kwamba “mahekalu matakatifu yanawezesha watu binafsi kurudi katika uwepo wa Mungu na kwa familia kuunganishwa milele.”
Mteule, na Dan Wilson
Nipo pamoja Nawe.
Wakati Mimi na Dada Uchtdorf tunapowaangalia wanafamilia wetu wakifanya maagano matakatifu na Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo wa milele, mioyo yetu inajawa na furaha na shukrani. Tunafurahi sio tu kwa watoto wetu na watoto wao bali pia kwa wazazi wetu na wazazi wao. Tunatafakari kwa upendo mkubwa jinsi maagano ya injili yanavyotuunganisha katika vizazi vyote.
Baraka ambazo Bwana aliahidi kwa Ibrahimu, Isaka, na kwa Yakobo katika ndoto yake zina kila kitu kinachohusiana na familia. Na zinatolewa kwa watoto Wake wote wa agano—ikijumuisha wewe na mimi. “Tazama,” Bwana alisema, “Mimi nipo pamoja nawe, na nitakulinda kila uendapo, … kwa maana sitakuacha” (Mwanzo 28:15).
Ninaahidi kwamba unapofuata na kushiriki mpango wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya familia, Yeye atakuwa pamoja nawe, hasa wakati majaribu yanapokuja kwako au kwa wapendwa wako. Atakubeba, atakuinua juu, na kukuongoza kwenye utimilifu wa shangwe pamoja Naye, pamoja na Mwanawe Yesu Kristo, na pamoja na familia yako—milele.