Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana
Safari ya kwenda Hekaluni
Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana Machi 2026


Sauti za Vijana

Safari ya kwenda Hekaluni

msichana akiwa hekaluni

Kielelezo na Katelyn Budge

Kulikuwa na wakati ambapo sikuweza kutembelea hekalu kwa takribani miaka sita. Miaka hii ilikuwa nyakati za giza za maisha yangu kwa sababu pia nilimpoteza mama yangu katika kipindi hiki. Nilitaka kwenda hekaluni, lakini ilikuwa karibu saa moja kutoka nyumbani, na nilikuwa sina pesa kwa ajili ya usafiri na hakuna mtu wa kunichukua.

Kisha mwaka jana niliitwa kama rais wa darasa la Wasichana. Wakati kiongozi wangu wa Wasichana aliponiomba nisaidie kupanga shughuli kwa mwaka huo, nilimwambia jambo la kwanza tunalopaswa kufanya ni kwenda hekaluni kama darasa. Nilipotangaza hili kwa wasichana, walisisimka sana! Kwa wengi wao, ingekuwa mara yao ya kwanza kuhudhuria. Nilisali na kufunga sana tulipokuwa tunajiandaa kwa ajili ya safari. Sikutaka kitu chochote kiende vibaya.

Hekaluni, nilijisikia kupunguziwa kila mzigo. Niliahidi kutembelea hekalu mara kwa mara. Lilikuwa ni tukio zuri sana na baraka. Nilisisimka sana kwamba mimi na vijana wenzangu tulikuwa tukishiriki katika kazi kuu ya Baba yetu wa Mbinguni.

Ninajua kwamba hekalu ni nyumba takatifu ya Bwana, mahali ambapo ibada takatifu hufanywa. Pale, tunaweza kumlilia Baba wa Mbinguni katika sala, na Yeye atafanya mambo kuwa sahihi katika wakati Wake, kutujaza na upendo, na kutupa amani isiyo na mwisho. Ninajua kwamba tunapomtegemea Kristo, tutaona miujiza tunayoihitaji. Sisi ni watoto wapendwa wa Baba yetu wa Mbinguni, na Ana kazi kubwa ya sisi kufanya—kuwakusanya Israeli pande zote mbili za pazia.

msichana

Precious K., miaka 17, Jimbo la Abia, Nigeria

Anapenda kusikiliza muziki, kuimba na kutengeneza marafiki wapya.