Hazina Zilizofichika
Kutafuta Upatanisho wa Mwokozi katika Agano la Kale.
Angalia kwa ukaribu; jifunze kwa kina.
Baadhi ya watu wanaweza kufikiria kwamba Agano la Kale, ambalo liliandikwa kabla Mwokozi hajazaliwa na halimtaji Yesu Kristo kwa jina, halina mengi ya kusema kuhusu Pasaka. Lakini kama vile Kitabu cha Mormoni kinavyofafanua, watu katika nyakati za kale walimjua na walikuwa na imani katika Mwokozi, pia (ona Yakobo 4:4).
Waisraeli walifundishwa kwamba kusudi la sheria ya Musa lilikuwa kuwaelekeza wao kwa Kristo. Kwa mfano, wakati walipo ponywa kutokana na kuumwa na nyoka wenye sumu kwa kumtazama nyoka wa shaba ambaye Bwana alikuwa amemwelekeza Musa kumtengeneza, Musa aliwafundisha kwamba hii ilikuwa ishara ya Mwokozi, ambaye angekuja na kuwaokoa kutokana na dhambi zao (ona Hesabu 21:7–9; Alma 33:18–20).
Kwa bahati mbaya, wingi wa uwazi huo unakosekana kutoka kwenye Biblia kama tulivyo nayo leo, kutokana na mabadiliko—yote ya kukusudia na ya bahati mbaya—kwa karne nyingi (ona 1 Nefi 13:23–27).
Lakini kama ukiangalia, bado unaweza kupata marejeleo mengi kuhusu Mwokozi na Upatanisho Wake katika Agano la Kale. Hebu tuzungumze kuhusu machache!
Jumapili ya Matawi, Gethsemane, na Hukumu
“Mfalme wako anakuja kwako: yeye ni mwenye haki, naye ana wokovu; ni mnyenyekevu, amepanda punda, naam mwana punda, mtoto wa punda” (Zakaria 9:9).
Hili lilitimizwa juu ya kile ambacho sasa kinajulikana kama Jumapili ya Matawi, siku saba kabla ya Pasaka, wakati Yesu kwa shangwe ya ushindi alipoingia Yerusalemu (ona Mathayo 21:15).
“Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; lakini tulimdhania yakuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa” (Isaya 53:4).
Katika Gethsemane, Mwokozi aliteseka kwa ajili ya dhambi zote—na kuhisi huzuni, maumivu, magonjwa, na mateso—ya kila mtu aliyewahi kuishi au ambaye angeishi duniani. Kwa sababu ya hili, Yeye Anajua jinsi ya kutufariji katika majaribu yetu (ona Alma 7:11–13; ona pia Mathayo 8:17).
“Alionewa, na aliteswa, wala hakufunua kinywa chake; kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake” (Isaya 53:7).
Yesu alibaki kimya wakati kuhani mkuu alipomhoji (ona Marko 14:60–61).
Kusulubiwa
“Kusanyiko la waovu wamenisonga; wamenitoboa mikono na miguu” (Zaburi 22:16).
“Wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura” (Zaburi 22:18).
“Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki” (Zaburi 69:21).
Kusulubiwa ilikuwa ni njia ya kawaida ya kuadhibu kwa kipindi hicho, lakini askari wa Kirumi walikuwa kiupekee wakatili katika dhihaka yao na mateso ya Mwokozi (ona Yohana 19:1–3; Mathayo 27:34–35, 48).
Ufufuko
“Amemeza mauti hata milele; na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo” (Isaya 25:8).
“Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi: Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi na minyoo lakini pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu” (Ayubu 19:25–26).
Bwana Yesu Kristo alifufuka. Yeye yu hai sasa! Maandiko na shuhuda zisizohesabika huthibitisha hili. Cha zaidi, Baba yetu wa Mbinguni alijua kutoka mwanzo kwamba tungemhitaji Mwokozi, na amekuwa akiwatayarisha watoto Wake kumpokea Mwokozi tangu nyakati za Agano la Kale.